SERIKALI YAELEZA UTEKELEZAJI WA MASUALA MBALIMBALI BUNGENI
Dodoma, Jumanne, Januari 31, 2017:
Serikali leo
imeainisha utekelezaji na kutoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali ya maendeleo
kwa wananchi katika sekta mbalimbali katika kikao cha kwanza cha Mkutano wa
Sita wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Majibu ya Serikali kwa baadhi
ya hoja ni kama ifuatavyo:
Ujenzi Nyumba za Walimu
Akijibu
hoja kuhusu ujenzi wa nyumba za walimu, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa, Selemani Jafo, ameliambia Bunge kuwa Serikali
ilitenga kiasi cha Sh. Bilioni 13.9 katika Bajeti ya mwaka huu kwa ajili ya
ujenzi wa nyumba za walimu wa Sekondari, na Shilingi bilioni 11.4 kwa nyumba za
walimu wa Shule za Msingi.
Aidha, Waziri
Jafo ameeleza kuwa tayari nyumba 146 za walimu zimeshajengwa nchini kupitia
Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari. Pia amezungumzia Serikali kuanza
kulipa madeni ya walimu.
Ujenzi wa Viwanda Nchini
Akijibu
swali kuhusu uwekezaji wa viwanda nchini hususani mkoani Tabora ambako kuna
kilimo cha Tumbaku na maeneo mengine yenye malighafi, Mhandisi Edwin Ngonyani
kwa niaba ya Waziri wa Viwanda ameliambia Bunge kuwa tayari Serikali
imeshafanya mazungumzo na wawekezaji kutoka Vietnam na kuzitaka Halmashauri
zote nchini kuendelea kuitikia wito wa kutenga maeneo ya uwekezaji.
“Kituo
cha uwekezaji Nchini (TIC) kimepewa maelekezo maalum kunadi fursa hii kwa
wawekezaji katika sekta ya tumbaku na sigara hapa nchini,” alisema Mhandisi
Ngonyani ambaye pia ni Naibu Waziri, Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
Tupende Bidhaa Zetu
Akijibu
hoja kuhusu bidhaa nyingi za Kenya kuingia nchini, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje
na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Suzan Kolimba amesema moja ya
changamoto inazozikumba bidhaa za Tanzania ni wananchi wake kupenda vya nje.
“Katika
kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali iliunda Kamati ya Kitaifa ya Kudhibiti
na Kusimamia Uondoaji wa wa Vikwazo visivyo vya Kiforodha na kuhamasisha
wafanyabiashara nchini kuzalisha bidhaa zenye ubora,” alisema.
Serikali yagharamia 100% umeme vijijini
Serikali
imesisitiza kuwa inagharamia ujenzi wa umeme vijijini kupitia Wakala wa
Kusambaza Umeme Vijijini (REA) kwa asilimia 100. Akijibu maswali ya wabunge,
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani, alisema wananchi
wanalazimika kuchangia Sh. 27,000 tu ambazo ni gharama za kodi ili
waunganishiwe huduma hiyo wakati mradi ukiwa unaendelea.
“Lengo ni
kuhamasisha na kuwawezesha wananchi wa vijijini wenye vipato vidogo kuweza
kupata huduma za umeme kwa gharama nafuu,” alisema akisisitiza kuwa wale ambao
huomba huduma hiyo baada ya wataalam wa REA kumaliza kazi yao ndio hulazimika
kulipia umeme huo kwa Sh. 177,000 tu badala ya Sh. 320,960/- wanazotozwa wakazi
wa mijini kwa umbali usiohitaji nguzo.
Bei
ya maji kupungua
Waziri wa
Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Gerson Lwenge amesema Serikali itaendelea
kupunguza gharama za maji nchini hasa vijijini kadiri gharama za umeme
zitakavyoendelea kupungua hasa wakati huu nchi inapoingia katika uchumi wa gesi.
Aliongeza
kuwa kwa upande wa vijijini miradi ya umeme wa jua na nishati nyingine za bei
nafuu pia itasaidia kupunguza gharama za umeme na kusaidia wananchi kupata maji
katika miradi mingi inayondelea sasa nchini.
Madai ya Unyanyasaji Zanzibar
Serikali
imewataka wananchi wote wanaodai kufanyiwa unyanyasaji na vikosi vya Serikali
ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kutoa taarifa za matukio hayo polisi ili hatua
stahiki zichukuliwe.
Waziri wa
Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba alisema kwa kuwa hakuna tarifa za kuripotiwa kwa matukio hayo katika
kituo chochote cha Polisi, atachukua pia hatua za kutuma maafisa wake kufanya
uchunguzi zaidi.
Imetolewa na:
Dkt. Hassan Abbasi,
Mkurugenzi Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa
Serikali
0 comments:
Post a Comment