Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Rais Jakaya Kikwete.
Kasi iliyoonyeshwa na Bunge lililopita katika
kuisimamia Serikali kiasi cha kumlazimu Rais Jakaya Kikwete, kufanya
mabadiliko ya baraza lake la mawaziri zaidi ya mara nne, inatajwa kuwa
chanzo cha kuibuka kwa vita inayoonekana wazi ya kutaka kudhibiti
mhimili huo muhimu wa dola.
Wakizungumza na Nipashe kwa nyakati tofauti jana, baadhi ya
wachambuzi wa masuala ya siasa walisema mkanganyiko ulioibuka kuhusiana
na uteuzi wa kamati mbalimbali za chombo hicho ni ishara ya wazi kwamba
kuna vita ya kutaka kudhibiti utendaji wa chombo hicho, ambayo mshiriki
wake mkuu ni serikali ya awamu ya tano.
Wakieleza zaidi, baadhi ya wachambuzi hao wamedai kuwa mwenendo wa
Bunge la 11, kuanzia mchakato wake wa kumpata Naibu Spika na hadi sasa
katika uteuzi wa wajumbe wa kamati za Bunge, unaashiria kuwa serikali
imepania kupunguza makali ya chombo hicho ambacho katika miaka kumi
iliyopita kimejitahidi kwa kiasi kikubwa kutekeleza wajibu wake wa
kuisimiamia serikali kiasi cha kuibua masuala kadhaa yaliyotikisa baraza
la mawaziri, mfano ukiwa ni kashfa za Richmond, uchotwaji wa Sh.
bilioni 133 za Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) iliyokuwa Benki
Kuu (BoT), Operesheni Tokomeza na pia uchotwaji wa mabilioni ya fedha
kupitia Akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa pia BoT.
Mwishoni mwa wiki, Spika wa Bunge, Job Ndugai, alitangaza wajumbe
wanaounda kamati mbalimbali za chombo hicho huku mjadala ukiibuka
kuhusiana na uamuzi wa kutowarejesha baadhi ya wabunge walioitikisa
serikali kutokana na kuibua kwao mambo kadhaa kupitia kamati
walizokuwamo. Wabunge wengi waliokuwa maaarufu wamejikuta wakikosa
nafasi katika kamati mbalimbali walizokuwapo awali ikiwamo nyeti ya
Hesabu za Serikali na Mashirika ya Umma (PAC), na kisha wengi wao
kuwekwa katika Kamati ya Huduma za Jamii.
Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, ni miongoni mwa wabunge
machachari waliojikuta wakiwekwa katika Kamati ya Huduma za Jamii,
wengine wakiwa ni Peter Serukamba ambaye awali alikuwa katika Kamati ya
Miundombinu na Tundu Lissu aliyeng’ara wakati alipokuwa katika Kamati ya
Katiba na Sheria na sasa kuwekwa pia katika kamati hiyo ya Huduma za
Jamii.
Mmoja wa wachambuzi hao alidai kuna uwezekano Bunge la sasa
linaelekea kuwa kibogoyo kwani zipo ishara kwa serikali kuingiza
ushawishi wake.
“Kama utakumbuka, mchakato wa kumpata Naibu Spika ulizua maneno kwa
sababu licha ya Dk. Tulia (Ackson) kuwa na sifa zote, bado kuna ukweli
kuwa hakuwahi kuwa mbunge hapo kabla. Hivyo, kama siyo Rais kumteua kuwa
Mbunge na muda mfupi baadaye kuchukua fomu za kugombea unaibu spika,
maana yake, isingetarajiwa kwa mtu asiyewahi kuwa mbunge leo hii kuwa
mtu wa pili kwa madaraka bungeni. Hii ni dalili kwamba kulikuwa na
uungwaji mkono wa serikali. Na hili la uteuzi wa wajumbe wa kamati ni
dalili nyingine kwamba tunakoelekea Bunge litakuwa kibogoyo. Tuombee
isiwe hivyo,” aliongeza mchambuzi huyo ambaye ni mhadhiri mwandamizi.
Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania
(THRDC), Onesmo Olengurumwa, alisema uteuzi wa wajumbe wa kamati za
Bunge ni wa kushangaza kwa kuwa wabunge machachari wamepelekwa kwenye
kamati ambazo hazisimamii wizara nyeti.
Alisema serikali ya Dk. John Magufuli, imejitambulisha kwa
ufuatiliaji wa karibu wa utendaji wa serikali na kuhoji mambo
mbalimbali, lakini inashangaza kuwa hapo hapo, wabunge ambao
wanafahamika kwa ufuatiliaji mzuri wa mambo wamewekwa kando ya kamati
nyeti kama PAC.
“Tunapata shaka…tulitarajia tuwe na wenyeviti wa kamati wenye
kuibua mambo, yeye (Rais) pekee hawezi kufika kila mahali, anahitaji
wabunge wafuatiliaji,” alisema, akiongeza kuwa uteuzi wa kamati za Bunge
la 11 umefanyika kama vile hakuna chama cha upinzani chenye nguvu
bungeni na kutoa taswira kuwa bado kuna bunge la mfumo wa chama kimoja
kwa kutafuta namna ya kuwafunga midomo wabunge machachari waliowezesha
kuibuliwa kwa maovu mengi kupitia kamati walizokuwapo awali.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika lisilo la kiserikali la Sikika,
Irenei Kiria, alisema udhaifu upo kwa wenyeviti wa baadhi ya kamati na
jambo hilo ni hatari kwa uimara wa Bunge.
“Ukishakuwa na kamati yenye mwenyekiti hafifu, ni wazi kuwa
watashindwa kuhoji Wizara husika. Hii itafanya tuwe na Bunge lisiloweza
kuiwajibisha serikali bali kuwa na Bunge la kuisaidia serikali,”alisema.
Mhadhiri kutoka Chuo kikuu cha Iringa, Essau Ntabindi, alisema kwa
mtazamo wake, uteuzi wa wajumbe katika kamati za bunge unaweza kuelezwa
kuwa wa njia mbili, moja ikiwa ni kisiasa na pili ikawa ni uteuzi wa
kawaida.
Alisema serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Magufuli
inaonyesha imedhamiria kuleta maendelea nchini, hivyo kuwaweka baadhi ya
wabunge ambao huibua hoja nzito bungeni kwenye kamati ya huduma za
jamii kunaweza kukawa na sababu ya kuimarisha sekta hizo.
Kwa mfano, alisema kuwaweka Zitto Kabwe na Serukamba katika kamati
ya huduma za jamii pia kunaweza kukasaidia kuboresha sekta hizo, ikiwamo
sekta ya afya na elimu na hilo ni jambo jema.
Aidha, alisema njia ya pili, ni kuwapo kwa mbinu ya serikali
kulipoza bunge ili isiingie katika mtikisiko wa kisiasa kama ilivyotokea
katika awamu ya serikali ya nne.
SARAKASI KAMATI ZA BUNGE
Awali, habari ambazo Nipashe ilizipata, zilieleza kwamba baadhi ya
wabunge ambao walikuwa machachari kwa kuibua mambo mengi mazito katika
Bunge la 10 na makada waliowahi kutikisa ndani ya Chama Cha Mapinduzi
(CCM) kwa hoja mbalimbali, walijikuta wakiondoshwa kwenye kamati
walizokuwa wamepangiwa awali kutokana na shinikizo kutoka kwa baadhi ya
vigogo.
Ilidaiwa kuwa baadhi ya wabunge waliohamishwa kwenye kamati
walizokuwa wamepangiwa awali siku moja ama saa chache kabla ya majina
yao kutangazwa ni pamoja na Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe, ambaye
awali alipangwa katika Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) na baadaye
kupelekwa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii.
Taarifa zilidai kuwa Zitto alipangwa pia kwenye kamati ya PAC,
lakini baadaye akapelekwa Ardhi, Maliasili na Utalii, kisha akahamishiwa
tena Kamati ya Bajeti kabla ya kufikishwa kwenye Kamati ya Huduma za
Maendeleo ya Jamii.
Ilielezwa zaidi kuwa Mbunge wa Ilala, Mussa Zungu, awali alipangwa
kwenye kamati ya Uwekezaji na Mitaji kabla ya kupelekwa kwenye Huduma za
Maendeleo ya Jamii.
Kwa upande wake, Mbunge wa Kigoma Kasikazini, Serukamba, awali
alipangwa kwenye kamati ya Viwanda na Biashara kabla ya kujikuta pia
kwenye kamati ya Huduma za Maendeleo ya Jamii.
Kadhalika, Mbunge wa Shinyanga Mjini, Stephen Masele, awali
alipangiwa katika Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kabla
baadaye kujikuta kwenye Kamati ya Bajeti.
Hata hivyo, akizungumza na Nipashe jana, Spika wa Bunge Job Ndugai,
alikanusha madai ya kuwapo kwa shinikizo kutoka kokote bali,
kilichotokea ni kutekeleza uamuzi wa Bunge kuhakikisha kuwa wabunge wa
zamani hawapangwi katika kamati walizowahi kuzitumikia awali.
Alisema katika Bunge la sasa, asilimia 80 ni wapya huku asilimia 20
wakiwa wa zamani na kwamba hivi sasa, wabunge wote wa zamani wako
kwenye kamati nyingine na siyo walizokuwapo awali.
"Isifike mahali kamati fulani ikaonekana ni ya mtu fulani peke
yake, kwa hiyo hakuna aliyerudi kamati ya zamani," alisema Ndugai.
KASHFA ZILIZOTIKISA BUNGE
Kashfa ya mkataba tata wa kampuni ya kufua umeme ya Richmond
iliibuliwa bungeni mwaka 2006 na kuvunja baraza lote la mawaziri baada
ya aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa kulazimika kujiuzulu baada ya
kutakiwa ajipime kutokana na mazingira ya kashfa hiyo.
Mwaka 2008, Bunge liliibua kashfa ya EPA iliyoitikisa vilivyo
serikali. Baadaye, mabadiliko ndani ya Baraza la Mawaziri yalimuweka nje
aliyekuwa Waziri wa Fedha, Zakia Maghji huku Gavana wa BoT, Daudi
Balali (sasa marehemu) akifutwa kazi.
Mei 2012, wakati ilipotolewa Ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG) na kujadiliwa bungeni, ulitokea mtikisiko mkubwa
uliowang’oa mawaziri sita na manaibu wawili.
Makali ya Bunge yaliichachafya tena Serikali ya Rais Kikwete,
Desemba 2013 kutokana na kashfa ya Operesheni Tokomeza Ujangili. Baraza
la Mawaziri lilitikiswa na mawaziri kadhaa waling’olewa.
Novemba 2014, ripoti ya PAC bungeni baada ya kuchambua ile ya CAG,
iliyochunguza miamala ya Akanti ya Tegeta Escrow ilisababisha mtikisiko
mkubwa na mawaziri kufutwa kazi, ambao ni aliyekuwa Waziri wa Nishati na
Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment