SHIRIKA la Uvuvi Tanzania (Tafico) limeondolewa katika mchakato wa
kubinafsishwa na sasa Serikali iko katika mpango wa kulifufua. Naibu
Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Ajira, Kazi na Vijana, Anthony Mavunde
alisema hayo jana alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Kigamboni, Dk
Faustine Ndugulile (CCM).
Katika swali hilo lililoulizwa kwa niaba yake na Mbunge wa Viti
Maalumu, Mariam Kisangi (CCM), Dk Ndugulile alitaka kujua Serikali ina
mpango gani wa kufufua shirika hilo ambalo zamani lilikuwa na makao
makuu yake Kigamboni, Dar es Salaam.
Pia alitaka kuelezwa Serikali imejipanga vipi kusimamia uvuvi katika
bahari kuu ili Taifa linufaike na mapato. Akifafanua majibu hayo kwa
kuelezea historia ya shirika hilo, Mavunde alisema Tafico ilianzishwa
mwaka 1974 na kukabidhiwa kwa lengo la kuendesha shughuli za uvuvi
kibiashara.
Kwa mujibu wa Mavunde, mwaka 1996 shirika hilo liliwekwa chini ya
iliyokuwa Tume ya Rais ya Kurekebisha Mashirika ya Umma (PSRC) kwa ajili
ya utaratibu wa ubinafsishaji. Mwaka 2007 kwa mujibu wa Mavunde,
shirika hilo liliondolewa kwenye orodha ya mashirika yaliyotakiwa
kubinafsishwa PSRC na kurejeshwa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa
ajili ya kuendeleza ubinafsishaji wake.
Hata hivyo, mwaka 2007, Mavunde alisema Baraza la Mawaziri
lilisitisha uuzwaji wa shirika hilo na kuelekeza kuwa mali zake
zisizohamishika ikiwemo ardhi zibaki kwa ajili ya matumizi ya serikali.
Kwa sasa Mavunde alisema wizara kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya
uvuvi, inaendelea na mpango wa kufufua shirika hilo ikiwa ni pamoja na
kuwasilisha mapendekezo katika Baraza la Mawaziri kwa hatua husika.
Chanzo Gazeti La Habari Leo
0 comments:
Post a Comment