Home » » Wabunge wa CCM ‘wavamia’ nafasi za wapinzani bungeni

Wabunge wa CCM ‘wavamia’ nafasi za wapinzani bungeni

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Naibu Spika Dk Tulia Ackson.
KUSUSA na kutolewa nje mara kwa mara kwa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni, kumegeuka kivutio baada ya baadhi ya wabunge wa CCM kujaza nafasi zinazokuwa wazi za upinzani, wakati wakiwa wamesusa.
Mbali na kujaza nafasi hizo na kuchangia hoja huku wakijiita wabunge wa kambi mbadala, baadhi ya wabunge hao wa CCM jana waliamua kuchukua jukumu la maswali ya wabunge wa upinzani, wakati wabunge hao wanapokuwa nje katika harakati zao za kususa au baada ya kutolewa nje.
Juzi usiku wakati Bunge lilipokaa kuwa Kamati ya Matumizi ya kupitisha Bajeti ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Mbunge wa Korogwe Vijijini, Steven Ngonyani (CCM) maarufu Profesa Majimarefu na Mbunge wa Kilolo, Venance Mwamoto (CCM), walikalia viti vya viongozi wa upinzani na kujitambulisha kuwa kambi mbadala.
Akichangia hoja ya kuendeleza miradi ya maji iliyosimama, Mwamoto alisema; “Upande wetu wa kambi mbadala, tunatoa ushauri kwa CCM, kuwekeza katika uvunaji wa maji kwani mwaka huu mvua zimenyesha na maji mengi tumeyapoteza.”
Naye Ngonyani akichangia hoja hiyo alisema; “natoa ushauri kwa CCM, sisi kambi mbadala tunashauri mabwawa ya maji yaliyochimbwa, yaondolewe magugu maji kwa kuwa serikali ilitumia fedha nyingi kuyachimba, lakini magugu hayo yanayakausha.”
Jana asubuhi, wabunge hao wa Kambi Rasmi ya Upinzani, waliingia bungeni na kusaini kwa njia ya kielektroniki ili wasinyimwe posho na kususa kikao kilichokuwa kikiongozwa na Naibu Spika, Dk Tulia Ackson.
Kutokana na kutokuwepo kwa wabunge hao, baadhi ya maswali ya wabunge wa upinzani ikiwemo swali namba 272 lililokuwa liulizwe na Mbunge wa Viti Maalumu, Upendo Peneza (Chadema), liliulizwa kwa niaba yake na Mbunge wa Viti Maalumu kutoka CCM, Ritha Kabati.
Chanzo Gazeti La Habari Leo

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa