Home » » Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kushirikiana na Mamlaka nyinginezo kulinda Viwanda vya ndani.

Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kushirikiana na Mamlaka nyinginezo kulinda Viwanda vya ndani.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. Na Benedict Liwenga, MAELEZO, Dodoma.

SERIKALI kupitia Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji inashauriana na Wawekezaji wa Viwanda vinavyofanya kazi kwa kusuasua pamoja na vile vilivyofungwa ili kuviwezesha viwanda hivyo kufanya kazi.

Kauli hiyo imetolewa leo Bungeni mjini Dodoma na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe. Charles Mwijage wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Savelina Mwijage ambaye alitaka kujua Serikali ina mpango gani wa kuviboresha viwanda vya kizamani ili viweze kufanya kazi vizuri kwa faida ya nchi.

Mhe. Mwijage amesema kuwa, viwanda vingi vinavyotumia teknolojia ya zamani ambavyo havifanyi kazi au kuzalisha kwa kusuasua ni vile vilivyobinafsishwa ambapo katika tathmini iliyofanywa na Wizara hiyo kwa kushirikiana na Ofisi ya Msajili wa Hazina inaonyesha kuwa kati ya viwanda vilivyobinafsishwa, viwanda 24 vinafanya kazi kwa kusuasua na viwanda 37 vimefungwa kote nchini.

Aidha, katika mkoa wa Kagera, Kiwanda cha NMC Old Rice Mill kimefungwa wakati kiwanda cha Kagera Tea Co. Ltd (MARUKU) kinafanya kazi kwa kusuasua.

“Kusuasua kwa kiwanda hiki na vingine vyote nchini kunatokana na uchakavu wa mitambo katika baadhi ya Viwanda, ushindani katika soko, kupungua kwa mtaji na kutopatikana kwa malighafi”, alisema Mhe, Mwijage.

Ameongeza kuwa, Serikali inafanya majadilaino na wawekezaji wa viwanda vinavyofanya kazi kwa kusuasua pamoja na vile vilivyofungwa ili kuviwezesha viwanda hivyo kufanya kazi tena ambapo katika majadiliano hayo yanayoendelea, yanahimiza matumizi ya ya teknolojia ya kisasa katika uzalishaji viwandani.

“Tunawashauri wawekezaji walioshindwa kuendesha ipasavyo viwanda vyao kuingia ubia na wawekezaji wengine wenye uwezo wa kuviendesha kwa tija ili tuongeze ajira, tuzalishe bidhaa kwa ajili ya soko la ndani na nje na kulipa kodi”, alisema Mhe. Mwijage.

Amesisitiza kuwa, Wizara yake kwa kushirikiana na Mamlaka nyingine itaendelea kulinda viwanda vya ndani kwa kuhakikisha bidhaa zote ziingiazo zinakidhi viwango na zinatozwa tozo stahiki.

“Tutahakikisha kuwa tunaboresha wepesi wa kufanya biashara kwa kuondoa tozo kero na kuhakikisha kuna umeme wa uhakika wakati wote”, alisisitiza Mhe. Mwijage.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa