Home » » WIZARA YA FEDHA NA MIPANGO: UFAFANUZI WA HOJA ZA WAHESHIMIWA WABUNGE AKICHANGIA HOTUBA ZA WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO MHE. DKT. PHILIP I. MPANGO (MB) AKIWASILISHA BUNGENI TAARIFA YA HALI YA UCHUMI 2015 NA MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA 2016/17 PAMOJA NA BAJETI KUU YA SERIKALI KWA MWAKA 2016/17

WIZARA YA FEDHA NA MIPANGO: UFAFANUZI WA HOJA ZA WAHESHIMIWA WABUNGE AKICHANGIA HOTUBA ZA WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO MHE. DKT. PHILIP I. MPANGO (MB) AKIWASILISHA BUNGENI TAARIFA YA HALI YA UCHUMI 2015 NA MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA 2016/17 PAMOJA NA BAJETI KUU YA SERIKALI KWA MWAKA 2016/17

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 


JUNI 20, 2016
DODOMA
A.          UTANGULIZI

1.          Mheshimiwa Spika, napenda kutumia fursa hii kukushukuru  wewe binafsi, Naibu Spika na Wenyeviti wa Bunge kwa kuendesha vizuri majadiliano kuhusu Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa 2015 na Mpango wa Maendeleo wa 2016/17 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka 2016/17, niliyowasilisha tarehe 8 Juni, 2016.

2.          Mheshimiwa Spika, Kipekee,  ninampongeza sana Mhe. Naibu Spika kwa umahiri na weledi wa hali ya juu alioonesha katika kusimamia Kanuni za Bunge wakati wote wa kikao hiki cha Bunge la bajeti. Hakika viwango vyake ni vya kimataifa. Japokuwa Mhe. Joseph Kakunda, mwanafunzi wangu Idara ya Uchumi Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam alichomekea sehemu fulani akidai kwamba mimi ni bahiri, (nadhani alimaanisha bahiri wa kutoa maksi za upendeleo!),  nataka niliambie Bunge lako tukufu kwamba kwa viwango ambavyo Mhe. Naibu Spika alivyoonesha humu ndani, hakika ningempa maksi za haki asilimia 100 kama walivyofanya maprofesa wake wa sheria UD na UCT. Hongera sana.

3.          Mheshimiwa Spika, napenda kutambua michango iliyotolewa na: Kamati ya Bajeti, chini ya M/kiti wake Mheshimiwa Hawa Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini; Mheshimiwa David Ernest Silinde, Mbunge wa Momba, Naibu Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu Wizara ya Fedha na Mipango, na waheshimiwa Wabunge wote waliochangia kwa kuzungumza au kwa maandishi hapa Bungeni. Ninawashukuru wote.
4.          Mheshimiwa Spika, jumla ya Wabunge 158 wamechangia hoja niliyowasilisha. Kati ya hao, 133 wamechangia kwa kuzungumza na 25 kwa maandishi.

B:        HATUA ZILIZOPONGEZWA NA WABUNGE WENGI

5.          Mheshimiwa Spika, Hatua zilizopongezwa na Wabunge wengi wakati wa mjadala juu ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Bajeti ya Serikali 2016/17 ni pamoja na zifuatazo:

·        Kuthubutu kutenga asilimia 40 ya bajeti yote kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo, ikiwa pamoja na kuanza ujenzi wa reli mpya ya kati kwa kiwango cha standard gauge, barabara, umeme, ununuzi wa meli mpya ziwa Victoria na ndege tatu za abiria;
·        Kuongeza ukusanyaji wa kodi na mapato yasiyo ya kodi hadi kufikia wastani wa shilingi 1.2 trilioni kwa mwezi kwa kuziba mianya ya uvujaji wa mapato na kuimarisha matumizi ya vifaa vya kielektroniki (EFDs) katika ukusanyaji wa mapato, na Hazina kutoa fedha hizo kama ilivyopangwa;

·        Kusimamia nidhamu ya matumizi na kupunguza matumizi yasiyo ya lazima ikiwa pamoja na safari za nje, posho, sherehe, kuondoa watumishi hewa katika utumishi wa umma;

·        Kuhimiza azma ya kufanya kazi na kurejesha nidhamu ya watumishi kazini kwa ajili ya maendeleo ya Taifa;
·        Kuwapunguzia wafanyakazi mzigo wa PAYE na SDL kwa waajiri;

·        Kuanzisha mahakama ya kushughulikia mafisadi;

·        Kuweka kipaumbele katika kufufua na kujenga viwanda ili kupanua fursa za ajira na wigo wa kodi; na

·        Kujielekeza kutekeleza Ilani ya CCM 2015, ahadi za viongozi wakuu na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 ili kutatua kero za wananchi, hasa masikini.
C:     USHAURI ULIOTOLEWA NA WABUNGE WENGI

6.          Mheshimiwa Spika, Wabunge wengi pia walitoa ushauri katika maeneo mbalimbali, ili yazingatiwe katika bajeti hii au bajeti zijazo. Naomba kurejea ushauri muhimu uliotolewa na Wabunge kama ifuatavyo:

·        Kuongeza tozo kwenye mafuta ili mapato hayo yatumike kupanua huduma za maji na na kukamilisha vituo vya afya na zahanati vijijini;

·        Kuboresha mfumo wa kodi ikiwa pamoja na kufuta kodi, ushuru na tozo za kero kwa wakulima, wafugaji, wavuvi, wafanyabiashara wadogo, wakati na wakubwa/ wawekezaji, lakini pia kutoa ahueni ya kodi kwenye taulo za akinamama na vifaa vya watu wenye ulemavu, vifaa vya michezo, zana za uvuvi, na kulinda viwanda vya ndani;
·        Kuchukua hatua za ziada kuimarisha sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi kwa kuongeza kilimo cha umwagiliaji, pembejeo, ugani, utafiti, mnyororo wa thamani, masoko, ruzuku, mikopo na bajeti ya kilimo;

·        Kuimarisha utalii kwa kuzingatia fursa za kipekee za Tanzania katika sekta hii;

·        Kuchukua hatua madhubuti kulinda mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi;

·        Shilingi milioni 50 zilizoahidiwa kwa kila kijiji ziwekewe utaratibu mzuri na endelevu;

·        Kuongeza kasi ya kulipa madeni ya ndani (watumishi, wastaafu, wakulima, watoa huduma & makandarasi);
·        Kuimarisha elimu na kuhakikisha inaendana na mahitaji ya wataalam wa Tanzania ya leo na kesho;

·        Kupanua wigo wa kodi hususan katika sekta zenye mapato makubwa kama mawasiliano, madini, maliasili na ardhi, na sekta nyingine zenye fursa kama uvuvi na biashara kwenda nchi jirani, e-commerce, gawio kutoka katika mashirika ya umma, sambamba na kuhakikisha kila mwananchi analipa kodi stahiki ili kuchangia maendeleo ya Taifa na kupunguza utegemezi;



·        Kupambana na uvujaji wa mapato hususan katika biashara ya mafuta, miamala ya kielektroniki, transfer pricing na misinvoicing, misamaha ya kodi, wizi na udanganyifu katika ukadiriaji wa kodi, maduka ya jumla, n.k.

·        Kuimarisha ushirikishwaji wa wadau ikiwa ni pamoja na Bunge, katika maandalizi ya mipango na bajeti ya Serikali;

·        Kuendeleza utulivu wa uchumi ikiwa pamoja na kudhibiti mfumuko wa bei, kuongezeka kwa kasi deni la Taifa, kushuka kwa thamani ya shilingi, matumizi ya dola sambamba na shilingi (dollarisation), kupanua huduma za kibenki hadi vijijini na kupunguza riba;

·        Kuboresha sheria mbalimbali ili kuboresha mazingira ya uwekezaji na kufanya biashara nchini;

·        Kuchukua tahadhari katika kufanya mageuzi katika mfumo wa kodi na tozo nchini ili kuepuka kudhoofisha halmashauri na utekelezaji wa dhana ya (ugatuaji madaraka D by D);

·        Kutoa msukumo zaidi kwa ushiriki wa sekta binafsi katika utekelezaji wa miradi ya kipaumbele, ikiwa pamoja na PPP;

·        Kuanzisha duka la kununua madini kutoka kwa wafanya biashara wadogo kutoka nchi jirani na kutoza kodi ya asilimia moja

·        Kuandaa mikakati mahsusi kwa ajili ya kukabiliana na umasikini katika mikoa masikini zaidi ikiwa ni pamoja na kuangalia upya uwiano katika mgawanyo wa fedha na rasilimali nyingine za umma; na
·        Kuongeza bajeti ya Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi ili kuiwezesha kufanya kazi zake kwa ufanisi;

D:     UFAFANUZI WA BAADHI YA HOJA

7.          Mheshimiwa Spika, zipo hoja zilizotolewa na Kamati ya Bajeti, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na kurudiwa na Waheshimiwa Wabunge wengi, ambazo baadhi yake napenda kuzitolea ufafanuzi kama ifuatavyo:

Hoja Na. 1: Pendekezo la kuongeza Tozo ya shilingi 50 kwenye mafuta kwa ajili ya kutunisha Mfuko wa maji na kukamilisha ujenzi wa vituo vya afya na zahanati vijijini

Ufafanuzi:
·        Mheshimiwa Spika, hili ni pendekezo lenye lengo zuri na Serikali inalipokea. Hata hivyo, ni vema kutambua kwamba kufuatia kupungua kwa bei ya mafuta katika soko la dunia, gharama ya mafuta yote yaliyoagizwa kutoka nje imepungua (kwa takriban 20%) na kuchangia kushuka kwa mfumuko wa bei (sasa umefikia 5.2%). Mwenendo huu hakika umeleta ahueni kwa wananchi wetu wengi. Hivyo, kwa sasa Serikali imeamua kutoongeza tozo kwenye mafuta ili wananchi waendelee kunufaika na unafuu huo wa bei ya mafuta. Ni dhahiri kuwa ongezeko la tozo katika mafuta ya petroli na dizeli litasabisha kupanda kwa bei ya mafuta nchini jambo ambalo litaongeza gharama za uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa chakula na bidhaa kama vifaa vya ujenzi na huduma nyingine.

·        Aidha, wataalam wa uchumi wanashauri kuwa kipindi kama hiki cha uwepo wa bei ndogo ya mafuta ni fursa nzuri kwa nchi kuwekeza, hususan katika ujenzi wa miundombinu, viwanda (energy-intensive sectors) na kuendeleza ujuzi na teknolojia. Ndiyo sababu Serikali inaona kuwa ni busara Zaidi badala ya kuongeza tozo kwenye mafuta, tujielekeze kuongeza bajeti ya kutekeleza miradi mikubwa ya miundombinu ya usafirishaji, nishati na elimu sambamba na kutumia fedha zilizopangwa kwa ufanisi Zaidi.

·        Hata hivyo, kwa kutambua umuhimu mkubwa wa kuboresha huduma ya maji nchini, ambayo ni ahadi ya muhimu katika Ilani ya CCM, bajeti ya maendeleo kwa Wizara ya Maji kwa mwaka wa fedha 2016/17 fedha za ndani zimeongezwa kwa asilimia 85 kutoka shilingi bilioni 373.01 mwaka 2015/16 hadi Shilingi bilioni 690.16 mwaka ujao wa fedha 2016/17. Kufuatia jitihada kubwa zinazoendelea kuongeza ukusanyaji wa mapato, Serikali itahakikisha fedha hizi zinapatikana na kutolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji vijijini kama ilivyokusudiwa. Aidha, kwa upande wa haja ya kukamilisha ujenzi wa zahanati vijijini na vituo vya afya katika kata, Wizara ya afya inajipanga kufanya kwanza tathmini ya majengo hayo katika mwaka 2016/17 kwa ajili ya utekelezaji 2017/18.
Hoja Na. 2: Pendekezo la kuondoa msamaha wa kodi ya Mapato kwenye kiinua mgongo cha Waheshimiwa Wabunge.

Ufafanuzi: 
Mheshimiwa Spika,
·        Kwa mujibu wa Sheria ya Kodi ya Mapato, Sura 332 kodi ya mapato hutozwa kwenye vyanzo vyote vya mapato (global income);


·        Kiinua mgongo ni chanzo kimojawapo cha mapato kinachotambuliwa na Sheria na hutozwa kodi;

·        Kupitia Jedwali la Pili la Sheria ya Kodi ya Mapato, kiinua mgongo kinacholipwa kwa wabunge wakati wanamaliza muhula wa miaka mitano kimesamehewa kodi;

·        Msamaha huu hauzingatii kanuni ya usawa ya utozwaji kodi, kwani watu wengine wote wanaopata malipo ya kiinua mgongo, iwe katika sekta binafsi au utumishi wa umma, hutozwa kodi katika mapato hayo. Kwa hiyo, hatua hii imechukuliwa ili kujenga misingi ya usawa na haki katika ulipaji wa kodi; na

·        Lengo la kufanya marekebisho hayo sasa ni kwa ajili ya kuweka utaratibu wa kisheria ambao utatumika kukokotoa stahili za Mbunge endapo ukomo wa Mbunge yeyote utatokea katika kipindi cha kuanzia Julai, 2016 na kuendelea. Aidha, mabadiliko haya yanafanyika sasa ili kuzingatia msingi wa utozaji kodi ambao inataka kodi iwe inatabirika (predictability principle).

·        Mheshimiwa Spika, Naomba niliarifu Bunge lako Tukufu kwamba siku nilipowasilisha pendekezo hili kwa Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliridhia mara moja na kusisitiza kwamba kulipa kodi ni wajibu wa Watanzania wote ili tujenge nchi yetu. Na kwa kuwa kiongozi lazima aongoze kwa mfano alielekeza kuwa yeye ni Mbunge wa Tanzania nzima na anapenda awe wa kwanza kukatwa kodi stahiki kwenye mafao yake ya kustaafu!

·        Hivyo, napenda kufafanua kwamba marekebisho niliyowasilisha mbele ya Bunge lako Tukufu tarehe 8 Juni 2016 katika hotuba yangu ya Mapendekezo ya Serikali Kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha kwa mwaka 2016/17 maana yake ni kuwa kiinua mgongo cha viongozi wote wa kisiasa waliotajwa kusamehewa kodi chini ya Sheria ya Mafao ya Viongozi wa kisiasa (The Political Service Retirement Benefits Act 1995) sasa kitakatwa kodi! Hivyo, kiinua mgongo cha Mhe. Samia Suluhu Hassan Makamu wa Rais, kitakatwa kodi! Mhe. Kassim M. Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa Ruangwa naye atakatwa kodi! Vivyo hivyo, Mhe. Spika na Naibu Spika watakatwa kodi! Aidha, Mawaziri (wakianza na Waziri wa Fedha) na Naibu Mawaziri wote sisi ni wabunge, hivyo kiinua mgongo chetu kitakatwa kodi! Wakuu wa Mikoa na Wilaya kadhalika kiinua mgongo chao kitakatwa kodi!! Mabadiliko haya ni kwa mujibu wa kifungu 10(3) cha Sheria ya Kodi ya Mapato ambacho kimeweka sharti la kutotambua misamaha mingine yoyote ya kodi ya mapato ambayo haijatolewa kwa mujibu wa sheria hii.

Hoja Na.3: Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi (NAO) ametengewa fedha kidogo sana kuweza kutekeleza majukumu yake ipasavyo. Hivyo, bajeti ya ofisi hiyo iongezwe.

Ufafanuzi:
Mheshimiwa Spika,
·        Ukomo wa bajeti ya matumizi mengineyo (OC) uliotengwa kwa mafungu mbalimbali umezingatia maamuzi na mkakati wa Serikali wa kupunguza matumizi ya kawaida na kuelekeza fedha nyingi katika bajeti ya miradi ya maendeleo;

·        Katika kufikia ukomo wa matumizi mengineyo kwa Serikali nzima (Wizara, Idara, Taasisi za Kiserikali, Mikoa na Halmashauri) uchambuzi wa kina ulifanyika kubaini mahitaji ya fedha ambayo siyo ya lazima kwa wakati huu na hivyo hayawezi kuathiri utendaji wa taasisi husika. Miongoni mwa mahitaji yaliyopunguzwa ni: gharama za kumbi za mikutano, mafunzo na safari nje zisizo za lazima, maadhimisho na sherehe, posho na kudhibiti matumizi ya magari kwa mafungu yote. Aidha Serikali iliangalia miradi ambayo inaweza kutekelezwa kwa awamu;


·        Hata hivyo, Serikali inatambua umuhimu na majukumu ya msingi ya Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi, kama ilivyo kwa taasisi nyingine nyeti, ikiwemo vyombo vya ulinzi na usalama, mihimili mingine ya Dola na uwezo wa kukabiliana na dharura. Hivyo, endapo kutajitokeza mahitaji ya lazima ambayo yatakwama kutekelezwa na ofisi ya CAG kutokana na ufinyu wa bajeti, Serikali itahakikisha mahitaji hayo yanazingatiwa wakati wa mapitio ya utekelezaji wa bajeti kwa kipindi cha nusu mwaka.

Hoja Na.4: Ushuru wa bidhaa kutozwa kwenye ada ya miamala ya uhawilishaji wa fedha utaathiri mtumiaji wa mwisho na si makampuni ya simu

Ufafanuzi:
Mheshimiwa Spika,
·        Ushuru wa bidhaa unaopendekezwa katika miamala ya fedha (Excise Duty on Money Transfer) hautakatwa kwenye fedha zinazotumwa au kupokelewa, bali katika ada inayotozwa na benki au kampuni ya simu;

·        Kwa sasa Sheria inatamka kwamba ada hii itatozwa katika kutuma fedha tu.  Hata hivyo, baadhi ya kampuni za simu na benki zimekuwa zikitumia mwanya wa Sheria hiyo kupunguza wigo wa kodi kwa kutoza ada wakati wa kupokea tu;

·        Kwa mapendekezo haya, ushuru wa bidhaa utatozwa kwenye ada ya miamala ya uhawilishaji fedha ama wakati wa kutuma au kupokea fedha au vyote viwili kadri itakavyotozwa; na
·        Mantiki yake ni kuwa, ushuru huu utalipwa na benki au kampuni ya simu na siyo mtumaji au mpokeaji. Hata hivyo, Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), itawajibika kuhakikisha kwamba tozo hiyo inaendana na uhalisia wa huduma itolewayo na kufanya ukaguzi (cyber forensic audit) wa miamala ya makampuni ya simu kabla na baada ya tozo ili yasihamishie mzigo kwa mtumiaji wa mwisho.

Hoja Na. 5 Tathmini ya hali ya umasikini kimkoa
Ufafanuzi:
Mheshimiwa Spika,
·        Viashiria vya kupima hali ya umaskini nchini hupatikana kwa kutumia Utafiti wa Mapato na Matumizi katika kaya ambao hufanyika kila baada ya miaka mitano hapa Nchini. Utafiti wa mwisho ulifanyika mwaka 2011/12.

·        Mheshimiwa Spika,
                     i.        Hali ya umaskini katika kaya hupimwa kwa kuangalia mahitaji ya msingi (basic needs) kwa kila mwanakaya ukijumuisha mahitaji ya chakula yenye kiwango cha kilo kalori 2,200 kwa mlo kwa siku na hii ni kutokana na Kipimo cha Shirika la Afya Duniani - WHO. Mbinu hii inaonesha kiwango cha chini kabisa cha kipato anachohitaji mtu kwa ajili ya kukidhi mahitaji mbali mbali ya msingi.

                    ii.        Kiwango cha umaskini wa chakula hupimwa kwa gharama ya kiwango cha chini cha aina mbali mbali ya vyakula vyenye kufikia kiwango cha kilo kalori 2,200 kinachohitajika kwa mlo wa mtu maskini kwa siku katika mwezi. Kwa utafiti huu gharama ya kununulia chakula cha mtu mmoja kwa siku bila kujali eneo alilotoka ni Shillingi 858. Kiwango cha umaskini wa chakula ni gharama ya matumizi yote ya kaya ambayo yapo chini ya gharama wanayohitaji ili kukidhi mahitaji ya chakula yaani (Food Poverty Line). Na kwa umaskini wa mahitaji ya msingi ambao huhusisha chakula ni Tshs. 1,216 (Basis Needs poverty line) kwa siku kwa kila mtu mmoja tu.


·        Mheshimiwa Spika, utafiti wa kukusanya taarifa za kupima hali ya umasikini nchini hukusanya matumizi na mapato ya kaya.  Taarifa zinazokusanywa ni umri, hali ya ndoa, elimu na afya, manunuzi na matumizi ya kaya, umiliki wa bidhaa za matumizi na mali, makazi na vifaa vya ujenzi, upatikanaji wa huduma na vifaa, shughuli za ajira na kiuchumi, utalii na shughuli za kilimo. Uchambuzi wa kina wa hali ya umaskini katika ngazi ya mkoa na wilaya yaani (Poverty Mapping) uliongozwa na wataalam wa REPOA na ulibainisha kuwa:
Region
Watu Wanaoishi Chini Mstari wa Umaskin 2000/01 (%)
Watu Wanaoishi Chini Mstari wa Umaskini 2011/12 (%)
Mwanza
43
35
Kagera
29
39
Kigoma
38
49
Singida
49
38
Geita
Included in Mwanza
44
·        Mheshimiwa Spika, sababu zinazoeleza kwanini kiwango cha umasikini katika Mikoa kama Mwanza, Kigoma, Singida, Geita, na Kagera ni kikubwa zaidi ukilinganisha na mikoa ya Lindi na Mtwara ni nyingi.

·        Umasikini wa kipato ni mkubwa zaidi pale ambapo wananchi wengi zaidi wanaishi vijijini (33.3%) ikilinganishwa na mijini (21.7%). Mfano: Mwaka 2000/01 umaskini wa Kipato mkoa wa Mwanza ulikuwa 48%. Baada ya kugawanywa na kutolewa Wilaya ya Geita ambayo ilikuwa inaongoza kwa Umaskini wa Kipato 62.3% na kuwa Mkoa mpya wa Geita kiwango cha umasikini Mkoa wa Mwanza kinaonekana kupungua kutoka 43% (2000/01) hadi 35% (2011/12). Aidha, kwa mkoa wa Geita, sababu mojawapo ya umasikini wa kipato (44%) ni kiwango kikubwa cha uzazi (wastani wa watoto 7 kwa kila mwanamke mwenye umri wa kuzaa). Hivyo, shughuli za kiuchumi zinaelemewa na ongezeko kubwa la idadi ya watu (population explosion).

Aidha, wilaya za Kwimba na Sengerema umaskini wa kipato ni 39% na Misungwi 50% mwaka 2011/12. Wilaya za Mijini ambazo ni Nyamagana na Ilemela umaskini wa kipato ni 17% na 15%.  Hivyo wananchi wengi vijijini kutegemea kilimo, ufugaji na uvuvi usio na tija, havitoshi kupunguza umaskini wa kipato kwa kasi inayotakiwa. Hivyo, zitahitajika jitihada za makusudi kuongeza tija katika shughuli za msingi za kiuchumi vijijini.


·        Mheshimiwa Spika, umasikini katika mkoa wa Kigoma unachangiwa na miundombinu hafifu ya usafirishaji ambao unapunguza fursa za masoko. Pia Kigoma inabeba mzigo mkubwa wa wakimbizi na hivyo kusababisha ziada inayozalishwa kutumika zaidi kulisha wakimbizi na kupunguza ustawi wa Kaya katika mkoa husika.

·        Kwa mikoa ya Lindi na Mtwara umaskini huenda umepungua kutokana na kuongezeka kwa shughuli za biashara na uchumi kufuatia ugunduzi wa gesi asilia na ujenzi wa Kiwanda cha Saruji.  Aidha, ongezeko la idadi ya watu kwa mwaka kwa mikoa hii ni chini ya wastani wa Taifa wa 2.7%. maana yake ni kuwa kinachozalishwa kinatumika katika kustawisha uchumi katika kaya zao.

·        Mheshimiwa Spika, kwa mkoa wa Pwani, Wakazi wake wengi wanafanyia shughuli zao za kuongezea kipato katika Jiji la Dar es Salaam ambalo lina fursa nyingi Kiuchumi. Kadhalika, Pwani imepata fursa nyingi za Wakazi wake kujiongezea kipato chake kutokana na kuimarika kwa miundombinu ya barabara, maji na umeme ambazo ni vichecheo vya kuinua kipato cha Mwananchi mmoja mmoja.




Hoja Na. 6 Wizara ya Fedha na Mipango iangalie upya kuondoa misamaha ya kodi kwenye taasisi za dini kwa kuwa zinatoa huduma za kijamii kama shule, hospitali, n.k.

Ufafanuzi:
Mheshimiwa Spika,
·        Baada ya kupokea maoni kutoka kwa wadau mbalimbali pamoja na waheshimiwa wabunge, utaratibu niliopendekeza kwa taasisi za kidini kulazimika kulipa kodi kwanza kwa bidhaa watakazonunua au kuagiza nje na kodi hiyo kurejeshwa baada ya ukaguzi kufanyika na kujiridhisha kuwa bidhaa hizo zimetumika kwa malengo yaliyokusudiwa umeonekana unaweza kukwamisha au kuchelewesha utekelezaji wa miradi inayotekelezwa na taasisi za kidini na kusababisha athari katika upatikanaji wa huduma muhimu kwa jamii. Kwa kutambua mchango mkubwa wa taasisi mbalimbali za kidini katika utoaji wa huduma za elimu na afya, napendekeza kufuta utaratibu niliotangaza katika hotuba ya bajeti na badala yake Serikali itaimarisha zaidi hatua mbalimbali za udhibiti wa misamaha ya kodi kama ifuatavyo:

                       i.      Taasisi za kidini kuwasilisha vifaa vinavyotarajiwa kununuliwa kutoka nje ya nchi kila mwanzo wa mwaka wa kalenda, na kuthibitisha kama vifaa vilivyopewa msamaha mwaka uliopita vilitumika kama sheria inavyotaka;

                      ii.      Kuwasilisha majina ya watu walioidhinishwa na Shirika au Taasisi kuandika barua za kuomba msamaha wa kodi, wakiainisha cheo, saini, picha, anwani na namba zao za simu. Taarifa hizo ni muhimu katika kuiwezesha Mamlaka ya Mapato Tanzania kufuatilia bidhaa zilizoombewa na kupewa msamaha kama zimepata kibali cha taasisi hizo na zimetumika kutekeleza miradi iliyotarajiwa.  Pia wanapaswa kuandika barua ya kumuidhinisha wakala wa forodha waliomteua kutoa mizigo itakayokuwa ikiagizwa kutoka nje;

                    iii.      Kila wanapoomba msamaha wanapaswa kupata barua kutoka kwa Afisa Mtendaji wa Serikali ya Mtaa na Mkuu wa Wilaya mahali Taasisi au Mradi unaotekelezwa ulipo ili kuthibitisha kuwepo kwa Taasisi au mradi na mahitaji ya vifaa vinavyoombewa msamaha;

                    iv.      Magari yanayoagizwa kwa msamaha yawe na namba na rangi maalum za utambuzi mfano: TEV 222 AXZ kama njia ya kudhibiti matumizi yake; na

                     v.      Taasisi ya dini itakayothibitika kutumia vibaya msamaha wa kodi itafutiwa usajili na Serikali.

·        Mheshimiwa Spika, utaratibu na hatua mbalimbali za udhibiti wa misamaha ya kodi kwa wafanyabiashara, watumishi wa umma na taasisi zisizo za kiserikali utatangazwa katika gazeti la Serikali na kupitia vyombo vya habari.





Hoja Na.7: Uwezo wa TRA kukusanya Kodi ya Majengo
           
Ufafanuzi
Mheshimiwa Spika,
·        TRA ni mamlaka ambayo ina uzoefu wa kutosha katika ukusanyaji kodi za Serikali na ina vituo vya ukusanyaji kodi katika Wilaya na Mikoa yote Tanzania;

·        TRA inatekeleza majukumu yake kupitia sheria mbalimbali ambazo zinarahisisha ukusanyaji wa kodi kwa kupitia utaratibu wa kisasa wa Benki pamoja na njia za kielektroniki. Aidha, Kamishna Mkuu anaruhusiwa kama ataona inafaa, kuazima baadhi ya watumishi wenye uzoefu wa utozaji kodi ya majengo toka maeneo mengine ya serikali ikiwemo serikali za mitaa kwa lengo la kujenga ushirikiano na kuongeza ufanisi; na

·        Kwa kutumia uzoefu na mifumo iliyopo ya TRA, ni wazi kuwa kodi ya majengo itakusanywa kwa ufanisi mkubwa na kwa uwazi zaidi, tofauti na sasa ambapo wananchi wengi hawalipi kodi hiyo.

Kuhusu Viwango vya Kodi ya Majengo
·        Waziri wa Fedha na Mipango ataweka viwango vya kodi ya majengo baada ya kushauriana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI ili kuweka uwazi na kujumuisha maoni ya wadau wote muhimu zikiwemo Halmashauri husika; na

·        Kodi ya majengo itatozwa kwa kuzingatia mazingira ya maeneo husika ambapo TRA itakuwa na jukumu la kutoza, kukusanya na kuwasilisha makusanyo hayo kwenye akaunti maalumu kwa manufaa ya serikali za mitaa.

·        Mapato kutokana na kodi ya majengo yataingizwa katika mfuko mkuu. Mawaziri wenye dhamana ya Fedha na TAMISEMI watashauriana kuhusu mgawanyo wa fedha hizo kwa kuzingatia bajeti za Halmashauri husika.

Hoja Na.8: Kutoza Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) katika Huduma za Utalii

Ufafanuzi:
Mheshimiwa Spika,
·        Kabla ya hotuba ya bajeti ya  2016/17 nchi zote wanachama wa Jumuiya Afrika Mashariki  zilikuwa zinatoza  VAT kwenye huduma ya utalii isipokuwa Tanzania ambayo imependekeza kutoza katika bajeti yake ya mwaka 2016/17;

·        Mwaka 2014 Serikali kupitia Bunge ilitunga sheria ya  VAT.  Sheria hii ilitungwa ili kutatua upungufu uliokuwepo katika sheria ya VAT ya mwaka 1997;

·        Msamaha wa VAT kwenye huduma za utalii ulifutwa mwaka 2014 baada ya kukubaliana na wadau ambao waliiomba Serikali mwaka moja toka Novemba 2014   ili kulinda mikataba iliyoingiwa kabla ya kutunga sheria ya VAT ya mwaka 2014;


·        Idadi ya watalii waliotembelea mbuga za wanyama kwa kipindi 2011 hadi 2014 katika nchi za Tanzania, Kenya na Afrika Kusini zinaonyesha kwamba Tanzania licha ya kutotoza VAT kwenye huduma hii bado imetembelewa na watalii wachache kuliko nchi hizo kama ifuatavyo:

Mwaka
Idadi ya Watalii
Tanzania
Hakuna VAT
Kenya
Kuna VAT
Afrika Kusini
Kuna VAT
2011
867,994
1,750,000
8,339,000
2012
1,077,058
1,619,000
9,188,000
2013
1,095,884
1,434,000
9,537,000
2014
1,140,156
1,261,000
9,549,000








·        Serikali inapendekeza kutoza VAT kwenye huduma za utalii kwa sababu VAT sio kigezo kikubwa kinachoangaliwa na Mtalii wakati anafanya maamuzi kufanya utalii. Baadhi ya vigezo muhimu vinavyoangaliwa ni vivutio, usalama, huduma kwa watalii na hali ya usafiri.

Hoja Na.9: Serikali ina mkakati gani wa kukabiliana na tatizo la watoa huduma kutoza bei kwa kutumia fedha za kigeni kama Dola ambalo linapelekea kushuka kwa thamani ya shilingi?

Ufafanuzi:
Mheshimiwa Spika,
·        Dollarization ni matumizi ya sarafu ya kigeni katika nchi moja sambamba na sarafu ya nchi hiyo;
·        Matumizi makubwa ya fedha za kigeni katika uchumi husababishwa na mambo kadhaa yakiwemo vita vya muda mrefu katika nchi, kuongezeka kwa mfumuko wa bei na kuporomoka kwa thamani ya sarafu ya nchi husika ikilinganishwa na sarafu ya kigeni. Kama nilivyoeleza katika hotuba yangu, kushuka kwa thamani ya shilingi yetu kulitokana na kuimarika kwa Dola ya Kimarekani, kuchelewa kwa upatikanaji wa fedha za kigeni kwa ajili ya bajeti ya serikali pamoja na mapato madogo ya fedha za kigeni yasiyokidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma nje;

·        Kwa ujumla, mahitaji ya fedha za kigeni kwa ajili ya uagizaji wa bidhaa na huduma nje ya nchi hayawiani na uuzaji wa bidhaa na huduma nje. Kwa mfano katika mwaka 2015, thamani ya mauzo ya bidhaa na huduma nje ilikuwa Dola za Kimarekani milioni 9,450.0 ikilinganishwa na Dola milioni 12,528.2 zilizotumika kuagiza bidhaa na huduma kutoka nje. Hali hii inasababisha kuongezeka kwa nakisi ya urari wa biashara ya bidhaa na huduma;

·        Mwenendo wa thamani ya Shilingi umekuwa ni chanzo kikuu kwa wafanya biashara nchini kupanga bei za bidhaa na huduma zao kwa fedha za kigeni. Hivyo basi, namna nzuri na endelevu ya kupunguza au kuondoa matumizi ya fedha za kigeni katika matangazo ya bei au malipo ya bidhaa na huduma mbalimbali kwenye soko la ndani ni kuimarisha thamani ya Shilingi yetu na kuendelea kudhibiti mfumuko wa bei. Hali hii itawezekana kwa kuendelea kutekeleza sera madhubuti ya fedha na kuhakikisha kunakuwa na ongezeko la uzalishaji wa chakula pamoja na kuboresha usambazaji wa chakula nchini. Hii inajumuisha pia kuboresha miundombinu itakayowezesha kilimo cha umwagiliaji na kusafirisha chakula kirahisi kutoka sehemu zenye ziada kwenda sehemu zenye upungufu;

·        Aidha, kuongeza uzalishaji wa bidhaa za mauzo nchi za nje kutapunguza nakisi katika urari wa biashara ya bidhaa na huduma nchi za nje na hivyo kusaidia kudhibiti kuporomoka kwa thamani ya Shilingi. Hivyo basi, kupunguza matumizi ya fedha za kigeni (dollarization) ni suala la muda wa kati linalohitaji kuimarisha sera madhubuti za uchumi jumla ikiwa ni pamoja na kuendelea kuweka mifumo thabiti itakayoleta ongezeko la haraka la uzalishaji wenye tija na hivyo kuongeza mauzo ya bidhaa na huduma nje;  

·        Si nia ya Serikali kurejesha sera ya udhibiti wa umiliki wa fedha za kigeni (administrative de-dollarisation) kwani madhara yake ni makubwa na baadhi ya nchi zilishajaribu zikashindwa na hivyo kurudisha sera ya soko huria. Udhibiti wa umiliki wa fedha za kigeni utaleta ushawishi kwa watanzania kutunza fedha za kigeni katika mabenki ya nje kinyume na sheria (capital flight). Hii itasababisha upungufu mkubwa wa fedha za kigeni na hivyo kufanya nchi kushindwa kulipia mahitaji yake kutoka nje. Pia, hali hii itasababisha kushamiri kwa soko lisilo rasmi (parallel market) la fedha za kigeni cf. IMF (2015) Dollarization in SSA: Experience and Lessons;

·        Serikali itaendelea kusimamia kwa karibu kuhakikisha kwamba matumizi ya fedha za kigeni katika uchumi wetu yanafanyika kwa kufuata utaratibu uliowekwa kisheria. Sheria ya Benki Kuu ya mwaka 2006, sehemu ya tatu, kipengele cha 26, inatamka wazi kuwa shilingi ya Tanzania itakubalika na kutumika kama fedha halali kwa malipo (legal tender) ndani ya nchi yetu. Hii inamaanisha kuwa shilingi ya Tanzania ndiyo fedha pekee ambayo haiwezi kukataliwa na mtu yeyote kwa malipo halali ndani ya nchi yetu.  Hivyo, ni kosa kukataa kupokea shilingi ya Tanzania kwa malipo halali nchini; na

·        Vile vile, Sheria ya Usimamizi wa Fedha za Kigeni ya mwaka 1992 (The Foreign Exchange Act, 1992) inaruhusu mtu yeyote kupokea, kumiliki na kutumia fedha za kigeni kwa shughuli zake za kiuchumi. Vile vile, Sheria hiyo inatamka kwamba mtu yeyote anaruhusiwa kuwa na akaunti ya fedha za kigeni katika benki iliyoruhusiwa na Benki Kuu kwa ajili hiyo.

Hoja Na.10: Serikali ipunguze kukopa katika mabenki ya ndani ili kutoa fursa kwa sekta binafsi kupata mikopo.

Ufafanuzi:
Mheshimiwa Spika,
·        Nakisi ya bajeti kwa mwaka 2016/17 ni asilimia 4.5 ya Pato la Taifa ikilinganishwa na asimilia 3.7 mwaka 2013/14, asilimia 3.6 mwaka 2014/15 na asilimia 4.2 mwaka 2015/16. Kiwango cha nakisi ya bajeti kimeongezeka kwa asilimia 0.3 ya Pato la Taifa ikilinganishwa na mwaka 2015/16. Ongezeko hilo limetokana na nia nzuri ya Serikali ya kutekeleza kwa dhati Mpango wa pili wa maendeleo wa miaka mitano;

·        Kigezo kimojawapo cha uchumi mpana katika kuanzishwa kwa Umoja wa Fedha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ni kuwa na kiwango cha nakisi ya bajeti kwa Pato la Taifa cha asilimia 3 pindi ifikapo 2021/22. Katika kutekeleza hili, Serikali imepanga kupunguza kiwango cha nakisi hatua kwa hatua bila kuathiri utekelezaji wa bajeti;

·        Katika mwaka 2016/17, Serikali imepanga kuziba nakisi ya bajeti ya asilimia 4.5 ya Pato la Taifa kwa kukopa kutoka katika vyanzo vya ndani na nje. Kati ya kiasi hicho, asilimia 3.0 ya Pato la Taifa itakopwa kutoka vyanzo vya nje na asilimia 1.5 ya Pato la Taifa itakopwa kutoka katika vyanzo vya ndani. Ukopaji huo hufanyika kwa kuuza hatifungani kwenye soko la ndani la fedha badala ya kukopa moja kwa moja kwenye benki za biashara; na

·        Kwa maana hiyo, kiasi kitakachokopwa kutoka soko la ndani kinazingatia ukomo wa ukopaji ambao hauathiri utoaji wa mikopo kwa sekta binafsi ambapo mikopo kwa sekta binafsi imekuwa ikiongezeka kwa zaidi ya asilimia 20 kwa mwaka. Ongezeko hili linawiana na lengo la ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi kama ilivyoainishwa katika Tamko la Sera ya Fedha. Aidha, kiwango cha mikopo ambayo imekuwa inayotolewa na benki za biashara kwa sekta binafsi ni zaidi ya asilimia 80 ya mikopo yote, wakati mikopo inayotolewa na benki za biashara kwa Serikali ni chini ya 2%

Hoja Na. 11: Kuondolewa kwa misamaha ya kodi katika maduka na migahawa ya vyombo vya ulinzi na usalama kunaondoa motisha katika taasisi hizo. Ikiwa msamaha wa kodi utafutwa, bidhaa na vifaa vilivyopo katika bohari za majeshi yetu zitapelekwa wapi? Na zipo kiasi gani?

Ufafanuzi:
Mheshimiwa Spika,
·        Uamuzi wa Serikali wa kuwapa motisha watumishi wa vyombo vya ulinzi na usalama bado upo palepale. Mapendekezo ya kuondoa msamaha wa kodi katika maduka na migahawa ya vyombo vya ulinzi na usalama ni kutokana na misamaha hiyo kutumika vibaya. Ili kuondoa kasoro hiyo, Serikali imeamua kuweka utaratibu wa kuwalipa posho watumishi wa vyombo vya ulinzi na usalama ili wanufaike moja kwa moja kama walengwa. Kiasi cha posho atakayolipwa askari kitakokotolewa baada ya mashauriano na vyombo husika.

·        Serikali inakamilisha utaratibu wa bidhaa ambazo zimesamehewa kodi katika maduka yote ya vyombo vya ulinzi na usalama. Utaratibu huo utakapokamilika wahusika watajulishwa.


Hoja Na.12: Kodi kwenye “transit goods” ni kinyume na taratibu kwa kuwa kodi hiyo hulipwa na mlaji. Hii itasababisha waagizaji wa mizigo kuhamia bandari nyingine za Beira na Mombasa.

Ufafanuzi:
Mheshimiwa Spika,
·        Sheria ya VAT ya Mwaka 2014 imeweka viwango viwili vya kutoza kodi ambavyo ni asilimia 18 kwa bidhaa na huduma zinazotumika hapa nchini na asilimia 0 pale bidhaa na huduma inaposafirishwa nje ya nchi (Exported);

·        Huduma zinazotolewa kwenye mizigo inayosafirishwa kwenda nchi za jirani kupitia Tanzania siyo “exports” bali zinatolewa na kutumiwa ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa maana kodi ya ongezeko la thamani (VAT) haitozwi kwenye transit goods bali hutozwa kwenye huduma ambapo mtumiaji na mtoaji wako Tanzania.  Huduma hizi zinaweza kutolewa mahali popote ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na siyo bandarini tu, na hivyo ni sahihi kabisa huduma hizi kutozwa asilimia 18;

·        Utafiti uliofanywa kubaini kama kutoza kodi ya VAT huduma hizi kunaathiri biashara kwenye bandari umeonesha kwamba katika kipindi cha Julai, 2015 hadi April, 2016 mizigo iliyopita kwenye bandari ya Dar es Salaam imepungua kwa asilimia 15 ukilinganisha na mizigo iliyopita katika Mwaka wa Fedha 2014/15 katika kipindi kama hicho.  Katika Bandari ya Mombasa ambapo huduma hizi zimesamehewa kodi ya VAT mizigo imepungua kwa asilimia 25 katika kipindi hicho.  Kwa ujumla biashara ulimwenguni kote imeshuka katika kipindi hiki, na hivyo kuathiri ukuaji wa uchumi jumla; na

·        Kwa misingi hiyo si sahihi kusema kwamba kutoza kodi ya VAT kwenye huduma zinazotolewa kwenye mizigo inayosafirishwa kwenda nchi jirani ndicho chanzo cha kushuka kwa biashara katika bandari zetu.

Hoja Na.13: Serikali iangalie upya mfumo wa “Single Customs Territory” unaodaiwa kusababisha kupungua kwa mapato ya bandari kutokana na baadhi ya nchi jirani kuepuka kutumia bandari ya Dar es Salaam.

Ufafanuzi:
Mheshimiwa Spika,
·        Mfumo wa “Single Customs Territory (SCT)” ulianza kutumiwa na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Mfumo huu ulionesha manufaa makubwa katika kuwezesha biashara na kudhibiti uvujaji wa mapato baina ya nchi husika. Mfumo huu huruhusu wafanyabiashara wanaotumia bandari zetu kupitisha mizigo kwenda nchi jirani kulipa kodi kwenye nchi zao kwanza na pindi mzigo huo unapowasili bandarini na kujiridhisha kuwa kodi husika zimelipwa, mzigo huo huruhusiwa na hivyo kuepusha uwezekano wa kuingizwa nchini bila kulipiwa kodi. Utaratibu huu pia hurahisisha uondoshaji wa kadhia forodhani. Mfano mzuri wa mafanikio ya mfumo huu ni mizigo inayokwenda Rwanda kwani imeongezeka kwa asilimia 16 kwa kipindi cha kuanzia Julai 2015 hadi Aprili 2016 ukilinganisha na kipindi kama hicho katika mwaka wa fedha 2014/15. Pia muda wakusafirisha mzigo kutoka muda wa kuingia na kutoka (from entry to exit) umepungua;
·        Mfumo huu wa SCT kwa mizigo inayokwenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) umeanza kutumika kufuatia makubaliano kati ya serikali za nchi hizi mbili.  Lengo lake ni kuharakisha biashara kwa kupunguza muda wa kutoa na kusafirisha mizigo kwenda DRC na kudhibiti mapato kwa nchi zote mbili. Hivyo kushuka kwa biashara kati ya Tanzania na nchi jirani hakujasababishwa na SCT;

·        Kwa upande mwingine, dunia imeshuhudia kupungua kwa biashara ya kimataifa katika kipindi hiki ambako kumesababishwa na kudorora kwa uchumi wa China, kushuka kwa bei ya bidhaa (commodities) na mafuta ikiwa pamoja na madini mbalimbali. Hivyo, kupungua kwa mizigo inayokwenda nchi jirani na ile inayotumika hapa nchini, hakujaiathiri Tanzania peke yake bali hata bandari ya Mombasa mizigo ya nchi jirani yaani transit ilipungua kwa asilimia 25 kwa kipindi cha kati ya Julai 2015 hadi Machi 2016 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2014/15. Utafiti uliofanywa hivi karibuni na TRA/Serikali umebainisha sababu za muda mfupi na muda mrefu zilizosababisha kupungua kwa mizigo kwenye bandari ya Dar es Salaam ikiwa ni pamoja na mizigo inayokwenda nchi jirani na ile kwa ajili ya matumizi ya ndani ya nchi (imports);

·        Sababu za muda mfupi ni pamoja na:- Maandalizi ya Uchaguzi Mkuu kwenye Nchi za kanda yetu kama vile Tanzania, Uganda, Burundi, machafuko nchini Burundi na Sudan Kusini,  kushuka kwa bei ya shaba katika soko la dunia kuliathiri uchumi wa Zambia na hivyo kushuhudia kupungua kwa mizigo ya kwenda na kutoka Zambia, na maboresho ya miundombinu yaliyofanywa na nchi ya Msumbiji na Afrika kusini kwa mfano Msumbiji imejenga reli ya standard gauge na kuboresha bandari na hivyo kuifanya bandari kuwa na miundombinu bora ukilinganisha na bandari yetu. Hali hii   imeifanya bandari ya Beira kupendelewa zaidi na nchi jirani;

·        Sababu za muda mrefu ni pamoja na:- Ufanisi mdogo wa bandari ya Dar es Salaam ukilinganisha na bandari zingine, miundombinu hafifu ya kusafirisha mizigo hususan kwa njia ya reli na hivyo kufanya njia pekee ya uhakika kusafirisha mizigo kuwa ni barabara ambayo ni ghali zaidi ukilinganisha na reli; na

·        Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kikamilifu kuondokana na changamoto hizo ikiwa ni pamoja na kuboresha huduma za bandari na kuimarisha miundombinu ya usafirishaji ikiwa ni pamoja na kujenga reli ya kati kwa kiwango cha standard gauge.





Hoja Na.14: Tamko la kufuta retention kwenye Taasisi za kimkakati kama TPDC, Serikali ikishindwa kupeleka fedha kwa wakati, itapoteza mapato mengi kwa sababu watashindwa kusimamia kwa ufanisi mapato kutoka kwa wawekezaji.

Ufafanuzi:
Mheshimiwa Spika,

·        Utaratibu wa kubakiza sehemu ya mapato (Retention) ulikuwa na lengo la kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa shughuli kwa baadhi ya Wizara na Taasisi.  Katika baadhi ya Wizara na Taasisi hizo ufanisi wa ukusanyaji maduhuli umeongezeka;
 
·        Hata hivyo, kumejitokeza dosari katika utekelezaji wa utaratibu huo, ikiwa ni pamoja na matumizi makubwa yasiyowiana na majukumu ya msingi na kutochangia inavyostahili katika mfuko mkuu wa Serikali; na 

·        Ili kurekebisha dosari na kuhakikisha kuwa Taasisi husika zinapata fedha kwa wakati, Serikali imeelekeza Taasisi hizo kuwasilisha mpango kazi na mtiririko wa mahitaji ya fedha (action plan and cash flow), vigezo ambavyo vitazingatiwa katika utoaji wa fedha





Hoja Na. 15 Ushuru wa Forodha kwenye Sukari ya Viwandani

Ufafanuzi:
Mheshimiwa Spika,
·        Katika ukurasa wa 71 kwenye kitabu cha Hotuba ya Bajeti 2016/17 niliyoisoma hapa Bungeni nilieleza kuwa, waagizaji wa sukari ya viwandani watatakiwa kulipa ushuru wa asilimia 15 kwenye sukari wanayoagiza badala ya asilimia 10 wanayolipa sasa katika mwaka wa fedha 2015/16.  Hilo lililenga kutekeleza maamuzi ya Baraza la Mawaziri wenye dhamana ya masuala ya fedha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ya kupunguza msamaha kwenye sukari ya viwanda hatua kwa hatua hadi kufikia asilimia 25 kama ifuatavyo: mwaka 2016/17 kiwango kitakuwa asilimia 15, 2017/18 kiwango kitakuwa cha asilimia 20 na 2018/19 kiwango kitakuwa asilimia 25.

·        Mheshimiwa Spika, pamoja na kuwa maamuzi ya kuanza kutoza ushuru wa forodha wa asilimia 15 kwenye sukari inayoingizwa nchini kwa matumizi ya viwanda ulikuwa ni uamuzi wa pamoja wa mawaziri wenye dhamana ya masuala ya  fedha  wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ni Tanzania pekee ndiyo ingetekeleza maamuzi haya katika mwaka wa fedha 2016/17.  Nchi za Burundi, Kenya na Uganda zimeomba muda wa kujiandaa ili waweze kuanza kutekeleza hatua hii katika mwaka wa fedha 2017/18. Rwanda wanatumia mfumo tofauti ambapo sukari yote hutozwa asilimia 25 badala ya kutumia ushuru wa forodha wa asilimia 100 au Dola za Marekeni 460 kwa tani moja kwa kutegemea kiwango kipi ni kikubwa zaidi. Sababu ya nchi hizi kutotumia kiwango hicho cha ushuru wa forodha ni ukweli kuwa bidhaa hizi hazizalishwi ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.  Aidha,  ili kujiandaa kwa utekelezaji wa hatua hii, Kenya imepewa unafuu wa ushuru wa forodha kwa kuruhusiwa kuingiza sukari ghafi kwa kutumia kiwango cha  asilimia 0 badala ya asilimia 100 au Dola za Marekani 460 kwa tani kwa kipindi cha mwaka mmoja.  Baada ya kupokea maoni ya watengenezaji wa vinywaji pamoja na kutafakari juu ya umuhimu wa bidhaa hiyo ambayo hutumika kama malighafi ya viwanda vyetu, Serikali imeamua kusitisha utekelezaji wa hatua hii hadi mwaka wa fedha 2017/18 kama ilivyo kwa nchi nyingine za Jumuiya ya Afrika Mashariki.  Hata hivyo, Serikali itaendelea kuwataka watumiaji wa sukari hii kuendelea kulipia kodi ya asilimia 25 kwanza na kurejeshewa asilimia 15 baada ya kuthibitisha uhalali wa matumizi. 

Hoja Na.16: Wizara ya Fedha na Mipango ijihadhari na madalali wa mikopo (transaction agents) maana wataongeza gharama za mikopo.

Ufafanuzi:
Mheshimiwa Spika,
·        Ukopaji wa fedha unafanywa kwa mujibu wa Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada Sura 134. Sheria hiyo imetoa Mamlaka kwa Waziri wa Fedha na Mipango kukopa mikopo ya ndani na nje kwa niaba ya Serikali. Kwa mujibu wa taratibu zilizoainishwa katika sheria hiyo, Waziri wa Fedha na Mipango hujadiliana moja kwa moja na wakopeshaji ambao wanaweza kuwa ni Nchi (Bilateral Creditor), Benki moja moja au kundi la mabenki;

·        Hata hivyo, kutokana na muundo (structure) wa soko la fedha la ndani au la kimataifa, wakati mwingine Waziri wa Fedha anaweza akateua taasisi nyingine kumsaidia ili kurahisisha upatikanaji wa fedha kutoka soko la fedha husika. Mathalan, kwa sasa Benki Kuu ya Tanzania inatumika kama wakala (Agent) wa Serikali katika kuuza Hati Fungani na Dhamana za Serikali na kuiwezesha Serikali kupata Fedha kutoka Soko la Ndani;

·        Kwa upande wa soko la fedha la kimataifa, mikopo mikubwa huchangiwa na taasisi nyingi za fedha yakiwemo mabenki na wakopeshaji wengine. Taasisi hizo huteua benki au taasisi moja miongoni mwao kuwa Wakala yaani Agent/lead arranger au lead manager kuwasikilisha mabenki hayo katika majadiliano na mkopaji. Huu ni utaratibu wa kawaida kwenye masoko ya fedha ya kimataifa na hufanya hivyo ili kurahisisha majadiliano na upatikanaji wa fedha kwa wakati;

·        Sifa za Wakala huyo anayechaguliwa na mabenki au wawekezaji kwenye soko la fedha la kimataifa lazima ni pamoja na kuwa uwezo wa kuitangaza nchi kikamilifu katika soko la fedha la kimataifa hivyo kuifanya nchiyo kupata fedha na kwa gharama nafuu ya soko, kwa upande mwingine, Wakala huyo anatakiwa awe na taarifa za kutosha za mkopaji ikiwemo hali ya uchumi, siasa na masuala ya kijamii ya nchi husika na uwezo wa nchi hiyo kurejesha mikopo. Aidha, mkopaji lazima ajiridhishe na kukubali kutumia Wakala huyo; na

·        Utaratibu huu hutoa uhakika kwa Serikali kupata mikopo kwa masharti yanayokubalika baina ya pande mbili zinazo husika. Kwa mujibu wa Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada SURA 134. Sheria hii imeweka utaratibu maalum wa kuufuata wakati wa kukopa. Kwa mujibu wa Sheria hii kuna Kamati Maalum ambazo huchambua masharti ya kila mkopo na kujadiliana na wakopeshaji na baada ya majadiliano kukamilika, Kamati hizi ndizo zinamshauri Waziri wa Fedha na Mipango kukopa mkopo husika.

Hoja Na.17: Serikali ishirikishe Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti katika maandalizi ya bajeti.

Ufafanuzi:
Mheshimiwa Spika,
·        Serikali imekuwa ikiishirikisha Kamati ya Bunge ya Bajeti na Waheshimiwa Wabunge katika hatua mbalimbali za maandalizi ya bajeti. Ushirikishwaji huo hufanyika katika hatua zifuatazo:

·        Maandalizi ya Mwongozo wa Mpango na Bajeti Kamati za Kudumu za Bunge za Kisekta; na

·        Kamati ya Bunge ya Bajeti, ambayo hushirikishwa kikamilifu katika kuchambua makadirio ya bajeti ya Serikali; kupitia rasimu ya mfumo wa bajeti; kupitia hoja za kibajeti zinazoibuka kwenye sekta mbalimbali; kushauriana na Serikali kuhusu vyanzo vipya vya mapato.

·        Hata hivyo, ili kulinda kazi ya Bunge ya kuishauri na kuisimamia Serikali ni muhimu kwamba Bunge lisijiingize katika kazi za kiutendaji katika maandalizi ya bajeti na badala yake Bunge lichambue na kushauri kuhusu mapendekezo ambayo tayari yanakuwa yameridhiwa na Serikali.

F:     HITIMISHO

8.          Mheshimiwa Spika, tuna dhamana ya kuleta mabadiliko makubwa katika uendeshaji wa shughuli zote za umma na matumizi ya rasilimali za Taifa ili kuwezesha kupiga hatua kubwa ya kuiondoa nchi yetu katika umaskini. Katika hili, kila mwananchi atambue  wajibu wake wa kufanya kazi kwa bidii, kuwa na nidhamu ya hali ya juu katika nyanja zote na uzalendo kwa Taifa letu.

9.           Mheshimiwa Spika, nirudie tena kuzielekeza Wizara, Idara zinazojitegemea, Taasisi na Wakala za Serikali, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuzingatia hatua za kuimarisha ukusanyaji wa mapato; usimamizi wa matumizi ya Serikali na hatua za kupunguza gharama; na kulipa na kuzuia ongezeko la madeni ya Serikali. Serikali ina dhamira ya dhati kabisa  ya kuchukua hatua hizo na ninaomba Watanzania wote watambue kwamba ni lazima kujinyima, kujituma na kuvuja jasho ili kupata maendeleo na kupunguza utegemezi. Wajibu wa kwanza wa kuiendeleza Tanzania ni wa Watanzania wenyewe. Tuna akili za kutosha, rasilimali nyingi na fursa tele kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda na Uchumi wa Kipato cha Kati ifikapo 2025.

10.     Mheshimiwa Spika, ninawaomba tena Waheshimiwa Wabunge kuunga mkono hatua zinazoongozwa na Serikali ya Awamu ya Tano kuhakikisha kuwa tunaimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani ya kodi na yasiyo ya kodi na kuelekeza matumizi kwenye maeneo yenye tija kwa manufaa ya watanzania wote.

11.     Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa