Home » » LAITI FEDHA ZA BUNGELA KATIBA ZINGETUMIKA KATIKA SECKTA YA ELIMU

LAITI FEDHA ZA BUNGELA KATIBA ZINGETUMIKA KATIKA SECKTA YA ELIMU

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Nusu ya fedha zilizotumika katika Bunge la Katiba zingeweza kumaliza kabisa tatizo sugu la madeni ya walimu, ambayo Rais Jakaya Kikwete anasema ni kama Sh9 bilioni.Serikali inasema shule za msingi zinakabiliwa na uhaba wa madawati  1, 464,895. Fedha za Bunge la Katiba  zingeweza kununua madawati 300,000 kwa mwaka na kumaliza tatizo ndani ya miaka mitano.   

Kuanzia Februari 18 hadi Aprili 25 wajumbe wapatao 629 wa Bunge Maalumu la Katiba walikutana mjini Dodoma kwa lengo la kupitia Rasimu ya Pili ya Katiba iliyoandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Hizo ni siku 67 sawa na miezi miwili na zaidi, kipindi ambacho taarifa rasmi zinaonyesha kila mjumbe alikuwa akitia kibindoni Sh300,000 za posho kila siku.
Kwa kuangalia idadi ya wajumbe, fedha walizolipwa kwa kipindi chote ni Sh27 bilioni.  Pia Bunge hilo lilitanguliwa na matengenezo ya ukumbi wa Bunge.
Tunaelezwa kuwa gharama za matengenezo hayo zilifika Sh 8.2 bilioni. Taarifa hii ni kwa mujibu wa Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashilillah aliyoitoa kwa wanahabari mwezi Februari.
Kwa pamoja fedha za maandalizi ya ukumbi na posho zilifikia Sh 35.2 bilioni. Kiasi hiki cha fedha hakijumuishi gharama nyingine kadhaa za kuendesha Bunge hilo la aina yake katika historia ya nchi.
Bila shaka hizi ni fedha za umma, ni fedha za Watanzania walipakodi  na wala sio msaada kutoka nchi wahisani au marafiki.
Pamoja na gharama hizi kubwa, awamu ya kwanza ya Bunge hilo lililokuwa na mvuto kutokana na vitimbi na vioja vya wajumbe wake, linatuhumiwa kwa kukosa tija iliyokusudiwa. Baadhi ya watu wanasema fedha za walipakodi zimepotea bure bileshi.
Mhadhiri na mchumi kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dk Romanus Dimoso, anasema Bunge la Katiba halikukidhi haja iliyokusudiwa na kuwa fedha zilizotumika zingeweza kufanya makubwa kama zingepelekwa katika miradi ya maendeleo ya kijamii.
 “Kuna shule za kata nchi nzima hazina maabara, watoto wanafeli masomo ya sayansi. Pia  kuna tatizo la zahanati zisizokuwa na dawa, fedha hizo zingeweza kuondoa changamoto hizo kwa kiwango kikubwa,” anaeleza.
Matumizi katika elimu
Fedha zilizotumika  kuandaa Bunge la Katiba na posho walizolipwa wajumbe zingeweza kufanya makubwa kama zingepelekwa katika sekta ya elimu.
Kwa mfano, shule nyingi za umma hazina madawati na hii imekuwa changamoto tete inayoihangaisha Serikali. Serikali yenyewe imeshakiri kuwa madawati ni tatizo katika shule za umma hasa zile za msingi.
Akizungumza katika uzinduzi wa Wiki ya Elimu mkoani Dodoma wiki iliyopita, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alisema takwimu zinaonyesha shule za msingi pekee zinakabiliwa na uhaba wa madawati 1,464, 895.
Kunusuru wanafunzi na tatizo hili, Waziri Pinda akitumia makadirio ya kila dawati kutengenezwa kwa Sh 120, 000, anasema kama Serikali itatumia Sh 36 bilioni kwa mwaka, ina uwezo wa  kuziondolea aibu shule zetu kwa kuzisambazia madawati 300,000.
Kiasi hicho ni sawa na kulishughulikia tatizo kwa asilimia 20.5 kila mwaka. Baada ya miaka mitano, Pinda anasema hakutakuwa na tatizo la madawati shuleni.
 Makadirio ya hesabu za Waziri Mkuu ni zaidi  (takriban milioni 800) ya fedha zilizovunwa na wajumbe na pia kuboresha ukumbi wa Bunge (ambazo jumla yake ni Sh 35.2 bilioni).
Hata chini ya makadirio haya, Serikali inaweza kutumia Sh 24 bilioni kwa mwaka kutengeneza madawati 200,000 hivyo kutumia miaka saba kumaliza tatizo.
Miradi mingine               
Ukiondoa madawati, fedha za Bunge Maalumu la Katiba zingeweza kutumika katika miradi kadhaa muhimu ya elimu kama ujenzi wa nyumba za walimu na vyumba vya madarasa.
Kwa mfano, makadirio ya ujenzi wa nyumba moja kwa mujibu wa viwango vya Wizara Elimu na Mafunzo ya Ufundi ni kati ya Sh 30,000,00 (ikijengwa kwa ushirikiano kati ya serikali na wananchi) hadi 50,000,00 (ikijengwa kupitia mkandarasi).
Kwa kutumia makadirio ya juu ya Sh 50,000,000, Sh 35.2 bilioni zinaweza kutumika kujenga nyumba 704 kila mwaka. Si haba kiasi hicho ikiwa shule zitakazonufaika na ujenzi wa nyumba hizo ni zile zilizopo katika mazingira magumu.
Aidha, kwa kiwango hichohicho, au chini yake, serikali inaweza kujenga zaidi ya vyumba vya madarasa 1000 kila mwaka, na hatimaye kuwaokoa watoto wa Kitanzania wanaolazimika kusoma chini ya miti kwa kukosa madarasa.
Matumizi yasiyofuata kipaumbele
Ni kama ada kwa nchi hii kuona sehemu ya bajeti za vyombo mbalimbali vya serikali ikitumika nje ya miradi muhimu ya maendeleo. Sekta ya elimu haiwezi kujitenga na hali hii.
Chanzo:Mwananchi

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa