Home » » HATI YA MUUNGANO YATINGA OFISI ZA BUNGE

HATI YA MUUNGANO YATINGA OFISI ZA BUNGE

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu),Stephen Wasira.
Hati  ya Muungano licha ya kupokelewa katika ofisi za Bunge kutoka Ikulu, haijasambazwa kwa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kwa sababu za kisheria.
Nakala ya nukushi (fax) ya hati hiyo, ilifikishwa kwenye Ofisi za Bunge mjini hapa juzi na kujadiliwa na Kamati ya Uongozi, ambayo Mwenyekiti wake ni Samuel Sitta.

Katibu wa Bunge Maalumu, Yahya Khamis Hamad, aliliambia NIPASHE jana na kufafanua kuwa kamati ilimshauri Mwenyekiti kwamba, wasubiri nakala iliyothibitishwa kisheria, badala ya kugawa kivuli cha nukushi (fax) iliyopokelewa.

Alisema mashaka hayo yalitokana na nakala za kwanza zilidaiwa ni feki ama zilighushiwa jambo, ambalo hawataki litokee tena.

Aliongeza kuwa nakala iliyothibitishwa na mahakama ndiyo itakayosambazwa ili kuondoa tashwishwi zinazoweza kuibuka kutokana na utata kughubika nakala ya hati hiyo.

Hamad alisema huenda nakala zitapatikana leo na kusambazwa kwa wajumbe wakati wowote kabla ya mapumziko ya Sikukuu ya Pasaka.
Juzi asubuhi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wasira, alitangaza bungeni kwamba, hati hiyo ipo na kwamba, ingewasikishwa kwa Mwenyekiti wa Bunge hilo ndani ya siku mbili.

Alitoa maelezo hayo baada ya Mjumbe John Mnyika, kuomba mwongozo wa kumkumbusha Mwenyekiti kuhusu ombi alilowasilisha kuomba apatiwe hati hiyo limefikia wapi na ndipo Wasira alipotoa taarifa hiyo.

Siku hiyo, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, aliionyesha hati hiyo kwenye vyombo vya habari jijini Dar es Salaam ikiwa ni nakala.

Hati hiyo ilizua mjadala tangu wajumbe wa kamati 12 za Bunge hilo walipoanza kuzichambua, kuzijadili na kuziamua kwa kura sura mbili ya kwanza na ya sita za rasimu ya katiba zinazohusu Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na muundo wa Muungano.

Kilicholeta utata ni maelezo kuwa msingi wa rasimu hiyo ni hati za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na wajumbe kutaka kuiona kuthibitisha uwapo wa makubaliano ya Muungano.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa