Home » » MBUNGE AKANA KUPOKEA RUSHWA KUTOKA KWA DED

MBUNGE AKANA KUPOKEA RUSHWA KUTOKA KWA DED

 
Mbunge wa Bahi, Dodoma, Omary Badwel (CCM).
 
 Mbunge wa Bahi, Dodoma, Omary Badwel (CCM), amedai hajawahi kuomba wala kupokea rushwa ya Sh. milioni moja kutoka kwa aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga, Sipora Liana.
 
Ameiomba mahakama imetendee haki kwa madai ya kwamba tuhuma dhidi yake zilikuwa njama za kuchafua jina lake.
 
Badwel alidai hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mbele ya Hakimu Mkazi Hellen Riwa, alipokuwa akitoa utetezi wake.
 
Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, Badwel anadaiwa kati ya Mei 30 na Juni 2, 2012, katika maeneo tofauti mkoani Dar es Salaam, alishawishi apewe rushwa ya Sh. milioni nane kutoka kwa Sipora.
 
Inadaiwa Badwel aliomba rushwa hiyo ili ashawishi wajumbe wengine wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), kupitisha hesabu za halmashauri hiyo.
 
Pia anadaiwa Juni 2, 2012 katika hoteli moja iliyoko wilayani Ilala, alipokea rushwa ya Sh.  milioni moja kutoka kwa Sipora.
 
Akiongozwa na Wakili wa utetezi Mpare Mpoki, Badwel, alidai hajawahi kuomba rushwa wala kuwa na nia hiyo.
 
“Sijawahi kupokea rushwa ya kiasi hicho kutoka kwa Sipora. na wala sijawahi kumshawishi na katika maelezo yake Sipora aliyoyatoa mahakamani amekiri sijawahi kumuomba rushwa,” alidai Badwel 
 
Alidai katika kamati hiyo kuna wabunge 15 na yeye ni mmoja wa wajumbe, hivyo asingeweza kuwashawishi kwa sababu hakuwa na mamlaka hayo.
 
Alidai jukumu moja wapo la kamati hiyo ni kupokea taarifa za ukaguzi wa fedha kutoka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ambapo inazipitia na kuwaita mkurugenzi na wakuu wa idara za halmashauri husika na kuwasomea taarifa na kutoa ushauri.
 
Alidai lengo ni utaratibu wa uwajibikaji wa watu kufanya kazi na kukaguliwa na kutolewa taarifa na iwapo halmashauri zimefanya vizuri wanaishauri serikali kuzipongeza na ikiwa hazijafanya vizuri zichukuliwe hatua.
 
Alidai taarifa ambayo imeshakaguliwa na CAG, kamati ya Bunge haina uwezo wa kuibadilisha kwa namna yoyote.
 
CHANZO: NIPASHE
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa