Home » » Mwenendo huu wa Bunge haukubaliki

Mwenendo huu wa Bunge haukubaliki


Tahariri
MKUTANO wa nane wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ulioanza Juni 12, mwaka huu, unaendelea mjini Dodoma, ambapo shughuli kuu ni kujadili makadirio ya mapato na matumizi ya serikali (bajeti) kwa mwaka wa fedha wa 2012/2013.
Kwa ujumla mijadala ya bajeti kwa miaka yote huwa mikali kutokana na unyeti wa hoja yenyewe, na mara nyingi wabunge karibu wote huwa wakali dhidi ya mawaziri na serikali kwa ujumla katika kutetea masilahi ya wananchi waliowachagua kuwawakilisha bungeni, na hilo si kosa kwani huo ndio wajibu wa kila mbunge mwenye kuwajibika kwa wapiga kura wake.
Hata hivyo, mienendo ya wabunge tuliyoanza kuishuhudia kuanzia juzi Jumatatu na jana Jumanne, imeanza kututia wasiwasi na kutufanya tujiulize kama kweli wabunge wote waliomo bungeni wanaujua wajibu wao, na kama wanajua tofauti ya mijadala ya vijiweni au katika vilabu vya pombe na ile inayofanyika bungeni.
Pia inatutia shaka kuamini kama kweli viongozi waliopewa dhamana ya kusimamia mijadala bungeni hususan wenyeviti na naibu spika, wanaijua vema kazi na mamlaka yao wawapo bungeni.
Tulichokishuhudia juzi na jana ni baadhi ya wabunge badala ya kutumia muda waliopewa kuchangia hotuba ya bajeti ya serikali wametumia muda huo kutukana na kudhalilisha wenzao walioikataa bajeti hiyo.
Kwa mfano, kauli za Mbunge wa Iramba Mashariki, ambaye pia ni Katibu wa Uchumi na Fedha wa chama tawala-Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mwigulu Nchemba, ambaye alitumia muda wake wote kuwatukana na kuwadhalilisha wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa kuwaita waigizaji, wamesomea sheria za kichawi, wamesomea kuchezesha disko, wamejawa na pepo wa kutaka madaraka, na kwamba maoni yao ya bajeti ni uchafu.
Kwa namna yoyote ile, hatuungi mkono kauli hizi zisizofaa kwani hazikubaliki katika jamii yetu.
Kauli nyingine zisizofaa na zisizovumilika ni za Mbunge, John Komba, ambaye alidiriki kutamka bungeni kuwa wabunge wa upinzani ni vichaa au wendawazimu na kwamba walipaswa kupelekwa Hospitali ya Milembe mjini Dodoma, kupimwa akili kabla ya kuapishwa kuwa wabunge.
Ni jambo la kusikitisha kwamba wakati matusi na udhalilishaji huu unafanyika, kiti cha Spika hakikuchukua hatua thabiti dhidi ya wahusika ili kuzuia hali hiyo isirudiwe na wabunge wengine katika siku za usoni.
Sisi tukiwa chombo huru cha habari na kwa kutambua wajibu wetu kwa umma wa Watanzania, tunasema mwenendo huu wa Bunge letu haukubaliki, mwenendo wa wabunge wetu hauwatendei haki Watanzania waliowachagua, mwenendo huu unawanyima wananchi fursa ya kuelimika kupitia mijadala ya wabunge, na kwa vyovyote vile mwenendo huu unapaswa kukomeshwa mara moja.
Tunawataka wabunge wajisahihishe, tunawaagiza wafanye majukumu tuliyowatuma kufanya, waache kutetea vyama vyao, na badala yake watetee wananchi wa Tanzania.
Kutukanana na kudhalilishana hakuna tija kwa yeyote kwani mwisho wa siku mwananchi wa kawaida ndiye mwathilika mkuu. Wabunge acheni mzaha na badala yake chapeni kazi kwa maendeleo ya nchi yetu.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa