Home » » DK.KAMANI AWAKUMBUSHA WANANCHI KUSIMAMIA MIRADI MAENDELEO

DK.KAMANI AWAKUMBUSHA WANANCHI KUSIMAMIA MIRADI MAENDELEO

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi,Dk. Titus Kamani
Serikali imesema haina mpango wa kupeleka polisi kusimamia na kulinda miradi ya maendeleo kwa kuwa hilo ni jukumu la wananchi kwa faida yao.
Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Titus Kamani, alisema hayo kwa nyakati tofauti, wakati akikagua na kufungua miradi yenye thamani ya zaidi ya Sh. milioni 155.5 katika vijiji vya kata za Ngasamo na Badugu, wilayani Busega, mkoa wa Simiyu.

Miradi hiyo inahusisha ujenzi wa zahanati ya Kijiji cha Mwamwenge (Ngasamo), kisima kirefu cha Kijiji cha Manala, maabara ya Sekondari Kata ya Badugu na zahanati ya Kijiji cha Busami (Badugu).

“Nimefurahishwa na juhudi mnazofanya kujiletea maendeleo. Kwa kuwa wajibu wa serikali ni kusapoti nguvu za wananchi, nitatoa bati zote za kupaua jengo hili la zahanati yenu ya Mwamwenge,” alisema Dk. Kamani, wakati akikagua jengo la zahanati hiyo linalojengwa kwa nguvu za wananchi na halmashauri ya wilaya hiyo kwa thamani ya zaidi Sh. milioni 27.

Akifungua kisima cha Manala kilichogharimu Sh. milioni 42 kabla ya kuzindua maabara ya sekondari ya Badugu, Dk. Kamani, ambaye pia ni Mbunge wa Busega, alisema: “Serikali inatumia fedha nyingi kutekeleza miradi ya maendeleo yenu. Msipoitunza na kuilinda ikahujumiwa mtakuwa mmejikwamisha wenyewe. Serikali haitaleta polisi wa kuwasimamia na kuilinda.”

Kisima hicho kimejengwa kwa ufadhili wa Kanisa la Nazareth Compassion la nchini Marekani kwa kushirikiana na wananchi wa kijiji hicho, Halmashauri ya Wilaya ya Busega na ofisi ya mbunge, ambayo ilichangia Sh. milioni 6.5 kutoka katika mfuko wa jimbo.
 
Dk. Kamani alisema yeye siyo mbunge wa maneno, bali wa vitendo na kwa kuwa sera ya serikali ya CCM ni kuhakikisha kila kijiji kinakuwa na zahanati, atatoa mifuko 100 ya saruji yenye thamani ya zaidi ya Sh. milioni 1.8, kwa ajili ya ujenzi wa zahanati ya Busami, ambayo ujenzi wake uko katika hatua ya msingi.

Alisema kwa mwaka huu wa fedha serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Busega itachimba kisima kirefu kimoja katika Kijiji cha Jisesa na imetenga Sh. milioni 731 kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa maji Manala, ambayo yatasambazwa katika vijiji vya Kata ya Badugu.
 
SOURCE: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa