Home » » Sekondari kongwe za umma kurejeshewa makali

Sekondari kongwe za umma kurejeshewa makali

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako.
WIZARA ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi imewasilisha bajeti yake ya mwaka ujao wa fedha kwa kuomba iidhinishiwe Sh trilioni 1.3 ambazo pamoja na masuala mengine, imeahidi kuzirudishia shule kongwe hadhi na ubora.
Waziri Profesa Joyce Ndalichako alisoma bajeti hiyo jana bungeni na kusema kwamba wataalamu wameshaanza kazi ya kukagua shule hizo kwa ajili ya kuziboreshea mazingira ya kufundishia na kujifunzia. Alisema awamu ya kwanza itaanza na shule 33 ambazo zitakarabatiwa.
Shule hizo na mikoa yake kwenye mabano ni Ihungo (Kagera), Ilboru (Arusha), Kilakala (Morogoro), Mwenge (Singida), Msalato (Dodoma), Mzumbe (Morogoro), Nganza (Mwanza), Pugu (Pwani), Same (Kilimanjaro), Tabora Wavulana na Tabora Wasichana (Tabora).
Nyingine Azania (Dar), Jangwani (Dar), Kantalamba (Rukwa), Mpwapwa (Dodoma), Tosamaganga (Iringa), Malangali (Iringa), Milambo (Tabora), Nangwa (Shinyanga), Kibiti (Pwani), Minaki (Pwani), Ifakara (Morogoro),Songea Wavulana (Ruvuma), Ndanda (Ruvuma), Kibaha (Pwani) na sekondari ya Kigoma.
Shule nyingine zitakazorudishiwa hadhi yake kwa kukarabatiwa ni shule za ufundi za Bwiru Wavulana (Mwanza), Ifunda (Mbeya), Iyunga (Mbeya), Moshi (Kilimanjaro) ,Mtwara (Mtwara), Musoma (Mara) na shule ya ufundi ya Tanga.
Mabadiliko sheria, kanuni Aidha, Profesa Ndalichako alisema katika mwaka ujao wa fedha, serikali itafanyia marekebisho baadhi ya sheria na sera zake na kuhakikisha wanakabiliana na changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa sera ya utoaji wa elimu bure.
Alisema wataendelea kutekeleza sera ya elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 pamoja na kufanya mabadiliko ya sheria ya Elimu na kupitia Sheria, Kanuni na taratibu za taasisi zilizo chini ya wizara.
Taasisi hizo ni Baraza la Mitihani,Taasisi ya Elimu Ithibati na Udhibiti, Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu na Mamlaka ya Elimu Tanzania. Elimu bure Akizungumzia utekelezaji wa elimu bure, Ndalichako alisema waraka wa elimu uliweka bayana majukumu ya wadau muhimu katika utoaji elimu bila malipo kuwa wazazi wanatakiwa kununua sare za shule na michezo,vifaa vya kujifunzia, chakula kwa wanafunzi wa kutwa na kugharimia matibabu kwa watoto wao.
Pia wanawajibika kulipia nauli ya kwenda shule na kurudi kwa wanafunzi wa kutwa. Kampasi ya Mloganzila Alisema ujenzi wa Kampasi mpya ya Mloganzila ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili (MUHAS), uliofanywa kwa ushirikiano wa serikali na serikali ya Korea, unakamilika mwezi ujao. Alisema chuo kitakuwa na hospitali, itakayokuwa na uwezo wa kuchukua wagonjwa 571 na kulazwa kwa wakati mmoja.
Chanzo Habari Leo

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa