Masoud Masasi,Dodoma yetu
MKUU wa Mkoa wa Dodoma Dk. Rehema Nchimbi amewataka wananchi wa mkoa
wa huo kutokuwa wavuvi katika kupima afya kwa kuwa kufanya hivyo
kutasaidia kuweza kujua magonjwa wanayowakabili haraka na kuweza
kuyatibu kwa wakati muafaka.
Pia mkuu huyo wa mkoa aliwataka wananchi hao kujitokeza katika
uchangiaji damu kwa kuwa kumeonyesha asilimia 11.8 ya wagonjwa
waliofika hospitali ya mkoa waligundulika kuwa na upungufu wa damu
jambo ambalo amesema inabidi wananchi wachangie damu ya kutosha
kukabili mahitaji yote ya damu na hata dharura.
Dk Nchimbi aliyasema hayo juzi wakati wa uzinduzi wa kampeni ya siku
mbili ya kuhamashisha wananchi juu ya upimaji wa afya zao na
uchangiaji wa damu ili kuondoa upungufu unaoikabili benki ya damu ya
mkoa huo.
Alisema kuwa watu wamekuwa wakitembea huku wakiwa wanakabiliwa na
magonjwa bila wenyewe kujijua kwa sababu hawana desturi kabisa ya
kupima afya zao jambo alilosema ni hatari kwa maisha yao.
Alibainisha kuwa afya bora kwa wananchi ndio msingi wa kupiga hatua
kwenye shughuli za maendeleo na uzalishaji kwani wananchi wakiwa na
matatizo ya kiafya hawawezi kufanya shughuli za uzalishaji na
maendeleo na wakati mwingine inagharimu sana kutibu magonjwa pale
wanapozembea kutambua afya zao na kushughulikia tatizo likiwa hatua za
awali au kujikinga kabisa.
“Pia ndugu zangu tujitokeze kuchangia damu kwenye benki yetu maana hii
asilimia 11.8 si ndogo ya wagonjwa wenye upungufu wa damu hivyo ni
wajibu wetu kuchangia damu”alisema Dk Nchimbi.
Kwa upande wake Mkuu wa idara ya Magonjwa ya ndani katika hopsitali ya
Mkoa wa Dodoma Dk Zainab. Chaula alisema kuwa takwimu zinaonesha kuwa
mwaka 2011 wagonjwa 6000 waliolazwa kwenye hospitali hiyo asilimia 12
kati yao walibainika kuwa na magonjwa yasiyoambukizwa jambo ambalo ni
vigumu kubaini mpaka mtu awe na desturi ya kupima afya.
Alibainisha kuwa kuwa miongoni mwa vitu vinavyoleta matatizo ya afya
ni pamoja na kutozingatia lishe bora na mazoezi, unywaji wa pombe wa
kupindukia, uvutaji wa sigara, matumizi ya dawa bila kuzingatia
maelekezo ya kitaalam na kukosa muda wa kupumzisha mwili.
Katika kampeni hiyo, timu ya wataalam wa huduma za afya kutoka
hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Dodoma wamekuwa wakitoa huduma
mbalimbali bila malipo ikiwemo kutoa elimu juu ya utunzaji wa afya,
kufanya vipimo na tiba (dawa) za magonjwa mbalimbali kama shinikizo la
damu, sukari, ushauri nasaha na kupima ukimwi na magonjwa mengine.
0 comments:
Post a Comment