Home » » BAJETI YAIKALIA VIBAYA SERIKALI

BAJETI YAIKALIA VIBAYA SERIKALI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

MBUGE wa Kawe kwa tiketi ya CHADEMA, Halima Mdee, amesema Serikali ya CCM inastahili kupigwa mawe na wakulima, wavuvi pamoja na wafugaji kutokana na kutoa ahadi zisizotekelezeka.

Aliyasema hayo Bungeni mjini Dodoma Jana wakati akichangia hotuba ya Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2014/15. Alisema Serikali ya CCM iliahidi wananchi kuwa kufikia mwaka 2010 kilimo kitakuwa kimepanda kwa asilimia 10, lakini mpaka mwaka huu kimepanda kwa asilimia 4.

Alisema inashangaza sana kuona safari za Rais zinatengewa sh. bilioni 50 wakati kilimo kinachotegemewa na asilimia 75 ya wananchi kinatengewa fedha kidogo, jambo ambalo linafanya maendeleo ya wakulima kusuasua.

"Inashangaza kuona Rais anaruka na ndege ya kukodi kwenda Dodoma kucheza na wasanii wakati kilimo kikiwa na hali mbaya," alisema. Alisema Serikali kutoa huduma kwa wananchi si jambo la hisani, bali ni lazima kwani pesa za maendeleo zinatoka kwa wananchi wenyewe.

Aliongeza kuwa matajiri wenye kampuni kubwa ndiyo vinara wa kukwepa kodi nchini wakati wananchi wa kipato cha chini ndio walipa kodi wazuri, kwani wanalipa kwa kila bidhaa wanazonunua kila siku.

Mdee alisema wananchi nao wamekuwa wakikaidi kulipa kodi kutokana na kuona matajiri wakikwepa kulipa kodi na mzigo mkubwa unawaelemea wao."

Mdee alisema kuwa Serikali iache kutoa taarifa za upotoshaji kwa wananchi kuwa pato la taifa limepanda wakati kuna Watanzania wa kipato cha chini ambao hawawezi hata kupata sh. 10,000 kwa siku jambo ambalo ni kinyume na takwimu za kupanda kwa uchumi.

Alisema wabunge wapunguze matumizi yasio ya lazima na fedha hizo zihamishiwe kwenye miradi ya maendeleo na Serikali iwe na dhamira katika kuzuia upotevu wa fedha, kwani kila mwaka trilioni 3 hupotea.

Pia Mdee alimtaka Mbunge mwenzake kutoka CHADEMA, Leticia Nyerere, kuachia kiti chake cha ubunge na kama anataka kwenda CCM aende kwani Rais Kikwete, amebakiwa na nafasi mbili za kuteua atamteua ila awe makini kwani atakiona kiti hicho cha moto.

Alisema wapo walioasi upinzani mpaka sasa wanasota.

Aliendelea kusema kuwa jukumu la Upinzani ni kukosoa Serikali na Idara zake kwa lengo la kuboresha utendaji na si kusifia Serikali ya CCM.

Mdee alitoa kauli hiyo kutokana na mbunge huyo wa CHADEMA (Leticia) kusema kwamba Serikali imepeleka maji na umeme kwenye jimbo lake. "Si kila kitu lazima tupinge ikiwa umeletewa maji na umeme...unapaswa kushukuru kwa haya ambayo Serikali imefanya," alisema Nyerere wakati akichangia juzi.

Kwa upande wake Mchungaji Peter Msigwa, alisema Serikali kupanga bajeti isiyo tekelezeka ni sawa na kuwaadaa wananchi, kwani haitekelezi mipango ya maendeleo.

Alisema utamaduni wa nchi hii ni watu kuwa waoga, wanafiki na wa kuogopa kusema ukweli jambo ambalo linakwamisha maendeleo kwa kiasi kikubwa.

Aliongeza kuwa haiwezekani kumtengea Rais kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya safari, wakati sekta za maendeleo zikitengewa kiasi kidogo cha fedha.

Mchungaji Msigwa, alisema tatizo la nchi hii ni watu kupeana nafasi za uongozi katika sekta muhimu bila kuwa na vigezo na matokeo yake ufanisi unakuwa mbovu.

"Kambi ya upinzani imetoa ushauri sana kwa Serikali lakini tunaona viongozi wa CCM na Serikali yake wameweka pamba masikioni," alisema Msigwa.

Aliongeza kuwa wabunge hawapaswi kushangilia na kupongezana kwa kupiga makofi wakati wa kujadili bajeti kuu Bungeni wakati wananchi wanateseka kwa kukosa huduma muhimu.

Hali ya uchumi

Katika hatua nyingine Wabunge wameishangaa Serikali kuwa uchumi wa nchi umekua kwa kiwango kikubwa wakati kipato cha wananchi ni kidogo sana.

Wakichangia Bajeti ya Serikali kuu walisema misamaha ya kodi iwekwe wazi kwani misamaha ya kodi inaua uchumi wa nchi kwa asilimia kubwa.

Akichangia bungeni jana Mbunge wa Viti maalumu CCM, Mary Mwanjelwa, alisema soda, juisi, bia na sigara ni vitu ambavyo vinatumiwa na wananchi wengi kupandisha kodi katika vitu hivyo ni sawa na kuwaumiza wananchi.

Aliitaka Serikali kuangalia sehemu nyingine ya kukusanya mapato kutoka kwenye kampuni kubwa.

Kwa upande wake mbunge wa Rungwe Magharibi, Profesa David Mwakyusa, aliitaka Serikali kujenga viwanda kwani nchi zote zilizoendelea zinategemea viwanda kwa ajili ya kuinua uchumi wa nchi zao.

Alisema kuwa Tanzania inajitapa kuwa asilimia 80 ya wananchi wanategemea kilimo kuendesha maisha yao wakati bado kilimo hakijaonesha mchango wake katika kuinua uchumi wa wananchi kutokana na kuchangia asilimia ndogo katika pato la taifa.

Naye mbunge wa Viti maalumu CCM, Cynthia Ngowi, alisema Serikali inategemea sana mapato ya nje yanayotokana na utalii lakini bado watalii wanawekewa kodi kubwa kuingia nchini.

Alisema makaa ya mawe endapo yataendelezwa yanaweza kuiondoa Tanzania kwenye janga la umaskini lakini hayapewi umuhimu kwani yanaweza kuchangia pato la taifa na kuinua uchumi wa nchi.

Mbunge wa Kisarawe Mkoa wa Pwani kupitia tiketi ya CCM, Selemani Jafo, aliitaka Serikali kufuta misamaha ya kodi hili kukusanya fedha za kujenga miradi ya maendeleo.

Aliitaka Wizara ya Fedha kutafuta mbinu za kuwafanya wananchi wapende kulipa kodi. Alisema ujenzi wa bandari kavu ya Kisarawe itapunguza msongamano wa maroli katika jiji la Dar es Salaam na hii itafanya uchumi kukua, kwani maroli hayo yamekuwa yakisababisha uharibifu mkubwa wa barabara.

Alisema Bandari hiyo ikijengwa itakuwa katikati ya reli mbili ambazo ni reli ya kati na ya Tazara na hii itasaidia sana kupunguza mrundikano ndani ya jiji hilo, kwani mizigo mingine itasafirishwa kupitia reli hizo.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa