Na; Lilian Lundo - MAELEZO - Dodoma
Katika
kipindi cha kuanzia Julai, 2016 hadi kufikia Desemba, 2016 Serikali
imetumia jumla ya shilingi Bil. 2,570.1 kulipia madeni ya ndani na nje
yaliyoiva.
Waziri
wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango aliyasema hayo leo Bungeni, Mjini
Dodoma alipokuwa akitoa kauli ya Serikali kuhusu mwenendo wa hali ya
uchumi wa Taifa.
“Katika
kipindi cha kuanzia Julai, 2016 hadi kufikia Desemba, 2016 Serikali
ilitumia jumla ya shilingi Bil. 2,570.1 kulipia madeni ya ndani na nje
yaliyoiva. Kati ya kiasi hicho malipo ya deni la ndani ni shilingi Bil.
1,822.3 na deni la nje ni shilingi Bil. 747.8 ,” alifafanua Dkt. Mpango.
Ameeleza
kuwa katika malipo ya deni la ndani yanajumuisha malipo ya mtaji
(rollover) ya shilingi Bil. 1,367.1 na malipo ya riba ya shilingi Bil.
455.2.
Aidha Dkt. Mpango amesema kuwa Serikali inatambua umuhimu wa kupeleka fedha katika Halmashauri kwa kuwa ndiko utekelezaji wa miradi ya maendeleo na utoaji wa huduma mbalimbali kwa wananchi yanapofanyika.
Hivyo basi, katika robo ya kwanza ya mwaka 2016/2017, Serikali ilipeleka jumla ya shilingi Bil. 114.7 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo na matumizi mengineyo katika Halmashauri mbalimbali nchini.
Aidha,
katika robo ya pili ya mwaka, Serikali iliongeza mgao wa fedha
zilizoenda kwenye Halmashauri ambapo kiasi cha shilingi bilioni 203.4
zilipelekwa.
Dkt.
Mpango alitaja madai mengine yaliyolipwa na Serikali katika kipindi cha
kufikia Juni 30, 2016 kuwa ni kiasi cha Shilingi Bil. 3,113.7 ambazo
ziliwasilishwa ikiwa ni madai ya wakandarasi, watumishi, wazabuni na
watoa huduma mbalimbali.
Serikali
ilifanya uhakiki kupitia kwa Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali
ilibainika kuwa madai halali yalikuwa shilingi Bil. 2,934.2 na madai
yaliyokosa vielelezo na hivyo kukosa uhalalli yalikuwa shilingi Bil.
179.5.
Vile
vile katika kipindi cha nusu mwaka wa 2016/17, Serikali imelipa jumla ya
shilingi Bil. 600.2 ambapo kati ya kiasi hicho, shilingi Bil. 42.35
zilikuwa kwa ajili ya madai ya watumishi, shilingi Bil. 49.46 kwa ajili
ya wazabuni, shilingi Bil. 11.2 kwa ajili ya watoa huduma, shilingi Bil.
30.0 kwa ajili ya madai ya vyombo vya Ulinzi na Usalama, shilingi bil.
67.2 kwa ajili ya wakandarasi mbalimbali ikijumuisha shilingi Bil. 2.0
kwa ajili ya makandarasi wa maghala na skimu za maji.
Mwisho..
0 comments:
Post a Comment