Home » » SERIKALI KUMLINDA MKULIMA KWA KUANZISHA VITUO VYA UNUNUZI WA MAZAO.

SERIKALI KUMLINDA MKULIMA KWA KUANZISHA VITUO VYA UNUNUZI WA MAZAO.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Na Tiganya Vincent, Dodoma
Wakala wa Vipimo kwa kushirikiana na Mamlaka ya Serikali za Mitaa inakusudia kuanzisha  vituo maalum vya ununuzi wa mazao ya wakulima (buying centres) katika vitongoji nchi nzima ili kuondoa unyonyaji na ukandamizaji unaofanwa na wachuuzi wa mazao ya wakulima.

Kauli hiyo imetolewa leo mjini Dodoma na Waziri wa Viwanda,Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles Mwijage wakati akijibu swali la Mbunge wa Mlalo Mhe. Rashid Shangazi aliyetaka kujua ni lini Serikali itasimamia sheria kuondoa unyonyaji unaofanywa na wachuuzi wakati wa kununua mazao ya wakulima.

Alisema kuwa katika kutekeza hayo hakuna mfanyabiashara atakayeruhusiwa kusafirisha mazao ambayo yamefungashwa kinyume kinyume cha Sheria ya vipimo na kuongeza kuwa katika kusimamia jambo hilo vitaanzishwa vituo maalum vya ukaguzi bila kusabaisha usumbufu katika ufanyaji biashara.

Mhe. Mwijage amewaagiza Maafisa Ugani walioko vijijini watumike kusimamia matumizi ya vipimo rasmi katika vituo hivyo na kutoa taarifa zote muhimu kwa Wakala wa Vipimo.

Aidha ,alisema kuwa Serikali imeamua kufanyia mapitio Sheria ya Vipimo sura 340 ili kuondokana na unyonyaji na ukandamizaji unaofanywa na wachuuzi wa mazao ya wakulima.

Alisema kuwa Serikali imeamua kufanyia mapitio ya Sheria hiyo ili kuweka mazingira mazuri kwa lengo la kumlinda muuzaji kwa kuwadhibiti manunuzi wanaotumia njia za udandanyifu wakati wanaponunua mazao ya wakulima.
Mhe. Mwijage alisema kuwa katika kipindi kifupi kijacho Serikali itawalisha mabadiliko hayo bungeni ili ifanyiwe marekebisho yanayostahili.

Aidha , Waziri huyo alisema kuwa pamoja na marekebisho ya Sheria ya Vipimo yanatarajia kufanywa , Wakala wa Vipimo imewasilisha Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) mapendekezo ya kutungwa kwa sheria ndogo(by laws)  ili ziweze kuwaongoza wakulima na wafanyabiashara kufungasha mazao.
 
Mwisho

SERIKALI KUTOA MAFUNZO MAALUM YA ELIMU YA FEDHA KWA WANANCHI

Na Tiganya Vincent, Dodoma

Wizara ya Fedha na Mipango imesema kuwa  iko tayari kutoa mafunzo maalum ya elimu ya fedha kwa wananchi wote wakiwemo wakinamama kuhusu ili kuleta uelewa mpana wa upatikanaji wa huduma za fedha na taratibu zinazohusu mikopo.

Kauli hiyo imetolewa leo mijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kachwamba Kajaji wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Anna Lupembe aliyetaka kujua mipango ya Serikali ya kupeleka huduma za kibenki vijijini ili wanawake waweze kupata mikopo.

Aidha, alisema kuwa Wizara ya Fedha na Mipango kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BOT) imehakikisha kuwa huduma za kibenki zinawafikia wananchi wengi ili kurahisisha shughuli zao mbalimbali za kiuchumi katika maeneo ya mjini na vijiji.

Alisema kuwa baadhi ya Benki zimeanzisha huduma za Kibenki kupitia mawakala, na huduma za kifedha kupitia simu za mikononi ambazo zimewasaidia wananchi kwenye sehemu ambako hakuna matawi ya Benki.

Mhe. Dkt.Kajaji aliongeza kuwa  Wizara ya Fedha na Mipango kupitia Benki Kuu inaendelea kuweka mazingira wezeshi ili kusaidia nguvu za wananchi na sekta binafsi kuanzisha benki au taasisi za fedha.

Alitoa wito kwa wananchi kutumia fursa ya mazingira mazuri ya uwekezaji yaliyopo hapa nchini kuzishawishi Benki kuanzisha huduma za kibenki katika maeneo yao.

Mhe. Dkt.Kajaji alisema kuwa Wizara ya Fedha na Mipango itaendelea kushawishi Benki nchini kupanua shughuli zao ili ziwafikie wananchi wengi hasa wale wa vijijini wakiwemo akina mama.

Aidha, Naibu Waziri huyo alisema kuwa Serikali kwa kushirikiana na BOT iko tayari kutoa mafunzo maalum ya elimu ya fedha kwa wananchi wote wakiwemo wakinamama kuhusu utumiaji wa huduma za kifedha ili kuleta uelewa mpana wa upatikanaji wa huduma za fedha na mikopo.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa