Home » » DIRA: Serikali isiogope uhuru wa vyombo vya habari

DIRA: Serikali isiogope uhuru wa vyombo vya habari

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Kati ya mijadala ya Bunge la Bajeti linaloendelea mjini Dodoma, ule  wa Wizara Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ulinigusa zaidi kutokana na taaluma ninayofanyia kazi.
Baada ya waziri wake na naibu wake, Juma Nkamia kuwasilisha hotuba zao, wakarejea ahadi ya Serikali ya kila mwaka ya kuleta muswada wa habari.
Baadhi ya wabunge akiwamo Esther Bulaya (CCM), Joseph Mbilinyi au Sugu ambaye pia ni waziri kivuli wa wizara hiyo, Juma Mtanda, Felix Mkosamali na wengineo waliwakomalia mawaziri hao kuhusu muswada huo.
Mwisho, naibu waziri  Nkamia akasema muswada wa sheria ya kusimamia vyombo vya habari umekamilika baada ya kupitia hatua zote muhimu na kwamba sasa taratibu za kuuleta bungeni zinaandaliwa na kwamba utaletwa katika mkutano ujao wa Bunge ambao hakuna shaka utakuwa Oktoba.
Majibu hayo yanazua wasiwasi mwingi. Kwa nini Serikali imeuchelewesha hivyo muswada huo?
Hadi sasa muswada huo umekuwa ukijadiliwa kwa zaidi ya miaka 17 sasa, kila mwaka Serikali inasema itauleta bungeni.
Wamepita  mawaziri lukuki, kila anayekuja anaukuta mwiba huo, anaukwepa na kuishia tu kutoa ahadi hewa.
Kwa maana nyingine, mawaziri waliopita na kuahidi kuletwa kwa muswada huo walikuwa wakilidanganya Bunge lakini hawajachukuliwa hatua yoyote.
Hata hao wa sasa hatujui kama nao wamelidanganya Bunge kama wenzao au pengine mwaka huu kitendawili hicho kitateguliwa. Hata hivyo, tusubiri tuone.
Ni dhahiri kwamba Serikali inauhofia muswada huo kwa kuwa utakuwa mwiba kwake.
Kwa sasa, Serikali imekumbatia Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976  inayompa mamlaka  waziri husika kufungia magazeti pale atakapoona yamekiuka sheria hiyo.  Sheria hiyo pamoja na nyinginezo 40 zilishapendekezwa kufutwa na Tume ya Jaji Francis Nyalali mwaka 1992, lakini Serikali ikagoma na kufunga masikio.  Ni sheria mbovu inayokiuka utawala wa sheria unatambua uwepo wa mahakama, hivyo kama Serikali ni mlalamikaji haiwezi tena kuwa mtoa hukumu, tena hata bila mlalamikiwa kusikilizwa.
Serikali inaogopa vyombo vya habari huru, kwani vinaweza kuhatarisha uwepo wake. Hii ni dalili kwamba pengine tuna Serikali dhaifu  iliyojaa woga na kuogopa ukweli na uwaz
Kuna harufu ya ufisadi, rushwa, upendeleo na maovu mengine yanayofichwa na ndiyo kisa cha kuchelewesha muswada huo.
Kila mwaka mawaziri wa wizara hiyo wanajifanya eti kuwalilia waandishi wa habari wasio na ajira.
Kama kweli ina uchungu nao, mbona inauchelewesha muswada huo wenye vipengele vya kuwatetea?
Halafu, Nkamia anasema eti Serikali imetoa uhuru mkubwa wa vyombo vya habari na ndiyo maana kuna idadi kubwa ya magazeti.
Jamani idadi inahusianaje na uhuru wa habari? Ni heri tuwe na vyombo vya habari vichache, lakini vyenye uhuru wa kufanya kazi bila kuingiliwa na Serikali, kuliko ilivyo sasa.
Chanzo;Mwananchi

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa