Imeandikwa na Maulid Ahmed, Dodoma
SPIKA wa Bunge, Job Ndugai ameunda kamati za kushughulikia sekta ya
gesi na ya uvuvi wa bahari kuu ili kufahamu kwa nini hazichangii pato la
taifa.
Ndugai alimrudisha tena mbunge wa Bukombe, Dotto Biteko kuwa
mwenyekiti wa kamati ya gesi ambapo aliwahi kuwa kwenye kamati
iliyochunguza ya madini kwa ajili ya kubaini dosari zilizomo katika sera
na sheria zake na Mbunge wa Ilala, Mussa Azzan Zungu akipelekwa sekta
ya uvuvi.
Akitangaza jana Spika alisema anatumia kanuni ya 5 (1) ya kanuni za
Bunge toleo la 2016 ambayo inampa madaraka ya kuunda kamati kwa kadri
atakavyoona inafaa. Alisema kumekuwa na hali ya kusuasua kwa sekta hizo
ambapo uvuvi wa bahari kuu unachangia pato la taifa kwa asilimia 1.4
ambayo ni sawa na Sh bilioni 3.2 wakati kuna zaidi ya Sh bilioni 400
ambazo zinapotea bure.
Alisema ukubwa wa ukanda wa bahari katika uvuvi wa Tanzania
unalingana na Namibia ambayo inaingiza pato kwa asilimia 10, hivyo kuna
kila sababu ya kupitia upya sekta hiyo ikiwemo kuangalia mirahaba ya
leseni za uvuvi wa meli zinazovua bahari kuu.
Wajumbe wa kamati ya uvuvi ni Zungu, Salum Mwinyi Rehani, Masoud
Salim Abdala, Tauhida Nyimbo na Mbaraka Dau. Wengine katika kamati hiyo
ni Dk Immaculate Semesi, Dk Christina Ishengoma, Stanslaus Mabula, Mussa
Mbarouk na Cosato Chuma ambao wataongozwa na Mwenyekiti wao Anastazia
Wambura.
Kamati ya sekta ya gesi itakuwa chini ya wajumbe Innocent Bashungwa,
Dunstan Kitandula, Dk Seleman Yusufu, Wanu Hafidhi Ameir, Oscar Mukasa
na Ruth Molell. Wajumbe wengine katika kamati hiyo ambayo iko chini ya
uenyekiti wa Biteko ni Richard Mbogo, Omari Kigua, Abdallah Mtolea na
Sebastian Kapufi.
Ndugai alimwagiza Katibu wa Bunge kuangalia namna ya kuwawezesha
wabunge hao ili waanze kazi na kamati zao zimetakiwa kufanya kazi ndani
ya siku 30 tangu siku watakayokabidhiwa majukumu yao.
Sambamba na kuunda kamati, Ndugai amesema atawachongea Mawaziri kama
watashindwa kupeleka bungeni sheria inayotambua Dodoma kuwa Makao Makuu
ya nchi. “Mmetupiga danadana sana, hivi ni nani aliyekalia Muswada huo
ama mnataka siku moja niamue kwenda Dar es Salaam tena, nasema kama bado
nimekalia kiti hiki hakuna mtu ataweza kupenyeza ajenda hiyo,” alisema.
Kiongozi huyo alisema mawaziri wamekuwa wakilidanganya Bunge kila
wakati kuwa Muswada huo unapelekwa bungeni lakini kila wakati Bunge
linamaliza mkutano hakuna kitu kama hicho licha ya kuwa hata tamko la
Makao Makuu ya Dodoma ni la Rais John Magufuli mwenyewe.
Alimwagiza Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwa akishindwa kupeleka
Muswada huo katika mkutano wa 10 wa Bunge la 11 angalau kusomwa kwa mara
ya kwanza, basi atamwambia Rais nini kinachoendelea.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment