Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Balozi Amina Salum Ali akizungumza na waandishi
wa habari jijini Dar es Salaam jana wakati akitangaza nia yake ya
kugombea kiti cha urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Picha:
Hellen Mwango
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam
kuhusu nia yake hiyo, mwanasiasa huyo ambaye pia ni Balozi wa Kudumu wa
Umoja wa Afrika (AU) katika Umoja wa Mataifa (UN), alisema wanawake
wamekuwa wanyonge kugombea nafasi za juu za uongozi kwa kukosa fedha,
lakini sasa ni wakati mwafaka kwao kujiamini katika jamii kwani uongozi
siyo fedha bali ni uzalendo, kujikubali na kujiamini.
“Nimeona nina uzalendo, ninajiamini na ninaweza kuifikisha nchi
yangu katika uchumi wa kwanza kwa kutumia rasilimali zetu zikiwamo gesi,
mafuta, kilimo na utalii. Ninajiamini kwamba wakati wangu umefika
kuwaongoza Watanzania wenzangu kwa kushika nafasi za juu,” alisema
mwanasiasa huyo mkongwe.
Amina ambaye aliwahi kushika nafasi za juu za uongozi Zanzibar na
Tanzania Bara, ukiwamo uwaziri wa fedha Zanzibar, alisema serikali
inatambua mchango wa wanawake katika jamii hivyo kupewa nafasi kubwa
kama vile ujaji na uhakimu ili kuongeza zaidi ufanisi wao kiutendaji.
“Wanawake wengi wanaogopa kujitokeza wakihofia kugombea nafasi za
juu za uongozi kwamba kunahitaji fedha hivyo wanaishia kuwa wanyonge.
Siyo kweli, wajitokeze kwa wingi ili kitimiza ndoto za kuwajibika kwa
taifa letu,” alisema.
Kwa mujibu wa mwanasiasa huyo, wanawake wamepigana sana dhidi ya
mfumo dume na kwamba baada ya miaka 20 ya maazimio ya Mkutano wa Dunia
wa Wanawake uliofanyika mjini Beijing, China mwaka 1995, hali kwa sasa
imebadilika na wanawake wanapewa nafasi mbalimbali za uongozi.
Alisema sheria hazitoshelezi kumlinda mwanamke, lakini mfumo dume
umepungua kwa kiasi kikubwa hata kama haijafikia asilimia 50 kwa 50.
“Jambo kubwa kwa mwanamke ni kujiamini katika mambo yote… wanawake
wa Tanzania hatuna utaratibu wa kuchangiana katika harakati za uchaguzi.
Utaratibu wa mwanamke kupata fedha za mitaji kwa hapa nchini bado mgumu
hasa katika mabenki lakini tusiogope. Mimi nina amini ninaweza
kuiongoza jamii yetu,“ alisema Balozi Amina.
Balozi Amina ametangaza ni ya kuwania nafasi hiyo kubwa kuliko zote
nchini wakati kesho vikao vikao vya juu vya maamuzi vikitarajiwa kuanza
kwa ajili ya maandalizi ya mchakato wa uteuzi wa wagombea wa CCM kwa
ajili ya uchaguzi mkuu wa udiwani, ubunge na urais Oktoba, mwaka huu.
Vikao hivyo ni Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec).
Kesho itaanza CC na kufuatiwa na Nec ambayo inahitimisha mchakato huo
Jumapili ijayo.
Baadhi ya makada wameshatangaza nia ya kuwania nafasi hiyo na wengine wanatajwa.
Waliotangaza nia ni Waziri Mkuu, Mizengo Pinda; Waziri wa Maliasili
na Utalii, Lazaro Nyalandu; Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia, January Makamba; Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba;
Mbunge wa Nzega, Dk. Khamis Kigwangallah na Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais (Kazi Maalum), Prof. Mark Mwandosya.
Makada wanaotajwa kugombea nafasi ya hiyo kupitia chama hicho ni
Waziri wa Chakula, Kilimo na Ushirika, Steven Wasira; Waziri wa Ujenzi,
Dk. John Magufuli; Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta; Waziri wa Katiba
na Sheria, Dk. Asha Rose Migiro na Spika wa Bunge, Anna Makinda.
Wengine ni mawaziri wakuu wastaafu, Fredrick Sumaye na Edward
Lowassa; Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard
Membe; Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja na Mbunge wa Songea Mjini,
Dk. Emmanuel Nchimbi.
Balozi Amina alihitimu Chuo Kikuu cha New Delhi (India) - shahada
ya kwanza ya uchumi (B.A), mwaka 1079, amehitimu Institute of Management
Pune, India - Diploma ya utawala wa mambo ya fedha na utafiti wa
uendeshaji mwaka 1980, pia mwaka 1981 alihitimu Chuo Kikuu cha Pune,
India - (Symbiosis College of management) -MBA in Marketing (Masoko) na
mwaka 1983 Chuo Kikuu cha Helsinki, Finland - Diploma ya utafiti wa
masoko na uuzaji wa bidhaa nje (mafunzo maalum ya PRODEC).
NYADHIFA ALIZOPITIA
Mwaka 1981 hadi 1982 Mchumi Mwandamizi -Tume ya Mipango Zanzibar,
mwaka 1982 hadi 1983 Mkurugenzi Biashara za Nje - Wizara ya Biashara ya
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na mwaka 1983 hadi 984 Katibu Bodi ya
Biashara Zanzibar-Wizara ya Biashara Zanzibar.
Nafasi nyingine ni, mwaka 1984 hadi 1985, Mchumi Mwandamizi - Tume
ya Mipango, Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Zanzibar, mwaka 1985 hadi
1990- Mbunge Bunge la Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, mwaka 1985 hadi
1986- Naibu Waziri wa Fedha Wizara ya Fedha na Mipango Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mwaka 1986 hadi 1989- Waziri wa Nchi
,Wizara ya Mambo ya Nje.
Nyingine ni, mwaka 1989 hadi 1990- Waziri wa Nchi Wizara ya Fedha
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mwaka 1990 hadi 2000
-Mbunge Bunge la Jamhuri ya Muungano Tanzania, Mjumbe wa Baraza la
Wawakilishi Baraza la Wawakilishi Zanzibar, mwaka 2001 hadi 2005-
Waziri wa Fedha, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar , Mjumbe wa Tume ya
Mipango Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, mwaka 2005 hadi 2006- Mjumbe
Baraza la Wawakilishi .
Nyingine ni, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Kiongozi Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar, mwaka 2006 - Mwakilishi wa Kudumu wa Umoja wa Afrika
(AU) kwenye Umoja wa Mataifa.
UZOEFU KATIKA CHAMA
Mwaka 1968 alijiunga na Umoja wa Vijana wa ASP (ASP Youth League) na kuendelea na uanachama hadi kuzaliwa kwa CCM mwaka 1977.
Mwaka 1977 alijiunga na Chama Cha Mapinduzi baada ya kuunganishwa
kwa vyama vya ASP na TANU na kuzaliwa CCM, mwaka 2006 alikuwa Mjumbe
wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi hadi alipolazimika
kujiuzulu kufuatia kuteuliwa kuwa Mwakilishi wa Kudumu wa Umoja wa
Afrika (AU) katika Umoja wa Mataifa.
Nafasi nyingine katika chama ni mjumbe wa kamati mbalimbali
zilizoundwa na CCM kwa kipindi chote alichokuwa Mjumbe wa Halmashauri
Kuu ya CCM na Mlezi wa chama Mkoa Morogoro.
Mlezi wa Jumuia ya Vijana Wilaya ya Mjini mwaka 1992 hadi 2006 na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM hadi alipoteuliwa AU.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment