WAZIRI
wa Fedha, Bi. Saada Mkuya Salum, jana aliwasilisha Bajeti Kuu ya
Serikali bungeni Mjini Dodoma, kwa mwaka wa fedha 2014/15 ambayo ni
zaidi ya sh. trilioni 19.8 ikiongeza makali ya kodi kwenye bia na
sigara.
Katika bajeti hiyo,
watumiaji pombe kali na juisi za matunda ambayo yanazalishwa nchini,
wameguswa na makali hayo pamoja na kudaili ukomo wa umri wa magari
yanayopaswa kuingizwa nchini kutoka miaka 10, hivi sasa yataanzia miaka
minane kushuka chini.
Bi. Salum alisema lengo
la Serikali ni kulinda mazingira, kupunguza wimbi la uagizaji magari
chakavu ambayo yanasababisha ajali, vifo na kuongeza gharama kwa kutumia
fedha za kigeni kuagiza vipuri mara kwa mara.
Alisema Serikali
imebadilisha ukomo wa umri wa magari ya uzalishaji na yasiyobeba abiria
yanayotozwa ushuru wa uchakavu asilimia tano kutoka miaka 10 na zaidi
hadi minane kushuka chini.
Upande wa matrekta,
alisema hayatatozwa kodi na wale wanaoingiza mabasi ya kubeba abiria,
watatozwa kodi ya asilimia 10 tofauti na awali ambapo walitozwa asilimia
25. Lengo la hatua hiyo ni kurahisisha usafiri wa abiria na kuwawezesha
wananchi kupata unafuu.
Hatua zingine
zilizochukuliwa na Serikali ni kurekebisha viwango maalum vya ushuru wa
bidhaa zisizokuwa za mafuta kwa asilimia 10 ambazo ni vinywaji baridi,
mvinyo, pombe na vinywaji vikali.
Alisema bidhaa za
sigara zitatozwa ushuru wa bidhaa asilimia 25 ili kutekeleza matakwa ya
Mkataba wa Udhibiti wa Matumizi ya Tumbaku wa Shirika la Afya Duniani
ambapo Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizoridhia mkataba huo.
Ushuru wa vinywaji
baridi, Bi. Salum alisema umeongezeka kutoka sh. 91 kwa lita hadi sh.
100 kwa lita ikiwa ni ongezeko la sh. 9 kwa lita ambapo ushuru wa bidhaa
kwenye maji ya matunda (juisi) ambayo imetengenezwa kwa matunda
yanayozalishwa nchini, umepanda kutoka sh. 9 kwa lita hadi sh. 10 kwa
lita.
Upande wa bia, ushuru
wa bia inayotengenezwa kwa nafaka za Tanzania ambayo haijaoteshwa kama
vile Kibuku, umepanda kutoka sh. 341 kwa lita hadi sh. 375.
Ushuru wa bia nyingine
zote umeongezeka kutoka sh. 578 kwa lita hadi sh. 635 kwa lita ambapo
ushuru wa mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu inayozalishwa nchini kwa
kiwango kinachozidi asilimia 75, umeongezeka kutoka sh. 160 kwa lita
hadi sh. 176.
Alisema ushuru wa
mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu inayozalishwa nje ya nchi kwa kiwango
kinachozidi asilimia 25, umeongezeka kutoka sh. 1,775 kwa lita hadi sh.
1,953 kwa lita ikiwa ni ongezeko la sh. 178 kwa lita na ushuru wa
vinywaji vikali, umepanda kutoka sh. 2,631 kwa lita hadi sh. 2,894 kwa
lita.
Ushuru wa Mafuta
Akizungumzia Sheria ya
Ushuru wa Mafuta, Sura 220, Bi. Salum alisema anapendekeza kufanya
marekebisho katika Sheria hiyo, ili kuondoa mamlaka ya Waziri wa Fedha
kutoa msamaha wa Ushuru wa Mafuta, isipokuwa misamaha inayotolewa kwenye
mikataba iliyosainiwa baina ya Serikali na washirika wa maendeleo ili
kutekeleza miradi ya maendeleo kama vile miundombinu ya barabara, maji
na mingine.
Mikopo
Kuhusu mikopo ya
kibiashara ndani na nje, alisema kwa kuzingatia mahitaji makubwa ya
kuendeleza miradi ya miundombinu nchini, Serikali itaendelea kukopa
mikopo yenye masharti ya kibiashara kutoka ndani na nje ya nchi kwa
ajili ya kugharamia bajeti ya maendeleo.
Alisema mwaka 2014/15,
Serikali inategemea kukopa katika soko la ndani sh. bilioni 2,955.2 kati
ya hizo, sh. bilioni 689.56 sawa na asilimia 1.1 ya Pato la Taifa ni
kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo na sh. bilioni 2,265.7
kulipia hatifungani na dhamana za Serikali zinazoiva kwa utaratibu.
Bi. Salum alisema
Serikali inatarajia kukopa sh. bilioni 1,320.0 kutoka masoko ya fedha ya
nje kwa masharti ya kibiashara kwa ajili ya kugharamia miradi ya
maendeleo.
Alisema uamuzi wa
kuendelea kukopa kwa masharti nafuu na ya kibiashara umezingatia
tathmini ya uhimilivu wa deni la Taifa pamoja na umuhimu wa kuendeleza
miradi ya kipaumbele hususan miundombinu ambayo itafungua fursa za
kiuchumi na kuwa kichocheo kikubwa cha ukuaji wa uchumi.
Misamaha ya Kodi
Bi. Salum alisema kila
baada ya robo mwaka, kila misamaha ya kodi itakuwa inawekwa hadharani
kwa kuhusisha kila taasisi, Wizara, kampuni na kuonesha jinsi taasisi
zilizopata misamaha jinsi zilivyofaidika.
Alisema lengo la hatua hiyo ni kuongeza wigo wa uwazi kwa jamii kuelewa kinachoendelea pamoja na kujua waliopewa misamaha.
Walimu
Alisema Serikali
inaendelea na utaratibu wa ujenzi wa nyumba za walimu kwa awamu. Mwaka
2013/14, halmashauri 40 kila moja ilipewa sh. milioni 500 ili zianze
ujenzi wa nyumba za walimu na kiasi kama hicho kitatolewa kwa
halmashauri hizo kwa mwaka 2014/15.
Aliongeza kuwa, sh.
milioni 500 zitatolewa kwa halmashauri 80 zaidi, hivyo kufanya jumla ya
halmashauri 120 kunufaika na utaratibu huo.
Kuhusu malipo ya madai
ya walimu, alisema Serikali inaendelea na utaratibu wa kulipa madai ya
walimu yaliyohakikiwa, ambapo mwaka 2013/14, kiasi cha sh. bilioni 5.6
kimelipwa na mwaka 2014/15, madai ya walimu ambayo yatakuwa yamehakikiwa
yataendelea kulipwa.
Wanafunzi
Bi. Salum alisema mwaka
2014/15, Serikali itaendelea kuboresha huduma kwa wanafunzi katika
shule na vyuo mbalimbali ili kuhakikisha vijana wanasoma katika
mazingira tulivu na bora.
Hatua hiyo itaenda
sambamba na kujenga maabara katika shule, vyuo na kuzipatia vifaa
muhimu, pamoja na kutumia maabara zinazotembea ili kuwafikia wanafunzi
wengi zaidi, kutenga fedha kwa ajili ya kutoa mikopo kwa wanafunzi walio
vyuoni na watakaojiunga na vyuo vya elimu ya juu.
Alisema pia Serikali itajenga maktaba mpya, kukarabati na kuimarisha zilizopo kwa kuzipatia vitabu zaidi vya kiada na ziada.
Nafuu kwa watumishi
Katika hotuba hiyo,
alisema mwaka 2014/15 Serikali imepunguza kodi kwa watumishi kutoka
asilimia 15 hadi 13 ambapo mkakati huo ni endelevu hadi kuhakikisha
msamaha huo unafikia tarakimu moja ili kuwapunguzia mzigo wafanyakazi.
Bajeti ya Kisekta
Bajeti ya Nishati na
Madini, imetengewa sh. bilioni 1,090.6, miundombinu ya usafirishaji sh.
bilioni 2,109.0, kilimo sh. bilioni 1,084.7, elimu sh. bilioni 3,465.1,
maji sh. bilioni 665.1, afya sh. bilioni 1,588.2, utawala bora sh.
bilioni 579.4.
Alisema mwaka 2014/15
kwa kuzingatia sera za uchumi, misingi na shabaha ya bajeti, sura ya
bajeti itakuwa kama ifuatavyo; Serikali imepanga kukusanya jumla ya sh.
bilioni 19,853.3 kutoka kwenye vyanzo vya ndani na nje.
Mapato ya kodi na
mapato yasiyo ya kodi yanatarajiwa kufikia sh. bilioni 12,178.0 sawa na
asilimia 19.2 ya Pato la Taifa. Mapato kutokana na vyanzo vya
halmashauri yanatarajiwa kufikia sh. bilioni 458.5 sawa na asilimia 0.7
ya Pato la Taifa.
Maoni ya Bajeti
Wakati huo huo,
Serikali imeombwa kuangalia maeneo muhimu hususan sekta ya madini na
riba katika benki ili kusaidia wananchi wa kawaida badala ya kukimbilia
kupandisha kodi katika maeneo ambayo wananchi wengi hupata mahitaji yao.
Waziri Mkuu mstaafu,
Bw. John Samwel Malecela, aliyasema hayo jana wakati akitoa maoni yake
baada yake bajeti hiyo kusomwa bungeni na kuongeza kuwa, bajeti ni nzuri
kwani imekuwa tofauti na miaka iliyopita ikiwa imeondoa baadhi ya kero
zinazokuwa zikilalamikiwa na wananchi.
"Bajeti ya mwaka huu ni
tofauti na ya miaka ya nyuma, kama mlivyosikia baadhi ya kodi
zimeondolewa hivyo italeta unafuu kwa mwananchi wa kawaida, " alisema.
Naye Mwenyekiti wa
Chama Cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahimu Lipumba, alisema bado
matatizo ya msingi ambayo yapo pale pale kwa kuwa Serikali haikuweza
kubainisha sekta ya madini imeingiza kiasi gani na itaingiza kiasi gani
ambapo fedha za ndani haziwezi kukidhi mahitaji ya kawaida.
Alisema kasi ya ongezeko la deni la Taifa linamtisha pamoja na ukopaji umeongezeka kwa kasi tangu mwaka 2007 hadi sasa.
"Kwanza nampongeza kwa
jambo zuri moja ambalo ni kutoa taarifa za misamaha ya kodi ili watu
kufahamu...awali kulikuwa na utaratibu huo lakini sasa umerudishwa hivyo
ni jambo zuri pamoja na Waziri kujitoa katika kuidhinisha misamaha ya
kodi.
Aliongeza kuwa, Bi.
Salum ameshindwa kueleza sekta ya madini imechangia kwa kiasi gani
lakini deni ya Taifa limekuwa kubwa tangu 2007 na haioneshi jinsi
litakavyoweza kupungua.
Naye Mwenyekiti wa
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Bw. Freeman Mbowe, alisema
bajeti hiyo ni ya maumivu kwa wananchi kwani imeongeza kodi katika
maeneo muhimu kama vinywaji baridi ambavyo wananchi wengi hutumia.
Mbunge wa Korogwe
Vijijini, Bw. Stephen Ngonyani, alisema bajeti hiyo ni nzuri lakini
haiwasaidii wananchi wa hali ya chini kutokana na riba kubwa kwenye
benki ambazo huchukua mikopo.
"Kama bajeti ingekuwa
kweli ina nia ya kuwasaidia wananchi, riba ingekuwa ndogo katika benki
zote ambazo wakulima huenda kukopa, katika jimbo langu baadhi ya
wananchi wamekimbia nyumba zao kwa kuogopa kudaiwa na benki baada ya
kukopa wakiamini wangepata mazao lakini haikuwa hivyo matokeo yake benki
zinachukua nyumba zao," alisema.
Mwananchi wa kawaida,
Bi. Justina Saimon, mkazi wa Dar es Salaam,alisema bajeti hiyo ni nzuri
kwani imebana misamaha ya kodi lakini bado haijamsaidia mwananchi wa
hali ya chini.
Alisema Serikali
imeacha sekta ya madini ambayo ndiyo inayoingiza fedha nyingi za kigeni
lakini kodi kubwa imepandishwa kwa mahitaji muhimu ya wananchi wa
kawaida.
"Bajeti ya Serikali
tumeizoea kwani kila mara inaacha kupandisha kodi kwenye sekta muhimu
inakimbilia maeneo ambayo wananchi wengi wanayatumia hivyo ni sawa na
kuendelea kuwaumiza," alisema.
0 comments:
Post a Comment