KUSUSA na kutolewa nje mara kwa mara kwa Kambi Rasmi ya Upinzani
bungeni, kumegeuka kivutio baada ya baadhi ya wabunge wa CCM kujaza
nafasi zinazokuwa wazi za upinzani, wakati wakiwa wamesusa.
Mbali na kujaza nafasi hizo na kuchangia hoja huku wakijiita wabunge
wa kambi mbadala, baadhi ya wabunge hao wa CCM jana waliamua kuchukua
jukumu la maswali ya wabunge wa upinzani, wakati wabunge hao wanapokuwa
nje katika harakati zao za kususa au baada ya kutolewa nje.
Juzi usiku wakati Bunge lilipokaa kuwa Kamati ya Matumizi ya
kupitisha Bajeti ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Mbunge wa Korogwe
Vijijini, Steven Ngonyani (CCM) maarufu Profesa Majimarefu na Mbunge wa
Kilolo, Venance Mwamoto (CCM), walikalia viti vya viongozi wa upinzani
na kujitambulisha kuwa kambi mbadala.
Akichangia hoja ya kuendeleza miradi ya maji iliyosimama, Mwamoto
alisema; “Upande wetu wa kambi mbadala, tunatoa ushauri kwa CCM,
kuwekeza katika uvunaji wa maji kwani mwaka huu mvua zimenyesha na maji
mengi tumeyapoteza.”
Naye Ngonyani akichangia hoja hiyo alisema; “natoa ushauri kwa CCM,
sisi kambi mbadala tunashauri mabwawa ya maji yaliyochimbwa, yaondolewe
magugu maji kwa kuwa serikali ilitumia fedha nyingi kuyachimba, lakini
magugu hayo yanayakausha.”
Jana asubuhi, wabunge hao wa Kambi Rasmi ya Upinzani, waliingia
bungeni na kusaini kwa njia ya kielektroniki ili wasinyimwe posho na
kususa kikao kilichokuwa kikiongozwa na Naibu Spika, Dk Tulia Ackson.
Kutokana na kutokuwepo kwa wabunge hao, baadhi ya maswali ya wabunge
wa upinzani ikiwemo swali namba 272 lililokuwa liulizwe na Mbunge wa
Viti Maalumu, Upendo Peneza (Chadema), liliulizwa kwa niaba yake na
Mbunge wa Viti Maalumu kutoka CCM, Ritha Kabati.
Chanzo Gazeti La Habari Leo
0 comments:
Post a Comment