Home » » PINDA AWAASA UKAWA WAREJEE BUNGENI

PINDA AWAASA UKAWA WAREJEE BUNGENI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda amewataka wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa),  waliosusia vikao vya bunge hilo, kurejea bungeni  ili kuendelea na mchakato wa kujadili rasimu ya Katiba Mpya.
Alisema hayo jana wakati akitoa hoja ya kuahirisha Bunge la  Bajeti mjini Dodoma. Bunge Maalum la Katiba linatarajiwa kuanza mwezi Agosti.

Pinda, alisema kama wajumbe hao wanaona kuna kasoro katika mchakato huo, njia sahihi ni kukaa mezani na kuzirekebisha badala ya kususia mchakato mzima.

“Natoa wito kwa wajumbe wote wa Bunge Maalum la Katiba ambao wamesusia vikao, warejee bungeni ili tuendelee na mjadala wa rasimu ya Katiba huku tukitumia utaratibu wa maridhiano uliowekwa kikanuni kutatua tofauti zilizopo,” alisema.

Aliwataka Ukawa kutafakari kuhusu uamuzi na matendo yao, kwa kutambua masharti ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba  na kanuni za Bunge Maalum la Katiba na wajibu wao kwa wananchi.

Alisema Ukawa wana wajibu wa kukamilisha kazi hiyo muhimu waliyopewa kisheria ya kuhakikisha Watanzania wanapata Katiba mpya iliyo bora.

Aidha, aliwashauri Ukawa ambao miongoni mwao ni wabunge, kutumia mifumo iliyowekwa na Bunge Maalum kupeleka malalamiko yao ili kupata  ufumbuzi ndani ya chombo hicho na si vinginevyo.

Kuhusu misamaha ya kodi, Waziri Mkuu alisema serikali inatambua jukumu la  kuhakikisha kwamba misamaha ya kodi inayotolewa kwa wawekezaji na wadau wengine inatumika vizuri katika miradi iliyokusudiwa na si vinginevyo.

“Nitoe wito kwa wote watakaopata misamaha hii kuwa waadilifu na kuitumia kwa malengo yaliyokusudiwa, hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakayetumia vibaya misahama hiyo,” alionya Waziri Mkuu.

Alisema kuwa serikali kwa upande wake itaimarisha zaidi usimamizi wa matumizi ya misamaha hiyo ili itumiwe kwa lengo lililokusudiwa.

Wakati Pinda akitoa kauli hiyo, viongozi kadhaa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamekuwa wakiwabeza Ukawa na kudai kuwa hata wasiporejea (bungeni), mchakato wa Katiba mpya utakamilika.

 MAUJI YA WANAWAKE
Akizungumzia mauaji ya wanawake mkoani Mara, Pinda alisema kuanzia Januari hadi Mei mwaka huu wanawake tisa wameripotiwa kuuawa kinyama katika kata nne za Mugango, Etaro, Nyegina na Nyakatende.

Alisema katika kukabiliana na mauaji hayo, serikali imepeleka kikosi maalum cha makosa dhidi ya binadamu pamoja na vitendea kazi kutoka makao makuu ya  upelelezi ya Jeshi la Polisi, kikiongozwa na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Isaya Mungulu kwa ajili ya uchunguzi na ufuatiliaji.

Alisema timu hiyo yenye wataalam katika eneo la upelelezi wanaendelea kufuatilia matukio hayo sambamba na kutoa elimu kuhusu ulinzi shirikishi wa namna ya kukabiliana na matukio kama hayo.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa