NSSF YAWATAKA WATANZANIA KUJIWEKEA AKIBA


*Yasema imenzisha skimu maalumu kwa ajili waliojiajiri wenyewe pamoja na walioajiriwa lakini wanapenda kujiwekea akiba 

Na MWANDISHI WETU,
Dodoma. Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umewataka Watanzania kujenga utamaduni wa kujiwekea akiba kwa kujiunga na kuchangia NSSF ili waweze kujikinga na majanga kama vile uzee na ukosefu wa kipato kwa kunufaika na mafao yanayotolewa na Mfuko.

Aidha, NSSF imesema imenzisha skimu maalumu kwa ajili ya kuwafikia wananchi waliojiajiri wenyewe wakiwemo wakulima, wafugaji, wavuvi, wachimbaji wadogo wa madini, mama lishe, bodaboda na wajasiriamali wengine ili waweze kujiwekea akiba kwa ajili ya kesho yao iliyokuwa njema.

Hayo yalisemwa na Meneja wa NSSF wa sekta isiyo rasmi, Bi. Rehema Chuma, tarehe 20 Novemba 2024 jijini Dodoma kwenye mkutano wa Chama Cha Wahasibu Wanawake Tanzania. 

Amesema NSSF umeanzisha mpango wa kitaifa kwa sekta isiyo rasmi kwa lengo la kuwafikia watanzania wote waliojiajiri wenyewe ambapo wanaweza kujiwekea akiba kwa kima cha chini cha shilingi 30,000 ambapo atanufaika na mafao pamoja na huduma ya matibabu kwa mtu mmoja na atakeyejiwekea akiba ya 52,200 atanufaika na mafao pamoja na huduma za matibabu yeye mwenyewe na familia yake na kuwa mtu anaweza kuchangia hata shilingi 1000 kwa siku.

Amesema utaratibu wa kujichangia ni rafiki na rahisi sana ambapo unaweza kutumia namba ya kumbukumbu ya malipo na kuwasilisha michango popote ulipo bila ya kulazimika kufika katika ofisi za Mfuko au kutumia wakala.

"Kujiunga na skimu hii ni rahisi sana unaweza kutumia simu ya kiganjani kwa kupiga *152*00# kisha unaenda namba 3, kisha unaenda namba 6 unachagua NSSF, kisha namba Moja ambapo utaingiza namba ya NIDA na hapo hapo utakuwa umesajiliwa ambapo pia unaweza kutumia mfumo huo kujilipia michango yako na kuangalia taarifa nyingine," amesema Bi. Rehema.

Kuhusu skimu ya uchangiaji wa ziada, Bi. Rehema asema ni kwa ajili ya Watanzania walioajiriwa lakini wanapenda kujiwekea akiba kwa hiari ili kuongeza kipato wakati wa kustaafu.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wahasibu Tanzania, Tumaini Lawrence, ametoa wito kwa wahasibu ba wataalamu wa kada nyingine kuchangamkia fursa ya kujiunga na kuchangia NSSF kupitia mpango wa ziada (Supplementary Scheme) na wa sekta isiyo rasmi ili waweze kujiwekea akiba kwa ajili ya kesho yao iliyokuwa njema.

"Katika mkutano huu tupo na ndugu zetu wa NSSF ambao wapo hapa kwa ajili ya kutupa elimu hasa kupitia skimu ya uchangiaji wa ziada pamoja na ile ya sekta isiyo rasmi ambapo unaweza kujiwekea akiba hata kama ni mwajiriwa wa Serikali NSSF wanakuruhusu kujichangia kwa ajili ya kesho iliyokuwa njema," amesema Bi. Tumaini.

Kwa upande wake, Bw. John Masatu, Afisa Matekelezo kutoka sekta isiyo rasmi amesema mwanachama anaweza anaweza kujisajili popote alipo kwa kutumia simu ya kiganjani na kuwa wataendelea kuwafikia wananchi wengi wengi zaidi kuwapa elimu ya hifadhi ya jamii na kuwahamasisha kujiunga.



KAILIMA AZUNGUMZA NA WAENDESHA BVR DODOMA


Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Bw. Kailima Ramadhani akizungumza na washiriki wa mafunzo ya waandishi wasaidizi na waendesha vifaa vya Bayometriki (BVR) watakaohusika na zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwenye Halmashauri ya Jiji la Dodoma, mkoani Dodoma Septemba 23,2024. Mzunguko wa tano wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura utajumuisha mkoa  wa Dodoma katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Halmashauri za Wilaya ya Bahi, Chamwino na Kongwa, mkoa wa Manyara katika Halmashauri ya Mji wa Mbulu na Wilaya ya Kiteto na Simanjoro na mkoa wa Singida unaanza leo Septemba 25, 2024 hadi Oktoba mosi, 2024 na vituo vitakuwa vinafunguliwa kuanzia saa 2:00 asubuhi na kufungwa saa 12:00 jioni. (Picha na INEC). 

PROF MKENDA AITANGAZA RASMI SAMIA SCHOLARSHIP EXTENDED ILIYOTENGEWA BAJETI YA BILIONI 1.6.



Na Janeth Raphael MichuziTv -Dodoma


WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof.Adolph Mkenda amesema kuwa wamegundua uwepo wa uhaba mkubwa wa wataalam katika nyanja ya Sayansi na Teknolojia ya Nyukilia hapa Nchini ambapo uhalisia unaonesha kuna idadi ndogo ikiwemo Afya,Elimu,Nishati, Viwanda,Kilkmo na kwingineko.

Prof. Mkenda ameyasema hayo leo hii Jijini Dodoma katika mkutano na Wanahabari wakati akitangaza rasmi kuhusu ufadhili huo wa Samia Scholarship Extended wenye lengo la kuendeleza mpando wa kukuza Sayansi,Tehama,Hisabati,Uhandisi,Elimu na fani zilizo kipaumbele cha Taifa.

Katika kuongeza amesema mfano katika sekta ya Afya takwimu zinaonesha kuwa kuna Nyukilia Medicine Doctors 6 tu hapa Nchini, Wataalam wa kutengeneza na kuchanganya madawa ya mionzi wapo 2 tu na Wataalam wa Ekolojia wako chini ya 100 hapa Nchini.


"Sasa tumegundua kuwa tuna uhaba mkubwa sana wa Wataalam katika nyanja ya Sayansi ya Teknolojia ya nyukilia hapa Nchini, uhalisia unaonesha kuwa kuna idadi ndogo sana ya wataalam wa Sayansi na Teknolojia ya Nyukilia katika Sekta mbalimbali ikiwemo Afya,Elimu,Nishati,Viwanda,Kilimo na kwingineko".

"Mfano katika eneo la Sekta ya Afya tuna Medical Physist 6 tu hapa Nchini, tuna Nyukilia Medicine Doctors 6 tu,Radio Chemistry 1 tu,Wataalam wa kutengeneza na kuchanganya madawa ya mionzi wapo 2 tu Nchini na wataalam wa Ekolojia wapo chini ya 100 hapa Nchini".


"Katika sekta ya Elimu ambapo tunahitaji kuwa na wahadhili wengi wanaofundisha watu wetu napo tuna uhaba mkubwa ambapo wenye PhD takwimu sasahivi zinaonesha tunao 10 tu,wengine tuliokuwa nao mahiri kabisa wamestaafu mfano wa Dkt Mohamed Gharib Bilal ambaye alikuwa Makamu wa Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,kwahiyo tuna upungufu mkubwa sana nyanjia hizo na tunazihitaji sana".


Aidha Waziri ameeleza kuwa kuanzia mwaka wa fedha wa 2022/2023 Serikali kupitia Wizara ya Elimu ilianza kutoa ufadhili wa asalimia 100 kwa wahitimu wenye ufaulu wa juu katika masomo ya Sayansi kwenye mitihani ya kidato cha sita endapo wahitimi hao watachagua kusoma maosoma ya Sayansi, Tehama,Hisabati,Uhandisi na Elimu Tiba ambapo wameendelea kufanya mfululizo na wanufaika ni wengi.


"Kama mnavyofahamu Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia inatekeleza mpango wa kukuza Sayansi, Tehama,Uhandisi,Hisabati na Elimu Tiba pamoja na fani nyingine za kipaumbele zikiwemo fans ambazo zina wataalam wachache hapa Nchini. Kama mnakumbuka kuanzia mwaka wa fedha 2022/2023 Wizara ilianza kutoa ufadhili wa asilimia 100 kwa wahitimu wenye ufaulu wa juu katika masomo ya Sayansi katika mtihani wa kidato cha sita,endapo tu wahitimu hao watachagua kwenda kusoma masomo ya Sayansi, Tehama,Uhandisi, Hisabati na Elimu Tiba kwa vyuo vya ndani ya Nchi,hayo tumekuwa tukiyafanya mfululizo na wanufaika ni wengi".


Mbali na hayo pia Waziri ametoa msimamo wa Wizara kwa kushirikiana na Taasisi zake zote kuwa imeamua kuongeza wigo wa Samia scholarship kwa wanafunzi wa kidato cha sita wanaokwenda chuo kikuu ikiwa lengo ni kuhakikisha kwamba wale waliofaulu vizuri katika masomo wanafanya masomo hayo tu na sio kurudi katika masomo mengine yasiyo ya Sayansi.


"Kwahiyo Wizara kwa kushirikiana na Taasisi zake zote imeamua kuongeza wigo wa Samia Scholarship kwa wanafunzi wa kidato cha sita wanaokwenda chuo kikuu na lengo lake ni kuhakikisha kwamba wale waliofaulu vizuri kwenye masomo ya Sayansi hawaondoki kwenda kufanya masomo mengine".


Naye Prof Najat Mohammed ambaye ni Mkurugenzi wa Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) katika mkutano huo ametoa maelezo juu ya sifa za mwombaji anazopaswa kuwa nazo ambapo amesema kuwa ni pamoja na kuwa Raia wa Tanzania na asiyezidi umri wa miaka 35,awe muhitimu wa chuo kikuu shahada ya awali kwa kipindi kisichozidi miaka 5 na kuwa na ufaulu wa juu kuanzia kiwango cha GPS ya 3.5 ya 5 au wastani wa ufaulu wa B kwa shahada ambazo hazina GPA.


"Ili kuweza kupata ufadhili wa Samia Scholarship wa shahada ya umahiri wa Sayansi na Teknolojia ya Nyukilia, muombaji anatakiwa kuwa na sifa zifuatazo".


"Kwanza awe Mtanzania mwenye umri usiozidi miaka 35, Pili awe maehitimu chuo kikuu shahda ya awali aliyemaliz kipindi kisichozidi miaka 5. Tatu awe na ufaulu wa juu kuanzia kiwango cha GPA ya 3.5 kati ya 5 au wastani wa ufau wa B kwa shahada ambazo hazina GPA,wenye matokeo ya jumla katika shahada ya awali ya Sayansi ya Uhandisi, Hisabati,Tehama,Elimu Tiba, Nishati,Kilimo na fani zingine za kipaumbele cha Taifa".


Fedha hii ya Shilingi Bilioni 1.6 iliyotengwa ni ya kuanzia walau kwa Watanzania wa tano katika fani zilizoainishwa na kuwepo uhaba wa Wataalam.





TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI: ENDELEENI KUWAHAMASISHA WANANCHI WAEPUKE TABIA ZEMBE - MAJALIWA

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

 

ENDELEENI KUWAHAMASISHA WANANCHI WAEPUKE TABIA ZEMBE - MAJALIWA

 

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameitaka Wizara ya Afya iendelee kuwahamasisha wananchi wabadili mitindo ya maisha ili kuepuka tabia zembe zinazochochea ongezeko la magonjwa yasiyoambukizwa.

 

Wizara ya Afya iendelee kushirikiana na wadau kuhamasisha Watanzania kubadili mwenendo wa maisha kwa kuepuka tabia zembe zinazochochea ongezeko la magonjwa yasiyoambukizwa. Tuendelee kuzingatia mazoezi ili kuimarisha afya zetu na kuipunguzia Serikali mzigo wa kugharamia tiba ya magonjwa yasiyoambukizwa,” amesema.

 

Akizungumza na viongozi, wananchi na wadau mbalimbali walioshiriki mbio za NBC Dodoma Marathon za mwaka 2024 kabla ya kutoa tuzo na zawadi kwenye uwanja wa Jamhuri, jijini Dodoma, leo (Jumapili, Julai 28, 2024), Waziri Mkuu amesema takwimu za Wizara ya Afya zinaonesha kuwa idadi ya watu wenye magonjwa yasiyoambukiza imeongezeka.

 

Amesema magonjwa yasiyoambukiza ambayo yanaongoza nchini ni pamoja na kisukari, moyo, figo na afya ya akili na akatumia fursa hiyo kuwapongeza wananchi walioshiriki mbio za hisani za NBC Dodoma Marathon za mwaka 2024. “Kujitokeza kwenu kwa wingi leo, maana yake ni kwamba mmetambua kuwa kukaa bwete ni kukaribisha magonjwa yasiyoambukiza,” amesisitiza.

 

Waziri Mkuu pia ameitaka Benki ya NBC iendelee kuweka mikakati ya kuhakikisha mashindano hayo yanakuwa endelevu na yanaendelea kugusa maisha ya Watanzania wengi zaidi.

 

Vilevile, amezitaka taasisi na asasi zisizo za Serikali zijitokeze kuunga mkono jitihada za Serikali kwa kuandaa matukio kama hayo ili wananchi waanze kuzoea kufanya mazoezi. “Tulishatoa maelekezo kwa Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya ili wawakusanye wananchi na kufanya mazoezi kama hivi,” amesema.

 

Amesema Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuhakikisha ustawi na afya ya mtoto zikiwemo kutekeleza Mpango wa Mama Samia Mentorship ambao ni mahsusi kwa utoaji mafunzo ya muda mfupi kazini kwa madaktari bingwa na wakunga. “Hadi kufikia Juni 2024, halmashauri 184 zilishafikiwa na mpango huo na idadi ya wanufaika ni watumishi 4,796,” amesema. 

 

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma alisema benki ya NBC ni wadau wakubwa katika sekta ya michezo kwa kudhamini ligi ya soka ya Tanzania yaani NBC Premier League, kamati ya hamasa inayochangia timu za Taifa na pia ni wadau wakubwa katika mfuko wa utamaduni wenye lengo la kukopesha miradi ya kazi za sanaa nchini. Pia wanaendesha marathon ambayo fedha zake hutumika kuchangia huduma za afya.

 

Amesema kuwa mbali na mbio hizo kutumika kuimarisha afya na kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza, pia zinatumika kama sehemu ya kuibua vipaji kwa wanamichezo hasa wanariadha ambao wamekuwa wakitumika katika michezo mbalimbali ya kitaifa na kimataifa.

 

Mapema, akitoa taarifa kuhusu mbio hizo, Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Theobald Sabi, alisema hii ni mara ya tano kwa mbio hizo kufanyika Dodoma huku lengo likiwa ni kutangaza utalii wa Dodoma.

 

Alisema kwa mara ya kwanza mbio hizo zilifanyika Novemba 11, 2020 zikiwa na washiriki 1,944 na waliweza kukusanya sh. milioni 100 lakini mwaka huu zimeweza kupata washiriki 8,000 ambapo wameweza kukusanya sh. milioni 300.

 

Amesema makusanyo ya mwaka huu yatatumika kwenye ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wa taaluma ya ukunga kwa kushirikiana na Taasisi ya Benjamin Mkapa; pia watasaidia mapambano dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi kwa wanawake ambayo itakabidhiwa kwa taasisi ya Saratani ya Ocean Road.

 

“Pia fedha nyingine itatumika kuchangia ujenzi wa chumba cha upasuaji katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili,” alisema.

 

Washiriki wa mbio hizo walikuwa ni wa km.5, km.10, km.21 na km.42

MAVUNDE APIGA MARUFUKU WAMILIKI WA LESENI ZA UCHIMBAJI MDOGO WA MADINI KUINGIZA WAGENI


Na Janeth Raphael MichuziTv -Dodoma

Waziri wa Madini Mhe Anthony Peter Mavunde amepiga marufuku kwa wamiliki wa Leseni za uchimbaji mdogo wa Madini kuingiza wageni kutoka nje ya Nchi kwenye leseni zao bila kuwa na mikataba au makubaliano yaliyopitishwa kwa mujibu wa Sheria.

Waziri Mavunde ameyasema hayo leo Jijini Dodoma July 28,2024 wakati akizungumza na Wanahabari kuhusu Mwendendo wa makusanyo ya maduhuri yatokanayo na rasilimali madini Nchini kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2023/2024 na Katazo la Wageni kuungia kwenye PMLs bila kuwa na makubaliano ya msaada wa kiufundi(TSA).

Na kupiga marufuku kwa Wageni wenye leseni kubwa za biashara ya madini hususan wa madini ya vito kwenda machimboni kukusanya Madini kwani kwa kufanya hivyo ni kupora haki ya ajira ya Watanzania.

Na kusema kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua kali za kisheria kwa Wamiliki wa leseni za uchimbaji mdogo wa madini pamoja na wageni kutoka nje ya nchi watakaobainika kukiuka matakwa ya Sheria.

"Nachukua nafasi hii kupiga marufuku kwa wamiliki wa leseni za uchimbaji mdogo wa madini, kuingiza wageni kutoka nje ya nchi kwenye leseni zao bila kuwa na mikataba/makubaliano ya msaada wa kiufundi (Technical Support) yaliyopitishwa kwa mujibu wa Sheria".

" Pia nichukue fursa hii kupiga marufuku wageni wenye leseni kubwa za biashara ya madini (dealer’s Licence) hususan wa madini ya vito kwenda machimboni kukusanya madini. Kufanya hivi ni kupora haki ya ajira ya Watanzania ambao kwa mujibu wa Sheria,kazi ya kufuata madini machimboni inapaswa kufanywa na Watanzania pekee wenye kumiliki leseni ya “broker”.

"Ndugu wanahabari, Serikali haitasita kuchukua hatua kali za kisheria kwa wamiliki wa leseni za uchimbaji mdogo wa madini pamoja na wageni kutoka nje ya nchi watakaobainika kukiuka matakwa ya Sheria.Ndugu wanahabari, Katika kumalizia, naomba nitoe rai kwa wawekezaji wote wenye leseni za uwekezaji katika Sekta ya Madini kuzingatia matakwa ya Sheria ya Madini, Sura ya 123. Aidha, Wizara ya Madini itaendelea kuwapa ushirikiano wawekezaji wote wa ndani na nje ya nchi wenye nia ya kufanya uwekezaji wenye tija na kukuza uchumi wa taifa letu kutokana na uvunaji wa rasilimali madini".

Mbali na hayo pia Waziri ameeleza kuwa kumetokea tabia ya wamiliki wa leseni za uchimbaji mdogo wa madini kuingia makubaliano yasiyo rasmi na wageni wakati leseni za uchimbaji mdogo wa madini zinatolewa kwa Watanzania pekee kwa mujibu wa kifungu cha 8(2) cha Sheria ya Madini Sura 123.

"Ndugu wanahabari, Kumetokea tabia ya wamiliki wa leseni za uchimbaji mdogo wa madini kuingia makubaliano yasiyo rasmi na wageni kutoka nje ya nchi na kuwaruhusu kufanya kazi katika leseni zao. Ikumbukwe kwamba, leseni za uchimbaji mdogo wa madini zinatolewa kwa Watanzania pekee kwa mujibu wa Kifungu cha 8(2) cha Sheria ya Madini, Sura 123".

Waziri ameweza pia kuzungumzia suala la uvunjaji wa rekodi katika ukusanyaji wa maduhuli ambapo amesema Wizara ilikuwa ikikusanya kiasi kidogo cha maduhuli ukilinganisha na sasa kwani ndani ya kipindi kifupi limeshuhudiwa ongezeko la makusanyo ya muduhuli yatokanayo na shughuli za uchimbaji mfano mwaka wa fedha 2023/2024 Wizara ilipanga kukusanya jumla ya Shilingi 882,121,205,00 lakini hadi Juni 2023 Tume ya Madini ilikusanya jumla ya Shilingi 753,815,646,,857.13 sawa. A asilimia 85.45 ya lengo lililopangwa.

"Nisema tu Hapo nyuma kidogo, Wizara ilikuwa ikikusanya kiasi kidogo cha maduhuli ukilinganisha na sasa. Mathalan, Mwaka wa Fedha 2014/2015, Wizara ilikuwa na lengo la kukusanya Shilingi 209,957,882,999.00 na kufanikiwa kukusanya TZS 168,043,402,877.13. Aidha, Mwaka wa Fedha 2015/2016 lengo la makusanyo lilikuwa ni Shilingi 211,957,882,999.00 na kufanikiwa kukusanya Shilingi 207,917,127,854.55. Hata hivyo, ndani ya kipindi kifupi tunashuhudia ongezeko la makusanyo ya maduhuli yatokanayo na shughuli za uchimbaji wa madini. Mabadiliko haya ni mafanikio makubwa ambayo wadau wote wa Sekta hii wanatakiwa kujivunia".

"Ndugu Wanahabari, Mafanikio haya yanatokana na jitihada jumuishi za wadau mbalimbali kuanzia kwa wachimbaji wa madini wakubwa kwa wadogo, wafanyabiashara wa madini pamoja na Taasisi zote zinazohusika katika kuilea na kuisimamia Sekta ya Madini Nchini.".

"Nitumie fursa hii kuwapongeza wadau wote kwenye Sekta kwa mchango wao, na kuwahamasisha kuendeleza jitihada za kuhakikisha Sekta inazidi kukua na kuongeza zaidi mchango wake katika kukuza uchumi wetu".

Vitendo vya udanganyifu kwenye baishara ya madini pamoja na Utoroshwaji wa madini ni moja kati ya vitu vilivyopingwa vikali na Waziri huyo.

"Aidha, nitumie nafasi hii tena kukemea vitendo vya udanyanyifu kwenye biashara ya madini pamoja na utoroshaji wa madini vinavyofanywa na watu wachache ambao katika vitendo vyao, wanaturudisha nyuma katika malengo yetu. Wizara itaendelea kuchukua hatua kali kwa wahusika wote watakaobainika wanajihusisha na utoroshaji wa madini.

Hii ni moja kati ya Makatazo ambayo yamekuwa yakitolewa na Waziri huyu mwenye dhamana ya Wizara ya Madini ikiwemo ya Wamiliki wanaohodhi maeneo bila kuyaendeleza.



KONDOA MJI WAISHUKURU SERIKALI KULETA CHEREHANI 100 KUPITIA UNICEF

Afisa Elimu Awali na Msingi katika Hamashauri ya Mji Kondoa Mwalimu Hassan Mtamba ameishukuru Serikali kupitia shirika la Watoto duniani (UNICEF) ambao ni wafadhili wa program ya Elimu changamani kwa vijana (IPOSA) kwa kuleta chereheni 100 kwa ajili ya kuzigawanya katika vituo 5 ambavyo vinatekeleza program hiyo.

Akiongea baada ya mapokezi ya vifaa hivyo Mwalimu Mtamba amesema cherehani hizo zimekuja na matanki 8 ya maji ya ujazo wa lita 200 kila moja yatasambazwa katika vituo viwili ambavyo vipo katika Shule ya Msingi Kolowasi na King’ang’a ikiwa ni vifaa vya wamu ya pili ambapo awali wamepokea vifaa vya ufundi seremala.

Akiongea kwa upande wake Mwalimu Ashura Mwaya mratibu wa Program ya IPOSA amesema mpango huu ulianzishwa na serikali kwa ajili ya kuwasaidia vijana wa kike na kiume walio nje ya mfumo rasmi wa shule ili waweze kupata ujuzi mbalimbali utakaowasaidia kujipatia kipato kwa kujiajiri au kuajiriwa.

“Katika Halmashauri ya Mji Kondoa vituo vipo katika Shule ya Msingi Maji ya Shamba, Shule ya Msingi Kondoa, Shule ya Msingi King’ang’a, Shule ya Msingi Chandimo na Shule ya Msingi Kolowasi ambapo jumla wapo wanafunzi 449 ambao wanaendelea na mafunzo ya fani mbalimbali yanayotolewa,”amesema Mwalimu Ashura

Ameongeza kuwa vijana wenye umri wa miaka 14 hadi 22 ndio wanaoruhusiwa kujiunga katika mpango huo ili waweze kupata ujuzi wa ufundi seremala, ushonaji, uchomeleaji, mapishi na ujasiriamali kama kutengeneza sabuni na karanga ambavyo wanaweza kuviuza na kujipatia kipato kitakachowasaidia wao na taifa kwa ujumla.

Aidha amesema kuwa mafunzo hayo yanatolewa katika vituo hivyo bila malipo yoyote kwani serikali imegharamia vifaa na kuwalipa walimu na wanafunzi wanajiunga muda wowote hakuna muda maalum wa kujiunga ili kupata vijana wengi ambao wapo nje ya mfumo rasmi.

Programu ya IPOSA ilianza mwaka 2019 katika Halmashauri ya Mji Kondoa ambapo vituo vitano vilichaguliwa na vina jumla ya wanafunzi 449 ambao wapo nje ya mfumo rasmi wa elimu kutokana na changamoto mbalimbali kama kuacha shule au kushindwa kuendelea na masomo baada ya kumaliza elimu ya msingi.


 

WAZIRI SIMBACHAWENE AIPONGEZA TARURA KUFUNGUA BARABARA KWENYE MILIMA MIKALI KATA YA MANG’ALIZA


#Barabara za zege zaonesha ufanisi, zafungua maendeleo   

#TAMISEMI kuhakikisha mlima huo unaboreshwa na kupitika muda wote

Na. Catherine Sungura, Kibakwe - Mpwapwa

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Mbunge wa Kibakwe, Mhe. George Simbachawene  ameishukuru na kuipongeza Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA)  kwa kuanza kujenga barabara za zege kwenye milima mikali iliyopo kata ya Mang’aliza-Kibakwe wilayani Mpwapwa.

Waziri Simbachawene ameyasema hayo wakati wa ziara  ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa miundombinu inayosimamiwa na TARURA  iliyofanywa na Naibu Katibu Mkuu wa OR-TAMISEMI anayeshughulikia miundombinu  Mhandisi Rogatus Mativila .

“Niwashukuru sana TARURA na kuwapongeza kwa kutusaidia tulio kwenye mazingira magumu, jimbo langu la Kibakwe lipo katika maeneo tambarare na milimani, na hii ni milima mikali ambayo ipo karibu kata sita na hakuna namna yoyote ya kutengeneza barabara zaidi ya barabara za zege”.

Ameongeza kusema kuwa utaratibu huo wa TARURA wa kujenga barabara za zege  waliouanza miaka michache iliyopita umeanza kuleta ufanisi mkubwa hususani kufungua maendeleo pamoja na kuwaletea huduma nyingine wananchi ikiwemo umeme, shule ya sekondari pamoja na kituo cha afya.

“Kata ya Mang’aliza haikuwa na maendeleo kabisa lakini hii  barabara ilivyofunguliwa hivi karibuni imeleta maendeleo kwa wananchi kwani miaka ya nyuma nilikuwa nakuja huku kwa pikipiki  lakini sasa hivi nakuja kwa gari na hata magari makubwa yanafika kuleta vifaa vya ujenzi ambapo kuna shule ya sekondari inajengwa, kwasababu sehemu korofi zote wameweka zege, kwakweli nawapongeza TARURA”, aliongeza Mhe. Simbachawene.

“Hata hivyo ombi langu tu waendelee kutenga fedha kwa maeneo mengine kwani Ilani na sera  yetu sasa ni kuwapelekea umeme na huduma nyingine wananchi lakini  changamoto ilikuwa ni barabara ila kusema ukweli TARURA wamejitahidi sana kwani fedha zinazohitajika ni nyingi ila kwa hicho kidogo wamefungua hizo barabara na sasa zinapitika na shughuli za kijamii zinaendelea kama kawaida" alisisitiza. 

Aidha, Mhe. Simbachawene  aliwapongeza  Mhe. Rais  Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuhangaika kutafuta  rasilimali fedha, watendaji wa TARURA kwa kazi nzuri pamoja na TAMISEMI kwa usimamizi ambapo ana imani nia ya kufungua barabara zaidi itaendelea.

Naye, Naibu Katibu Mkuu OR-TAMISEMI Mhandisi Rogatus Mativila amesema mlima huo wenye urefu wa Km. 5 umekuwa mgumu sana kupitika wakati wa kiangazi na hata masika ambapo chini ya mlima huo  kuna uzalishaji mkubwa kutoka kwa wafugaji na wakulima wa mazoa mbalimbali ambapo TARURA  wameweza kutengeneza maeneo korofi kwa kujenga barabara za zege la saruji lililochanganywa na kototo pamoja na nondo ambapo hivi sasa barabara hiyo inapitika.

Mhandisi Mativila amesema kwamba wao kama OR-TAMISEMI wataendelea kuhakikisha mlima huo unaboreshwa na kupitika muda wote na kuahidi kuendelea kutoa fedha zaidi ili wananchi waendelee kuzalisha mazao mbalimbali  na kupatiwa huduma za kijamii ikiwemo shule na afya.

 

Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan azungumza na Machifu wa Tanzania, Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha ya pamoja na Viongozi wa Machifu Kitaifa, Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma tarehe 20 Julai, 2024.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha ya pamoja na Machifu kutoka Mikoa mbalimbali, Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma tarehe 20 Julai, 2024.

Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan azungumza na Machifu wa Tanzania, Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwahutubia Machifu kutoka Mikoa mbalimbali nchini katika viwanja vya Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma tarehe 20 Julai, 2024.


 

Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan azungumza na Machifu wa Tanzania, Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma

 


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwahutubia Machifu kutoka Mikoa mbalimbali nchini katika viwanja vya Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma tarehe 20 Julai, 2024.

CCM Dodoma wampongeza Rais kuwasaidia watoto wenye Mahitaji Maalum


Kamati ya siasa mkoa wa Dodoma wamempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali na kuwasaidia wenye mahitaji maalum ikiwemo kuwajengea mabweni mawili kwa ajili yao katika Shule ya Msingi Iboni iliyopo katika Halmashauri ya Mji Kondoa kata ya Chemchem.

Pongezi hizo zimetolewa na Katibu wa CCM mkoa wa Dodoma Ndg. Pili Agustino wakati wa ziara ya kutembelea mradi wa mabweni mawili yaliyojengwa katika shule hiyo hivi karibuni.

“Nakumbuka nilikuja hapa mwaka 2023 tulikuja hapa tulikuwa bado hatujaanza ujenzi tukaongea na kupokea changamoto za hawa watoto ambapo wengine walikuwa wanatembea umbali mrefu na wazazi wao walikuwa wanashindwa kuwaleta hapa kutokana na changamoto ya kipato walizonazo,”amesema Katibu Pili

Ameendelea kueleza kuwa kutokana na kuwa Mheshimiwa Rais ni msikivu na anawapenda watoto akasikia kilio chao na akawaletea fedha kwa ajili ya ujenzi wa mabweni mawili ya watoto wenye mahitaji maalum ambapo wanasoma makika mazingira mazuri na salama na kuondokana na hali ya awali ambapo walikuwa wanasoma katika mazingira magumu.  

Aidha amewataka walimu kuyatunza mabweni hayo na kuhakikisha wanafunzi wanayatumia vizuri ili wenzao watakaokuja waweze kuyatumia yakiwa katika hali nzuri na imara kwani watoto hao ni wenye mahitaji maalum na wanatakiwa walelewe vizuri na kuelekezwa kufanya vitu mbalimbali.

“Tuna imani shule hii itaendelea kuwapokea na watoto wengine kutoka mikoa na wilaya nyingine si Kondoa tu hivyo tunawakaribisha wazazi wenye watoto wenye mahitaji maalum kwani mabweni ni mazuri na salama na tuache tabia ya kuwaficha watoto ndani tuwalete shule kwani wanaweza kusoma na kufaulu vizuri na kupata kazi,”amesisitiza Katibu Pili

Akiongea kwa niaba ya wenzake mwanafunzi Rahma Ramadhani mwenye ulemavu wa macho amemshukuru Rais kwa kuwajengea mabweni na kumuombea ili apate fedha zaidi ambazo zitasaidia katika ununuzi wa vifaa vya kujifunzia shuleni hapo ambavyo vinakosekana shuleni hapo.

Akisoma awali taarifa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Iboni Mwalimu Charles Phabian amesema shule hiyo ilipokea fedha shilingi milioni 142 kutoka Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) kwa ajili ya ujenzi wa bweni moja, vitanda na magodoro pamoja na shilingi milioni 128 kutoka serikali kuu kwaajili ya ujenzi wa bweni na vitanda vya wanafunzi wenye mahitaji maalum ambayo yote yamekamilika.

Mabweni yaliyojengwa katika Shule ya Msingi Iboni kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum yamekamilika ambapo Kamati ya Siasa mkoa imeshauri yaanze kutumika mapema mwezi Agosti na yatahudumia wanafunzi kutoka ndani nan je ya Kondoa na yana uwezo wa kubeba wanafunzi 200 wakike 120 na kiume 80 ambapo kwa sasa kuna jumla ya watoto 30 wenye mahitaji maalum kwenye shule hiyo.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kondoa Ndg. Said Majaliwa akitoa ufafanuzi wa jambo wakati wa ziara ya ukaguzi wa miradi katika Shule ya Msingi Iboni
Mkuu wa Shule ya Msingi Iboni Mwalimu Charles Phabian akisoma taarifa ya mradi wa ujenzi wa mabweni mbele ya kamati ya siasa mkoa wa Dodoma
Wanafunzi wenye mahitaji maalum wakiwa wamejipanga na kusikiliza ujumbe kutoka kwa viongozi wa kamati ya siasa mkoa wa Dodoma baada ya kutembelea shuleni hapo.
Muonekano wa Bweni lawanafunzi wa kiume wenye mahitaji maalum lililojengwa katika Shule ya Msingi Iboni Kondoa Mji
Muonekano wa Bweni la wanafunzi wa kike wenye mahitaji maalum  lililojengwa katika Shule ya Msingi Iboni  Kondoa Mji
 

TANROADS YATEKELEZA AGIZO LA WAZIRI MKUU




Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), imetekeleza kwa vitendo maagizo yaliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu ya kuchagua na kuendesha mafunzo ya vinara wa ufuatiliaji na uthamini katika taasisi za umma.

Mmoja wa Waratibu wa mafunzo ya vinara yaliyotolewa na wawezeshaji kutoka ofisi ya Waziri Mkuu, hivi karibuni Bw. Elirehema Saiteru, Meneja Mipango, Ufuatiliaji na Tathmini wa TANROADS amesema kuwa wameendesha mafunzo kwa watumishi kutoka Makao Makuu na mikoa yote 26 ya Tanzania, yaliyofanyika mkoani Morogoro, kulingana na mwongozo uliotolewa mwezi Juni 2024 jijini Dodoma.

Bw. Saiteru amesema kuwa mafunzo hayo ni utekelezaji wa mwongozo wa kuchaguliwa kwa vinara watakaokuwa wakifanya ufuatiliaji na tathimini ya miradi iliyopo chini ya taasisi hii.

“Baada ya uzinduzi wa hii miongozo kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu tulipewa maelekezo kuanza mara moja utekelezaji wake, na awali kama taasisi tulikuwa tayari tumeshaanza kuandaa miongozo yetu na sasa tupo katika nafasi nzuri ya utekelezaji kwa kuwa inakwenda sambamba,” amesema Bw. Saiteru

Hatahivyo, amesema hatua inayofuata ni kuandaa nyaraka ya upimaji utayari wa taasisi wa kufanya kazi ya ufuatiliaji na tathmini.

Mwakilishi wa washiriki, Mhandisi Cecilia Kalangi ameshukuru kwa taasisi kuendesha mafunzo haya, ambayo yatasaidia kupata ufumbuzi wa haraka kwenye miradi yenye changamoto tangu awali.

Nawe Mha. Magesa Chacha, Mkuu wa Idara ya Mipango kutoka TANROADS mkoa wa Mwanza amesema washiriki wameweza kujifunza namna ya kufanya ufuatilia na tathmini kwa kuzingatia maono ya Dunia na ya serikali ya mwaka 2025 na pia mifumo iliyoibuliwa na Wizara ya Ujenzi ya kuweka taarifa zote za miradi.

“Nawasihi washiriki wenzangu kuzingatia kila hatua ya mafunzo haya kwani ndio mwarubaini ya miradi ambayo baada ya kuanza inaonekana ikiwa na changamoto, wakati ingeweza kutambulika katika hatua za awali ingetatuliwa mapema,” amesisitiza Mha. Kalangi.

Naye mwezeshaji Bw. Chalton Meena kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu amesema ofisi hiyo inasimamia utendaji wa serikali kwenye wizara na taasisi zake, hivyo wote hawana budi kufuata mwongozo huo wa mwaka 2024.

Bw. Meena amezitaja nyaraka hizo kuwa ni Mwongozo wa Tathmini wa Kitaifa (National Evaluation Manual); Mwongozo wa Usimamizi wa Tathmini nchini na Ufuatiliaji na Tathimini (Monitoring & Evaluation Readness Assessment Tool for Government Institutions).

KAIMU KATIBU MKUU MITAWI AONGOZA KIKAO KAMATI TENDAJI MRADI WA EMA


Kamati ya Usimamizi wa Mradi wa Kuimarisha Uwezo wa Kitaasisi wa Utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira (EMA) imekutana kwa ajili ya kupitia taarifa za utekelezaji wa mradi huo.

Katika kikao hicho cha nne kilichofanyika leo Jumatatu Julai 15, 2024 kimeongozwa na Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Bw. Abdallah Hassan Mitawi ambapo amesema mradi huo utaongeza uwezo wa kitaasisi katika kuimarisha uzingatiaji wa sheria na mifumo ya utekelezaji.

Utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira umekabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo upungufu wa rasilimali watu na rasilimali fedha katika utekelezaji, ufuatiliaji na tathmini ya rasilimali mazingira katika ngazi zote. Mradi huu umekuja na suluhisho la changamoto hizi amesema Mitawi.

Wajumbe wa kikao hicho pia walipitia taarifa ya utekelezaji wa mradi kwa mwaka wa fedha 2023/24 pamoja na bajeti ya 2024/25, ambapo Mitawi amewahimiza kuusimamia vyema mradi katika utekelezaji wa sheria ya usimamizi wa mazingira

Pia wajumbe wa kikao hicho walipata fursa ya kuipitia taarifa ya mpango wa matumizi kwa mwaka wa fedha ulioanza Julai 2023 na kukamilika Juni 2024 kama ulivyowasilishwa na Mratibu wa Mradi Bw. Richard Masesa.

Itakumbukwa kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais imefanya jitihada kadhaa za kulinda na kuhifadhi mazingira ikiwa ni pamoja na kuweka Sera ya Kitaifa ya Mazingira (1997) pamoja na Sheria ya Usimamizi wa Mazingira (2004).

Mradi wa EMA unaofadhiliwa na Serikali ya Sweden kupitia Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Swedish (SIDA) unakusudia kushughulikia changamoto kuu za mazingira na kuondoa vizuizi vya kisekta vilivyopo katika Wizara na mamlaka maalumu za kisheria na kuongeza wigo wa utendaji.

Mradi wa EMA unatekelezwa na Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).



 

WAZIRI MKUU AHIMIZA USIMAMIZI KUELEKEA SIKU YA MASHUJAA

Na Mwandishi wetu-Dodoma

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa ameagiza ofisi yake kuhakikisha inaendelea kufanya maandalizi kwa ajili ya Maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa itakayofanyika Jijini Dodoma Julai 25,2024.

Mhe. Majaliwa ametoa agizo hilo leo tarehe12 Julai, 2024 Jijini Dodoma wakati akikagua maendeleo ya maandalizi ya Maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa.

“Kwa kuwa tupo kwenye maandalizi na tunaendelea, maboresho yote yaendelee, Ofisi ya Waziri Mkuu muda wote watakuwa hapa, Maafisa, wahusika wote wawe hapa kuhakikisha kila hatua na kitu chochote kikikwama basi mawasiliano yasiwe ya kutafuta mtu akiwa mbali” amebainisha Waziri Mkuu

Aidha, Mhe. Majaliwa ameridhishwa na maandalizi katika maeneo ya ujenzi na upande wa Gwaride la Majeshi ya Ulinzi na Usalama lenye vikosi vitano ikiwemo Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza pamoja na Jeshi la Uhamiaji.

Vilevile, Waziri Mkuu amemtaka mkandarasi anayehusika na ujenzi wa eneo hilo kukumilisha ujenzi kwa viwango na ubora unaotakiwa.

“Msimamizi wetu wa ujenzi chini ya JKT, taarifa yenu nimeipokea na niamini mpaka tarehe 22 Julai, 2024 kila kitu kitakuwa tayari muhimu sasa tuongeze kasi ya ujenzi, tuongeze muda wa ujenzi mchana na usiku ili shughuli zote ziende vizuri na tunataka eneo hili liwe“smart” vile ambavyo itavutia” amefafanua Waziri Mkuu.

Awali akitoa maelezo kuhusu maandalizi hayo, Msanifu Mradi wa Uwanja wa Mashujaa Liberatus Mrema amesema kuwa ujenzi wa awamu ya kwanza umefikia asilimia 84% na unatarajiwa kukamilika tarehe 22 Julai, 2024.

Akieleza kuhusu umuhimu wa kuadhimisha siku ya Mashujaa Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi amesema kuwa “Sherehe za mashujaa ni mahsusi zilizowekwa na nchi yetu kwa ajili kuenzi na kukumbuka mchango wa watu mbalimbali ambao wamejitolea kwa ajili ya uhai wa taifa letu”.

Dkt. Yonazi ameongeza kuwa, mashujaa hao ni watu mbalimbali ambao wamepigana vita au wametoa mchango kwa namna moja ama nyingine ili kulifanya Taifa la Tanzania kuwa namna lilivyo, kwa ulinzi wake, kwa usalama wake lakini pia kwa maendeleo ya uchumi.


 

NAIBU WAZIRI UMMY AKAGUA MAANDALIZI MAADHIMISHO YA SIKU YA MASHUJAA 2024

Na Mwandishi wetu - Dodoma

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga leo tarehe 10 Julai, 2024 amekagua maandalizi ya Maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa inayotarajiwa kufanyika tarehe 25 Julai, 2024 jijini Dodoma.

Mhe. Ummy ameridhishwa na maandalizi hayo yanayoendelea na anaimani kwamba maandalizi hayo yatazidi kufanyika vizuri na yatakamilikalika kwa wakati.

Aidha, maadhimisho hayo yatashirikisha gwaride la Majeshi ya Ulinzi na Usalama lenye vikosi vitano ambavyo ni Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Jeshi la Poliosi, Jeshi la Magereza pamoja na jeshi la Uhamiaji.

Awali akitoa maelezo kuhusu maandalizi hayo, Mkurugenzi wa Kitengo cha Maadhimisho na Sherehe za Taifa Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Batholomeo Jungu amebainisha kuwa, maadhimisho hayo yatatanguliwa na uwashaji wa Mwenge siku ya tarehe 24 Julai, 2024 usiku ambapo Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma.

Maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa yatafanyika tarehe 25 Julai, 2024 jijini Dodoma ambapo Mgeni Rasmi wa Maadhimisho hayo anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mheshimiwa. Samia Suluhu Hassan.


 

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa