Na Benny Mwaipaja, WFM-Dodoma
Serikali
imeiongezea Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora nchini kiasi cha
shilingi bilioni 2.6 katika Bajeti yake ya mwaka 2017/2018 kwa kutambua
na kuthamini majukumu yake katika Taifa.
Kauli hiyo imetolewa Bungeni
mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango (MB),Mhe. Dkt. Ashatu
Kijaji alipokuwa akijibu swali la msingi la Mbunge wa Viti Maaluum
(CCM), Mhe. Mwantumu Dau Haji aliyetaka kujua mpango wa Serikali
kuiwezesha Tume hiyo kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Mhe.
Mwantumu Haji amesema kuwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora
imekuwa ikitengewa fedha kidogo sana katika bajeti kwa zaidi ya miaka
mitatu mfululizo hali inayosababisha Tume hiyo kushindwa kutekeleza
majukumu yake ipasavyo.
Akijibu
swali hilo, Dkt. Kijaji alisema kuwa katika mwaka wa fedha 2017/18,
Serikali imetenga bajeti ya Sh. 6,166,978,000 kwa Tume ya Haki za
Binadamu na Utawala Bora ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 42.31 ya
bajeti ya mwaka 2016/17 ambayo ilikuwa Sh. 3,557,589,200.
Alisema
kuwa viwango vya ukomo wa bajeti kwa mafungu, hutegemea vipaumbele vya
Taifa na maoteo ya mapato katika kipindi husika hivyo ongezeko la ukomo
wa bajeti ya Tume hiyo kwa mwaka 2017/18 linaonesha dhahiri kuwa
Serikali inatambua umuhimu wa Tume hiyo pamoja na majukumu yake.
Dkt.
Kijaji aliongeza kuwa Serikali inaendelea kuimarisha mikakati ya
ukusanyaji wa mapato ya ndani il kuhakikisha mafungu yote ya kibajeti
ikiwemo Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora yanaendelea kupata
fedha za kutosha ili kutekeleza majukumu yao kikamilifu.
“Napenda
kulitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba, tarehe 01/06/2017 Mhe. Dkt. John
Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alizindua mfumo
wa ukusanyaji mapato ya ndani ujulikanao kama ‘Revenue Gateway System’
ikiwa ni moja ya mikakati ya Serikali kuimarisha ukusanyaji mapato yake
yatakayowezesha upatikanaji wa fedha za kutoa huduma mbalimbali kwa
wananchi”, alifafanua Dkt. Kijaji.
Mwisho
0 comments:
Post a Comment