Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
WANANCHI wa Kijiji cha Chonde, Kata ya Makanda, Tarafa ya Mundemu,
Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma, wanalazimika kufuata huduma za afya
umbali wa kilomita tisa, kutokana na kijiji chao kutokuwa nazo tangu
uhuru.
Kijiji hicho kina kaya 684 zenye idadi ya watu 3,426 ambapo kati yao wanaume ni 1,606 na wanawake 1,820.
Kutokana na kadhia hiyo, wajawazito hulazimika kujifungulia njiani
hali inayochangia watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano kukosa
huduma bora za kiafya kama inavyostahili.
Taarifa hiyo ya kusikitisha ilitolewa na Katibu wa CCM Kata ya
Mundemu, Daud Mrutu wakati wa harambee ya kuchangia ujenzi wa zahanati
katika kijiji hicho, iliyoandaliwa na Diwani wa Kata ya Makanda, Anton
Lyamnda (CCM).
Mrutu alisema kuwa kutokana na kuwepo kwa adha kubwa ya wanakijiji
kutembea kilometa tisa kutafuta huduma ya afya, wakazi wa kijiji hicho
wamekuwa wakikosa haki yao ya kupatiwa huduma ya matibabu kwa ufasaha.
Alisema kuwa kutokana na Halmashauri ya Bahi kuonekana kuwatelekeza
wanakijiji hao, kwa sasa hawana imani tena na halmashauri yao.
“Katika mwaka wa fedha 2011/12 wilaya ilituma barua kwenye Kijiji cha
Chonde kuwa imekitengea bajeti ya sh. milioni 65 kwa ajili ya ujenzi
wa zahanati, lakini hakuna utekelezaji wa aina yoyote ulioonekana.
“Pia katika bajeti ya mwaka wa fedha wa 2013/14, wilaya ilitenga
bajeti ya sh. milioni 30 kwa ajili ya ujenzi wa zahanati, lakini hadi
leo hatujaona utekelezaji wowote. Wananchi wamekosa imani na
halmashauri yao,” alisema Mrutu.
Diwani Lyamnda alisema ili jengo la zahanati liweze kukamilika
litagharimu sh. milioni 98 ambapo hadi sasa zimetumika sh. milioni 7.8.
Katika harambehe hiyo ambayo ilihudhuriwa na Mbunge wa Bahi, Omar
Badwel (CCM), mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa, Ally
Nyange, madiwani pamoja na wananchi, zilichangwa sh. miloni 11.1 ambapo
kati ya hizo sh. milioni 9.8 zilikuwa ahadi.
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment