Christina
Njovu-NEC, Dodoma
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imekabidhi Taarifa ya Tathmini baada ya
Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani wa mwaka 2015 kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya
Waziri Mkuu , Sera, Bunge, Kazi , Ajira, Vijana na Walemavu Mh. Jenista Mhagama mjini Dodoma leo.
Akikabidhi taarifa hiyo
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Mstaafu Damin Lubuva alisema kuwa
Tathmini hiyo imeonesha kuwa Tume hiyo imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuendesha
na kusimamia uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani uliofanyika Oktoba 25
mwaka 2015.
Alisema kwa mujibu wa
tathmni hiyo Tume imebaini kuwa sheria, kanuni na zilizotumika wakati wa
Uchaguzi mkuu zilikuwa chachu ya kufanikisha Uchaguzi Mkuu, Watendaji wa
Uchaguzi walionesha kuwa na uelewa wa kutosha wa Shriea na Kanuni za Uchaguzi.
Jaji Mst. Lubvuva
alisema kuwa lengo la tathmini hiyo ni kupata taswira halisi ya Tume kutoka kwa
Wadau kwa lengo la kujenga msingi bora wa utekelezaji wa chaguzi zijazo na
kujua kwa nini baadhi ya maeneo yalikuwa na mwitikio mdogo katika kupiga kura
wakati yalikuwa na mwitikio mkubwa kwenye
kuandikisha wapiga kura kwenye Daftari la kudumu la Wapiga Kura.
Alisema kuwa Tathmini
hiyo ni ya kwanza kufanyika tangu kuanzishwa kwa Tume hiyo mwaka 1993 ambayo imeweza kuwapatia mrejesho juu ya utekelezaji
wa Uchaguzi Mkuu kutoka kwa wadau wa Uchaguzi .
Alibainisha kuwa wakati
wa tathmini hiyo wadau wengi walionesha kuridhishwa na utendaji wa Tume katika
kusimamia Uchaguzi Mkuu na kutangaza matokeo kwa kufuata sheria na kanuni zilizopo.
Akipokea Taarifa hiyo
, Waziri wa Nchi Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Ajira,
Vijana na Walemavu Mhe. Jenista Mhagama
ameipongeza Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kuweza kufanikisha Uchaguzi
Mkuu ulikuwa na changamoto nyingi na ushindani
mkubwa wa kisiasa na kufanikiwa kufanya tathmini ya Uchaguzi Mkuu ambayo imekabidhia kwake kwa niaba ya
Serikali.
“Ni kweli kwamba
wananchi wengi wamekuwa na mwamko wa kisiasa katika jamii yetu, hasa vijana ,
hivyo taarifa hii itasaidia sana wananchi kuifahamu vyema zaidi namna Tume
inavyosimamia , kuendesha na kuratibu mchakato mzima wa Uchaguzi kuanzia
uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, hadi kutangaza matokeo.”
Alisema Waziri Mhagama.
Alisema Tathmini hii
itawawezesha wadau mbalimbali kuitumia kama nyenzo muhimu katika kushiriki na
kufanya maandalizi ya chaguzi zijazo.
Naye Mkurugenzi wa
Uchaguzi wa NEC, Bw. Ramadhan Kailima katika maelezo ya utangulizi alieleza
kuwa tathimini hiyo ilitumia njia ya mahojiano ya ana kwa ana na majadiliano na
ilijumuisha makundi 192 ya wazee wenye umri wa zaidi ya miaka 60 na makundi 192
ya vijana wenye umri kati ya miaka 18 na 35.
Alisema matokeo ya
tathmini hiyo yanaonesha kuwa kati ya watendaji 1,029 walihojiwa na watendaji wengi
kati wao walisema taratibu mbalimbali za uchaguzi hadi kutangaza matokeo
zilizingatiwa.
Bw. Kailima aliongeza
kuwa kuhusu Elimu ya Mpiga Kura wadau wa Uchaguzi 1,915 waliohojiwa kuhusu
uelewa wao juu ya Elimu ya Mpiga Kura kati yao Wadau 1,463 sawa na asilimia
76.4 walisema kuwa walikuwa na uelewa wa Elimu ya Mpiga Kura na Watu 452 sawa
na asilimia 23.6 hawakuwa na uelewa.
Kutokana na tathmini
hiyo Bw. Kailima alisema kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi imejipanga kutoa Elimu
ya MpigaKura kwa lengo la kuwafikia wananchi na wadau moja kwa moja na imeweza
kushiriki katika maonyesho mbalimbali yakiwemo ya Sabasaba, Nanenane , Mkutano
wa Tawala za Mitaa Tanzania na Wiki ya Vijana iliyofanyika Mkoani Simiyu.
Sambamba na hilo,
aliongeza kuwa Tume imepanga kuhudhuria na kutoa Elimu katika mikutano ya
viongozi mbalimbali ikwemo viongozi wa Dini, Mabaraza ya Madiwani na mikutano
mikuu ya vijiji na mitaa.
Kutoa elimu ya Mpiga
Kura kwa njia ya luninga, redio, mabango na mitandao ya kijamii, Kutoa vibali vya kutoa elimu ya Mpiga kura
kwa Taasisi na Asasi.
Kufanyika kwa
tathmini Baada ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani wa mwaka 2015 ni
mojawapo ya ukamilishaji wa mzunguko wa Uchaguzi huo ambao ulitanguliwa na
zoezi kukabidhi ripoti ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani kwa Mh.
Rais Wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ikulu jiji Dar es Salaam na ni mwanzo
wa kuanza kwa mchakato wa Uchaguzi mwingine.
0 comments:
Post a Comment