Na Benedict Liwenga, MAELEZO, Dodoma.
SERIKALI
kwa kushirikiana na na Sekta Binafsi nchini imeandaa mikakati
inayolenga kuongeza tija na uzalishaji wa mbegu za mazao ya mafuta
hususan zao la alizeti ambao uzalishaji wake umekuwa ukiongezeka mwaka
hadi mwaka.
Hayo
yamesemwa leo na Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mhe. Tate
William Ole-Nasha wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe.
Jesca Kishoa kuhusu Serikali kuweka msukumo kwa mazao ya mafuta katika
mikoa husika kwa faida ya nchini na wakazi wa mikoa hiyo.
Mhe.
Ole-Nasha amesema kwamba, Taifa limekuwa likitumia fedha nyingi za
kigeni katika kuagiza mafuta ya kula wakati kuna vyanzo vingi vya mafuta
ikiwemo alizeti na michikichi, hivyo ili kukabiliana na changamoto
hiyo, Serikali inashrikiana na Sekta Binafsi kuweka mikakati itayolenga
kuongeza tija na uzalishaji wa mbegu za mazao ya mafuta hususani
alizeti.
Amesema
kuwa, katika mkoa wa Singida vikundi mbalimbali vimeundwa na taasisi
mbalimbali za Serikali na zile zisizo za Kiserikali ambapo moja ya
malengo ya vikundi hivyo ni kuongeza thamani ya zao la alizeti na
upatikanaji wa pembejeo ili kukuza tija na uhakika wa soko kwa wakulima.
“Kigoma
ni mkoa pekee nchini unaolima zao la michikichi kwa kiwangho kikubwa
ikilinganishwa na maeneo mengine nchini”, alisema Ole-Nasha.
Ameongeza
kuwa, Hadi sasa mkoa una zaidi ya hekta 18,924 za michikichi zenye tija
ya tani 1.6 kwa hekta, uzalishaji huo bado ni mdogo ikilinganishwa na
tani 4 kwa hekta zinazoweza kuzalishwa.
Amesema
pia ili kuongeza tija, mkoa kupitia Halmashauri zake unaendelea
kuhamasisha wananchi kufufua mashamba ya zamani ya michikichi kwa
kuyapalilia, kuondoa majani yaliyozeeka na kuanzisha mashamba mapya
yatakayokuwa yanapandwa mbegu bora.
“Mkoa
kwa kushirikiana na wadau wengine umeshaanza kuzalisha miche bora ya
michikichi ambayo itasambazwa kwa wakulima kwa gharama nafuu ili kila
mkulima apande miche 137 inayotosha hekta moja", aliongeza Ole-Nasha.
Ametoa
wito kuwa, Serikali Kuu na ya Mkoa zinakaribisha wawekezaji zaidi
kuwekeza katika uzalishaji mkubwa na viwanda vya kati na vikubwa vya
kukamua mafuta na bidhaa nyingine zitokanazo na michikichi.
0 comments:
Post a Comment