Home » » SERIKALI YASAMEHE KODI TRILIONI 1.5/-

SERIKALI YASAMEHE KODI TRILIONI 1.5/-

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), imeonyesha kuwa serikali imeendelea kutoa misamaha mikubwa ya kodi ambayo ni asilimia kumi ya bajeti ya mwaka 2012/13.

Kwa mujibu wa ripoti ya ukaguzi wa fedha za Serikali Kuu kwa mwaka huo, iliyowasilishwa jana na Ofisi ya CAG kwa Kamati ya Hesabu za Serikali Kuu (PAC), inaonyesha kuwa misamaha ya kodi ni Sh. bilioni 1,515.6 sawa na asilimia kumi ya bajeti ya mwaka huo ya Sh. Trilioni 15.191.

 Wakati serikali ikiendelea kutoa misamaha mikubwa ya kodi, kumekuwapo na malalamiko kwamba misamaha hiyo ipunguzwe ili serikali ipate mapato zaidi kwa ajili ya kugharimia miradi ya maendeleo na kutoa huduma muhimu kwa wananchi.

Kumekuwapo na mapendekezo kutoka kwa makundi ya jamii wakiwamo wabunge kwamba kiwango cha misamaha ya kodi kisizidi asilimia moja.

Ripoti hiyo iliwasilishwa mbele ya kamati hiyo na Kaimu CAG, Athumani Selemani.Ripoti hiyo imebainisha kuwa serikali haikutoa kiasi cha Sh. bilioni 863.2 sawa na asilimia sita ya bajeti ya mwaka huo.

“Uchambuzi wa Hesabu  Jumuifu katika kipindi husika Serikali ilipangwa kutumia zaidi ya Sh. Trilioni 11 kwa matumizi ya kawaida ikilinganishwa na kiasi halisi zaidi ya Sh. Trilioni 10.7 na kupelekea kuwapo kwa kiasi cha zaidi ya Sh. bilioni 353.9 ambazo hazikutolewa (sawa na asilimia tatu) ya bajeti ya matumizi ya kawaida,” inaeleza.

Ilieleza kuwa zaidi ya Sh. bilioni 31.9 hazikutumika na kwamba zaidi ya Sh. Trilioni 4.2 zilitengwa kwa ajili ya maendeleo, lakini kilichopokelewa kutoka Hazina ni zaidi ya Sh. Trilioni 3.7 wakati Sh. bilioni 509.2 ambazo ni sawa na asilimia 12 ya bajeti ya maendeleo hazikutolewa.

“Licha ya kutoa fedha pungufu za maendeleo, akaunti ya fedha za maendeleo ilikuwa na salio la fedha ambayo haikutumika kiasi cha Sh. bilioni 40 kutokana na matumizi ya Sh. Trilioni 3.6,” ripoti inabainisha.

Kadhalika, CAG anaeleza kuwa hakuna kitengo kilichoandaliwa kufuatilia na kutathmini miradi inayotekelezwa kwa fedha za mikopo.

Aidha, imebainisha udhaifu mkubwa katika mifumo ya udhibiti wa matumizi, malipo, ukosefu wa nyaraka za malipo, matumizi yasiyo na manufaa, matumizi yasiyoridhisha, kukosekana kwa hati za malipo, masurufu yasiyorejeshwa na udhibiti dhaifu wa bajeti.

CAG alisema hadi kufikia Juni 30, mwaka 2013, taarifa jumuifu za Taifa zilionyesha kiasi cha Sh. bilioni 3.616.2 zilitumika katika miradi ya maendeleo kati yake Sh. Trilioni 2.2 kilitokana na mapato ya ndani na Trilioni 1.3 ikiwa ni sawa na asilimia 39 ya fedha za maendeleo iliyotumika kama misaada kutoka kwa washirika wa maendeleo.

Ripoti hiyo imebainisha kuwa upotevu wa Sh. bilioni 13.2 ambazo ni mali na vifaa ikiwa ni ongezeko la zaidi ya Sh. milioni 206.5 ya fedha zilizopotea mwaka 2011/12.

 Pia, CAG amebainisha udhaifu wa mfumo wa udhibiti wa ndani ambao unafanyakazi chini ya kiwango kutokana na uhaba wa watumishi, rasilimali na mapungufu katika muundo wa kamati za ukaguzi.

Ukaguzi huo umebaini kuwa wizara, idara za serikali na sekretarieti za mikoa hazikuwa na sera inayoongoza matumizi ya teknolojia ya habari iliyoandikwa na kutolewa kwa watumiaji wote wa vifaa vya kompyuta.

CAG alibainisha mishahara ambayo haikulipwa na haikurejeshwa Hazina ni zaidi ya Sh. milioni 269.3 katika wizara, idara, wakala na sekretarieti za mikoa.

WATUMISHI HEWA
Vile vile, alibainisha malipo hewa kwa watumishi ambao hawapo kwenye utumishi zaidi ya Sh. milioni 779.3 huku kukiwa na madai ya watumishi zaidi ya Sh. bilioni 1.1.

CAG alisema serikali imenunua mali zenye thamani ya zaidi ya Sh. milioni 239.9 na hazijatumika na kwamba kulikuwa na malipo ya Sh. bilioni 480 kwa bodi za zabuni bila idhini ya bodi.

Kamati hiyo inaendelea na vikao vyake kwa kuwaita wakurugenzi wa mashirika ya umma na serikali, na kwa leo watakutana na Msajili wa Hazina kwa ajili ya ufafanuzi wa masuala mbalimbali ya serikali.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa