Home » » “HATURUHUSU WAFUNGWA KUFANYA TENDO LA NDOA MAGEREZANI”

“HATURUHUSU WAFUNGWA KUFANYA TENDO LA NDOA MAGEREZANI”

Wafungwa gerezani
WIZARA ya Mambo ya Ndani ya Nchi, imeendeleza msimamo wake kuwa Tanzania bado haina sheria ya kuwaruhusu wafungwa kukutana kifaragha na waume au wake zao.
Hii ni mara ya tatu kwa serikali kutoa majibu hayo kutoakana na maswali ya wabunge, ambako mara kadhaa swali hilo limekuwa likiulizwa na Mbunge wa Viti Maalumu Mariam Msabaha (CHADEMA).
Jana, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereila Ame Silima, alikiri kuwa Tanzania haina sheria hiyo na akajibu kuwa, ujauzito ambao huwapata wafungwa wanawake, unatokana na kuupata nje ya magereza.
Alitoa majibu hayo kutokana na swali la Mbunge wa Viti maalum, Rukia Kassim Ahmed (Cuf), ambaye alitaka kujua ni kwa namna gani wafungwa wanawake wanapata ujauzito wanapokuwa ndani ya magereza yao.
Mbunge huyo, pia alihoji kama magerezani kuna usiri, ni kwa namna gani mahabusi ambao ni mashehe kutoka Zanzibar wanafanyiwa vitendo vya ulawiti gerezani.
Naibu Waziri huyo, alisema kuwa Jeshi la Magereza lina utaratibu wa kutenganisha wafungwa wa kiume na wa kike, kwani kila watu hutunzwa kwa sehemu zao na hulindwa na watu wa jinsia zao.
Kuhusu tuhuma za kulawitiwa kwa Mashehe wa Zanzibar, Waziri wa Mambo ya Ndani Mathias Chikawe, alisema kuwa sakata la Sheikh Salum Ali Salumu, linafanyiwa kazi na kwamba kiongozi huyo ameshafanyiwa uchunguzi wa awali katika hospitali ya Amana.
“Jambo hilo lipo mikononi mwetu, tumempeleka hospitali ya Amana na kesho (leo) tutampeleka hospitali ya Muhimbili kwa uchunguzi zaidi, lakini tunachunguza pia tabia ya kiongozi huyo na mwenendo wake kabla ya kuingia gerezani,” alisema Chikawe.
Hata hivyo, Chikawe alisema kumekuwa na mkanganyiko mkubwa kwa watuhumiwa hao, kwani tangu mwanzo hakuwa ameripoti vitendo hivyo lakini alipofika mara ya nne gerezani ndipo akaripoti kufanyiwa vitendo hivyo na mmoja wa askari polisi.
Chanzo:Tanzania Daima
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa