Home » » MAKUSANYO YA KODI YA PANGO LA ARDHI YAONGEZEKA MARADUFU.

MAKUSANYO YA KODI YA PANGO LA ARDHI YAONGEZEKA MARADUFU.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Na. Hassan Mabuye, Kitengo cha Mawasiliano, Wizara ya Ardhi.
Serikali imefanikiwa kukusanya jumla ya kiasi cha shilingi bilioni 76 cha makusanyo ya kodi ya pango la ardhi hadi kufikia tarehe 13 Mei 2017 kiwango ambacho hakijawahi kufikiwa.

Akiongea katika mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Yamungu Kayandabila amesema kiwango cha makusanyo ya kodi ya ardhi hakijawahi kufukiwa ukilinganisha na miaka ya nyuma ambapo kwa sasa Wizara ya Ardhi imeisha kusanya kiasi cha shilingi bilioni 76 cha kodi ya pango la ardhi.

Juhudi za kukusanya kodi ya pango la ardhi kwa viwanja vilivyopimwa zinaendelea vizuri licha ya changamoto iliyopo hususan muamko wa wananchi katika kulipa kodi, amesema Dkt. Kayandabila.

“Ni matumaini yangu kuwa katika kipindi kilichobaki Wizara itafikia lengo la kukusanya kiasi cha makusanyo ya kodi ya pango la ardhi kilichowekwa kwa mwaka wa fedha 2016/2017 ambacho ni kiasi cha shilingi bilioni 111.7”. Amesema Dkt. Kayandabila.

Amesema, Serikali kuanzia mwezi julai, 2017 kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi itaanza kukusanya kodi ya pango la ardhi kwenye viwanja na mashamba yasiyopimwa. Lengo la utaratibu huu ni kuongeza wigo wa mapato yatokanayo na kodi ya pango la ardhi.
Utaratibu huu utawafanya wananchi wote wanaomiliki ardhi waweze kulipa kodi. Hata hivyo, ni vema ieleweke kuwa uamuzi huu hauna lengo ya kupunguza juhudi za Wizara katika kupanga, kupima na kumilikisha ardhi kwa wananchi, isipokuwa utaratibu huu unajenga dhana ya uwajibikaji kwa wananchi wote katika kulipa pango la ardhi kwenye maeneo yao.

Aidha, serikali imeanza Ujenzi wa mfumo wa kielektronic wa kumbukumbu za Ardhi (Integrated Land Management System) ambao umeanza kutekelezwa. Mfumo huo ukikamilika utasaidia sana kuwa na kumbukumbu sahihi za wamiliki wa ardhi na hivyo kurahisisha ukusanyaji wa kodi za Ardhi.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa