NAIBU Spika wa Bunge, Job Ndugai amesema kuwa mauaji yanayotokea wilayani Kiteto yanatisha na kwamba huwezi kuamini kama ni sehemu ya Tanzania.
Ndugai ambaye pia ni mbunge wa Kongwa, wilayani Kongwa inayopakana na wilaya ya Kiteto, alisema hayo jana wakati akifafanua mwongozo wa mbunge wa Viti Maalum, Moza Abeid Said (CUF).
Katika mwongozo wake, Moza alisema hivi karibu kulikuwa na mauaji ya mtu mmoja aliyemtaja kwa jina moja la Muhogo, ambaye alidaiwa kuawa na kundi la wafugaji.
Alisema mbali ya mauaji hayo, kuanzia Februali hadi sasa watu zaidi ya 30 wameuawa na zaidi watu 200 wamejeruhiwa.
"Mh. Spika hali ya mauaji Kiteto inatisha na Serikali imefumbia macho. Tumemwita Mkuu wa wilaya hadi sasa hajafika katika eneo hilo na hali inazidi kuwa mbaya. Mimi naomba mwongozo wako kutaka kujua serikali ina mpango ganialihoji Moza.
Akifafanua mwongozo huo, Ndugai alisema suala la Kiteto hataki kulizungumzia tena kwani alishawahi kulizungumzia kwa uchungu bila kupatiwa ufumbuzi.
"Hali ya mauaji inatisha Kiteto, Kiteto sio sehemu ya Tanzania, watu wanauana mchana kweupe, familia zina miliki bunduki za SMG, bastola, visu mapanga utadhani hakuna Serikali," alisema Ndugai.
Alisema kwa mtu asiyeishi au kufika Kiteto ni vigumu kujua tatizo hilo, lakini alisisitiza kuwa matukio ya mauaji yanatisha wilayani humo.
Wakati wa Bunge la Bajeti, Ndugai aliwahi kuzungumzia tatizo na kumlaumu kwa kiasi kikubwa Mkuu wa wilaya hiyo, Matha Umbula kuwa chanzo cha mauaji hayo.
Akijibu mwongozo huo, waziri wa nchi ofisi ya rais (Kazi Maalum), Profesa Mark Mwandosya, alisema kuwa katika mkutano wa Bunge unaoendelea mjini hapa, Bunge litapata taarifa ya Kamati Teule ya Bungu kuhusu hali ya Kiteto na kujua hatma yake.
Chanzo:Tanzania Daima
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment