Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Wengi tumezoea kusikia kuwa mchakato wa utengenezaji wa
rangi, hauwezi kukwepa matumizi ya kemikali. Huo siyo ukweli, Mtanzania
Saidi Mjulishi amepewa tuzo na Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech)
ikimtambua kama mgunduzi wa rangi maalumu za asili zisizotumia kemikali.
Sifa moja kubwa ya bidhaa nyingi anazotumia
mwanadamu ama zinatokana na kemikali au mchakato wa utengenezaji wake
unahusisha matumizi ya kemikali.
Hivi ndivyo ilivyo kwa bidhaa mbalimbali muhimu kwa mwanadamu, vikiwamo vyakula, vinywaji na vinginevyo.
Hapa nchini wakati sayansi na teknolojia
vikielezwa kushika kasi, Mtanzania aitwaye Said Mjulishi ameingia katika
orodha ya wagunduzi kwa kubuni rangi maalumu za asili anazosema hazina
mchanganyiko wowote na kemikali kama ilivyo kwa rangi nyingine za
viwandani.
Katika mahojiano na mwandishi wetu, Maimuna
Kubegeya, Mjulizi ambaye ni kitaaluma ni mhandisi, anaelezea kwa kirefu
ugunduzi wa rangi hizo anazosema zina uwezo mkubwa wa kuboresha
mazingira.
Swali: Tueleze historia yako kwa kifupi
Jibu: Mimi ni mwenyeji wa Mkoa wa
Kagera. Baada ya kumaliza elimu yangu ya msingi nilijiunga na
kilichokuwa Chuo cha Ufundi cha Dar es Salaam, sasa kinafahamika kwa
jina la Dar es Salaam Insititute of Technology (DIT).
Nikiwa chuoni nilisomea kozi ya uhandisi. Baada ya
kumaliza niliajiriwa na kampuni ya Said Salim Bakhresa na kufanya kazi
katika kitengo cha mashine za kusaga.
Swali: Ilikuwaje ukaangukia kwenye ugunduzi hasa huu wa rangi za asili?
Jibu: Ni historia ndefu, lakini
kwa kifupi ni kwamba ule ujuzi wangu nilionao katika masuala ya
uhandisi, umekuwa ni chanzo cha kuniongezea udadisi. Unajua unapokuwa
na kiu ya kutaka kujua jambo, inakuwa ni rahisi kupata suluhisho. Kwa
muda mrefu nimekuwa nikishuhudia watu wakipata athari wanapotumia rangi
zenye kemikali.
Wako watu wangu wa karibu walioathiriwa na hata
kupata matatizo kadhaa yakiwamo ya ngozi na hata mzio kutokana na
matumizi ya rangi zenye kemikali.
Baada ya kufikiria kwa kina nikapata wazo la
kufanya utafiti kupitia miti ili nione kama naweza kugundua rangi
zisizokuwa na athari kiafya.
Swali: Nini kikafuata baada ya kuamua kufanya utafiti huo?
Jibu: mwaka 2006 nikaanza mradi
wa kwanza wa utafiti kwa kutumia miti kadhaa na baadaye nikafanikiwa
kugundua miti aina mbili ambayo ni mfumbo na mtuntu. Mwaka 2012, baada ya kushuhudia kazi zangu, Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech) ilinitangaza rasmi kama mgunduzi wa rangi.
Swali: Rangi za aina gani ulizogundua kupitia utafiti huo?
Jibu: Kwa sasa nimegundua rangi
za aina mbili na bado naendelea na utafiti wa rangi nyingine. Rangi
zilizopo sasa ni zambarau na hudhurungi. Rangi hizi zinaweza kutumika
kwenye nguo, lakini hii ya hudhurungi pia inaweza kutumika kwenye mbao
kama dawa ya kuulia wadudu au rangi tu ya kawaida hasa kwa mbao nyeupe.
Sifa ya rangi hizi ni kuwa zina uwezo wa
kupambana na wadudu wanaobungua mbao, hivyo ni suluhisho tosha kwa wale
wanaohitaji kupaka rangi kwenye mbao za kujengea.
Swali: Ukoje mwitikio wa jamii kuhusu matumizi ya rangi ulizogundua?
Jibu: Kwa sasa tuko katika
kampeni ya kuhakikisha watu wengi wanaelewa umuhimu kutumia rangi hizi.
Kwa kushirikiana na wadau kama Shirika la Viwanda Vidogo Vidogo (SIDO)
na Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech), tumekuwa tukiendesha mafunzo
kuhusu matumizi yake.
Kwa mfano, tayari tumeshaangaza kutoa mafunzo ya
utengenezaji wa batiki kwa kutumia rangi hizi. Kimsingi, rangi hizi
hazina athari yoyote kiafya tofauti na zile zilizozoeleka. Hadi sasa
tumeshawafundisha watu zaidi ya 60 katika awamu ya kwanza ya mafunzo,
mipango yetu ni kuwafikia watu wengi zaidi.
Kwa upande wa rangi za mbao, tayari tumeanza
kusambaza katika maduka kadhaa ya Dar es Salaam. Aidha, tuna mpango wa
kwenda mbele zaidi na kuwafikia Watanzania wengi.
Swali: Huoni kuwa ni uharibifu wa mazingira kutumia miti kutengeneza rangi?
Jibu: Miti hii tunayotumia kwa
kawaida huwa na tabia ya kujivua magamba na hii ndiyo sifa ya pekee ya
miti hii. Tunachotumia ni magamba yake hivyo hatuna haja ya kukata
miti, tunachokitumia kama malighafi yetu kubwa ni yale magamba. Halafu
hata mabaki bado ni rafiki wa mazingira, kwani yanaweza kutumika kama
kuni au hata mbolea.
Swali: Una wito gani kwa Serikali na jamii kwa jumla
Jibu: Serikali itoe msaada kwa wagunduzi kwani kwa
kufanya hivyo tutaweza kukuza teknolojia yetu. Kwa upande wa wananchi,
nawasihi wahamasike kutumia vitu vinavyogunduliwa na watafiti wa ndani.
Hii itasaidia kuwapa hamasa ya kugundua mambo mengi zaidi.
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment