Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
MBUGE
wa Kawe kwa tiketi ya CHADEMA, Halima Mdee, amesema Serikali ya CCM
inastahili kupigwa mawe na wakulima, wavuvi pamoja na wafugaji kutokana
na kutoa ahadi zisizotekelezeka.
Aliyasema hayo Bungeni
mjini Dodoma Jana wakati akichangia hotuba ya Bajeti Kuu ya Serikali kwa
mwaka wa fedha 2014/15. Alisema Serikali ya CCM iliahidi wananchi kuwa
kufikia mwaka 2010 kilimo kitakuwa kimepanda kwa asilimia 10, lakini
mpaka mwaka huu kimepanda kwa asilimia 4.
Alisema inashangaza
sana kuona safari za Rais zinatengewa sh. bilioni 50 wakati kilimo
kinachotegemewa na asilimia 75 ya wananchi kinatengewa fedha kidogo,
jambo ambalo linafanya maendeleo ya wakulima kusuasua.
"Inashangaza kuona Rais
anaruka na ndege ya kukodi kwenda Dodoma kucheza na wasanii wakati
kilimo kikiwa na hali mbaya," alisema. Alisema Serikali kutoa huduma kwa
wananchi si jambo la hisani, bali ni lazima kwani pesa za maendeleo
zinatoka kwa wananchi wenyewe.
Aliongeza kuwa matajiri
wenye kampuni kubwa ndiyo vinara wa kukwepa kodi nchini wakati wananchi
wa kipato cha chini ndio walipa kodi wazuri, kwani wanalipa kwa kila
bidhaa wanazonunua kila siku.
Mdee alisema wananchi
nao wamekuwa wakikaidi kulipa kodi kutokana na kuona matajiri wakikwepa
kulipa kodi na mzigo mkubwa unawaelemea wao."
Mdee alisema kuwa
Serikali iache kutoa taarifa za upotoshaji kwa wananchi kuwa pato la
taifa limepanda wakati kuna Watanzania wa kipato cha chini ambao
hawawezi hata kupata sh. 10,000 kwa siku jambo ambalo ni kinyume na
takwimu za kupanda kwa uchumi.
Alisema wabunge
wapunguze matumizi yasio ya lazima na fedha hizo zihamishiwe kwenye
miradi ya maendeleo na Serikali iwe na dhamira katika kuzuia upotevu wa
fedha, kwani kila mwaka trilioni 3 hupotea.
Pia Mdee alimtaka
Mbunge mwenzake kutoka CHADEMA, Leticia Nyerere, kuachia kiti chake cha
ubunge na kama anataka kwenda CCM aende kwani Rais Kikwete, amebakiwa na
nafasi mbili za kuteua atamteua ila awe makini kwani atakiona kiti
hicho cha moto.
Alisema wapo walioasi upinzani mpaka sasa wanasota.
Aliendelea kusema kuwa
jukumu la Upinzani ni kukosoa Serikali na Idara zake kwa lengo la
kuboresha utendaji na si kusifia Serikali ya CCM.
Mdee alitoa kauli hiyo
kutokana na mbunge huyo wa CHADEMA (Leticia) kusema kwamba Serikali
imepeleka maji na umeme kwenye jimbo lake. "Si kila kitu lazima tupinge
ikiwa umeletewa maji na umeme...unapaswa kushukuru kwa haya ambayo
Serikali imefanya," alisema Nyerere wakati akichangia juzi.
Kwa upande wake
Mchungaji Peter Msigwa, alisema Serikali kupanga bajeti isiyo tekelezeka
ni sawa na kuwaadaa wananchi, kwani haitekelezi mipango ya maendeleo.
Alisema utamaduni wa
nchi hii ni watu kuwa waoga, wanafiki na wa kuogopa kusema ukweli jambo
ambalo linakwamisha maendeleo kwa kiasi kikubwa.
Aliongeza kuwa
haiwezekani kumtengea Rais kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya safari,
wakati sekta za maendeleo zikitengewa kiasi kidogo cha fedha.
Mchungaji Msigwa,
alisema tatizo la nchi hii ni watu kupeana nafasi za uongozi katika
sekta muhimu bila kuwa na vigezo na matokeo yake ufanisi unakuwa mbovu.
"Kambi ya upinzani
imetoa ushauri sana kwa Serikali lakini tunaona viongozi wa CCM na
Serikali yake wameweka pamba masikioni," alisema Msigwa.
Aliongeza kuwa wabunge
hawapaswi kushangilia na kupongezana kwa kupiga makofi wakati wa
kujadili bajeti kuu Bungeni wakati wananchi wanateseka kwa kukosa huduma
muhimu.
Hali ya uchumi
Katika hatua nyingine
Wabunge wameishangaa Serikali kuwa uchumi wa nchi umekua kwa kiwango
kikubwa wakati kipato cha wananchi ni kidogo sana.
Wakichangia Bajeti ya
Serikali kuu walisema misamaha ya kodi iwekwe wazi kwani misamaha ya
kodi inaua uchumi wa nchi kwa asilimia kubwa.
Akichangia bungeni jana
Mbunge wa Viti maalumu CCM, Mary Mwanjelwa, alisema soda, juisi, bia na
sigara ni vitu ambavyo vinatumiwa na wananchi wengi kupandisha kodi
katika vitu hivyo ni sawa na kuwaumiza wananchi.
Aliitaka Serikali kuangalia sehemu nyingine ya kukusanya mapato kutoka kwenye kampuni kubwa.
Kwa upande wake mbunge
wa Rungwe Magharibi, Profesa David Mwakyusa, aliitaka Serikali kujenga
viwanda kwani nchi zote zilizoendelea zinategemea viwanda kwa ajili ya
kuinua uchumi wa nchi zao.
Alisema kuwa Tanzania
inajitapa kuwa asilimia 80 ya wananchi wanategemea kilimo kuendesha
maisha yao wakati bado kilimo hakijaonesha mchango wake katika kuinua
uchumi wa wananchi kutokana na kuchangia asilimia ndogo katika pato la
taifa.
Naye mbunge wa Viti
maalumu CCM, Cynthia Ngowi, alisema Serikali inategemea sana mapato ya
nje yanayotokana na utalii lakini bado watalii wanawekewa kodi kubwa
kuingia nchini.
Alisema makaa ya mawe
endapo yataendelezwa yanaweza kuiondoa Tanzania kwenye janga la umaskini
lakini hayapewi umuhimu kwani yanaweza kuchangia pato la taifa na
kuinua uchumi wa nchi.
Mbunge wa Kisarawe Mkoa
wa Pwani kupitia tiketi ya CCM, Selemani Jafo, aliitaka Serikali kufuta
misamaha ya kodi hili kukusanya fedha za kujenga miradi ya maendeleo.
Aliitaka Wizara ya
Fedha kutafuta mbinu za kuwafanya wananchi wapende kulipa kodi. Alisema
ujenzi wa bandari kavu ya Kisarawe itapunguza msongamano wa maroli
katika jiji la Dar es Salaam na hii itafanya uchumi kukua, kwani maroli
hayo yamekuwa yakisababisha uharibifu mkubwa wa barabara.
Alisema Bandari hiyo
ikijengwa itakuwa katikati ya reli mbili ambazo ni reli ya kati na ya
Tazara na hii itasaidia sana kupunguza mrundikano ndani ya jiji hilo,
kwani mizigo mingine itasafirishwa kupitia reli hizo.
0 comments:
Post a Comment