Rose Muhando akiimba kwenye moja ya onesho lake.
* Watakuwepo pia Rebecca Malope, Solomon Mukubwa
TAMASHA la Pasaka linalotarajiwa kufanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Aprili 8, mwaka huu, limepangwa kusheheni waimbaji kochokocho wa nyimbo za injili.
Miongoni mwa wasanii hao ni mwimbaji galacha wa nyimbo za injili, Rose Muhando ambaye anasema amepania kukonga nyoyo za mashabiki atakapopanda jukwaani katika tamasha hilo lililoliandaliwa kwa lengo la kuchangisha fedha kwa ajili ya watoto yatima na kuwasaidia mitaji ya biashara wajane wasiojiweza.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Msama Promotions, Alex Msama anasema tamasha hilo la Sikukuu ya Pasaka ambalo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, litasindikizwa na wasanii kochokocho wa muziki wa injili.
Muhando anasema amepania kufanya mambo makubwa kama alivyofanya alipozindua albamu zake zilizopita za Uwe Macho, Nyota ya Ajabu (Zawadi ya Krismasi) na Jipange Sawa Sawa.
Mwanamuziki huyo anayeabudu katika Kanisa la Anglikana la Chimuli lililoko Area E, Dodoma, anasema amejiandaa vyema kukonga nyoyo za mashabiki wake na mbali na kufanya mazoezi, pia amekuwa akifunga na kusali ili Mungu amfanyie miujiza.
Anawaomba mashabiki wamiminike kwa wingi uwanjani Aprili 8 kuona mambo mazuri aliyowaandalia na kuongeza kuwa kwa vile anamtukuza Mungu aliyemtoa kwenye shida na majaribu mengi ya Shetani, anaamini atawapa kile wanachotaka kutoka kwakwe.
Anasema anatarajia kuimba nyimbo mbalimbali akipata nafasi zikiwemo alizoimba na wanakwaya wa Kanisa la Anglikana Chimuli ikiwa ni pamoja na Kitimutimu, Imani, Onjeni, Sikilizeni Enyi Makahaba, Mungu Wangu, Moyo Wangu, Najitoa Sasa, Hey Mbona Watenda Dhambi na Wapendwa.
Pia ataimba baadhi ya nyimbo kutoka katika albamu yake ya kwanza ya Mteule Uwe Macho zikiwemo Mteule Uwe Macho, Nipe Uvumilivu, Yesu Nakupenda, Akina Mama, Nakuuliza Shetani, Yerusalemu, Mwambieni Mungu na Nakaza Mwendo. Pia ataimba za albamu ya Zawadi ya Krismasi.
"Katika tamasha la Pasaka mwaka huu ndipo Rose Muhando atapata fursa ya kutambulisha albamu yake ya nne ya Utamu wa Yesu ambayo haijawahi kuzinduliwa tangu aikamilishe," anasema Msama.
Albamu ya Utamu wa Yesu inabeba nyimbo saba ambazo ni Utamu wa Yesu uliobeba jina la albamu hiyo, Raha Tupu, Tamalaki, Ndivyo Ulivyo, Woga Wako, Imbeni na Kusifu na Achia.
Msama ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya tamasha hilo, anasema wamewaandalia mashabiki wa muziki wa injili mambo mazuri yatakayowaburudisha na kuridhika.
Msama anajinaki (jinasibu) kuwa tamasha hilo litafana kwa vile kutakuwa na waimbaji wengi wa muziki wa injili watakaowapa mashabiki vionjo mbalimbali. Anasema pia watakuwepo wageni waalikwa.
Wasanii wengine wa nyimbo za Injili watakaopamba tamasha hilo ni Maryanne Tutuma na Anastazia Mukabwa wote kutoka Kenya.
Anasema mbali ya waimbaji hao galacha wa nyimbo za injili, wengine wa nyimbo za Injili watakaopamba tamasha hilo ni Rebecca Malope, Christina Shusho, Upendo Nkone, Upendo Kilahiro, Solomon Mukubwa, Atosha Kissava, Ephraim Sekeleti na kundi la Glorious Celebration.
Pia kwaya mahiri ya Kinondoni Revival inayotamba na albamu yao mpya ya Mtu wa Nne, inatarajia kutumbuiza katika tamasha la Pasaka na Mwinjilisti Faraja Ntaboba kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
"Kuna orodha ndefu ya waimbaji wa nyimbo za injili ambao tumefanya nao mazungumzo na wamethibitisha kushiriki," anasema Msama.
Mkurugenzi huyo anasema pia Muhando ataimba pamoja na Anastazia Mukabwa aliyeshirikiana naye katika albamu ya Vua Kiatu, na baada ya kutikisa Uwanja wa Taifa, mashambulizi mengine yatahamia kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma Aprili 9 mwaka huu ambako mgeni rasmi atakuwa Naibu Spika, Job Ndugai.
Albamu ya Vua Kiatu inabeba nyimbo nane ambazo ni Vua Kiatu uliobeba jina la albamu hiyo, Ee Mungu, Usiwe Manamba, Nzizilela, Nishike Mkono Bwana, Wanaokudharau na Mfalme.
Kiingilio katika tamasha la mwaka huu kimetengwa katika kategoria tatu na kitakuwa sh. 2,000 kwa watoto, sh. 5,000 kwa viti vya kawaida na viti maalumu sh. 10,000.
Tamasha la Pasaka la mwaka huu litashirikisha waimbaji wa nyimbo za Injili kutoka nchi za Afrika ambazo ni Kenya, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Afrika Kusini na Zambia. Pia kutakuwa na kwaya.
0 comments:
Post a Comment