Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
BAADHI ya wabunge wamekosoa Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa mwaka
2016/2017 uliowasilishwa juzi na Waziri wa Fedha, Dk. Philip Mpango.
Wakichangia bungeni jana, wabunge hao walisema mpango huo hauwezi
kufanikiwa pasikuwapo na juhudi za ziada na wengine wakisema una nia ya
kuua mashirika ya umma na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
Katika kuimarisha ukusanyaji wa mapato, Serikali kupitia mpango huo
imepiga marufuku utaratibu wa kutumia sehemu ya maduhuli (retention),
hivyo mapato yote yatakayokusanywa na halmashauri na mashirika ya umma
yatawasilishwa katika Mfuko Mkuu wa Serikali (Hazina).
Akichangia mjadala wa mpango huo, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Peter
Serukamba (CCM), aliwataka wabunge wenzake kuungana kupinga uamuzi huo
wa Serikali, akisema unalenga kuua halmashauri na mashirika ya umma.
“Utaratibu wa kufuta retention scheme sikubaliani nao, mambo haya
ndiyo yaliua viwanda vyetu miaka iliyopita kwa sababu walikuwa wakitaka
kufanya hata matengenezo ya mashine wanashindwa hawana fedha, fedha zote
zimehifadhiwa Hazina.
“Leo mnataka kuua halmashauri jambo hili haliwezekani, wabunge
tupinge ‘retention scheme’ Serikali mnataka kuyapeleka wapi mashirika ya
umma?
“Yaani leo Tanapa (Shirika la Hifadhi za Taifa) likikusanya fedha
zote ziende Central Government (Serikali Kuu), mtaua mbuga zetu kwa
utaratibu huu. Kama ni fedha za Serikali sawa wekeni Hazina, lakini
fedha zinazozalishwa sehemu nyingine ziacheni zibaki huko,” alisema.
Serukamba ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Maendeleo na
Huduma za Jamii, alisema uamuzi huo unakinzana na dhana ya ugatuaji wa
madaraka kutoka Serikali Kuu kwenda Serikali za Mitaa
(Decentralization).
Mbunge huyo pia alizungumzia suala la ujenzi wa reli mpya na kuitaka
Serikali kuainisha katika bajeti ya mwaka huu ujenzi wa reli mpya katika
kiwango cha Standard Gauge kutoka Dar es Salaam hadi Kigoma itajengwa
lini.
“Katika mpango huu naona suala la ujenzi wa reli limewekwa kijumla
jumla tu, nataka mtuambie ujenzi huu wa reli mpya kwa kiwango cha
‘Standard Gauge’ kuanzia Dar es Salaam hadi Kigoma, Kaliua hadi Mpanda
au ni kutoka wapi kwenda wapi?” alihoji.
Bashe
Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM), akizungumza nje ya
viwanja vya Bunge, alisema msimamo wa wabunge kanda ya magharibi mwaka
huu ni kupigania reli.
“Hilo tumelisema wazi, tutakwamisha bajeti ya mwaka huu kama
Serikali itashindwa kukamilisha ahadi yake ya kujenga reli mpya kwa
kiwango cha Standard Gouge. Tumesema bila reli no bajeti.
“Hili limekuwa likisemwa kwa muda mrefu lakini utekelezaji wake
hakuna, reli ya kutoka Dar es Salaam hadi Kigoma, Tabora hadi Mwanza,
Kaliua hadi Mpanda na Uvinza hadi Msingati,” alisema.
Gekul
Mbunge wa Babati Mjini, Pauline Gekul (Chadema), alisema uamuzi wa
Serikali wa ‘retention’ hauna tija na ni uamuzi wa kutaka kuua
halmashauri nchini.
Gekul alisema uamuzi huo unairudisha nchi katika historia ambako
mwaka 1982 Serikali iliamua kugatua madaraka na kuyashusha chini, kwa
vile mpango wa zamani wa kila kitu kuwa Serikali Kuu ulikuwa na
madhara.
“Utaratibu huu utaua halmashauri zetu, lazima tujue Serikali za Mitaa
zina mamlaka yake, huko wanaajiri wenyewe na wanakusanya wenyewe leo
kusema makusanyo yote lazima yaende Hazina ndiyo waanze kuwapimia wakati
wamekusanya wenyewe, hii si sawa.
“Inakuwaje wakusanye wengine halafu wapange wengine? Kwa mtindo huu
maendeleo yatakuwa hayapo huko chini, hili jambo litapunguza hata morali
kwa wanaokusanya huko chini.
“Mwalimu Nyerere aliliona hili tangu mwanzo ndiyo maana mwaka 1982
aligatua madaraka ya Serikali Kuu yakaenda Serikali za Mitaa kwa sababu
alijua Serikali haiwezi kufanya kila kitu,” alisema.
Sakaya
Mbunge wa Kaliua, Magdalena Sakaya (CUF) alisema licha ya Rais
Magufuli kuahidi kuwa anataka Tanzania iwe nchi ya viwanda, lakini haoni
dalili za kufikia huko.
Alisema ni aibu kwa Tanzania kugeuzwa soko la bidhaa za nchi nyingine
na akaeleza kukerwa na kukosekana kwa juhudi za kudhibiti matumizi ya
dola.
“Tunasema tunaka Tanzania ya viwanda, itawezekanaje wakati
tumeshindwa kudhibiti matumizi ya dola, hakuna nchi ambayo wananchi
wanapata huduma kwa dola.
“Ni Tanzania tu watu wanapata huduma madukani kwa dola, kuna utitiri
wa maduka ya chenji, ukienda Kariakoo watu wana dola mikononi, machinga
tu wanatembea na dola mikononi hii ni nchi gani?,” alihoji.
Kuhusu viwanda alisema: “Mnasema nchi ya viwanda, viwanda vyenywe
vipi? Tulikuwa na viwanda vingi tu vyote vimekufa, hatuwezi kufika huko
ikiwa hata tooth pick (vijiti vya kuchokonolea meno) tunaagiza nje,
this is a shame (ni aibu).
“Hii mipango ni mizuri lakini tusipojitahidi kubadilisha mindset
(mtazamo) za watendaji itakuwa kazi bure kwa sababu mipango hii haiendi
kutekelezwa na robot inakwenda kutekelezwa na watu,” alisema.
Hasunga
Mbunge wa Vwawa, Japhet Hasunga (CCM) alisema mpango huo utafanikiwa
iwapo watendaji wa Serikali watavaa uzalendo wakafanya kazi ya
kuwatumikia Watanzania.
Alisema Tanzania ina fursa nzuri za maendeleo lakini maendeleo hayapo kutokana na kukosa viongozi wazalendo.
“Tanzania tunayo ardhi nzuri, misitu, madini, mbuga, mito, maziwa, bahari lakini pia watu ni wengi takriban milioni 50.
“Tuna faida za ziada, lakini hatuwezi kufikia nchi ya kipato cha kati
kwa sababu tatizo ni viongozi. Nashukuru leo tumempata kiongozi mzuri,
Rais Magufuli, naamini tutasogea,” alisema.
Mpango wa Maendeleo ya Taifa na mwelekeo wa bajeti katika kipindi cha
mwaka 2016/2017 uliwasilishwa bungeni juzi, huku ukiweka mkazo katika
ukusanyaji wa mapato na kubana matumizi.
Mwelekeo huo unaonyesha kuwa bajeti itaongezeka kutoka Sh trilioni
22.495 mwaka 2015/2016 hadi Sh trilioni 22.991 mwaka 2016/2017, ambalo
ni ongezeko la asilimia 2.2.
CHANZO: MTANZANIA
0 comments:
Post a Comment