Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Kati ya mijadala ya Bunge la Bajeti
linaloendelea mjini Dodoma, ule wa Wizara Habari, Vijana, Utamaduni na
Michezo ulinigusa zaidi kutokana na taaluma ninayofanyia kazi.
Baada ya waziri wake na naibu wake, Juma Nkamia
kuwasilisha hotuba zao, wakarejea ahadi ya Serikali ya kila mwaka ya
kuleta muswada wa habari.
Baadhi ya wabunge akiwamo Esther Bulaya (CCM),
Joseph Mbilinyi au Sugu ambaye pia ni waziri kivuli wa wizara hiyo, Juma
Mtanda, Felix Mkosamali na wengineo waliwakomalia mawaziri hao kuhusu
muswada huo.
Mwisho, naibu waziri Nkamia akasema muswada wa
sheria ya kusimamia vyombo vya habari umekamilika baada ya kupitia hatua
zote muhimu na kwamba sasa taratibu za kuuleta bungeni zinaandaliwa na
kwamba utaletwa katika mkutano ujao wa Bunge ambao hakuna shaka utakuwa
Oktoba.
Majibu hayo yanazua wasiwasi mwingi. Kwa nini Serikali imeuchelewesha hivyo muswada huo?
Hadi sasa muswada huo umekuwa ukijadiliwa kwa zaidi ya miaka 17 sasa, kila mwaka Serikali inasema itauleta bungeni.
Wamepita mawaziri lukuki, kila anayekuja anaukuta mwiba huo, anaukwepa na kuishia tu kutoa ahadi hewa.
Kwa maana nyingine, mawaziri waliopita na kuahidi
kuletwa kwa muswada huo walikuwa wakilidanganya Bunge lakini
hawajachukuliwa hatua yoyote.
Hata hao wa sasa hatujui kama nao wamelidanganya
Bunge kama wenzao au pengine mwaka huu kitendawili hicho kitateguliwa.
Hata hivyo, tusubiri tuone.
Ni dhahiri kwamba Serikali inauhofia muswada huo kwa kuwa utakuwa mwiba kwake.
Kwa sasa, Serikali imekumbatia Sheria ya Magazeti
ya mwaka 1976 inayompa mamlaka waziri husika kufungia magazeti pale
atakapoona yamekiuka sheria hiyo. Sheria hiyo pamoja na nyinginezo 40
zilishapendekezwa kufutwa na Tume ya Jaji Francis Nyalali mwaka 1992,
lakini Serikali ikagoma na kufunga masikio. Ni sheria mbovu inayokiuka
utawala wa sheria unatambua uwepo wa mahakama, hivyo kama Serikali ni
mlalamikaji haiwezi tena kuwa mtoa hukumu, tena hata bila mlalamikiwa
kusikilizwa.
Serikali inaogopa vyombo vya habari huru, kwani
vinaweza kuhatarisha uwepo wake. Hii ni dalili kwamba pengine tuna
Serikali dhaifu iliyojaa woga na kuogopa ukweli na uwaz
Kuna harufu ya ufisadi, rushwa, upendeleo na maovu mengine yanayofichwa na ndiyo kisa cha kuchelewesha muswada huo.
Kila mwaka mawaziri wa wizara hiyo wanajifanya eti kuwalilia waandishi wa habari wasio na ajira.
Kama kweli ina uchungu nao, mbona inauchelewesha muswada huo wenye vipengele vya kuwatetea?
Halafu, Nkamia anasema eti Serikali imetoa uhuru mkubwa wa vyombo vya habari na ndiyo maana kuna idadi kubwa ya magazeti.
Jamani idadi inahusianaje na uhuru wa habari? Ni
heri tuwe na vyombo vya habari vichache, lakini vyenye uhuru wa kufanya
kazi bila kuingiliwa na Serikali, kuliko ilivyo sasa.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment