Home » » POLISI WATAKIWA KUISHI NA KUSHIRIKIANA NA VIONGOZI WA KATA

POLISI WATAKIWA KUISHI NA KUSHIRIKIANA NA VIONGOZI WA KATA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (ACP), David Misime
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (ACP),  David Misime, amewataka askari polisi wa kata kuishi ndani ya kata husika ili waweze kutatua kero mbalimbali kwa kushirikiana na viongozi wa maeneo hayo.
Alisema hayo juzi wakati alipofanya ziara ya kutembelea tarafa ya Chipanga Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma kwenye ziara yake ya kikazi kuhimiza utii wa sheria bila shuruti.

Tarafa ya Chipanga inaundwa na kata za   Chipanga, Chikole, Mpalanga, Chali, Chifutuka na Nondwa.Alisema ni muhimu kwa polisi kata kukaa kwenye kata husika badala ya kukaa mjini ili waweze kuwa karibu na  wananchi na kutatua kero mbalimbali.

Akizungumza  na  viongozi na wananchi wa tarafa hiyo na kutoa elimu ya Polisi jamii pamoja na kuwakabidhi rasmi wakaguzi wa tarafa na Polisi kata ili waweze kushirikiana nao kutoa elimu kwa jamii juu ya utii wa sheria bila shuruti, alisema kuna haja kujenga familia zisizokuwa na mhalifu na kubaini viini vya uhalifu, vurugu na migogoro katika maeneo yao.

Pia aliwataka kuimarisha kamati za ulinzi na usalama kuanzia ngazi ya chini na kukaa vikao kujadili kero zilizopo na kuzitafutia utatuzi na zile wanazoshindwa wapeleke kwenye ngazi husika.

Kwa mujibu wa mkaguzi wa Polisi kata ya Chipanga, Inspekta Msaidizi wa Polisi Maulid Kajualwake utekelezaji wa sera ya polisi jamii katika kata hiyo imepunguza kwa kiasi kikubwa vitendo vya kihalifu.

Alisema kila kitongoji kina kikundi cha ulinzi na kuna mradi wa ukamataji salama na klabu za polisi.

Aidha mradi wa safiri salama, askari wa usalama ambapo kazi yake ni kutoa elimu na kuelimisha madereva na abiria kutii sheria za usalama na  uvuvi salama ambapo eneo la Chikopelo lina bwawa na wananchi wamekuwa wakielimishwa juu ya uvuvi salama.

Alisema sasa matukio ya uhalifu yamepungua na hata matukio yaliyotokana na mila potofu, ushirikina na ukukutaji yamepungua.

Aidha alisema taarifa za uhalifu na wahalifu zimekuwa zikitolewa hali inayofanya wahalifu kukamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Mkuu wa Polisi Wilaya ya Bahi, Ramadhani Kato, alisema jukumu la ulinzi na usalama ni la kila raia na Kata hiyo haina matukio mengi ya uhalifu.

Aliwataka mgambo kufanya kazi zao kwa kuzingatia sheria na wananchi kusaidia polisi kudhibiti usafirishaji wa nyara za serikali na madawa ya kulevya.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa