Home » » MAKINDA: NAFASI ZA CHENGE, NGELEJA ZIKO WAZI

MAKINDA: NAFASI ZA CHENGE, NGELEJA ZIKO WAZI

 
Spika wa Bunge, Anne Makinda.
 
Spika wa Bunge, Anne Makinda, amewakana wenyeviti watatu wa Kamati za Bunge ambao Bunge liliazimia kuwa wavuliwe nafasi zao kutokana na kuhusishwa katika sakata la uchotwaji zaidi ya Sh. bilioni 300 kutoka akaunti ya Tegeta Escrow.
 
Hata hivyo, licha ya Spika kuwakana kuwa siyo wenyeviti halali wa kamati hizo, baadhi yao ‘wamemtunishia misuli’, baada ya kuamua kuendelea kuongoza vikao vya kamati zao.
 
Tafsiri hiyo imetokana na kauli ya Spika Anne Makinda, aliyoitoa kwa waandishi wa habari jana kwamba ‘anatambua wameshajiuzulu.’
 
Aidha, wakati msimamo wa Spika Makinda ukiwa hivyo, jana waandishi wa habari walishuhudia wenyeviti hao wakiendelea kuongoza vikao vya kamati zao.
 
Wenyeviti waliotakiwa kujiuzulu ni Andrew Chenge (Bajeti), William Ngeleja (Katiba, Sheria na Utawala) na Victor Mwambalaswa (Nishati na Madini). Hata hivyo, taarifa zinaeleza kuwa Chenge amekwishaachia wadhifa huo.
 
Ngeleja alitakiwa ajiuzulu kwa kuwa alipata mgawo wa Sh. milioni 40.2 zinazodaiwa kuchotwa katika akaunti ya Tegeta Escrow huku Chenge akigawiwa Sh. bilioni 1.6. Aidha, Mwambalaswa alitakiwa ajiuzulu kwa kuwa kamati yake inasimamia sekta ya Nishati na Madini yaani Wizara ya Nishati na Madini pamoja na mashirika yake.
 
Akijibu maswali ya waandishi wa habari katika ofisi ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam jana, Spika Makinda alisema azimio namba 8 la Bunge liliwataka wenyeviti hao wajiuzulu wenyewe na kwamba anaamini wamekwishafanya hivyo.
 
"Ukiniuliza mimi nitakuambia watu wote walishajiuzulu, mimi najua wamejiuzulu. Azimio lilitaka wajiuzulu siyo wawajibishwe," alisema.
 
Alipoulizwa ikiwa wameandika barua ama la alisema: "Barua ya nini wakati walitakiwa wajiuzulu na wajumbe wa kamati wachague Mwenyekiti mwingine? Ukiniuliza habari ya barua mimi sijui."
 
Makinda pia alisema kuwa yeye ndiyo mtu wa mwisho kutoa maamuzi na jambo la kuwa baadhi ya wenyeviti kuongoza vikao vya kamati halitambui.
 
"Habari za hao kuongoza vikao sijui ila mimi ndiyo nasema kuwa tayari wameshajiuzulu kutokana na jinsi azimio la Bunge linavyosema," alisema Makinda.
 
MAAZIMIO YA BUNGE
Maazimio kadhaa yalitolewa yakiwamo ya kuwawajibisha kwa kutengua uteuzi wa Profesa Muhongo, Maswi, Profesa Tibaijuka na Jaji Werema ambaye amejiuzulu mwenyewe.
 
Wengine waliopendekezwa kuvuliwa uongozi wao kwenye kamati za Bunge ni Endrew Chenge (Bajeti), William Ngeleja (Katiba, Sheria na Utawala) na Victor Mwambalaswa (Nishati na Madini). Chenge akipewa Sh. bilioni 1.6 na Ngeleja Sh. milioni 40.2, kwa mujibu wa taarifa ya CAG na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu (PAC).
 
Pia Bunge liliazimia, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru),  Jeshi la Polisi na vyombo vingine husika vya ulinzi na usalama, vichukue hatua stahiki kwa mujibu wa sheria za nchi kwa watu wote waliotajwa kuhusika na vitendo vyote vya jinai, kuhusu miamala ya akaunti ya Tegeta Escrow, na watu wengine watakaogundulika baada ya uchunguzi mbalimbali unaondelea katika vitendo hivyo vya jinai.
 
Miongoni mwao ni mmiliki wa kampuni ya PAP, Harbinder Singh Sethi, James Rugemalira wa VIP Engineering Ltd, Jaji Werema, Profesa Muhongo, Maswi, wajumbe wa Bodi ya Tanesco, ambao inasemwa kuwa walihusika kwa namna moja au nyingine kufanikisha kufanyika kwa miamala haramu ya fedha katika akaunti ya Tegeta Escrow kwenda PAP na VIP Engineering and Marketing Ltd.
 
Kuhusu ushiriki wa majaji katika kashfa hiyo, ni kwamba Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, imeweka utaratibu mahususi wa Tume ya Kijaji  ya Uchunguzi kuchunguza tuhuma za utovu wa nidhamu wa maadili dhidi ya Jaji Aloysius Mujulizi na Jaji Profesa Eudes Ruhangisa wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
 
Bunge liliazimia kushughulikia nidhamu ya majaji ambao kwa mujibu wa Katiba hiyo, unamtaka Rais aunde Tume ya Uchunguzi ya Kijaji kuchunguza tuhuma za utovu wa maadili dhidi ya majaji.
 
Pia Bunge liliazimia serikali iandae na kuwasilisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria iliyounda Takukuru kwa lengo la kuanzisha taasisi mahsusi itakayoshughulikia, kupambana na kudhibiti vitendo vya rushwa kubwa, ufisadi, na hujuma za uchumi zinazotishia uhai wa Taifa kiuchumi, kijamii na kisiasa kutokana na kushamiri kwa vitendo hivyo.
 
Kadhalika Serikali iangalie uwezekano wa kununua mitambo ya kufua umeme ya IPTL na kuimilikisha kwa Tanesco kwa lengo la kuokoa fedha za shirika hilo.
 
Bunge lilishauri kuwa hatua za haraka zichukuliwe na Kamati husika za Bunge kabla ya kuanza kwa mkutano wa 18 wa Bunge.
 
Novemba mwaka jana wakati wa kikao cha 16 na 17, Bunge liliazimia kwamba katika sakata la akaunti ya Tegeta Escrow wahusika wote wawajibishwe.
 
WALIOFIKISHWA KORTINI
Hadi sasa watumishi watano wa serikali wamefikishwa kizimbani kwa tuhuma za kupokea mgawo wa fedha za Escrow.
 
Vigogo wa kwanza kufikishwa mahakamani ni Teophil John, Mhandisi Mwandamizi kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na  Mkurugenzi wa Sheria wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Rugonzibwa Teophil walifikishwa mahakamani kwa madai ya kupokea rushwa kutoka kwa James Rugemalira.
 
Wengine ni Mkurugenzi wa Fedha wa Benki Kuu (BoT), Julius Angello; Mwanasheria Mwandamizi wa Tanesco, Steven Urassa na Meneja wa Misamaha ya Kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Kyabukoba Mutabingwa.
 
CHINA YALISAIDIA BUNGE
Wakati huo  huo, Spika wa Bunge, Anne Makinda, amesema mhimili huo utaanza kutumia Teknolojia ya Mawasiliano (Tehama) kuendesha shughuli zake na kwamba lengo ni kuwawezesha wabunge kutumia mtandao wawapo bungeni.
 
Spika Makinda alitangaza mageuzi hayo jana jijini Dar es Salaam, alipokuwa akipokea msaada wa vifaa vya Tehema kutoka kwa Balozi wa China nchini, Lu Youqing.
 
Alisema mkakati huo ukifanikiwa, utaongeza ufanisi kwa kuwa kila mbunge atakuwa na kompyuta ndogo (laptop) ambayo itakuwa na taarifa za shughuli zote za siku husika kwa wakati.
 
Aliishukuru serikali ya China kwa msaada huo na kuahidi kwamba Bunge la Tanzania limeazimia kuimarisha uhusiano na Bunge la nchi hiyo.
 
Kwa upande wake, Balozi Youqing, alisema vifaa hivyo ni mashine  kubwa za kudurufu (10),  mashine za kuchapa (10), fax (10), scanner (10), kamera (10), kompyuta mpakato (23), Ipad (13) na vifaa vingine muhimu.
 
Alisema urafiki wa Tanzania na China ni wa historia hivyo miongoni mwa majukumu yake ni kuhakikisha unaendelea kudumu.
 
CHANZO: NIPASHE
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa