Home » » Walioua watafiti wakimbia kijiji

Walioua watafiti wakimbia kijiji

HOFU na wasiwasi vimetawala katika kijiji cha Iringa Mvumi wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma huku baadhi ya watu wakiwa wamekimbilia porini na kuishi huko. Wamefanya hivyo kutokana na tukio la kuuawa kwa watafiti wawili na dereva mmoja wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Selian Arusha (SARI) katika mauaji yaliyofanywa mwishoni mwa wiki.
Waliouawa katika tukio hilo wametajwa kuwa ni Nicas Magazine, aliyekuwa dereva pamoja na watafiti wawili Teddy Lumanga na Jaffari Mafuru, ambao waliuawa na kisha miili yao kuchomwa moto baada ya kuhisiwa kuwa ni wanyonya damu.
Aidha, mume wa Teddy ameeleza jinsi ilivyomchukua saa moja, kuamini kuwa mkewe amefikwa na mauti na huku ikibainika kuwa Jaffari ni mtoto wa Mkurugenzi Mkuu wa SARI, Dk Januari Mafuru ambaye alikwenda kufanya utafiti huo kwa kuwa anapenda eneo hilo baada ya kumaliza masomo Chuo cha Mipango Dodoma.
Gazeti hili jana lilifika katika kijiji hicho kilichoko umbali wa takribani kilometa 60 kutoka Dodoma Mjini, ambako lilikuta hali ikiwa ya ukimya huku nyumba nyingi zikiwa zimefungwa na chache zimebaki na wazee na watoto.
Maduka, magenge yamefungwa na kusababisha shughuli za kiuchumi kusimama. Mmoja wa wanakijiji, Stanley Joseph alisema hali kijijini hapo si shwari, kwani watu wengi wamekimbilia porini kutokana na hofu ya kukamatwa kutokana na mauaji hayo, na kubainisha watu hao walijisalimisha na walitaka wapelekwe katika Kituo cha Polisi kama walikuwa na mashaka nao, lakini wananchi walihakikisha wanatekeleza azma yao.
“Kama mwananchi wa Iringa Mvumi kitendo hicho hakikunifurahisha, lakini serikali iwakamate na kuwachukulia hatua kali wote waliochochea mauaji yale hasa wale waliokuwa wakiwatangazia wananchi kufika eneo la tukio,” alisema Joseph.
Aliongeza kuwa hilo ni moja ya matukio ya kinyama, ambayo amewahi kushuhudia kwenye maisha yake, japo kwa siku za nyuma Julai mwaka huu mwanamke mmoja mkazi wa Mvumi Misheni, aliuawa kijijini hapo na kisha mwili wake kutupwa kwenye korongo.
Alisema watu wengi wakiwemo marafiki zake, wamehama kijijini na sasa wanaishi porini kwa hofu ya kukamatwa na polisi. Alisema kijiji hicho, hakina kituo cha Polisi na wanategemea Kituo cha Polisi cha Mvumi Misheni, ambacho kiko mbali wastani wa kilometa sita.
Alisema siku hiyo ya tukio baada ya wananchi kuwazingira watafiti hao, askari Polisi wawili walifika ambao walikuwa na silaha, lakini licha ya kupiga risasi hewani, wananchi walishindwa kutii hadi kuwapiga kisha kuwaua watafiti hao, kabla ya kwenda kuchukua mabua ya mahindi na kuwateketeza kwa moto.
Alisema siku ya tukio watu zaidi ya 200 walikusanyika baada ya kuitikia mwito wa Mwenyekiti wa Kijiji kuwa kuna majambazi wamekamatwa.
“Hali ni mbaya kijijini, hakuna shughuli yoyote ya kiuchumi inayoendelea, kila mtu anaishi kwa hofu, watu wakisikia mungurumo wa gari wanakimbia ndani kujificha,” alisema na kubainisha kuwa wananchi wengi wamejificha katika Mlima Momvu na kwenye makorongo. Mkazi mwingine wa kijiji hicho, Happyness Nyambui alisema alifika kijijini hapo jana kutokea Fufu na kukuta nyumba nyingi zikiwa zimefungwa.
“Sikuwakuta majirani nikaambiwa wamekimbia na watoto wao baada ya tukio la mauaji,” alisema Happyness. Alisema hajawahi kuona mtu kunyonywa damu, lakini huo ni uvumi ambao unaenezwa na watu. Alisema shughuli kuu ya uchumi kijijini hapo ni kilimo na ufugaji, lakini mara nyingi shughuli hizo, zimekuwa zikiathiriwa sana na ukame.
“Nikasikia watu wanasema majambazi wanakimbia, lakini mimi sikwenda huko,” alisema Michael Joel mkazi wa kijiji hicho. Alisema alikuwa safarini Mpwapwa na baada ya kurudi, alikuta kijiji kina watu wachache.
“Shughuli zote zimesimama kwa kuwa watu hawapo, ni kitendo cha kusikitisha sana na kimetushtua, kwani magari hapa kijijini yamekuwa yakipita mara nyingi tu, tunashangaa kuona gari lililochomwa moto kuhusishwa na wanyonya damu,” alisema.
Mwinjilisti Jacob Foda wa Kanisa la Waadventista Wasabato, alisema ni jambo la kusikitisha mno kuona binadamu anatoa hukumu kwa mwenzake bila ya kumsikiliza. Alisema tukio hilo limeathiri maisha ya watu kwani wanaishi kwa wasiwasi.
“Mimi ninahubiri neno la Mungu, lakini sasa sina wa kumhubiria nyumba nyingi zimefungwa watu wamekimbia,” alisema Foda na kuongeza kuwa kitendo cha Mchungaji wa Kanisa la Christian Family kuwatangazia watu wakafanye kosa la mauaji si la kiungwana.
“Alitakiwa atafakari kwanza kabla ya kuchukua uamuzi wowote badala ya kukurupuka,” alieleza mchungaji huyo katika tukio ambalo Polisi inawashikilia zaidi ya watu 30.
Jijini Arusha, Mkurugenzi Mkuu wa SARI, Dk January Mafuru alisema watafiti hao walikuwa kwenye mradi maalumu ulioanza kazi zake mwaka 2014 kwenye mikoa mbalimbali, ambako walikuwa wakishughulika na utafiti wa masuala ya udongo ili kukusanya taarifa za hali halisi ya udongo na wakulima waone mafanikio katika kilimo.
Dk Mafuru alisema watafiti hao walikuwa na barua walizozisambaza kwa wakurugenzi, serikali ya vijiji na mamlaka husika kila wanapoenda, lakini katika hali isiyotarajiwa, ndipo watafiti hao walipofika kijiji cha Iringa Mvumi wilayani Chamwino, walisimama na kuwasalimia akinamama waliokuwa wakichimba chumvi.
“Walipowasalimia wakasogea kwa mbele kidogo na kushuka kwa ajili ya kuanza utafiti wa udongo ndipo wakati wakiendelea na shughuli za utafiti wao ndipo alipotokea mama mmoja akampigia simu Mwenyekiti wa Kijiji na kisha habari zikafika kwenye Kanisa la Christian Family ambako Mchungaji wa madhehebu hayo, Patrick Mgonela alipiga yowe na waumini walitoka kwenda eneo walilokuwa watafiti hao na kuanza kuwapiga kwa mapanga, marungu na shoka, ” alieleza mkurugenzi huyo.
Alisema alifika eneo hilo na kujionea hali halisi ya tukio hilo, ambalo linasikitisha sana maana licha ya watafiti hao kuonesha vitambulisho na barua, lakini waliendelea kupigwa wakiwa kazini.
“Nimesikitika sana juu ya vifo hivi, hawa walikuwa kazini wakiendelea na majukumu yao ya kikazi na walijitambulisha kuwa wapo kazini, lakini cha ajabu watumishi hao walikumbana na mauti hayo,” alieleza kwa masikitiko.
Alieleza kuwa Magazine na Lumanga walikuwa waajiriwa wa SARI ambayo inafanya utafiti wa udongo na mazao ya chakula, lakini Jaffari Mafuru ni mwanawe ambaye alikuwa si mwajiriwa wa kituo hicho, bali alikuwa amehitimu Chuo cha Mipango Dodoma, na kwa sababu alikuwa akipenda masuala ya utafiti, aliungana na watafiti hao kwa ajili ya kujitolea kufanya utafiti kwa vitendo Dodoma.
Alisema Lumanga atazikwa Olasiti jijini Arusha na Magazine alisafirishwa jana kupelekwa Ifakara mkoani Morogoro kwa ajili ya maziko huku Mafuru akisafirishwa kwenda wilayani Bunda mkoa wa Mara pia kwa maziko. Akizungumzia kifo cha mkewe, mume wa Teddy Lumanga, Yona Mjema alisema ilimchukua zaidi ya saa moja kukubali taarifa ya simu aliyopigiwa na shemeji yake kuhusu kifo cha mkewe.
“Nimetafakari sana juu ya msiba huu na baada ya saa moja kupita nikiwa nyumbani eneo la Olasiti jijini Arusha juzi Jumapili ndipo nilipoanza kulia na majirani kufika nyumbani kujua kulikoni,” alieleza Mjema akizungumzia mkewe ambaye alikuwa Mtafiti wa Maabara na Udongo SARI.
Mjema alikuwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru, ambako Teddy na wenzake wawili miili hiyo iliwasili saa 1:45 asubuhi jana ikitokea mkoani Dodoma ambako waliuawa juzi Jumamosi jioni.
Baada ya miili hiyo kuwasili, ilifikishwa kituoni SARI ambako wafanyakazi hao waliwaaga wenzao kisha miili hiyo kuchukuliwa na kupelekwa Mount Meru kwa ajili ya kuhifadhiwa na taratibu nyingine za mazishi zikiendelea. Akiwa hospitalini hapo, Mjema alisema ni ngumu kuamini kama kweli mkewe Teddy amekufa, lakini akaongeza “sina jinsi, nashukuru Mungu kwa jambo hili.”
“Huu ni msiba mzito sana kwangu maana mara kwa mara mke wangu alikuwa akisafiri kikazi na hii safari yake ya utafiti ni ya mara ya pili kwenda mkoani Dodoma na huwa tuna tabia ya kuwasiliana kwa njia ya simu majira ya asubuhi na jioni,” alisema na kuongeza:
“Asubuhi (Jumamosi) niliongea na mke wangu Teddy tukajuliana hali na kuulizia familia yetu ipo vipi pamoja na watoto wetu wawili… nikaongea naye tuliyoongea na akaniambia anakwenda vijijini, hivyo tutawasiliana jioni. Lakini jioni ilipofika kila nikimpigia simu simpati na ndipo jana Jumapili (juzi) nilipopigiwa simu na shemeji yangu kuwa mke wangu amekufa kwa kuchomwa moto.
“Tukio hili ni ngumu sana kulipokea asubuhi niliongea na mke wangu na jana Jumapili napokea simu mke wangu amekufa, kweli ni ngumu kuamini ameniacha mimi na watoto wawili. Nimeumia sana na nashukuru Mungu kwa hili, sina la kusema,” alisema mume wa mtafiti Lumanga. . Imeandikwa na Sifa Lubasi, Dodoma na Veronica Mheta, Arusha
CHANZO GAZETI LAHABARI LEO
 

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa