Home » » MATUSI YA NGUONI,MIPASHO,JAZBA VYATAWALA MJADALA WA MUUNGANO

MATUSI YA NGUONI,MIPASHO,JAZBA VYATAWALA MJADALA WA MUUNGANO

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Dk. Hamis Kigwangalla.
 
Mjadala  wa sura ya kwanza na ya sita za Rasimu ya Katiba, ulianza jana jioni kwa baadhi ya wajumbe kuzungumza kwa hisia kali, mipasho, matusi na kukashifiana.
Miongoni mwa waliozungumza kwa hisia kali na ni Dk. Hamis Kigwangalla, (pichani) ambaye alizishutumu tume zote, ambazo ziliwahi kuundwa kwa ajili ya kukusanya maoni kuhusu muundo wa Muungano.

Dk. Kigwangalla alidai kuwa tume hizo za ujanja ujanja na kinyemela na ndiyo maana zilipendekeza muundo wa serikali tatu.

 Alisema mapendekezo ya tume zote ya Jaji Nyalali, Jaji Kisanga na ya Jaji Warioba  wake uhalali unakosekana.

Alitoa mfano kuwa tume ya Nyalali iliyoundwa mwaka 1990 ilikuwa ya ujanja ujanja na na kinyemela na kwamba, haikuwa na uhalali kutokana na wajumbe wake kugawanyika,

Alidai kutokana na mgawanyiko, wajumbe walishindwa kuafikiana na kumlazimisha Mwenyekiti, Jaji Nyalali kupiga kura ya turufu ya kuamua pamoja na kuwa alikuwa na msimamo wa serikali tatu.

Kigwangalla pia alidai kuwa tume hizo zilikuwa zinawaita watu wachache na kuwahoji faragha na kwa usiri na kutoa mfano kuwa Tume ya Jaji Kisanga walikuwapo Nyalali,
Kificho na Mwanasheria Mkuu wa kwanza wa Zanzibar, Walfang  Dourado, na walichokipata ni kile kile kwa kuwa kila mmoja alikuwa na upande wake.

Aliongeza kuwa mwendelezo wa tume hizo ni kuvuruga na limekuwa ni tatizo nchini.

Wakati akiendelea kuzishutumu tume hizo, Mjumbe John Mnyika aliomba fursa ya kutoa taarifa na kufafanua kuwa tume ya Nyalali ilikuwa na wajumbe 22 na kwamba, wajumbe 13 waliunga mkono serikali tatu na tisa hawakukubali.

 “Wajumbe 13 walipendekeza serikali tatu na tisa serikali mbili na siyo kweli kuwa Mwenyekiti Nyalali alipiga kura ya turufu,” alisema Mnyika.

 Mjumbe mwingine aliyechangia kwa hisia kali, ni Felix Mkosamali, ambaye aliwashambulia baadhi ya viongozi wakuu wa kitaifa kwamba, ni vigeugeu akidai kuwa baadhi yao waliwasilisha maoni ya taasisi zao katika tume ya Warioba wakipendekeza serikali tatu, lakini ghafla wamegeuka na kutetea serikali mbili.

MATUSI YA NGUONI
Mjumbe Asha Bakari wa kundi la walio wengi, alianza kumsakama mjumbe Ismail Jussa Ladhu kwa matusi makali.

Alimweleza Jussa kuwa CCM haitakubali Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) ichukuliwe, kwani haikupatikana kwa karatasi ni nchi iliyopinduliwa.

“Namwambia Jussa kuwa si kweli kuwa anaionea huruma nchi hii,” alisema na kuongeza kwa Kipemba hawa ni “wasaidaka si wapundaka bali ni wapumbaka,” alisema na Bunge kuhitaji tafsiri, ndipo akaeleza kuwa maana yake ni asiye na fadhila hafadhiliki naye ni Jussa.

Mjumbe huyo alidai kuwa Jussa alisomeshwa na SMZ kwenye vyuo vikuu vya Tanzania, lakini Jussa alipinga kuwa alisoma Uingereza.

Kugombana huko kulisababisha kuwapo maombi mengi ya mwongozo mengi yakimtetea Jussa
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa