Home » » KASHFA MABILIONI ESCROW MOTO BUNGENI

KASHFA MABILIONI ESCROW MOTO BUNGENI


Huku kukiwa na madai kuhusu baadhi ya wabunge kupitiwa kupoza kashfa ya kuchota kifisadi Dola za Marekani milioni 200 (Sh. bilioni 320) kwenye akaunti ya Tegeta Escrow ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), mvutano mkubwa umeibuka juu ya uhalali wa ripoti ya uchunguzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuhusiana na kashfa hiyo kuwasilishwa na kujadiliwa bungeni.

Mvutano huo, ambao umewahusisha upande mmoja na wabunge; Ezekia Wenje (Nyamagana-Chadema), Joshua Nasari (Arumeru Mashariki-Chadema), Zitto Kabwe (Kigoma Kaskazini-Chadema) na Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya upande mwingine.

WENJE
Mvutano huo uliibuka jana bungeni baada ya Wenje kuomba mwongozo wa spika akitaka kujua kama ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) itawasilishwa bungeni na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na ya Takukuru.

NDUGAI
Akijibu mwongozo huo, Ndugai alisema ripoti ya Takukuru haitawasilishwa bungeni na kwamba, itakayowasilishwa ni ile ya CAG pekee.

“Jibu lake (mwongozo huo) ni kwamba, ni hapana. Ripoti ambayo itapelekwa PAC ni ripoti ya CAG peke yake. Takukuru wakishafanya kazi yao, wakigundua kuna matatizo watachukua hatua moja kwa moja, hawana haja ya kupata ushauri wa Bunge,” alisema Ndugai.

NASARI
Hata hivyo, Nasari aliomba mwongozo wa spika na kupinga majibu hayo yaliyotolewa na Ndugai kwenye mwongozo wa Wenje akisema maamuzi ya kutaka CAG afanye ukaguzi katika kashfa ya Escrow ni ya Bunge.

Alisema pia Bunge liliazimia kuwa Takukuru ifanye uchunguzi kuhusiana na tuhuma za kashfa hiyo.

Hata hivvyo, alisema anastaajabishwa kusikia tena Ndugai akitamka kwamba, itakayojadiliwa na Bunge na ripoti ya CAG pekee, lakini ile ya Takukuru haitawasilishwa bungeni.

“Lakini Mheshimiwa Naibu Spika hili suala linazidi kuwa na utata zaidi na sintofahamu kubwa,” alisema Nasari.

Alisema hiyo inatokana na kwamba, wiki iliyopita Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk. Edward Hoseah, akiwa jijini Mwanza, alikaririwa akisema kuwa ripoti ya taasisi yake amekwishamkabidhi waziri mkuu.

Lakini akasema baadaye kupitia Bunge, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, akasema hajakabidhiwa ripoti hiyo.“Nini kinachofichwa hapa katikati? Kwa hiyo, mheshimiwa naibu spika, naomba mwongozo wako kwamba inakuaje Bunge linadharaulika? 

Na tunafahamu hizi fedha zimeliwa na watu wachache, ambao wametajwa kwenye ripoti, tayari taarifa tunazo na ndiyo sababu imegharimu kufichwa na ndiyo maana kwenye ratiba hii (ya shughuli za Bunge) hili suala limekuja kuwekwa kwa siku moja kabla ya Bunge kufungwa,” alisema Nasari.

Aliongeza: “Ni kwa sababu kuna hofu kwamba serikali inakwenda kuanguka, kuna watu wametajwa, kuna mawaziri wamo ndani, viongozi wakubwa. Mheshimiwa naibu spika, naomba mwongozo wako, wakati ambao nchi ina crisis ya dawa, wakati ambapo nchi ina crisis wanafunzi wanakosa mikopo, tunaomba mwongozo wako ni kwanini ripoti hii isiletwe ndani ya Bunge ya uchunguzi wa PCCB, kwa sababu lilikuwa ni azimio la Bunge na kama ni serikali kuanguka, ianguke kihalali.”

NDUGAI
Akijibu mwongozo huo wa Nasari, Ndugai alisema sehemu kubwa ya maelezo yake hayana ukweli kwa sababu hakuwa na taarifa sahihi mapema.

Alisema mwanzoni mwa mkutano wa Bunge, suala hilo liliibuliwa na Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila, na kwamba walikubaliana kwamba, Kamati ya Uongozi wa Bunge ikutane ili kutathmini na kuona namna gani Bunge litashughulikia jambo hilo.

Ndugai alisema kamati hiyo ilikutana na kubadilisha ratiba ya shughuli za Bunge, ambayo inaonyesha kuwa Novemba 26 ripoti ya suala hilo itawasilishwa bungeni.

Hata hivyo, alisema kulingana na utaratibu wa Bunge, ripoti haiwezi kuwasilishwa moja kwa moja bungeni kabla ya haijapitia kwenye kamati husika ya Bunge, ambayo huipitia kisha itawasilishwa mezani na kusomwa maoni yake na kamati hiyo ndani ya Bunge.

Alisema ahadi iliyokuwapo ni kwamba, kashfa hiyo ingeshughulikiwa na CAG na Takukuru.Ndugai alisema kwa upande wa ripoti ya CAG, ambayo imeahidiwa wakati wowote wiki hii itatolewa, utaratibu wake wa kibunge itapita PAC, ambayo itakaa na kuipitia kisha baadaye Novemba 26, ambayo imepangwa na Kamati ya Uongozi wa Bunge, itawasilishwa bungeni ili kuwapa fursa wabunge kuijadili na kutoa ushauri.

Kuhusu ripoti ya Takukuru, Ndugai alisema itachukua muda mrefu zaidi na kwamba, haijulikani, kwani inaweza kuchukua miezi mitatu au sita kwa kuwa ni ya uchunguzi, ambao utahusisha hadi nje ya nchi.

Alisema kisheria, Takukuru wakishafanya kazi yao, wanatakiwa kuchukua hatua moja kwa moja pale, ambako wanaona kuna matatizo, ikiwamo kumuandikia Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) na kwenda mahakamani.

“PCCB hana sababu ya kuja bungeni. Aje ili ajadili nini sasa? Ndiyo maana ripoti, ambayo itakuja hapa ni ripoti ya CAG kwa utaratibu wetu wa kibunge,” alisema Ndugai.
Alisema kama ilitakiwa ripoti ya Takukuru ipelekwe bungeni ilibidi ipelekwe kwenye Kamati ya Bunge ya Ulinzi na Usalama kisha mwenyekiti wake aipeleke bungeni jambo, ambalo haliwezekani.

“Kwa hiyo, jambo hilo haliko hivyo, liko hivi ambavyo naelezea. Kwa hiyo, hakuna kilichofichwa na mambo haya yamepangwa na Kamati ya Uongozi wa Bunge. Kwa hiyo, kama kuna hoja yoyote iambieni Kamati ya Uongozi na itakutana tena na tena na tena, kama kuna jambo tunarekebisha tu,” alisema Ndugai.

Aliongeza: “Lakini tusihisiane kwamba kuna mtu anajaribu kuficha chochote katika jambo hili, hapana hata kidogo. Ni mtiririko wa shughuli zenyewe za Bunge zilivyo na utaratibu wenyewe ulivyo. Tunachoweza kufanya kwa ratiba ya Bunge ni tarehe 26, 27 tutajadil jambo hilo kupitia kamati ya PAC, ambayo itakuwa imekwishaipitia na wabunge wote mtapata nakala, sioni ugomvi ni wa jambo gani.”

ZITTO
Zitto alisema namna Ndugai alivyoelezea ndivyo, ambavyo inapaswa kuwa, lakini akasema changamoto iliyopo kwa wabunge ni kwamba, ripoti ya CAG inazungumzia mchakato wa ufunguaji na utoaji wa fedha katika akaunti ya Escrow.

Alisema PAC itakapokuwa ikifanya kazi ni lazima iwe na taarifa ya ziada wakati itakapokuwa ikiwahoji watu, ambao wametajwa katika mchakato mzima.

“Kwa mfano, kabla ya kuthibitisha manunuzi kama yamefanyika ilitakiwa Brela (Mamlaka ya Usajili na Usimamizi wa Biashara) wawe wamefanya due delegency (kujiridhisha).

Kama Brela hawakufanya delegancy ni rahisi fraud (wizi) kuweza kutokea. Anayeweza kuditact (kubaini) fraud (wizi) ni PCCB (Takukuru),” alisema Zitto.
Aliongeza: “Kwa hiyo, anayeweza ni lazima PAC katika mchakato mzima iwe na taarifa ya PCCB.”

Pia alisema inasemekana kwamba, masuala ya kisheria, ambayo yamekuwa yakiandikwa na serikali kwa ajili ya suala la kampuni ya kufua umeme ya IPTL, yalikuwa yanaandikwa na wanasheria wa IPTL na kwamba, hilo wanalo Takukuru kwa sababu wao ndiyo waliokuwa wanaangalia mawasiliano ya kompyuta ya IPTL na ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Hivyo, akasema ili PAC iweze kumhoji vizuri AG, lazima iwe na ripoti ya Takukuru. “Yaani hakuna namna ambayo tunaweza tukaikwepa ripoti ya PCCB,” alisema Zitto.
Alisema kuna minong’ono na kampeni nyingi zinaendelea kuhusiana na suala la Escrow na kusema njia pekee ya kuondokana na hilo ni uwazi, kwani itakuwa rahisi kushughulikia jambo kama hilo na kuondoa mambo hayo aliyosema kuwa yanaendelea miongoni mwa wabunge.

Hivyo, akaomba Spika wa Bunge aiagize serikali ipeleke ripoti zote za CAG na ya Takukuru kwa pamoja bungeni ili wabunge wazishughulikie na pia mchakato mzima wa uendeshaji wa mahojiano ya kazi hiyo uwe kwa uwazi, na kwamba, usifanyike kwa siri.

“Tukiufanya kwa siri tutakuwa haya maminong’ono yanayoendelea miongoni mwa wabunge, wabunge mnajua mnapitiwapitiwa, ili tuyaondoe haya maminong’ono tufanye kwa uwazi ili kila mtu astahili adhabu kulingana na aliyoyafanya,” alisema Zitto.

PROFESA MWANDOSYA
Profesa Mwandosya alisema serikali imesikia kwa makini hoja za wabunge, lakini akasema haiwezi kuficha.

Aliitahadharisha PAC na wabunge kuhusiana na kazi watakayoifanya kuhusiana na kashfa ya Escrow, isije ikaingiliana na kazi za Takukuru, ambazo alisema zinaweza kusababisha mashtaka ya jinai yakafunguliwa dhidi ya baadhi ya watuhumiwa.

“Lakini kwa maana ya kuisaidia kamati kuna ripoti za aina mbili, moja inaweza kuja kwa maandishi. Lakini kamati inaweza kuiita Takukuru kuisaidia shughuli zake,” alisema Profesa Mwandosya.

Aliwataka wabunge kutozingatia ripoti akisema kwamba, hupelekwa bungeni kwa aina mbili, ambayo Takukuru inaweza kutoa kwa kamati ilimradi haitaharibu mchakato wake wa kupeleka makosa ya jinai mahakamani.

RIPOTI YA CAG KWA PINDA WIKI HII
Wakati hayo yakiendelea Kaimu Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Francis Mwakasalila, amesema ripoti ya uchunguzi wa suala hilo itawasilishwa kwa Waziri Mkuu  siku yeyote wiki hii. 

Mwakasalila ambaye hakuta kuzungumza kwa undani zaidi suala hilo, aliiambia NIPASHE jana kuwa kimsingi, uchunguzi umekamilika na kilichobaki ni kuipitia kwa ajili ya kuikabidhi.
 
CHANZO: NIPASHE
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa