Home » » Serikali yafanya tathmini uhaba wa chakula nchini

Serikali yafanya tathmini uhaba wa chakula nchini

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
 
Serikali inatarajia kutoa taarifa rasmi juu ya upungufu wa chakula katika baadhi ya maeneo hapa nchini baada ya kumalizika kwa kikao  cha kuchambua  taarifa ya upungufu wa chakula  iliyosomwa na  Waziri Mkuu, Mizengo Pinda wakati akiahirisha Bunge mjini Dodoma wiki iliyopita.
Akizungumza na NIPASHE jana, Kaimu Mkurugenzi Idara ya Usalama wa Chakula katika Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, Josephine Juma  alisema hivi sasa timu ya wataalamu iko mkoani Dodoma kuchambua taarifa hiyo.

Alisema timu hiyo inaundwa na maafisa kutoka Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika kwa kushirikiana na wa Ofisi ya Waziri Mkuu Kitengo cha Maafa pamoja na wadau wengine wa maendeleo.

Alisema  lengo la kupitia na kuchambua taarifa hiyo ni kubaini idadi kamili ya kaya na watu wenye uhitaji wa chakula  kwa ajili ya kutafuta ufumbuzi katika kipindi chote watakachokuwa na upungufu.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mawasiliano wa wizara  hiyo, Richard  Kasuga, alisema tathmini ya upungufu wa chakula ni endelevu na imekuwa ikifanywa kila mwaka kwa ajili ya kubaini maeneo yenye uhaba wa chakula.

Alisema sababu kubwa ambayo imekuwa ikichangia  uhaba wa chakula katika baadhi ya maeneo hapa nchini ni pamoja na kutokuwapo kwa mvua za kutosha.

Akisoma hotuba ya kuahirisha Bunge la 10 Mkutano wa 13 mkoani Dodoma,  Waziri Mkuu Pinda alisema halmashauri 61 zinatarajiwa kukumbwa na uhaba wa chakula.

Aliitaja mikoa ya halmashauri zitakazokabiliwa na uhaba huo kuwa ni, Manyara, Shinyanga, Simiyu, Arusha, Dodoma, Lindi, Tanga, Singida, Mara, Morogoro, Kilimanjaro, Mwanza, Pwani, Mtwara, Kigoma na Tabora.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa