Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Kuumbuana huko kuliegemea taarifa ya Mbunge wa
Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu kuwalipua baadhi ya mawaziri na
wabunge kwa kuchota fedha katika mfuko huo.
Sakata hilo lilienda mbali zaidi baada ya Kiongozi
wa Kambi Rasmi ya Upinzani, Freeman Mbowe kulipuliwa kuwa anadaiwa
zaidi ya Sh1 bilioni na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) na
tayari kuna hati ya kumkamata.
Hata hivyo, Mbowe alipoulizwa jana ofisini kwake
bungeni alisema: “...Sina taarifa yoyote ya kukamatwa. Nipo hapa bungeni
mbona sijakamatwa? Muulizeni aliyesema awaeleze imetolewa lini na
nani,” alisema Mbowe.
Wabunge hao walianza kuumbuana baada ya Mbunge wa
Mbinga Magharibi (CCM), John Komba kutaka mwongozo wa Spika, akidai
Lissu alimtaja kuwa naye ni miongoni mwa wabunge waliochota fedha LAPF.
“Kati ya wabunge hao wanaofilisi mashirika ya
umma, mimi sikumbuki wala sijui LAPF iko wapi wala ofisini kwa
mkurugenzi wake wala kwa mfanyakazi wake na sijachukua fedha yoyote
LAPF,” alisema.
Akionyesha kukerwa, Komba alisema anachokumbuka
Mfuko wa Maendeleo wa Nyanza ambao ni wadau wa LAPF waliomba msaada wa
kununua boti na walipewa Sh1.5 milioni... “Leo Lissu amekuja hapa
anawadanganya watu kuwa mimi nimehusika kutoa mapesa LAPF, sijui huu ni
wendawazimu ama nini?... Hizi ni siasa za majitaka kabisa naomba
mwongozo wako.”
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera,
Uratibu na Bunge), William Lukuvi alijibu hoja hiyo akisema wabunge
kuomba katika mashirika hayo si jambo la ajabu na kwamba yeye mwenyewe
aliomba kwa barua.
“Nilitaka kusema jambo hili si kubwa kiasi hiki kwa sababu fedha hizi zipo kwa ajili ya maendeleo...”
Hata hivyo, Lissu alipopewa fursa ya kujibu
alipigilia msumari akisema wabunge ndio wenye jukumu la kusimamia mifuko
hiyo na kwamba kama wanachukua fedha za mifuko hiyo wanaingia moja kwa
moja katika mgongano wa kimasilahi.
Aidha, alisema LAPF kwenye fungu hilo la msaada
kwa jamii inatoa kwa wabunge wa CCM pekee yake... “Kwa sababu wabunge
waliopewa fedha na nyaraka zake zipo ni hao wanaopiga kelele kina Pindi
Chana, Mwigulu Nchemba, wanaochukua fedha ni wa CCM tu.”
Alihoji kutumika kwa fedha za LAPF kununua jezi katika Jimbo la Chato linaloongozwa na Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli.
Pia alihoji Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ambayo hutengewa bajeti kununuliwa printa na kompyuta na LAPF.
Katika ufafanuzi wake, Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka alisema hakuna mtu anayepewa kitu bila kuomba.
“Kwenda kuomba misaada si tu katika mifuko ya
jamii tu, bali hata katika maeneo mengine kwa ajili ya maendeleo ya
majimbo yao inaruhusiwa. Katika mifuko ya jamii kuna sera ambazo
zimepanga kusaidia katika elimu, afya na masuala mengine ya kiuchumi
katika jamii.”
Kabaka alisema kama Lissu hajaomba msaada wa fedha hizo, asilazimishe kwamba mifuko hiyo inasaidia wabunge wa eneo moja.
“Si vizuri kusema kwa sababu ni masuala binafsi
lakini kuna waliokopa pesa kwenye mifuko ya jamii ukiwamo mfuko wa NSSF
ambao uko chini ya wizara yangu,” alisema Kabaka.
Alisema kuwa kuna hati ya kumkamata kumchukua mbunge aliyekopa bila kurejesha na kwamba hizo ndizo fedha ambazo si halali.
Wakati Kabaka akisema si vizuri kumtaja mbunge,
kelele za wabunge zilisikika zikimtaja Mbowe na Waziri wa Nchi Ofisi ya
Waziri Mkuu, Tamisemi, Hawa Ghasia, alimtaja Mbowe kuwa ndiye anayedaiwa
deni... “Mheshimiwa Kabaka hakumtaja lakini anayedaiwa ni Mbowe aende
akalipe deni hilo.”
Baadaye, Nchemba aliomba mwongozo wa Spika na
kueleza kuwa kanuni za Bunge zinamkataza mbunge kuzungumzia jambo ambalo
ana masilahi binafsi... “Mheshimiwa Lissu ni wakili lakini anamtetea
mfanyakazi aliyefukuzwa na LAPF kwa matumizi mabaya ya madaraka, leo
anaongea vibaya kuhusu shirika hilo, nadhani kuwa anakiuka.”
Alisema kanuni hiyo inamtaka aweke wazi kwanza masilahi yake katika mfuko huo kabla ya kuanza kuzungumza.
“Leo hii tunavyoongea baada ya Katibu Mkuu wa CCM
kupita jimboni kwangu na kukuta kijiji kimoja tu kina umeme nadhamiria
kuandika mradi mwingine niombe solar (umeme wa jua) nipeleke,” alisema.
Alisema kuwa ataomba fedha hizo kupitia mashirika
hayo ya kijamii na kwamba ni kazi ya mbunge kuhakikisha kuwa fedha
zinazotengwa kwa ajili ya kuisaidia jamii zinatumika ipasavyo.
Alitaka Bunge lichukue hatua kwa mbunge (Mbowe),
ambaye Kabaka alisema ana hati ya kukamatwa kwa kutokulipa zaidi ya Sh1
bilioni.
Hata hivyo, Ndugai alisema atatoa ufafanuzi kuhusu mwongozo huo baadaye.
Juzi, Mkurugenzi Mkuu wa LAPF, Eliud Sanga alisema
mfuko huo hulazimika kuwapa msaada zaidi wabunge wa CCM kwa kuogopa
kuwa wakiegemea kwa wa upinzani wataonekana wanawapigia debe.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment