Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Kuanzia Februari 18 hadi Aprili 25 wajumbe wapatao 629 wa Bunge
Maalumu la Katiba walikutana mjini Dodoma kwa lengo la kupitia Rasimu ya
Pili ya Katiba iliyoandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Hizo ni siku 67 sawa na miezi miwili na zaidi,
kipindi ambacho taarifa rasmi zinaonyesha kila mjumbe alikuwa akitia
kibindoni Sh300,000 za posho kila siku.
Kwa kuangalia idadi ya wajumbe, fedha walizolipwa
kwa kipindi chote ni Sh27 bilioni. Pia Bunge hilo lilitanguliwa na
matengenezo ya ukumbi wa Bunge.
Tunaelezwa kuwa gharama za matengenezo hayo
zilifika Sh 8.2 bilioni. Taarifa hii ni kwa mujibu wa Katibu wa Bunge,
Dk Thomas Kashilillah aliyoitoa kwa wanahabari mwezi Februari.
Kwa pamoja fedha za maandalizi ya ukumbi na posho
zilifikia Sh 35.2 bilioni. Kiasi hiki cha fedha hakijumuishi gharama
nyingine kadhaa za kuendesha Bunge hilo la aina yake katika historia ya
nchi.
Bila shaka hizi ni fedha za umma, ni fedha za Watanzania walipakodi na wala sio msaada kutoka nchi wahisani au marafiki.
Pamoja na gharama hizi kubwa, awamu ya kwanza ya
Bunge hilo lililokuwa na mvuto kutokana na vitimbi na vioja vya wajumbe
wake, linatuhumiwa kwa kukosa tija iliyokusudiwa. Baadhi ya watu
wanasema fedha za walipakodi zimepotea bure bileshi.
Mhadhiri na mchumi kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe,
Dk Romanus Dimoso, anasema Bunge la Katiba halikukidhi haja
iliyokusudiwa na kuwa fedha zilizotumika zingeweza kufanya makubwa kama
zingepelekwa katika miradi ya maendeleo ya kijamii.
“Kuna shule za kata nchi nzima hazina maabara,
watoto wanafeli masomo ya sayansi. Pia kuna tatizo la zahanati
zisizokuwa na dawa, fedha hizo zingeweza kuondoa changamoto hizo kwa
kiwango kikubwa,” anaeleza.
Matumizi katika elimu
Fedha zilizotumika kuandaa Bunge la Katiba na
posho walizolipwa wajumbe zingeweza kufanya makubwa kama zingepelekwa
katika sekta ya elimu.
Kwa mfano, shule nyingi za umma hazina madawati na
hii imekuwa changamoto tete inayoihangaisha Serikali. Serikali yenyewe
imeshakiri kuwa madawati ni tatizo katika shule za umma hasa zile za
msingi.
Akizungumza katika uzinduzi wa Wiki ya Elimu mkoani Dodoma wiki
iliyopita, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alisema takwimu zinaonyesha shule
za msingi pekee zinakabiliwa na uhaba wa madawati 1,464, 895.
Kunusuru wanafunzi na tatizo hili, Waziri Pinda
akitumia makadirio ya kila dawati kutengenezwa kwa Sh 120, 000, anasema
kama Serikali itatumia Sh 36 bilioni kwa mwaka, ina uwezo wa
kuziondolea aibu shule zetu kwa kuzisambazia madawati 300,000.
Kiasi hicho ni sawa na kulishughulikia tatizo kwa
asilimia 20.5 kila mwaka. Baada ya miaka mitano, Pinda anasema
hakutakuwa na tatizo la madawati shuleni.
Makadirio ya hesabu za Waziri Mkuu ni zaidi
(takriban milioni 800) ya fedha zilizovunwa na wajumbe na pia kuboresha
ukumbi wa Bunge (ambazo jumla yake ni Sh 35.2 bilioni).
Hata chini ya makadirio haya, Serikali inaweza
kutumia Sh 24 bilioni kwa mwaka kutengeneza madawati 200,000 hivyo
kutumia miaka saba kumaliza tatizo.
Miradi mingine
Ukiondoa madawati, fedha za Bunge Maalumu la
Katiba zingeweza kutumika katika miradi kadhaa muhimu ya elimu kama
ujenzi wa nyumba za walimu na vyumba vya madarasa.
Kwa mfano, makadirio ya ujenzi wa nyumba moja kwa
mujibu wa viwango vya Wizara Elimu na Mafunzo ya Ufundi ni kati ya Sh
30,000,00 (ikijengwa kwa ushirikiano kati ya serikali na wananchi) hadi
50,000,00 (ikijengwa kupitia mkandarasi).
Kwa kutumia makadirio ya juu ya Sh 50,000,000, Sh
35.2 bilioni zinaweza kutumika kujenga nyumba 704 kila mwaka. Si haba
kiasi hicho ikiwa shule zitakazonufaika na ujenzi wa nyumba hizo ni zile
zilizopo katika mazingira magumu.
Aidha, kwa kiwango hichohicho, au chini yake,
serikali inaweza kujenga zaidi ya vyumba vya madarasa 1000 kila mwaka,
na hatimaye kuwaokoa watoto wa Kitanzania wanaolazimika kusoma chini ya
miti kwa kukosa madarasa.
Matumizi yasiyofuata kipaumbele
Ni kama ada kwa nchi hii kuona sehemu ya bajeti za
vyombo mbalimbali vya serikali ikitumika nje ya miradi muhimu ya
maendeleo. Sekta ya elimu haiwezi kujitenga na hali hii.
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment