Home » » Serikali Yachukua Hatua Kuhakikisha Hali ya Chakula na Lishe ni Imara Nchini.

Serikali Yachukua Hatua Kuhakikisha Hali ya Chakula na Lishe ni Imara Nchini.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 


Na: Lilian Lundo – MAELEZO – Dodoma.

Katika kukabiliana na athari za ukame, Serikali imechukua hatua za makusudi kuhakikisha kuwa hali ya chakula na lishe ni imara nchini.

Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi  Dkt. Charles Tizeba ameyasema hayo leo Mjini, Dodoma katika Kikao  cha Bunge alipokuwa akitoa kauli ya Serikali kuhusu hali ya chakula na lishe kwa mwaka 2016/2017.

“Tathimini imebainisha kuwa Halmashauri za wilaya 55 zinahitaji jumla ya tani 1,969 za mbegu bora za mahindi, mtama na mizizi inayokomaa kwa muda mfupi na kustahimili ukame,” alifafanua Dkt. Tizeba.

Aliendelea kwa kusema kuwa mbegu hizo zinahitajika ziwafikie mwezi Februari 2017 iliziweze kupandwa katika msimu wa 2016/2017 katika maeneo yanayoendelea kupata mvua wakati huu wa mwaka.

Dkt. Tizeba alizitaja hatua ambazo Serikali inazichukua kuhakikisha kuwa hali ya chakula na lishe ni imara kuwa ni pamoja na;

Kusimamia usambazaji wa mbegu za mazao ya kilimo zinazostahimili ukame na zinazozaa kwa muda mfupi ambazo ni pamoja na mtama, uwele na mbegu za mazao aina ya mizizi za mihogo na viazi vitamu ili kuzitumia vizuri mvua zinazonyesha sasa.

Kuhamasisha wakulima kupanda mazao aina ya mizizi, mtama na uwele kwa maeneo yanayopata mvua za masika ambazo zinaendelea kunyesha na mawakala wa pembejeo pamoja na vivutio vya utafiti vilivyopo katika kanda mbalimbali hapa nchini.

Vile vile Serikali kupitia Wakala (NFRA) inaendelea kuhifadhi kwa uangalifu chakula kilichopo ili kitumike pale kitakapohitajika.

Hatua nyingine ni Kuhamasisha sekta binafsi kununua mazao ya chakula katika maeneo yaliyo na ziada na kuyauza katika maeneo yenye uhaba wa chakula. Aidha wafanyabiashara waliohifadhi mahindi wanaombwa kusambaza chakula hicho katika masoko ya ndani ya nchi ili kupunguza mfumuko wa bei.

Aidha Serikali inaendelea kuhimiza usindikaji wa mazao ya chakula kwa kuyaongezea thamani na kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhiimu wa kula vyakula vya aina zote.

Dkt. Tizeba amesema kuwa kutokana na hali ya mwenendo wa unyeshaji wa mvua za vuli na msimu kutoridhisha katika maeneo mengi ya nchi, Wakuu wa Mikoa na Wilaya wanashauriwa kuendelea kuhamasisha na kusimamia wakulima kutuma mbegu zinazokomaa mapema na kupanda mazao yanayostahimili ukame.

Aidha Serikali imewataka  wakulima kuendelea kuzitumia mvua zinazoendelea kunyesha kwa kupanda mazao yanayostahimili ukame na kukomaa kwa muda mfupi na pia waendelee kutunza na kutumia chakula walichonacho kwa uangalifu.


0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa