Na
Ally Daud-Maelezo
Ugonjwa
unaosababishwa na Sumukavu kwenye Mahindi ya chakula umegundilika katika Wilaya za Chemba na Kondoa
Mkoani Dodoma baada ya kupeleka jopo la Wataalam waliofanya utafiti na kugundua kuwepo kwa ugonjwa huo.
Akizungumza hayo
katika mkutano wake na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam Waziri
wa Afya, Maendeleo
ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bi. Ummy Mwalimu amesema kwamba matokeo ya
awali ya watafiti hao imeonyesha kwamba ugonjwa huo umesababishwa na ulaji wa chakula kilichokuwa na sumukuvu na kuleta
madhara.
“Hayo ni matokeo ya
awali ya watafiti wa wizara yangu hivyo basi nasubiri matokeo ya vipimo vya
damu na haja ndogo vilivyopelekwa kwa uchunguzi zaidi katika Maabara ya CDC, Atlanta
iliyopo nchini Marekani na matarajio
yetu ni kupata majibu hayo katika kipindi kisichozidi wiki moja” aliongeza Bi
Mwalimu.
Aidha Bi. Mwalimu amesema kwamba mpaka kufikia tarehe 24 Juni 2016, idadi ya wagonjwa imefikia 32, na
idadi ya vifo imebakia 7. Hii ni baada ya kuongezeka kwa wagonjwa 11 katika
kipindi cha wiki moja.
“Hadi jana kulikuwa na
jumla ya wagonjwa 9 ambao wamelazwa katika Hospitali ya Mkoa ya Dodoma, na 14
wako katika Hospitali ya Wilaya ya Kondoa. Wagonjwa watatu waliolazwa Hospitali
ya Mkoa Dodoma, na wawili waliolazwa Kondoa, bado hali zao ni tete” aliongeza
Bi. Mwalimu.
Pamoja na
hayo Bi. Mwalimu alisema kwamba Serikali itaendelea kuimarisha mikakati ya kitaifa ya kupunguza uchafuzi
wa sumukuvu katika vyakula, ikiwa ni pamoja na kujenga uwezo wa kupima vimelea
hivyo katika damu na mkojo miongoni mwa taasisi za ndani ya nchi.
“ Tutaendelea kutoa
matibabu kwa wananchi walioathirika na Ugonjwa huo, kwenye Hospitali ya Mkoa wa
Dodoma na Hospitali ya Wilaya ya Kondoa ili kudhibiti na kurudisha afya za
wananchi katika kiwango kinachohitajika” aliongeza Bi. Mwalimu
Aidha Bi. Mwalimu ametoa rai kwa wananchi na wakazi wa Dodoma kwamba wanapaswa kuchambua nafaka
zilizoharibika (zilizooza, kuvunjika, zilizobadilika rangi), kukoboa mahindi
kabla ya kusaga au kuacha kutumia nafaka zitakazoonekana kuharibika sana ili
kuepukana na kiasi kilichozidi sumukavu kwenye nafaka.
0 comments:
Post a Comment