Home » » TAARIFA YA KAMATI YA BUNGE YA BAJETI KUHUSU HALI YA UCHUMI WA TAIFA KWA MWAKA 2013 NA MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA KWA MWAKA 2014/15 PAMOJA NA TATHMINI YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA SERIKALI KWA MWAKA 2013/14 NA MAPENDEKEZO YA MAPATO NA MATUMIZI YA SERIKALI KWA MWAKA WA FEDHA 2014/15.‏

TAARIFA YA KAMATI YA BUNGE YA BAJETI KUHUSU HALI YA UCHUMI WA TAIFA KWA MWAKA 2013 NA MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA KWA MWAKA 2014/15 PAMOJA NA TATHMINI YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA SERIKALI KWA MWAKA 2013/14 NA MAPENDEKEZO YA MAPATO NA MATUMIZI YA SERIKALI KWA MWAKA WA FEDHA 2014/15.‏

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 



TAARIFA YA KAMATI YA BUNGE YA BAJETI KUHUSU HALI YA UCHUMI WA TAIFA KWA MWAKA 2013 NA MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA KWA MWAKA 2014/15 PAMOJA NA TATHMINI YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA SERIKALI KWA MWAKA 2013/14 NA MAPENDEKEZO YA MAPATO NA MATUMIZI YA SERIKALI KWA MWAKA WA FEDHA 2014/15.

1.0    UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Kanuni 105(8) ya Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la 2013 naomba kuwasilisha Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Bajeti kuhusu Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2013 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2014/15 pamoja na Tathmini ya Utekelezaji wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2013/14 na Mapendekezo ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2014/15.
Mheshimiwa Spika, Kama nilivyoeleza kwenye taarifa ya Kamati mwaka uliopita, Kamati ya Bajeti, pamoja na majukumu mengine ina jukumu la kuisimamia Serikali kwa kujikita zaidi kwenye kufuatilia mwenendo wa ukusanyaji wa mapato na kusimamia matumizi ya Serikali. Vile vile, Kamati hufanya uchambuzi wa hali halisi ya ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Mheshimiwa Spika, pamoja na Serikali kuendelea kutambua umuhimu wa Bunge katika mchakato wa Bajeti, bado Kamati imebaini kuwa Serikali haijaonesha utayari wa kupokea ushauri katika baadhi ya maeneo ambayo Kamati imekuwa ikitoa hususan eneo la ukusanyaji wa mapato kwa kutumia vyanzo vipya. Kamati inaona kuwa hii ni changamoto kubwa inayosababisha kutokuwepo kwa mabadiliko katika eneo muhimu la upanuzi wa wigo wa vyanzo vya mapato.
Mheshimiwa Spika, napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kuwa, Kamati itaendelea kutekeleza majukumu yake ya kuishauri Serikali kuhusiana na mikakati ya kutekeleza bajeti kwa ufanisi na kuimarisha uchumi wa Taifa letu.
2.0      UCHAMBUZI WA MASUALA MBALIMBALI KUHUSU MWENENDO WA UCHUMI KWA MWAKA WA FEDHA 2013.
Mheshimiwa Spika, Bunge lako Tukufu tayari limeshapokea taarifa kuhusu hali na mwenendo wa uchumi kwa mwaka 2013 na Mpango wa Maendeleo kwa mwaka 2013/14 kama ilivyowasilishwa tarehe 12 Juni, 2014 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu, Mheshimiwa Stephen Masatu Wassira.
Taarifa hiyo imebainisha kuwa madhumuni makubwa ya Mpango wa Maendeleo ni kuongeza kasi ya maendeleo ili ifikapo mwaka 2025 nchi iwe imetoka katika kundi la nchi maskini duniani na kuingia katika kundi la nchi zenye kipato cha kati (middle income country). Kwa kuzingatia azma hiyo, Tanzania haina budi kuhakikisha inajenga uchumi wenye misingi imara na uwezo wa ushindani utakaoiwezesha kukabiliana na changamoto za maendeleo, kuweka mazingira wezeshi kwa mahitaji ya uwekezaji na mabadiliko ya utoaji huduma, masoko, biashara na teknolojia katika kanda na ulimwengu kwa ujumla.
2.1      Ukuaji wa Uchumi na Kuondoa Umasikini
Mheshimiwa Spika, takwimu zinaonesha kuwa, mwenendo wa ukuaji wa uchumi kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo kuanzia mwaka 2010 – 2013 ni wa kuridhisha na umekua kwa wastani wa asilimia 6.8. Katika mwaka 2013 pato halisi la Taifa (GDP) lilikua kwa kiwango cha asilimia 7.0 ikilinganishwa na ukuaji wa kiwango cha asilimia 6.9 kwa mwaka 2012 ; asilimia 6.4 kwa mwaka 2011; na asilimia 7.0 kwa mwaka 2010. Ukuaji wa pato la Taifa kwa mwaka 2013, ulichangiwa zaidi na sekta ya mawasiliano (22.8%) ; huduma za fedha (12.2%) ; viwanda na ujenzi (8.6%) biashara ya jumla na reja reja (8.3%);huduma (8.2%) na huduma za Hoteli na Migahawa (6.3%). Sekta za  kilimo, mifugo, uvuvi na misitu hazijafanya vizuri na wastani wa mchango wake katika Pato la taifa ulikuwa ni chini ya 4%.

Mheshimiwa Spika, pamoja na uchumi mpana kukua kwa kasi ya kuridhisha kwa takribani miaka kumi mfululizo, umasikini miongoni mwa wananchi wetu haupungui kwa kasi inayoridhisha kama ambavyo sensa ya Mwaka 2012 inavyothibitisha. Hii inatokana na ukweli kwamba sekta zinazobeba na kugusa maisha ya watu wasiopungua asilimia 75 ya watanzania wote, yaani Kilimo, Mifugo na Uvuvi hazikui kwa kasi inayotakiwa. Hii inatokana na Serikali kutowekeza vya kutosha katika sekta hizo pamoja na kuwepo kwa muingiliano hafifu kati ya sekta zinazokua haraka na zile zinazokua polepole (weak sectoral interlinkages) na pia utekelezaji usio endelevu wa Sera na programu mbalimbali zinazowekwa na Serikali kama vile KILIMO KWANZA na ASDP na kadharika.

Mheshimiwa Spika, Kuna viashiria vinavyoshawishi kuwepo ukweli kuwa familia zinazojishughulisha na kilimo, mifugo, uvuvi na misitu, ndizo zimeendelea kuwa maskini zaidi. Baadhi ya watafiti wanasema kuwa pengo kati ya wananchi wenye kipato cha juu na wenye kipato cha chini limezidi kuongezeka.

Mheshimiwa Spika, moja kati ya changamoto zinazokabili sekta hizi ni kutokuwepo kwa viwanda vya kuchakata mazao ili kuongeza thamani, masoko ya uhakika, bei yenye tija, upatikanaji wa pembejeo na teknolojia sahihi na ya kisasa.

Mheshimiwa Spika, Serikali haina budi kuhakikisha kuwa shughuli zinazofanywa katika sekta hizi zinafanyika kwa tija na zinawaletea Wananchi manufaa na faida iliyo wazi na endelevu ili kupunguza umasikini haraka na kwa uhakika. Hivyo Serikali ina wajibu wa kuwekeza vya kutosha katika maeneo haya (asilimia 10 ya bajeti) ili kuweza kupata ukuaji wa uchumi unaotazamiwa.

Mheshimiwa Spika, zipo baadhi ya nchi za Afrika zilizowekeza vya kutosha katika kilimo na kufanikiwa kupunguza umaskini kwa kiasi kikubwa. Kati ya mwaka 2003 na 2010, Burkina Faso, Ethiopia, Guinea, Malawi, Mali, Niger na Senegal ziliweza kuwekeza kiasi cha asilimia 10 ya Bajeti zao katika kilimo. Nchi za Ghana, Madagascar na Zambia zilifuatia kwa kuwekeza kwa wastani wa asilimia 9. Inakadiriwa kwamba, kutokana na mchango wa uwekezaji huu, nchi hizi zitaweza kupunguza umaskini uliokithiri kwa zaidi ya nusu ifikapo mwaka 2015[1].

Mheshimiwa Spika tatizo la upatikanaji wa fursa za ajira nchini ni kubwa hasa kwa vijana. Ajira zinazotolewa na serikali pamoja na sekta ya umma hazitoshelezi kabisa katika kupunguza kwa kiasi kikubwa tatizo hili. Kwa mfano nafasi za kazi 70 za inspekta wasaidizi katika Idara ya Uhamiaji zilitangazwa, waliojitokeza kwenye usahili ni vijana 10,816! Hii ina maana kwamba kila nafasi moja imeombwa na watu 155. Tatizo la ajira nchini linaendana pia na viwango vya umasikini, kama ambavyo wananchi wengi masikini wamekuwa wakikimbilia mijini, ambako hali ya umasikini iko chini kuliko vijijini. Kwa mfano, Jiji la Dar es Salaam kulingana na takwimu, linaongoza kwa kuwa na umasikini wa chini sana ikilinganishwa na miji mingine na vijijini . Hivyo, haishangazi kuona kuwa idadi ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam imekuwa ikiongezeka kwa kasi kubwa. Tatizo la ajira litatatuliwa kwa kuishirikisha sekta binafsi kimkakati ili iweze kushirikiana na sekta ya umma, kuongeza uwekezaji kwenye sekta zinazohusisha wananchi wengi kama nilivyobainisha hapo awali. Kubwa na la msingi zaidi ni kwa Serikali kuhakikisha kuwa uchumi unakua kwa kasi zaidi ya asilimia 8 kuliko ilivyo sasa na ukuaji huo wa uchumi uwe endelevu kwa kipindi cha zaidi ya miaka kumi mfululizo . Hatua hiyo ndiyo itakayozalisha ajira nchini kwa kasi na kuongeza Pato la Mtanzania.

2.2      Mwenendo wa Mfumuko wa Bei na thamani ya shilingi
Mheshimiwa Spika, mwenendo wa mfumuko wa bei umepungua na umeendelea kuwa tarakimu moja toka asilimia 9.8 Machi, 2013 hadi asilimia 6.1 Machi 2014. Hii imetokana na juhudi za Serikali kusimamia mfumuko wa bei ya chakula hasa kwa upande wa bidhaa za mchele, ngano na mahindi.Mfumuko wa bei umeshuka pia kutokana na utaratibu wa Benki Kuu kupunguza mzunguko (ama ujazo) wa fedha nchini ama kwenye uchumi. Kamati inashauri jitihada za kudhibiti mfumuko wa bei ziendelezwe kwa namna ambayo haitaathiri ukuaji wa uchumi.

Mheshimiwa Spika, kwa kipindi cha mwaka 2012/2013 hadi 2013/14; thamani ya shilingi katika soko la mabenki imeendelea kushuka ukilinganisha na Dola ya Kimarekani. Wastani umeonesha kuwa thamani ya shilingi kwa dola za kimarekani  ilishuka kutoka shilingi 1,598.8 mwezi Machi, 2013 hadi hadi shilingi 1,634.3 mwezi Machi, 2014. Siku ya Ijumaa tarehe 12 Juni, thamani ya Dola moja ya Kimarekani ilipanda kufikia shilingi 1683.52. Hii imetokana pamoja na mambo mengine, na kuongezeka kwa mahitaji ya nchi kwa bidhaa toka nje ya nchi. Kamati inashauri Serikali izidi kuimarisha udhibiti wa soko la fedha za kigeni.

2.3      Deni la Taifa:
Mheshimiwa Spika, Hadi kufikia Machi 2014 Deni la Taifa linalojumuisha deni la Serikali na deni la nje la sekta binafsi lilifikia shilingi trilioni 30.56 ikilinganishwa na trilioni 23.67 Machi 2013. Deni hili ni sawa na asilimia 57.47 ya Pato la Taifa (kwa bei za sasa) ambalo ni shilingi trilioni 53.17. Kati ya kiasi hicho, Deni la Serikali ni shilingi bilioni 26,832 na Deni la Sekta Binafsi la nje ni shilingi bilioni 3,730.6

Mheshimiwa Spika, deni hili, pamoja na Serikali kusema ni himilivu ni mzigo mkubwa kwa Taifa letu hadi sasa na ni tishio kwa utengamavu wa uchumi jumla. Kamati inaona shaka kuhusiana na deni hili kutokuwa stahimilivu kwa kuzingatia vigezo vifuatavyo:-
i)        Kuna madai mengi ya ndani ambayo hayajajumuishwa katika deni la Taifa na taarifa zilizopo zinaonesha kuwa madai hayo yanaendelea kuongezeka kutoka 0.5% ya pato la Taifa mwaka 2012 hadi 1% ya pato la Taifa mwaka 2013.
ii)      Uwiano uliopo wa Deni la Taifa na pato la Taifa kiuchumi siyo wa kuridhisha. Ukubwa wa deni hili hauwiani na kiwango cha uzalishaji mali na ukuaji wa uchumi wa sasa wa asilimia 7.0
iii)     Udhaifu katika usimamizi wa matumizi ya fedha za Umma na ucheleweshaji wa uhakiki wa madai ya ndani. Taarifa ya Waziri wa Fedha ya nusu mwaka inaonyesha kuwa malimbikizo ya madai hayo hadi Desemba 2013 yalikuwa yamefikia shilingi trillion 2.09, ambayo ni asilimia 4 ya Pato la Taifa. Kiwango hiki kinaaminika kuwa ndicho kiwango cha malimbikizo ya madai (arrears) kwa Serikali kwa nchi nzima.

Mheshimiwa Spika, Serikali imekwishatoa maelezo mazuri ya kuweza kukabiliana na madeni haya (soma MKUKUTA II, Ripoti ya CAG ya 2012/13), hata hivyo utekelezaji wake bado siyo wa vitendo na  hivyo kubaki nadharia tu.

2.4      Mwenendo wa viwango vya riba na mikopo:
Mheshimiwa Spika, mwenendo wa viwango vya riba katika huduma mbalimbali za Benki na Taasisi za Fedha umeendelea kutokuwa wa kuridhisha na hivyo kuendelea kuathiri ukuaji wa uchumi. Takwimu zinaonesha kuwa, hadi mwezi Februari, 2014 wastani wa riba za mikopo zilikuwa asilimia 15.96 kutoka wastani wa asilimia 15.61 kwa mwaka 2013 kwa kipindi kama hicho. Riba za kuweka zimeimarika kwa asilimia 0.06 kutoka asilimia 11.50 kwa mwaka 2013 hadi asilimia 11.56 kwa mwaka 2014. Aidha, uwiano wa riba za kukopa na kuweka (interest rate spread) umepungua na kufikia wastani wa asilimia 2.56 kutoka wastani wa asilimia 2.70 kwa mwaka ulioishia Februari, 2013.

Mheshimiwa Spika, Kwa upande wa sekta binafsi, mikopo imeendelea kukua kwa asilimia 16.1. Hadi mwezi Februari 2014 kiasi cha shilingi bilioni 10,625.6 kilikuwa kimetolewa kama mikopo. Sekta zilizonufaika na mikopo hiyo na kukua kwa kasi zaidi ikilinganishwa na mwaka uliotangulia ni sekta ya ujenzi (asilimia 14.3), biashara (asilimia 14.1), mawasiliano na uchukuzi (asilimia 12.6), kilimo (asilimia 11.2) na uzalishaji wa viwandani (asilimia 9.8).

Mheshimiwa Spika, Kamati inatambua juhudi za Serikali katika kuhakikisha Mikopo inapatikana kwa sekta binafsi na inaendelea kuongezeka. Hata hivyo Kamati inaona kiwango hiki cha ukuaji kimekuwa ni kidogo kwa sababu sekta za kilimo na viwanda vidogo na vya kati vimekuwa havihudumiwi ipasavyo na taasisi za fedha (mabenki) kutokana na sababu kwamba havikidhi masharti ya kukopeshwa. Hali hii ikiendelea hatutaweza kujikwamua katika kuondoa umaskini wa kipato, kuongeza ajira mpya na kupunguza mzigo wa utegemezi katika kaya na hivyo kusababisha kudumaa kwa maendeleo ya kiuchumi.

2.5      Uuzaji, uagiziaji wa bidhaa na huduma nje:
Mheshimiwa Spika, uagizaji wa bidhaa na huduma toka nje umekuwa mkubwa kuliko uuzaji. Urari wa biashara unaonyesha kuwa nakisi ina mwenendo wa kuongezeka. Hali hii ina mchango mkubwa katika kudumaza uzalishaji na kuathiri thamani ya shilingi yetu na uchumi wa nchi kwa ujumla.

2.6      Ushauri wa jumla kuhusiana na hali ya uchumi wa nchi
Mheshimiwa Spika, baada ya kupata taswira hii ya Hali ya Uchumi kwa mwaka 2013 na Mwelekeo wake, Kamati imebaini kuwa bado kuna changamoto kubwa kwa Serikali kuandaa na kutekeleza mikakati ya kuhakikisha kuwa mafanikio ya uchumi mpana yanafika vijijini, hususan katika kuongeza kipato cha wananchi walio wengi na kupunguza umaskini wa kipato. Tutakapofanikiwa katika lengo hili, tutakuwa tunazungumzia ukuaji wa uchumi (economic growth) unaoenda sambamba na maendeleo ya jamii na kiuchumi (socio-economic development).
Mheshimiwa Spika, Kamati ina maoni kwamba kama Taifa, bado hatujatumia vema au kikamilifu fursa zilizopo kikamilifu kukuza uchumi wetu kupitia matumizi yenye tija na ufanisi wa rasilimali zetu.

3.0      MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA
3.1      Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka 2013/14
Mheshimiwa Spika, Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2011/12 -2015/16 unatoa mwongozo wa namna vipaumbele vya Taifa vitakavyotekelezwa ili kufungua fursa za ukuaji uchumi. Mwaka 2013/14 ni mwaka wa pili wa utekelezaji wa Mpango huo katika mfululizo wa miaka mitano iliyopangwa.
Mheshimiwa Spika, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2013/14 ulilenga kutoa kipaumbele kwenye sekta zinazotekeleza miradi ya Matokeo Makubwa Sasa (MMS ama BRN). Miradi hiyo ni Kilimo, Uchukuzi, Nishati, Elimu, Maji na Fedha. Kwa kiasi fulani Kamati haijaridhika na hatua ya utekelezaji wa baadhi ya miradi hiyo na sekta kama vile Maji, Fedha na Kilimo. Kutoridhishwa na utekelezaji huo kumetokana na ukweli kwamba miradi hiyo haikuwa imepelekewa fedha kama zilivyoidhinishwa na Bunge. Kutopelekwa kwa fedha kwa wakati kwa ajili ya kutekeleza miradi hiyo kumekuwa ni changamoto kubwa katika kuiwezesha miradi hiyo kukamilika kwa wakati na hivyo kupunguza kasi ya ukuaji wa maendeleo na pia kuchelewa kufikia Malengo ya Maendeleo ya Millennia (Millenium Developemnt Goals).
Mheshimiwa Spika, Kamati imepokea taarifa kuhusiana na hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa miradi hiyo ya kipaumbele, na imeona kwamba ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji. Kamati inashauri Serikali iendelee kusimamia kwa karibu utekelezaji wa sekta hizo ili matokeo yake yaonekane katika muda uliopangwa.
Mheshimiwa Spika, Jedwali lifuatalo linaonesha kiasi cha  fedha kilichoidhinishwa na Bunge na kilichotolewa na Hazina katika baadhi ya mafungu hadi kufikia mwezi Mei 2014.
Jedwali Na.1: Namna Mafungu yalivyopokea fedha hadi mwezi Mei, 2014
MAELEZO YA FUNGU
FEDHA ILIYOIDHINISHWA
FEDHA ILIYOTOLEWA
% ILIYOTOLEWA
JUMLA ILIYOTOLEWA
% YA JUMLA

NDANI
NJE
NDANI
NJE
NDANI
NJE


FUNGU 6 – President’s Delivery Bureau
4.964 bil
25.0 bil
 --
8.252 bil
0.0%
33.0%
8.252 bil
27.5%
Fungu 43 – Wizara ya Kilimo, C. na Ushirika
23.93 bil
57.11 bil
11.68 bil
47.54 bil
48.8%
83.2%
59.22 bil
73.1%
Fungu 46 – Wizara ya Elimu
18.83 bil
53.77 bil
8.26 bil
20.66 bil
43.9%
38.4%
28.92 bil
39.8%
Fungu 49 – Wizara ya Maji
312.06 bil
241.18 bil
86.0 bil
60.07 bil
27.6%
24.9%
146.07 bil
26.4%
Fungu 50 – Wizara ya Fedha
10.20 bil
223.47 bil
2.39 bil
222.67 bil
23.5 %
99.6%
225.07
96.3%
Fungu 58 – Wizara ya Nishati na Madini
742.55 bil
433.87 bil
431.01 bil
146.52 bil
58.0 %
33.8%
577.53 bil
49.1%
Fungu 62 – Wizara ya Uchukuzi
252.68 bil
167.84 bil
180.13 bil
-
71.3%
0.0%
180.13  bil
42.8%
Angalizo:Jedwali hili linaonyesha kuwa mafungu mengi hadi Mei 2014 yamepelekewa fedha na Hazina kwa kiwango chini ya asilimia 50.
Mheshimiwa Spika, kufuatia mashauriano kati ya Kamati ya kudumu ya Bajeti na Serikali, Waziri wa Fedha alitoa taarifa Bungeni kwamba shilingi bilioni 80 zitaongezwa Wizara ya Maji kabla ya mwaka wa fedha 2013/2014 kumalizika. Hadi taarifa hii inaandikwa, tayari shilingi bilioni 30 zilikwishatolewa. Ni matumaini ya Kamati kwamba kiasi kilichobaki kitatolewa kama Bunge lilivyoahidiwa.
Mheshimiwa Spika, kama inavyoonekana kwenye jedwali Na. 1 Hazina haikuweza kutoa kiasi chote cha fedha kilichoidhinishwa na Bunge na hivyo kuathiri utekelezaji wa malengo ya sekta hizo kwa mwaka 2013/14. Kwa mfano, Kamati imeshangazwa kuona Idara mpya iliyoanzishwa kwa ajili ya kutekeleza Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa kutopokea fedha yoyote ya ndani licha ya kwamba ilitengewa shilingi bilioni 4.964 ambayo ni sawa na aslimia 16.57 ya fedha yote iliyoidhinishwa kwa fungu hili. Kamati imeshindwa kuelewa iwapo mtekelezaji wa mfumo wa uratibu, ufuatiliaji na tathmini ya miradi hakupelekewa fedha za ndani kabisa isipokuwa za nje ambazo nazo zimetolewa asilimia 33 tu, je atawezaje kutekeleza majukumu yake ambayo kimsingi yapo katika mpango wa majaribio?
3.2      Mfumo wa Uratibu, Ufuatiliaji na Tathmini ya Miradi
Mheshimiwa Spika, Kamati imeridhishwa na hatua iliyochukuliwa na Serikali katika kuanzisha mfumo wa uratibu, ufuatiliaji na tathmini ya miradi kwa kuunda kitengo maalum cha kufanya shughuli hiyo chini ya Ofisi ya Rais (Presidential Delivery Bureau-PDB). Utaratibu huu ni mzuri kama ukitekelezwa ipasavyo.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeanzisha utaratibu wa BRN ili kuboresha utaratibu wa usimamizi wa utekelezaji wa miradi uliopo sasa. Kamati inapongeza hatua hii. Hata hivyo uchunguzi uliofanywa na Kamati unaonesha kuwa maeneo ya Matokeo Makubwa Sasa hayakupewa umuhimu uliostahili katika kupelekewa fedha kama jedwali Na. 2 linavyoonyesha.
Jedwali Na. 2: Mahitaji ya Rasilimali na Nakisi ya bajeti kwa ajili ya kutekeleza Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa mwaka 2013/2014 (Tshs Milioni)
Eneo la Matokeo Makubwa
Bajeti iliyopendekezwa
Kiasi kilichoidhinishwa
Mchango wa washirika wa Maendeleo
Nakisi ya Bajeti
Asilimia ya Nakisi
Kilimo
193.9
24.4
9.5
159.9
82%
Uchukuzi
1210.5
171.6
15.3
1023.7
85%
Elimu
194.2
105.5
0.7
88.0
45%
Nishati
2682.5
714.6
645.5
1322.2
49%
Upatikanaji wa Fedha
99.1
0.4
0
98.7
100%
Maji
482.0
248.4
115.3
118.4
25%
JUMLA
4862.1
1264.8
786.2
2811.0
58%
Chanzo: Raprid Budget Analysis 2013, synoptic note.
Mheshmiwa Spika, ni dhahiri kwamba kutokupatikana kwa rasilimali fedha kutaathiri sana utekelezaji wa miradi na programu zilizo chini ya BRN.
3.3      Ushiriki wa Sekta Binafsi
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na Sekta Binafsi iliandaa Sera na mikakati ya Ubia baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (Public Private Partnership-PPP) ya mwaka 2009 pamoja na Sheria ya Ubia baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi  Na. 18 ya mwaka 2010 na Kanuni za utekelezaji wa Sheria hii za mwaka 2011. Aidha, kwa kutambua kuwa ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi ni njia muafaka inayoweza kutatua matatizo yanayotokana na ukosefu wa fedha, usimamizi, uendeshaji na utunzaji wa rasilimali za umma kwa ufanisi, Serikali imeandaa mfumo mpya wa kubuni, kupanga na kutekeleza miradi ya maendeleo.
Mheshimiwa Spika, pamoja na kuwepo kwa malengo mazuri yalioanishwa katika sera na sheria ya ubia huo, Kamati bado haijaridhishwa na ushiriki wa Serikali katika kutekeleza miradi ya ubia inayolenga kuimarisha ushirikiano huu. Hali hii imejidhihirisha katika baadhi ya miradi ya maendeleo mfano uendelezaji wa reli ya kati, ukarabati na ujenzi wa bandari, miradi ya kufua umeme, miradi ya ujenzi wa Ofisi za Ubalozi na makazi ya watumishi wa balozi hizo nje ya nchi n.k ambayo mara zote Bunge limekuwa likisisitiza utekelezaji wa miradi hiyo kwa ubia baina ya sekta hizi mbili. Kamati haijaridhika na sababu inayotolewa mara kwa mara na Serikali kama kikwazo cha utekelezaji wa madhumuni na malengo ya sera na sheria ya PPP. Kutokana na Bajeti ya Serikali kuwa tegemezi, Kamati inaendelea kuishauri na kuitaka Serikali kuimarisha uhusiano na ushirikiano na sekta binafsi katika kuibua na kutekeleza miradi mbalimbali ya ubia. Pamoja na tamko la Serikali juu ya azma ya kuanzisha Mfuko Maalum, Kamati ya kitaifa na kituo cha miradi ya ubia, Kamati inaishauri Serikali kuharakisha uwasilishwaji na kupitishwa kwa mswada wa sheria ya marekebisho ya sheria ya Public Private Partnership ambao umesomwa mara ya kwanza katika Mkutano huu wa Bunge
Mheshimiwa Spika, ikumbukwe kwamba, ushiriki wa sekta binafsi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ni utaratibu ambao umeziwezesha nchi nyingi duniani kupiga hatua kimaendeleo na hivyo kuziwezesha nchi husika kukua haraka kiuchumi. Kama ilivyowahi kuelezwa na Mchumi na Mwana maendeleo, Bw. Jefrey Sachs kuwa “the path to long-term development would only be achieved through private sector involvement and free market solutions”. Tafsiri isiyo rasmi ni kwamba: “Maendeleo ya muda mrefu yanaweza tu kupatikana kwa njia ya ushiriki wa sekta binafsi na soko huria.”
Mheshimiwa Spika, pamoja na faida zinazotokana na ubia baina ya sekta binafsi na sekta ya umma, Kamati inatanabahisha kuwa Serikali isipokuwa makini, yapo mapungufu yanayoweza kujitokeza hususan kama Serikali haitakuwa makini katika kuandaa mikataba.
4.0      UTEKELEZAJI WA BAJETI YA SERIKALI KWA MWAKA 2013/14
4.1      Mwenendo wa Mapato
Mheshimiwa Spika, Kamati ya Bajeti imetathmini kwa kina mapitio ya utekelezaji wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2013/14. Mwenendo unaonyesha kuwa hadi kufikia mwezi Aprili 2014, Serikali imekusanya shilingi bilioni 12,882 sawa na asilimia 70 ya mapato yote ya mwaka yaliyoidhinishwa na Bunge. Kiwango hiki cha ukusanyaji wa mapato si cha kuridhisha na Kamati inaona kwamba sera za mapato kwa mwaka 2013/14 zimeshindwa kuleta mapato kama ilivyokusudiwa.

Mheshimiwa Spika, mfano mzuri tunauona katika mwenendo wa mapato ya ndani. Malengo hayakufikiwa kwa sababu ya kutokufanya vizuri kwa baadhi ya vyanzo vya kodi. Kwa mujibu wa hotuba ya Waziri wa Fedha, hadi kufikia mwezi Aprili, 2014 mapato ya kodi yalifikia shilingi bilioni 7,771.5 sawa na asilimia 75 ya makadirio; mapato yasiyo ya kodi yalifikia shilingi bilioni 425.5 sawa na asilimia 57 ya lengo; mapato ya halmashauri yalifikia shilingi bilioni 252.8 sawa na asilimia 66 ya lengo.

Mheshimiwa Spika, inatarajiwa kuwa, hadi kufikia mwisho wa mwezi Juni mwaka huu, makusanyo ya mapato yanayotokana na kodi yatafikia asilimia 93 ya lengo. Hii ina maana kwamba nakisi ya makusanyo itakuwa asilimia 7 sawa na shilingi bilioni 728. Kwa uelewa huo, Kamati imefanya  makadirio ya nakisi kwa vyanzo vingine vya mapato ya ndani hadi itakapofikia mwisho wa mwaka wa fedha kwa kuzingatia mwenendo wa miezi kumi hadi sasa, kwa sharti kwamba mwenendo huo wa makusanyo utaendelea kuwa kama ulivyo sasa. Matazamio ya mwenendo wa mapato hadi mwisho wa mwaka yameoneshwa kwenye jedwali Na. 3 ya Taarifa hii.

Jedwali Na. 3: Makadirio ya Makusanyo ya Mapato hadi kufikia Juni, 2014.
Aina ya Kodi
Lengo la mwaka
(trilioni)
Makusanyo ya Miezi 10
(trilioni)
Matarajio/Makisio ya Mieizi 12 (trilioni)
Asilimia ya Marajio ya Makusanyo ya miezi 12
(trilioni)
Nakisi ya Makusanyo
(trilioni)
Mapato ya kodi
10.4
7.772
9.672
93
0.728
Mapato yasiyo ya kodi
0.741
0.426
0.510
69
0.229
Mapato ya halmashauri
0.383
0.252
0.303
79
0.081
JUMLA NDOGO
1.038
Mikopo na misaada ya kibajeti
1.163
0.734
0.881
76
0.279
Mifuko ya kisekta
0.641
0.367
0.440
69
0.199
Mikopo na misaada ya miradi ya maendeleo
1.86
1.2
1.44
77
0.61
Mikopo ya kibiashara ya ndani
1.699
1.804
2.165
127
+0.459
Mikopo ya kibiashara kutoka nje
1.156
0.671
0.805
70
0.347
JUMLA NDOGO
0.976
JUMLA KUU
2.014
Chanzo: Hotuba ya Bajeti ya Mwaka wa fedha 2014/15

Mheshimiwa Spika, kama inavyoonekana kwenye jedwali Na.3, inakisiwa kwamba mpaka mwisho wa mwaka wa fedha 2013/2014, jumla ya nakisi ya Bajeti itafikia takribani shilingi trilioni 2.014, yaani mapato ambayo hayatapatikana katika mwaka wa fedha wa 2013/14.  Wakati huo huo, bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2014/15 imeongezeka kwa asilimia 8.8 (trilioni 1.6) ikilinganishwa na bajeti ya mwaka 2013/2014. Hii ina maana kwamba pamoja na kuwa Serikali itapata mapato pungufu mwaka huu wa fedha, bado inajiaminisha kupata mapato mengi zaidi mwaka huu wa fedha kufidia nakisi iliyojitokeza. Kamati inatarajia Serikali itatoa ufafanuzi kuhusu mipango madhubuti inayotoa uhakika wa kufikia malengo yaliyowekwa. Vinginevyo,  hali hii inaweza kutafsiriwa kuwa bajeti ya mwaka wa fedha 2014/2015 tayari ina pengo la shilingi trilioni 3.6, yaani shilingi trilioni 2 ambazo hazikuweza kupatikana mwaka wa fedha 2013/2014 na trilioni 1.6 ambayo imeongezeka ikilinganishwa na bajeti ya mwaka jana.

Mheshimiwa Spika, kama sehemu ya misaada na mikopo iliyosalia itapatikana kwa kiwango cha kuridhisha mpaka kufikia mwisho wa mwezi Juni, sehemu kubwa ya nakisi itatokana na mapato ya ndani, ambayo kwa makadirio ni shilingi trilioni 1.038.

Mheshimiwa Spika, madeni ya Serikali yaliyohakikiwa mwaka 2013/14 ambayo hayakulipwa na hayakuingizwa kwenye bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2014/15 yanakadiriwa kufikia shilingi trilioni 1.3 (sawa na asilimia 7.1). Ukijumlisha madeni haya ya shilingi trilioni 1.3 na pengo la shilingi trilioni 3.6 lililoelezwa hapo juu, Bajeti ya mwaka wa fedha 2014/15 ina pengo la shilingi trilioni 4.9, sawa na asilimia 24.68, karibia na asilimia 25.

Mheshimiwa Spika, Kamati inamashaka kama sera hizi za mapato zitaweza kuleta mabadiliko ya mapato yanayokusudiwa kwa mwaka wa fedha 2014/15. Kamati inashauri ni vema Serikali ipitie upya sera zake ili kubaini kiini cha tatizo yaani; Kwanini vyanzo vya mapato havikufanya vizuri? Nini kitafanya vyanzo hivi vifanye vizuri zaidi  kwa mwaka wa fedha wa 2014/15?

Mheshimiwa Spika, pamoja na kuwepo jitihada za Serikali katika kuongeza makusanyo ya kodi, bado kiwango hiki cha makusanyo si cha kujivunia sana. Katika mwaka wa fedha 2012/2013 Kamati iliishauri Serikali kuharakisha kufanya tafiti zitakazowezesha kubaini vyanzo vipya vya mapato vitakavyowezesha Serikali kukusanya mapato zaidi kwa kutumia rasilimali tulizonazo. Hatua hii ilitarajiwa kupunguza utegemezi wa bajeti.
Kamati inasikitika kuona kuwa Serikali kupitia Bajeti yake imeshindwa kuleta vyanzo vipya ambavyo vingeweza kutekelezwa katika mwaka huu na ujao wa fedha. Vile vile Kamati haijaridhishwa na kasi ya kufanyiwa kazi kwa vyanzo vilivyopendekezwa katika taarifa ya Kamati ya Spika ya Mapato ijulikanayo kama Chenge I. Baadhi ya vyanzo vipya vya kodi ambavyo Kamati inaamini vinaweza kuingizia serikali mapato mengi mara moja ni pamoja na: uvuvi wa bahari kuu; kupiga mnada vitalu vya misitu na vya uwindaji wa kitalii; kupiga mnada masafa ya mawasiliano; kodi za majengo n.k.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa uvuvi wa Bahari Kuu, Kamati inashangazwa na sababu inayotolewa na Serikali kwamba hatuwezi kukusanya mapato hayo hadi hapo Serikali  itakapojenga bandari maalum ya uvuvi (fish port) wakati kwa taarifa rasmi za serikali zilizotolewa Bungeni, Serikali inapoteza takribani Dola za Marekani milioni 222 sawa na Shilingi bilioni 372,960. Kamati inahoji, hadi hapo tutakapojenga bandari maalum ya uvuvi, tutakuwa tumepoteza mapato kiasi gani? Kamati inahimiza mapendekezo yaliyotolewa kwenye Chenge 1 yatekelezwe.
4.1.1   Maduhuli
Mheshimiwa Spika, bado Serikali haijaweza kufanya vizuri sana katika makusanyo ya mapato yasiyotokana na kodi. Kwa muda sasa baadhi ya Wizara, Idara na wakala mbalimbali wa Serikali hazijaweza kukusanya maduhuli kiasi cha kufikia malengo waliyowekewa.  Zaidi ya robo tatu ya Wizara, Idara na wakala za Serikali hazikuweza kufikia malengo ya makusanyo kwa asilimia 50 hadi kufikia mwezi Machi mwaka huu.
Mheshimiwa Spika, zipo baadhi ya Wizara ambazo sehemu ya bajeti yake inategemea makusanyo ya maduhuli. Kutofanya vizuri katika ukusanyajii wa maduhuli husika kuna athari ya moja kwa moja katika bajeti zao. Baadhi ya Wizara na Idara hizo ni kama vile Wizara ya Ardhi, Wizara ya Mambo ya Nje, Wizara ya Nishati na Madini, Wizara ya Maliasili na utalii, Wizara ya Mambo ya Ndani, Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Jeshi la Magereza, Jeshi la Polisi na Jeshi la Zimamoto.
Mheshimiwa Spika, angalizo la Kamati kwa Serikali kuhusu ukusanyaji wa maduhuli linatokana na ukweli kwamba maduhuli ni sehemu ya mchango wa bajeti ya Serikali. Udhaifu uliojionesha katika eneo hili unachangiwa kwa kiasi kikubwa na Wizara na Taasisi zinazokusanya maduhuli kutotimiza malengo yake ipasavyo na hivyo kupunguza mapato ya Serikali. Aidha, Kamati imebaini kuwepo kwa tatizo katika uwekaji wa malengo ya ukusanyaji wa maduhuli, ambapo malengo ya maduhuli hayazingatii hali halisi ya ukusanyaji kwa kufanywa malengo makubwa sana ama madogo sana ikilinganishwa na uwezo wa kukusanya.
Mheshimiwa Spika, Kamati inaishauri Serikali kuweka viwango halisia na kusimamia ukusanyaji wa maduhuli hayo kama Sheria ya Fedha ya mwaka 2001 inavyoelekeza. Aidha, Kamati inarejea wito wake kwa maafisa masuuli kuhakikisha kwamba jukumu la kukusanya maduhuli waliyopangiwa linapewa kipaumbele kama majukumu mengine ili Serikali ipate mapato stahiki. Ni wakati sasa kwa Serikali kuanza kuchukua hatua stahiki kwa mashirika na Taasisi za Serikali ambazo zinashindwa kukusanya maduhuli kama inavyotakiwa. Aidha, Kamati inaomba Bunge lipewe matokeo ya utafiti wa eneo maduhuli uliokuwa ukifanywa na Wizara ya Fedha kwa madhumuni ya kuboresha makusanyo katika eneo hilo.
Mheshimiwa Spika, Serikali ilifanya mabadiliko ya sheria ya Fedha za Umma  Sura ya 348, Sheria ya Msajili wa  Hazina Sura 148 na Sheria ya Wakala wa Serikali sura 245 ili kuweka sharti la wakala na Taasisi za Serikali kuwasilisha Hazina kiasi cha asilimia 10 ya mapato ghafi badala ya mapato ya ziada. Kamati inaipongeza Serikali kwa hatua hii, kwani imepelekea mashirika haya kuchangia zaidi katika mfuko mkuu wa Serikali.
4.1.2   Misaada na Mikopo
Mheshimiwa Spika, kama inavyofahamika nchi yetu ni miongoni mwa nchi zinazoendelea duniani. Mbali na mapato ya ndani, Bajeti ya Serikali hutegemea misaada na mikopo kutoka kwa washirika mbalimbali wa maendeleo.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa za Wizara ya Fedha, wafadhili wamejitahidi kutekeleza ahadi zao. Hata hivyo kwa upande wa fedha za miradi, mwenendo wa utoaji wa fedha hizo umeendelea kushuka mwaka hadi mwaka kutokana na Serikali kutotimiza mchango wake katika miradi hiyo. Katika mwaka wa fedha 2013/14 ambapo Serikali imeanza kutekeleza program yake kabambe wa tekeleza kwa Matokeo Mkubwa Sasa, hali ya kusuasua kwa utoaji wa fedha imeendelea kuonekana. Hali hii ya sintofahamu inaifanya Kamati kuangalia utaratibu mwingine unaoweza kutumiwa na wafadhili katika kugharamia miradi ya maendeleo. Kikubwa hapa ni kuhakikisha utaratibu utakaotumiwa uwe wa manufaa kwa nchi na uzingatie sheria na taratibu, hususani katika uingizaji wa vitendea kazi na malighafi ambazo hazipatikani nchini.
Mheshimiwa Spika, Kamati inaungana na Serikali kuwashukuru washirika wetu wa maendeleo katika kuchangia Sehemu ya bajeti yetu. Hata hivyo, ili kuwafanya washiriki wetu waweze kukamilisha ahadi zao kikamilifu na kwa wakati, Serikali izingatie kutekeleza makubaliano na ahadi zake za kibajeti hususani kwenye bajeti ya maendeleo katika kila mradi. Hatua hii itasaidia katika kuimarisha uwezo wetu wa ukusanyaji wa mapato ambayo yatasaidia kutekeleza miradi ya kiuchumi ambayo itaiingizia nchi mapato. Kwa kufanya hivyo, nchi itakuwa imejiweka katika hatua nzuri ya kupunguza utegemezi wa bajeti. Msisitizo wa Kamati katika eneo hili ni kwamba, makusanyo yaelekezwe zaidi kwenye kugharamia na kutekeleza miradi ya maendeleo na sio matumizi ya kawaida.
Mheshimiwa Spika, ni ukweli usiopingika kuwa tuna kila sababu nchi yetu kujikwamua kutoka kwenye utegemezi kwa kuangalia namna ambavyo baadhi ya nchi ambazo miaka ya 50 tulikuwa sawa kimaendeleo; mfano Korea Kusini ambayo imefuzu kutoka kuwa nchi tegemezi na kuwa nchi iliyoendelea. Nchi hiyo na nyingine nyingi, zilitumia aina tofauti za mifumo ya kimaendeleo kama vile uchumi wa soko (market-based) na mikakati ya ajira (job creating strategies) ambazo zimewawezesha kufika walipo sasa.
Mheshimiwa Spika, tunaweza tu kufikia malengo yetu ya kimaendeleo kama tutasimamia misingi iliyo imara. Ninukuu maneno ya Bw. Kofi Annan aliyesema:-
"The determination of Africans, and genuine partnership between Africa and the rest of the world, is the basis for growth and development."
Tafsiri yake isiyorasmi ni kwamba “'Uamuzi wa Waafrika wenyewe, na ubia wa kweli kati ya Afrika na maeneo mengine ya dunia, ndiyo msingi wa ukuaji wa uchumi na maendeleo.’’
Mheshimiwa Spika, maneno hayo yanatuongoza tu katika kuhakikisha kwamba tunatumia misaada vizuri ili kujiendeleza kiuchumi na hivyo kupunguza umaskini kama ambavyo sehemu ya malengo ya misaada hiyo yanavyoonesha.

4.1.3   Mikopo ya ndani na mikopo yenye masharti ya kibiashara
Mheshimiwa Spika,Kamati yangu inatambua jitihada za Serikali katika kutafuta fedha maeneo mbalimbali kwa ajili ya kuendeleza miradi ya maendeleo pamoja na kulipia madeni. Pamoja na ukweli kwamba mikopo ya masharti ya kibiashara ina riba kubwa ikilinganishwa na ile isiyo ya kibiashara, mikopo hii ndiyo iliyo na uhakika na uharaka katika upatikanaji wake. Katika kipindi cha Julai 2013 hadi Aprili, 2014 Serikali ilikopa shilingi bilioni 1,803.9 kutoka soko la ndani ambapo kiasi cha shilingi bilioni 690.6 ni kwa ajili ya kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo.
Mheshimiwa Spika, Kamati inaendelea kusisitiza kwamba mikopo yote (yaani mikopo nafuu na mikopo yenye masharti ya kibiashara) ielekezwe katika miradi ya maendeleo ili iweze kuleta tija badala ya fedha hizo kutumika kwa matumizi ya kawaida. Tujikumbushe mfano rahisi wa Mpango wa Marshal ulipokuwa unaanzishwa mwaka 1947, ambapo nchi nyingi za Ulaya ziliamua kuanza kupokea misaada kutoka vyanzo tofauti. Katika hali hiyo Benki ya Dunia ikaona kuwa inakabiliwa na ushindani na hivyo kuamua kubadili mwelekeo wake kwa nchi zisizokuwa za Ulaya. Hadi kufikia mwaka 1968, mikopo yake ilikuwa inatengwa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya kuzalisha mapato, kama vile bandari, mifumo ya barabara, na mitambo, ambayo ilikuwa ikizalisha mapato ya kutosha ili kuziwezesha nchi zinazokopa kulipa mkopo kupitia miradi hiyo.
Mheshimiwa Spika, zipo baadhi ya nchi ambazo zimefanikiwa kwa kutumia utaratibu huu. Tanzania tunachelewa wapi kuamua kufuata njia walizofuata wenzetu? Wakati wa kubadilika ni sasa, tukiendelea kusubiri muda hautusubiri, idadi ya watu inazidi kuongezeka na mahitaji, matatizo na changamoto pia vitazidi kuongezeka.
4.1.4   Maoni ya Kamati kuhusu makusanyo yaliyotokana na Hatua za Kodi zilizopendekezwa na Serikali kwa mwaka 2013/14.
            Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/14 Serikali ilifanya marekebisho katika maeneo 22 ya mfumo wa kodi, yaliyotarajia kuiingizia Serikali kiasi cha shilingi milioni 970,516.0 katika kipindi cha Julai hadi April 2014. Kati ya maeneo hayo 22 ni maeneo 11 tu ndio yaliweza kukusanya mapato kwa zaidi ya asilimia 70, maeneo 9 yalikusanya mapato kwa kiwango cha chini ya asilimia 70. Wakati huo huo maeneo 3 hayakukusanya mapato yoyote.
            Mheshimiwa Spika, pamoja na kutoridhika na ukusanyaji wa kodi kwa ujumla, hususan katika kipindi cha mwaka 2013/14, Kamati ilifarijika na hatua ya ukusanyaji wa kodi katika maeneo matano yafuatayo:-
Jedwali Na. 4: Makusanyo yaliyopatikana hadi April, 2014 kutokana na marekebisho ya viwango vya kodi
Na
Tax reform
Budget
Target YTD April, 2014
Actual YTD April, 2014
% Perfomance
1
Increase excise duty on non-utility vehicles aged more than 10 years from 20% to 25%
2,937.4
2,447.9
7,822.3
320%
2
Impose withholding tax on service at a rate of 5%
30,253.8
25,211.5
26,724.2
106%
3
Excise duty at 15 percent on fixed and wireless phones airtime
1,753.4
1,461.2
1,461.2
100%
4
Adjustment of specific Excise Duty rates for non-petroleum producs by 10%
55,580.2
46,316.8
43,537.8
94
5
Introduce petroleum fee (REA) of Tsh. 50/ltr on MSP, GO & IK Products respectively.
136,095.0
113,412.5
104,792.8
92
             Chanzo: Wizara ya Fedha, 2014
          Mheshimiwa Spika, ukusanyaji wa mapato kwa maeneo tajwa hapo juu kumesaidia Serikali kupata mapato ambayo kimsingi yasingeweza kupatikana kama marekebisho hayo yasingefanyika. Eneo la kodi zilizokusanywa kwa magari chakavu ambalo limewezesha Serikali kukusanya mapato kwa asilimia 320, limeonyesha kufanya vizuri na limeashiria ni kwa jinsi gani ushuru wa bidhaa zinazokataliwa (reject goods) unavyoweza kuleta matunda kwa baadhi ya maeneo. Pamoja na kwamba ushuru wa bidhaa umefanya vizuri katika eneo hilo la ukusanyaji wa mapato kutokana na magari chakavu, athari yake itaonekana kwa jamii kwa kuwa inasababisha uchafuzi wa hali ya hewa na kushusha kipato cha mwananchi wa kawaida ambaye hupoteza kiasi kikubwa cha fedha kwenye kununua vipuri. Ni wakati sasa wa Serikali kufikiria kushusha viwango vya kodi kwa magari mapya ili kuwezesha wananchi kununua magari hayo na hivyo kuondokana na athari zitokanazo na matumizi ya magari chakavu kama vile uchafuzi wa mazingira na ununuzi wa vipuri mara kwa mara. Pamoja na hayo Kamati ina taarifa kwamba hatua ya serikali kuongeza kodi kwa magari  yenye umri wa zaidi wa miaka 10 ili kupunguza uingizaji wake, wauzaji walishusha zaidi bei ili yaendelee kuwa nafuu kwa wanunuzi wa Tanzania, ikizingatiwa pia kuwa Tanzania ni mnunuzi pekee wa magari yenye umri mkubwa katika Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Spika, Aidha, kwa upande wa kodi zilizokunywa kutokana na ushuru wa mafuta ya taa na dizeli, ni eneo jipya kabisa na limeweza kuonyesha kufanya vizuri pia. Hivyo, ni maoni ya Kamati kwamba maeneo hayo na mengine ambayo hayakufanya vizuri yakiwekewa msukumo zaidi katika ufuatiliaji yataiwezesha Serikali kukusanya mapato zaidi.
            Mheshimiwa Spika, kwa upande wa kodi zilizotakiwa kutozwa baada ya kuondoa misamaha ya kodi kwenye sukari, mchele na ngano hakuna kodi yoyote iliyokusanywa kutoka katika bidhaa hizo. Hali hii imesababisha matarajio ya Serikali kutofikiwa kabisa. Hata hivyo, Kamati imeshindwa kuamini kama ni kweli bidhaa hizo hazikuingizwa nchini katika kipindi hicho kutokana na kuwepo kwa malalamiko kuhusu uwepo wa bidhaa hizo hususan sukari ambayo imezagaa kwa kiasi kikubwa katika maeneo mbalimbali nchini. Hivyo, Kamati inaamini kuwa bidhaa hizo zimeingizwa nchini kwa njia ya ujanja bila kutozwa kodi na hivyo kuisababishia Serikali hasara ya ukosefu wa mapato.
Mheshimiwa Spika, kwa msingi huo, Kamati inaishauri Serikali kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika maghala yanayohifadhi bidhaa hizo, ili kubaini tarehe zilipoingizwa bidhaa hizo na kama zililipiwa kodi. Aidha, Serikali iimarishe ulinzi kwenye mipaka yake, pamoja na ukaguzi wa bidhaa bandarini ili kuepusha uingizaji wa bidhaa nchini bila kulipiwa ushuru.
4.2      MWENENDO WA MATUMIZI
4.2.1   Matumizi ya Serikali kwa ujumla
Mheshimiwa Spika, matumizi ya Serikali bado ni changamoto kubwa katika utekelezaji wa bajeti. Kamati imebaini kuwa matumizi ya Serikali yamekuwa yakiongezeka mwaka hadi mwaka na kwamba ni makubwa kuliko mapato. Hali hii imechangiwa na kutokuwepo kwa nidhamu katika matumizi, hali ambayo imejidhihirisha zaidi katika upande wa manunuzi. Pamoja na kuanza kutumika kwa Sheria mpya ya Manunuzi ya mwaka 2011,  bado manunuzi mengi yamekuwa yakifanyika bila tija. Mfano manunuzi ya dharula yaliyofanywa na Mamlaka ya Bandari Tanzania ambayo hayakupata kibali cha Mlipaji Mkuu wa Serikali[2].Manunuzi hayo yalikuwa na gharama ya Dola za Kimarekani 810,000.
Mheshimiwa Spika, tatizo la kutosimamia kwa umakini matumizi ya serikali ulisababisha bajeti ya mwaka 2013/14 kuanza na deni (expenditure float) la    shillingi billion 611.4 ambayo ni matumizi ya mwaka wa fedha 2012/13 lakini hayakulipwa mwaka huo na deni hili halikuingizwa kwenye bajeti ya 2013/14. Hali hii inatarajiwa pia kujitokeza tena kwa kiwango kikubwa zaidi kwenye bajeti ijayo ya mwaka 2014/15. Malimbikizo ya madai hayo hadi Desemba 2013 yalikuwa yamefikia shilingi trillion 2.09[3], ambayo ni asilimia 4 ya pato la taifa. Tatizo hili ni lazima litafutiwe dawa haraka.
Mheshimiwa Spika, maeneo mengine yaliyobainika kuwepo kwa matumizi mabaya ya fedha kwenye baadhi ya miradi ni pamoja na: utekelezaji wa miradi chini ya kiwango; miradi kukabidhiwa bila kukamilika; miradi kutumia fedha zaidi ya viwango vilivyoidhinishwa; taasisi kubadili bei za mikataba ya miradi; na baadhi ya miradi iliyokamilika kutotumika kutoa huduma kwa walengwa kama ilivyopangwa[4]. Pia utoaji fedha kwenda kwenye miradi haukuzingatia vipaumbele vilivyowekwa, kukubalika na kupitishwa.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/14 utekelezaji wa bajeti katika baadhi ya mafungu ulifanyika kinyume na matarajio ya Serikali. Yapo baadhi ya mafungu ambayo hayakutengewa fedha lakini walipewa fedha nje ya bajeti za fungu husika. Hali hii ilisababisha baadhi ya mafungu ambayo yalikuwa yametengewa fedha kutopelekewa fedha kama walivyopangiwa. Mafungu ambayo yalipokea fedha nje ya bajeti za Mafungu hayo yameoneshwa katika Jedwali Na.5 ya Taarifa hii:
Jedwali Na.5: Ulinganisho wa Fedha zilizoidhinishwa na zile zilizotumika kwa baadhi ya Mafungu kwa mwaka 2013/14

FUNGU
FEDHA ILIYOIDHINISHWA  – 2013/14
FEDHA ILIYOTUMIKA – 2013/14
ONGEZEKO
SABABU YA ONGEZEKO
1
Fungu 28 : Wizara ya Mambo ya Ndani – Polisi
149.6 Bil
157.79 Bil
8.2 Bil=157.79%
Maboresho ya Jeshi la Polisi ikijumuisha mafunzo na vitendea kazi
2
Fungu 31 : Ofisi ya Makamu wa Rais
38.68 Bil
53.11Bil
14.4 Bil = 137%
Kugharamia mahitaji ya ziada ya transfer to Zanzibar (PAYE)
3
Fungu 34: Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa
103.46 Bil
120.11 Bil
16.65 Bil =116%
Kugharamia mahitaji mapya ya balozi za Comoro na the Hegue pamoja na safari za viongozi
4
Fungu 38: Ngome
184.5 Bil
198.16 Bil
13.7 Bil =107%
Kulipa Ration allowance
5
Fungu 42: Mfuko wa Bunge
100.0 Bil
112.45 Bil
12.45 Bil =112%
Kugharamia Bunge la Katiba
6
Fungu 56: TAMISEMI
180.58 Bil
186.35 Bil
5.8 Bil = 103%
Kugharamia matengenezo ya barabara  (Road fund) na mfumo wa EPICOR 9
7
Fungu 96: Wizara ya Mawasiliano, Utamaduni na Michezo
8.37 Bil
9.62 Bil
1.25 Bil =115%
Kulipia Deni la TBC Bunge na Maadhimisho ya Sherehe za Muungano
8
Fungu 98: Wizara ya Ujenzi
359.99 Bil
403.35 Bil
43.36Bil = 112%
Kugharamia matengenezo ya Barabara (Road Fund)

                         JUMLA
1,125.18 Trilioni
1,240.94 Trilioni
115.81 Bilioni *

Chanzo: Wizara ya Fedha,2014
Mheshimiwa Spika, kwa ujumla mafungu hayo yalitumia fedha za ziada kiasi cha shilingi bilioni 115.81 ambacho ni sawa na asilimia 10.3 ya jumla ya fedha ambayo iliidhinishwa kwa mafungu hayo katika mwaka wa fedha 2013/14.
Mheshimiwa Spika, kiasi hicho cha matumizi ya ziada kimetumika ndani ya miezi tisa ya utekelezaji wa Bajeti. Kutokana na Jedwali Na. 5 ni dhahiri kuwa bajeti za mafungu hayo ziliandaliwa bila kuzingatia mahitaji halisi kwenye mafungu hayo  isipokuwa kwa mafungu ya Fungu 28 – Jeshi la Polisi na Fungu 38 – Ngome ambayo yaliomba fedha za nyongeza wakati wa kupitisha bajeti zao lakini Hazina walishindwa kuridhia kutokana na ufinyu wa bajeti.
Mheshimiwa Spika, kwa Fungu kama vile Fungu 98 – Wizara ya Ujenzi ambalo katika kipindi hicho limetumia fedha za ziada ambazo zingeweza kuwa bajeti ya Wizara mbili, limekuwa miaka yote likitumia bajeti zaidi ya ile iliyoidhinishwa na Bunge. Kamati inauliza je, ni miaka yote Wizara hii inashindwa kuweka viwango halisi na sahihi vya shughuli zao?.
Mheshimiwa Spika, angalizo la Kamati kuhusiana na matumizi hayo nje ya bajeti halimaainishi kwamba mahitaji hayo yasingegharamiwa, bali ni msisitizo kuhusu umuhimu wa uandaaji wa bajeti halisia (realistic budget) na nidhamu ya matumizi. Lakini pia linaikumbusha Serikali kuhusu ushauri ilioutoa mwaka jana kuhusiana na usimamizi wa utekelezaji wa Bajeti, ambapo Kamati iliishauri Serikali kabla ya kuhaulisha (reallocate) fedha kutoka fungu moja kwenda jingine iwasiliane na Kamati ya Bajeti katika msingi ule ule wa mashauriano baina ya Bunge na Serikali ili kuhakikisha nidhamu ya bajeti  inazingatiwa.
Mheshimiwa Spika, iwapo maafisa Masuuli watashindwa kuweka viwango vya mahitaji yao kibajeti kuwa halisia, na iwapo Hazina itashindwa kuridhia fedha ambazo zinaombwa kama nyongeza kwa mafungu wakati wa kufanya mashauriano na Kamati ya Bajeti basi, matumizi nje ya bajeti halisia yatastahili kudhibitiwa kwa kuanzisha sheria ya bajeti.
4.2.2   Deni la Taifa
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/2013 jumla ya shilingi trilioni 2.735 zilitengwa kwa ajili ya kugharamia deni la Taifa. Hata hivyo, kiasi cha shilingi trilioni 3.341 zilitumika katika mwaka huo kugharamia deni hilo. Ugharamiaji wa deni hilo katika mwaka huo ni sawa na ongezeko la shilingi bilioni 606 ambalo halikuwa kwenye bajeti. Hata hivyo, ongezeko hilo ni pungufu kidogo ya ongezeko lililotumika katika mwaka wa fedha 2011/12 ambalo lilikuwa shilingi Bilioni 624. Kamati hairidhishwi na utaratibu huu.
Mheshimiwa Spika, ripoti ya CAG[5], imebaini kuwa uhakiki wa mseto wa Deni la Taifa umebaini akaunti saba (7) za wafadhili wanaodai Serikali zenye thamani ya Sh. 1.247 trilioni ambazo hazikufanyiwa malipo yoyote tokea mwaka 1998. Maelezo yaliyotolewa kuhusu akaunti hizo ni kwamba, malipo yake yamesimama kwa sababu mazungumzo kati ya Serikali na wafadhili yanaendelea kwa nia ya kuipatia Serikali nafuu ya madeni na hata pengine kuyafuta kabisa. Pamoja na kutolewa kwa maelezo hayo, hakuna vielelezo vyovyote vilivyotolewa kuthibisha kuwepo kwa mazungumzo hayo. Hali hii inaonesha kutokuwepo kwa uwajibikaji kuhusiana na madeni yetu.
Mheshimiwa Spika, Deni la Taifa hadi kufikia Machi, 2014 lilikuwa limefikia shilingi trilioni 30.563 ikilinganishwa na shilingi trilioni 23.67 mwezi Machi, 2013. Pamoja na sababu zilizotolewa na Serikali[6], Kamati hairidhishwa na usimamizi wa deni hilo kwa ujumla. Pia Kamati inaendelea kuishauri Serikali kuharakisha uanzishwaji wa Idara ya Usimamizi wa Deni la Taifa.
4.2.3   Malimbikizo ya Madai (watumishi na wazabuni)
Mheshimiwa Spika, lipo tatizo kubwa la malimbikizo ya madeni katika Wizara na Idara za Serikali. Katika hali ya kawaida, inatazamiwa kwamba Wizara na Idara za Serikali zitatumia fedha kulingana na bajeti iliyopangwa. Hata hivyo, hali hii imekuwa haitekelezeki kwa sababu mbalimbali zikiwemo ucheleweshwaji katika upatikanaji wa fedha za Bajeti. Endapo Wizara na Idara zitaendelea kutumia huduma, ama kulazimika kufanya hivyo bila kulipia, hali hii hutengeneza deni ambalo kama fedha za mwaka husika zisipotolewa, deni hilo huathiri bajeti inayofuata.
Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kuwa madai hayo yataachiwa mafungu husika yaingie nayo katika mwaka wa fedha ujao. Suala hili linaendelea kuathiri bajeti ya mwaka husika na hivyo kuwa changamoto kubwa katika utekelezaji wa bajeti. Kwa maana nyingine ni kwamba bajeti zetu mwaka hadi mwaka zimekuwa zikitumika kwa kiasi kikubwa kulipa madeni badala ya kutekeleza mipango iliyopangwa katika mwaka husika. Matokeo yake ni kutokamilika kwa wakati kwa miradi mingi lakini pia kuiongezea Serikali gharama pale ambapo miradi iliyopangwa kutekelezwa kuchelewa kukamilika au kutokamilika kabisa. Katika eneo hili Kamati inasisitiza juu ya umuhimu wa Serikali kuzitaka wizara na Idara za Serikali kuwa na kasma ya kulipia madeni yao kutoka katika mafungu yao ili kuondokana na utaratibu wa kuyaficha madeni hayo na kuacha yalipwe kwa kutumia bajeti ya mwaka wa fedha unaofuta.
Mheshimiwa Spika, eneo jingine lililogusa hisia za wajumbe kuhusu matumizi ni kwenye Balozi zetu zilizopo nje ya nchi. Ofisi hizi huendesha shughuli zake kwa kujitegemea na kasma zake husimamiwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. Kamati imebaini kwamba katika mwaka wa fedha 2012/13 baadhi ya balozi zilitumia fedha zaidi ya kiwango kilichoidhinishwa na Bunge. Kati ya balozi 32, balozi 16 zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu, zilionesha kutumia fedha nje ya kiasi kilichoidhinishwa na Bunge ambacho ni Shilingi bilioni 6,227,749,594 kwa malipo ya mishahara kwa watumishi waliostaafu[7] ya shilingi milioni 575.47 yaliyohusisha balozi tatu; baadhi ya watumishi kukaa zaidi ya muda wa mikataba yao ya miaka minne.
Mheshimiwa Spika, kutokana na kwamba baadhi ya Balozi zetu zimekuwa zikilalamika kuhusu ukarabati wa balozi zao lakini inashangaza kuona kwamba zinakua miongoni mwa zinazokuwa na matumizi makubwa zaidi ya kiwango wanachoidhinishiwa na Bunge. Mfano ubalozi wa Maputo ni miongoni mwa Balozi ambazo zinahitaji ukarabati katika ofisi zake na waliwasilisha maombi ya fedha za nyongeza kwa ajili ya ukarabati. Katika mwaka wa fedha, 2012/13 Ubalozi huo umetumia kiasi cha shilingi 117,400,068 nje ya bajeti iliyotengwa. Pamoja na kwamba maelezo kuhusu matumizi hayo hayakuwekwa bayana katika ripoti ya CAG, Kamati inashauri kuwa matumizi yote yanayofanyika nje ya bajeti iliyotengwa yawekwe bayana, na maafisa masuuli wazingatie kufanya matumizi yanayoendana na bajeti iliyotengwa.
Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa fedha kwa ajili ya kutekeleza majukumu ya kidiplomasia hasa sekta ya uchumi, Kamati inashauri Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kuzingatia ushauri uliotolewa na CAG kuhusu kuanzisha mfuko katika Fungu lake kwa ajili ya kufanya shughuli za diplomasia ya kiuchumi na kukuza vivutio vya utalii. Kwa kutambua kuwa Kamati imekuwa ikiihimiza Serikali kuendelea kubuni vyanzo vipya vya mapato, katika eneo hili Kamati inaona kwamba suala hili litakuwa kichocheo katika kukusanya mapato yatakayosaidia katika kugharamia mahitaji ya balozi hizo.
Mheshimiwa Spika, Kamati ya Bajeti imepokea taarifa kuhusuiana na kushindwa kufikia makubaliano kati ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii  NSSF na  Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa  kuhusu ujenzi wa majengo ya balozi zilizo nje ya nchi. Moja ya jukumu la Bodi ya Wadhamini ya Mifuko ya Jamii ni kuhakikisha kwamba mtaji unaongezeka kupitia faida zitokanazo na uwekezaji kwenye vitega uchumi mbalimbali ikiwepo milki (real estate). Hivyo, ubia baina ya Serikali na Mifuko hiyo una faida kwa pande zote mbili, kwamba Serikali itapata miundo mbinu inayohitaji kwa ajili ya ofisi na makazi ya watumishi wa balozi zake pamoja na kodi itakayolipwa kutokana na faida, na mifuko husika  itapata faida na hivyo kuongeza mtaji wao.
Mheshimiwa Spika, kwa msingi huo, Kamati inaishauri Serikali iharakishe kukamilisha mazungumzo baina ya mifuko ya hifadhi jamii na Wizara ya Mambo ya nje ili kukamilisha ujenzi wa majengo ya ofisi na nyumba za watumishi katika balozi zetu za Nairobi na Maputo. Kukamilika kwa ujenzi wa majengo hayo kutaipunguzia serikali mzigo wa kodi ya pango na itapata fedha za ziada kuhudumia balozi zetu zilizo kwenye nchi nyingine. Aidha, Serikali iharakishe kulipa deni lililobakia kwa Serikali ya New Zealand iliyotuuzia jengo nchini Ufaransa.
5.0      BAJETI YA SERIKALI KWA MWAKA 2014/15
5.1      Sura ya Bajeti
Mheshimiwa  Spika, Serikali imepanga kukusanya na kutumia jumla ya shilingi bilioni 19,853.3 kutoka vyanzo mbalimbali na kwa mahitaji yaliyoainishwa. Jedwali Na 6 (pie chart) katika Taarifa ya Kamati limetoa sura halisi ya Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2014/15 kama linavyosomeka:-
Jedwali Na.6. Sura halisi ya Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2014/15
5.2       Mapato ya Ndani
Mheshimiwa Spika, katika uchambuzi wa bajeti ya Serikali ya mwaka 2014/15 Kamati imebaini kuwa lipo tatizo la kimsingi tokea siku ya kwanza bajeti hiyo inapoanza kutekelezwa, ambalo ni kwamba:
·         Mapato yote ya ndani ni shilingi trillion 12.44;
·         matumizi yote ya kawaida ni shilingi trillion 13.408;
·         Mapato ambayo Serikali itakusanya ni asilimia 63.3 tu ya bajeti yote;
·         Nakisi ya Bajeti ya Matumizi ya Kawaida ni shilingi bilioni 968;
·         Nakisi hii haijumuishi expenditure float (wastani wa shilingi bilioni 611[8])
·         Mikopo na Misaada ya kibajeti inahitajika kulipia sehemu ya matumizi ya kawaida
·         Bajeti ya maendeleo ni shilingi trilioni 6.445
·         Nakisi hiyo inazibwa na mikopo ya ndani, mikopo ya nje na misaada ya miradi ya maendeleo
5.3       Matumizi ya Kawaida na Maendeleo
Mheshimiwa Spika, Kamati katika uchambuzi wa bajeti ya Serikali ya mwaka 2014/15 imebaini pia kuwa kuna tatizo la kimsingi kutokea siku ya kwanza Bajeti inapoanza kutekelezwa kwenye upande wa matumizi kama ifuatavyo;
  • Deni la taifa ni shilingi trilioni 4.354 ( 21.93% ya bajeti yote)
  • Mishahara ni shilingi trilioni 5.317 (26.78% ya bajeti yote)
  • Matumizi mengineyo (OC) ni shilingi trilioni 3.735 (18.82% ya bajeti yote)
  • Jumla ya Matumizi ya Kawaida ni shilingi trilioni 13.408 (67.54% ya Bajeti yote)
·         Misaada na mikopo ya kimaendeleo ni shilingi bilioni 2,019.4 (10.2%   ya bajeti yote) 

·         Misaada na mikopo ya kibajeti ni shilingi bilioni 922.2 (4.6% ya bajeti yote)

·         Mikopo ya Miradi ya maendeleo ni shilingi bilioni 1,745 (8.79% ya bajeti yote)

·         Mifuko ya pamoja ya Kisekta ni shilingi bilioni 274.1 (1.38% ya bajeti yote)

  • Miradi ya Maendeleo imetengewa shilingi trilioni 6.445 (32.46% ya bajeti yote)
Mheshimiwa Spika, Kamati ingependa Serikali itoe mchanganuo wa kuonesha  kiasi halisi cha misaada na mikopo ya kibajeti itakayopokelewa ili kuweka bayana takwimu hizo zinazoeleza kwamba misaada na mikopo ya kibajeti ni shilingi bilioni 922,168, na Mikopo na Misaada ya Miradi ya Maendelo ni shilingi bilioni 1,745.3[9] bila kuchanganua kiasi cha misaada na mikopo.
Mheshimiwa Spika, ukifuatilia kwa  makini sura ya bajeti, utaona kwamba makadirio ya makusanyo ya ndani ya shilingi trilioni 12.44 hayatoshi kugharamia mahitaji ya Mishahara (trilioni 5.317), Deni la Taifa (trilioni 4.354) na Matumizi yasiyoepukika (Trilioni 3.063) ambayo kwa ujumla yanatupa kiasi cha shilingi trilioni 12.734. Hivyo makusanyo yetu ya ndani ya kodi ni pungufu kwa shilingi trilioni 0.294.
6.0      MAONI YA KAMATI KUHUSU BAADHI YA HATUA ZA KODI ZINAZOPENDEKEZWA NA SERIKALI KWA MWAKA 2014/15
Mheshimiwa Spika, bila kuathiri maelezo yaliyotangulia, Kamati ya bajeti inaipongeza Serikali kwa kufanya maboresho ya mfumo wa kodi, ada, tozo na hatua nyingine za mapato kwa kurekebisha  sheria takribani 13 ambazo zitapelekea kuongeza mapato ya Serikali na hivyo kuweza kuhudumia wananchi  ipasavyo na kufikia malengo ya kiuchumi katika mwaka wa fedha wa 2014/15. Pamoja na hatua hizo nzuri za Serikali, Kamati ya Bajeti inatoa maoni katika maeneo yafuatayo:-
i)                    Kodi ya zuio ya asilimia 15 kwenye ada wanayolipwa wakurugenzi wa bodi kila mwisho wa mwaka iangaliwe upya kwa kuwa, Kodi ya zuio (WHT) kwa washauri binafsi ni asilimia 5 kwa kila mwisho wa mwaka.
ii)                  Kwa upande wa kiwango cha chini cha kutoza kodi ya mapato ya ajira kutoka asilimia 13 hadi asilimia 12. Kamati haijaridhika na punguzo hili, hivyo inashauri Serikali kupunguza kiwango hiki hadi kufikia tarakimu moja (single digit) kwa mwaka ujao wa fedha.
iii)                 Viwango vya ongezeko la kodi kwa wafanyabiashara wadogo kwa mapato ghafi yanayozidi shilingi milioni 4 kwa mwaka na yasiyozidi milioni 7.5 kwa mwaka kutoka asilimia 2 hadi 4 kwa mauzo kwa wenye kumbukumbu za mauzo; na kwa kuongeza kutoka laki 1 hadi shilingi laki 2 kwa wasikuwa na kumbukumbu za mauzo. Viwango hivi ni mara mbili ya viwango vya awali. Kamati ina maoni kuwa viwango hivi vitakatisha tamaa wafanyabiashara wadogo wanaolipa kodi na hivyo kutafuta mbinu za kukwepa kulipa kodi, na wale ambao bado hawajajiandikisha hawatajiandikisha kamwe na hivyo kusababisha Serikali kuokosa hata kile kidogo kilichotegemewa kupatikana. Kwa msingi huo Kamati inashauri:-
a)     Serikali kupunguza kodi iliyopendekezwa ifikie asilimia 3 badala ya 4 kwa wafanyabiashara waliosajiliwa. Kodi kwa wafanyabiashara ambao hawajasajiliwa ibakie shilingi laki moja
b)     Mazingira ya kufanyia biashara kwa wafanyabiashara wadogo wadogo yaboreshwe ili kuvutia wafanyabiashara wadogo wadogo kujitokeza na kusajiliwa.
iv)               Kubadilisha ukomo wa umri wa magari yasiyo ya uzalishaji (non-utility vehicles) yanayotozwa ushuru wa uchakavu wa asilimia 25 hivi sasa kutoka miaka kumi na zaidi kwenda miaka minane. Kamati inatambua kuwa nia ya Serikali ni kulinda mazingira ya nchi yetu, kupunguza gharama za uendeshaji na utunzaji wa magari na kupunguza ajali. Hata hivyo, Kamati inashauri Serikali kuwa na sera mahsusi ya kodi itakayohamasisha wananchi kununua magari mapya badala ya chakavu kwa kupunguza ushuru wa bidhaa kwa magari mapya.
v)                 Kuhusu Kurekebisha viwango maalum (specific rates) vya Ushuru wa Bidhaa zisizokuwa za mafuta (Non-petroleum products) kwa asilimia 10; vinywaji baridi, mvinyo, pombe, vinywaji vikali, n.k.
Kwa kuzingatia kuwa vinywaji baridi ni sehemu ya mahitaji muhimu ya binadamu, Kamati inashauri kuwa pendekezo la ongezeko la asilimia 10 kwa bidhaa hizo liondolewe. Aidha, kuhusu bidhaa za Sigara kutozwa Ushuru wa Bidhaa wa asilimia 25 ili kutekeleza matakwa ya Mkataba wa Udhibiti wa Matumizi ya Tumbaku (Framework Convention on Tobacco Control) wa Shirika la Afya Duniani, Kamati inaona kuwa kila mwaka kodi katika bidhaa hizi zinaongezeka na kulalamikiwa na wananchi. Ni vema Serikali ikatambua kuwa uvutaji wa sigara na hata unywaji pombe kwa baadhi ya watu hauwezi kuzuiwa/kupunguzwa kwa bei kubwa. Baadhi ya watu, hasa walio katika vipato vya chini, wataendelea kunywa na kuvuta kwa sababu mbalimbali kama vile addiction na msongo wa mawazo matokeo yake ni kuendelea kuongeza umasikini zaidi kwa na familia zao hasa kwa wale wa vipato vya chini. Hali kadhalika, kama hali itaendekea kuwa hivi kila mwaka kuna hatari ya Serikali kupoteza wawekezaji katika sekta hizo.
vi)               Ni muhimu kuzingatia kuwa ushuru wa leseni haupaswi kuwa kama chanzo cha mapato tu bali pia ni utambulisho na nyenzo ya kuwezesha kuanzisha, kuendeleza na kukuza biashara na hivyo  kupanua wigo wa kodi. Kamati inashauri kuwa, Serikali iangalie vizuri marekebisho ya viwango vya ushuru wa leseni za biashara inayotegemea kutoza.
vii)              kwa upande wa sheria ya forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, ni muhimu kujua hali halisi ya Tanzania katika aina mbalimbali za ushuru uliopunguzwa na kama kwa kupunguzwa kwa viwango vya ushuru huu kwa muda uliotajwa (mfano mwaka mmoja zaidi) wazalishaji wa Tanzania wanajiandaa au wanaandaliwa vipi kuweza kuwa kuumudu ushindani.

7.0                 MAONI NA USHAURI WA KAMATI
Mheshimiwa Spika, baada ya kufanya uchambuzi wa kina kuhusu Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2014/15, yafuatayo ni maoni na ushauri wa jumla wa Kamati ya Bajeti:-
7.1         Nidhamu ya matumizi ya fedha za umma
Mheshimiwa Spika, Pamoja na Serikali kuahidi kwamba itazingatia ushauri uliotolewa na Kamati kuhusu usimamizi na nidhamu ya matumizi bado hakuna mabadiliko ya kuonesha ushauri wa Kamati na Bunge lako tukufu kwamba umezingatiwa. Kamati inaendelea kusisitiza kwamba ushauri iliyotoa wakati wa kuchambua na kupitia Bajeti ya serikali ya mwaka 2013/14 ufanyiwe kazi.

Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza ushauri wa Bunge lako tukufu juu ya matumizi yasiyokuwa ya lazima, Serikali ilianzisha Ofisi ya Mkaguzi wa Ndani Mkuu kwa madhumuni ya kuimarisha  kaguzi za ndani katika wizara, idara na taasisi, sekretariati za mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Kamati za Bunge wakati zikichambua mapato na matumizi ya Serikali hazikuona mabadiliko yoyote katika kudhibiti mapato na matumizi ya Serikiali. Aidha taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali zinadhihirisha hili.

7.2      Misamaha ya Kodi
Mheshimiwa Spika, Kamati inaipongeza Serikali kwa kusikia kilio cha siku nyingi cha Wabunge kuhusiana na hatua ya kupunguza baadhi ya misamaha ya kodi ambayo haina tija. Pamoja na lengo zuri la Serikali la kupunguza misamaha ya kodi kwa hatua kufikia asilimia moja ya Pato la Taifa, Kamati inaishauri Serikali kuchukua hatua hizo bila kuathiri hatua nyingine za kuhamasisha uwekezaji nchini kama ilivyoelezwa na Serikali[10].
7.3      Madeni ya Mifuko ya Pensheni
Mheshimiwa Spika, uchambuzi wa taarifa ya CAG unaonesha kuwa Serikali imeendelea kukopa kutoka kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii kwa ajili ya kutekeleza miradi na mahitaji mbalimbali. Hata hivyo, kiasi kinachorejeshwa na Serikali ni kidogo sana. Ikumbukwe kwamba, fedha za mifuko ni za wanachama wa mifuko husika, hivyo kutorejeshwa kwa wakati kwa fedha hizo kutasababisha mifuko husika kushindwa kulipa pensheni kwa wanachama wake watakaokuwa wanastaafu kwa kiwango wanachostahili. Hadi  kufikia tarehe 30 Juni, 2013 Mifuko hii ilikuwa ikiidai Serikali takribani zaidi ya shilingi trilioni 3. Kamati inahimiza Serikali kuweka utaratibu endelevu wa kulipa madeni hayo.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa PSPF Serikali inadaiwa kiasi cha shilingi trilioni 3.3 ikiwa ni malimbikizo ya pensheni ya wanachama hadi kufikia Juni 1999. Serikali imekuwa ikilipa shilingi bilioni 50 kila mwaka ambacho ni kiasi kidogo sana ikilinganishwa na kiasi inachodaiwa. Kamati inashauri Serikali itumie utaratibu wa malipo kwa fedha taslimu na hati fungani ili kuokoa mfuko na hatari ya kufilisika. Aidha, Kamati inatambua kuwa Serikali imekuwa ikichangia asilimia 15 ya mshahara wa mtumishi kwenye mfuko wa PSPF, hata hivyo, ni maoni ya Kamati kuwa kiwango hicho ni kidogo ikilinganishwa na mzigo ambao Mfuko utabeba baada ya mtumishi kustaafu. Hivyo, Kamati inashauri Serikali iongeze kiwango cha michango kwa watumishi wa Serikali kufikia asilimia 20 ili kufanya jumla ya mchango wa wanachama kuwa asilimia 25 ya mshahara wake. 
7.4      Madeni makubwa ya Serikali 
Mheshimiwa Spika, uchambuzi wa bajeti ya serikali kwa mwaka 2013/14 umebaini kuwepo kwa madeni makubwa katika baadhi ya Wizara na taasisi za umma. Mfano Wizara ya Ujenzi ambayo imekuwa ikitekeleza miradi ya ujenzi wa barabara bila kuwalipa wakandarisi kwa wakati kwa kuzingatia mikataba yao na hivyo kujikuta ikianza kila mwaka wa fedha ikiwa na malimbikizo ya makubwa ya madeni. Hali hii imesababisha Wizara hii kutumia bajeti yake ya mwaka unaofuata kulipia madeni ya mwaka uliopita badala ya kutekeleza iliyoidhinishwa kwa mwaka wa fedha husika (current FY). Kamati inashauri Serikali itoe agizo kwa maafisa Masuuli wote kulipa madai ya wazabuni kwa wakati ili kuepuka kuzalisha madeni ambayo yanaigharimu Serikali kiasi kikubwa cha fedha na kusababisha hasara kwa wakandarasi kwa kuwapunguzia uwezo wa mitaji yao. Kwa madeni ya wizara na taasisi ikiwemo TANESCO ambayo yamelimbikizwa hadi sasa Kamati inashauri Hazina iyafanyie uhakiki na madai hayo kuyalipa mapema.
7.5      Vyanzo vipya vya mapato
Mheshimiwa Spika, uchambuzi wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2014/15 uliofanywa na Kamati umeonesha kwamba mzigo wa matumizi ni mkubwa mno ikilinganishwa na vyanzo vya mapato vilivyopendekezwa. Serikali imekosa ubunifu na haitaki kupokea ushauri kuhusiana na vyanzo vipya vya mapato, kwa kuwa imekuja na vyanzo vile vile vya kitamaduni vilivyozoeleka wakati kuna vyanzo vingine vingi. Vyanzo hivi ni pamoja na vilivyopendekezwa kwenye Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano unaoendelea, Mapendekezo ya Maabara ya BRN na Kamati ya Chenge I pamoja na mapendekezo ya Kamati ya Bajeti. Kamati inaendelea kuhimiza Serikali kufanyia kazi mapendekezo na ushauri uliotolewa ili kupunguza nakisi ya bajeti na mzigo kwa walipa kodi wale wale.
7.6      Mchango wa washirika wa Maendeleo katika bajeti ya Serikali
Mheshimiwa Spika, Washirika wa Maendeleo wamekuwa wakichangia takribani asilimia 15 ya Bajeti ya Serikali. Mwelekeo walionao hivi sasa ni wa kuhama kutoka kuchangia katika mfuko wa pamoja wa bajeti na kwenda kuchangia katika miradi ya kisekta yenye sura ya kibiashara. Kwa kutambua kuwa Bajeti ya Serikali bado ni tegemezi kwa kiasi kikubwa,  Kamati inashauri Serikali kujiandaa kupokea utaratibu huo mpya kwa kuhakisha kwamba inaainisha miradi muhimu ambayo itakuwa na matokeo makubwa ili iweze kutekeleza mara moja kupitia utaratibu huo kwa lengo kupata matokeo makubwa sasa.
7.7      Uagizaji wa bidhaa kwa pamoja (Bulk procurement)
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa utaratibu wa uagizaji wa pamoja katika sekta ya mafuta umekuwa na mafanikio makubwa, Kamati inashauri utaratibu huu utumike kwa  bidhaa nyingine zinazotoka nje kama vile sukari, mchele na saruji n.k zinazoingizwa kwa wingi.
Mheshimiwa Spika,kwa kuwa utaratibu wa bajeti kusubiri serikali ikusanye mapato kwanza ndiyo yasambazwe kwa watekelezaji huchelewesha sana utekelezwaji wa miradi na bajeti husika, Kamati inaishauri Serikali kufikiria kwa umakini na uharaka ushauri kwamba kuanzia mwaka ujao wa fedha wa 2014/15 Serikali ianzishe utaratibu kukopa ama ‘kuazima’ fedha toka vyanzo mbalimbali nafuu za kutekeleza bajeti ya serikali kwa kiwango cha kufikia walau robo moja, yaani shilingi trillion 5  ya bajeti ya mwaka. Utaratibu huu huitwa capital budget badala ya utaratibu wa cash budget, ambao umetumika kwa muda mrefu sasa wakati ulitakiwa kuwa mpango wa mpito.
Mheshimiwa Spika, kuna umuhimu mkubwa kuharakishwa kuletwa Bungeni sheria ya bajeti itakayofanya kazi sambamba na sheria ‘mpya’ ya manunuzi  ili kudhibiti  matumizi mabaya kinyume na sheria na kanuni kwa nia ya kuweka nidhamu katika utekelezaji wa bajeti ya serikali.
Mheshimiwa Spika, kuna haja ya Serikali kutazama upya ufanisi wa utoaji maamuzi stahili kwa muda. Hali hii inaligharimu sana taifa letu. Mifano iko mingi.





8.0     HITIMISHO
Mheshimiwa Spika, ukuaji wa uchumi wetu unatakiwa ushuke na uwafikie wananchi waliowengi kuliko ilivyo hivi sasa. Yanahitajika maono, dhamira na ubunifu kuweza kufanikisha lengo hili.
Mheshimiwa Spika, uchambuzi wa bajeti umeonesha kwamba bajeti imejaribu kugusa watu wa chini lakini katika mfumo ambao kwa namna fulani unaonekana kuwa na changamoto. Ni dhahiri kuwa mapendekzo ya mifumo ya kodi na tozo mbalimbali zilizoainishwa zinaonesha nia ya serikali katika kutaka kuongeza mapato lakini baadhi ya mapendekezo hayo yana ugumu ndani yake.
Mheshimiwa Spika,ongezeko la Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2014/15 kwa kiasi cha shilingi trilioni 1.605, ikilinganishwa na Bajeti ya Serikali inayomalizika ya mwaka 2013/14 linatia mashaka iwapo malengo ya ukusanyaji na matumizi yatafanikiwa. Inahitajika nidhamu kubwa ya utendaji ili kuweza kufikia malengo haya kwa upande wa Serikali.
9.0   SHUKRANI
Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua fursa hii kukushuruku kwa mara nyingine kwa kunipa fursa hii ili niweze kuwasilisha taarifa hii mbele ya Bunge lako Tukufu. Napenda nimshukuru Waziri wa Fedha, Mhe. Saada Mkuya, Mb, Naibu Waziri wake Mhe.  Adam K. Malima, Mb na Mhe. Mwigulu L. Nchemba, Mb .kwa ushirikiano wao walioutoa kwa Kamati. Namshukuru pia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Mahusiano na Uratibu Mhe Stephen Wassira , Mb kwa kushirikiana vyema na Kamati. Nawashukuru pia wataalamu wote kutoka Hazina na Tume ya Mipango ambao walishirikiana na Kamati katika hatua zote za kujadili na kuchambua utekelezaji wa bajeti ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, napenda kuwashukuru Wajumbe wa Kamati hii kwa umakini wao katika kujadili na kutoa mapendekezo mbalimbali yaliyohusu uchambuzi wa Bajeti ya Serikali.  Naomba kuwatambua Wajumbe hao kama ifuatavyo;
1.      Mhe. Andrew J. Chenge, Mb          -           Mwenyekiti
2.      Mhe. Dr Festus B. Limbu, Mb              -           Makamu Mwenyekiti
3.      Mhe. Amina Amour, Mb                    -           Mjumbe
4.      Mhe. Dr. Cyril Chami, Mb                  -                      
5.      Mhe. John M. Cheyo, Mb                 -                      
6.      Mhe. Mansoor Hiran, Mb                   -                      
7.      Mhe. Josephat Kandege, Mb          -                      
8.      Mhe. Christina M. Lissu, Mb                -                      
9.      Mhe James Mbatia, Mb                    -                      
10. Mhe. Godfrey W. Mgimwa, Mb       -                      
11. Mhe Assumpter Mshama, Mb          -                      
12. Mhe. Dkt. Goodluck J. Ole-Medeye, Mb  -          
13. Mhe. Hamad Rashid, Mb                  -                      
14. Mhe. Kidawa Saleh, Mb                     -                      
15. Mhe. Joseph Selasini, Mb                  -                      
16. Mhe. Saleh Pamba, Mb                     -                      
17. Mhe Beatrice Shelukindo,Mb           -                      
18. Mhe Ritha Mlaki, Mb                           -                      
19. Mhe Peter Serukamba, Mb               -                      
Mheshimiwa Spika, napenda kutumia fursa hii kukuhakishia wewe, Bunge lako Tukufu, na Watanzania kwa ujumla kwamba kazi iliyokuwa mbele yetu haikuwa rahisi, ilikuwa ngumu sana, ukizingatia kuwa Kamati hii ni mpya. Kamati imefanya kazi kwa kujituma, kwa muda mrefu mfululizo bila kupumzika. Ninapenda kuchukua fursa hii pia kumshukuru Katibu wa Bunge Dr. Thomas Kashililah na watumishi wote wa Ofisi ya Bunge kwa kuiwezesha Kamati kutekeleza majukumu yake vizuri. Aidha, napenda kuishukuru Sekretarieti ya Kamati inayoongozwa na Ndugu Elisa D. Mbise na Makatibu wa Kamati Ndugu Lina Kitosi, Ndugu Michael Chikokoto na Michael Kadebe kwa kuihudumia vema Kamati hadi kukamilika kwa taarifa hii.
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha, na naunga mkono hoja.



Andrew J. Chenge, Mb
MWENYEKITI
KAMATI YA BUNGE YA BAJETI
16 Juni, 2014



[1] Wasilisho la Mark Suzman, rais wa Global Policy and Advocacy at Bill and Melinda Gates katika mkutano wa Jukwaa la Uchumi wa Africa
[2]  Taarifa ya CAG kuhusu ukaguzi wa Mashirika ya Umma,2012/13.
[3] Taarifa ya Waziri wa Fedha kuhusu utekelezaji wa Bajeti kwa kipindi cha nusu mwaka 2013/14,
[4] Maelezo ya Waziri wa fedha akijibu hoja za Kamati ya Bajeti, 28 Mei, 2014.
[5] Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Fedha za Serikali Kuu kwa Mwaka ulioishia Tarehe 30 Juni, 2013. Uk.97-98.

[6]  Hotuba ya Waziri wa Fedha, 2014/15. Uk 18
[7] Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Fedha za Serikali Kuu kwa Mwaka ulioishia Tarehe 30 Juni, 2013. Uk.219
[8] Kama ilivyokuwa katika mwaka huu wa fedha wa 2013/2014; kuna taarifa kuwa kiwango kinaweza kuwa mara mbili ya kiasi hiki
[9] Hotuba ya Waziri wa Fedha  Kuhusu makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2014/15, ukurasa wa 66. Jedwali 2a
[10]  Hotuba ya Waziri Mkuu akiwasilisha Bungeni  Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi yake kwa mwaka wa fedha 2014/15. Aya 35.Uk. 26
 

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa