Masoud Masasi,Dodoma
SERIKALI imefanya mabadiliko katika halmashauri hapa nchini kwa
kuwateua wakurugenzi wapya 14 huku ikiwavua madaraka wengine nane
ambao walionekana kushindwa kuwajibika ipasavyo katika halmashauri zao
na kufanya ubadhirifu wa fedha za halmashauri zao.
Pia katika mabadiliko hayo wakurugenzi kumi na moja wamepewa onyo
kali huku wengine 22 wakihamishwa vituo vya kazi ambapo wakurugenzi
watatu wakipumzishwa kufanya kazi katika halmashauri hizo kutokana na
sababu mbalimbali ikiwemo ubadhilifu wa fedha .
Akitangaza mabadiliko hayo mbele ya waandishi wa habari jana mjini
Dodoma Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu,Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa(Tamisemi)Hawa Ghasia alisema mabadiliko hayo yanatokana na
kuboresha nidhamu na utendaji wa kazi kwa wakurugenzi hao.
‘’Wakurugenzi 14 wameteuliwa ili kuziba nafasi zilizoachwa wazi huku
wakurugenzi nane wakivuliwa madaraka hayo na Waziri Mkuu wengine
watatu wakipumzishwa kabisa ambapo wakurugenzi 22 wakihamishwa katika
vituo vyao na kupelekwa sehemu nyingine”
“Mabadiliko haya ni kuboresha utendaji wa kazi katika halmashauri zetu
pamoja na kuongeza nidhamu na uwajibikaji wa kazi kwa wakurugenzi
ambao walikuwa si waadilifu katika kutelekeza majukumu yao”alisema
Ghasia.
Waziri huyo aliwataja wakurugenzi wapya walioteuliwa kuwa ni Jenifer
Omollo ambaye anakuwa mkurugenzi wa Mji wa Kibaha,Fidelica
MyovelaMkurugenzi mtendaji Halmashauri ya Musoma na Khadija Maulid
Makuwani ameteuliwa mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.
Aliwataja wengine kuwa ni Ibrahim Matovu ameteuliwa kuwa mkurugenzi
halmashauri ya Muheza,Idd Mshili halmashauri ya Mtwara,Julius Madiga
Mkurugenzi Halmashauri ya Manispaa yaMorogoro na Kiyungi Mohamedi
Mkurugenzi mtendaji halmashauri ya Shinyanga.
Wengini ni Lucas Mweri ameteuliwa Mkurugenzi mtendaji halmashauri ya
Nanyumbu,Miriam Mmbaga halmashauri ya Kigoma,Mwamvua Mrindoko
Mkurugenzi mtendaji Nachingwea,Pendo Malembeja Halmashauri ya Kwimba
huku Pudenciana akiteuliwa mkurugenzi wa Ulanga,Ruben Mfume
Halmashauri ya Ruangwa na Tatu Selemani amekuwa mkurugenzi mtendaji
halmashauri ya wilaya ya Kibaha ambapo waziri Ghasia alisema uteuzi
huo ulifanyika april 24 mwaka huu.
Waziri huyo alisema wakurugenzi waliovuliwa madaraka kutokana na
makosa mbalimbali katika Halmashauri zao kuwa ni Consolata
Kamuhabwa(Karagwe),Ephraim Kalimalwendo(Kilosa),Elly Jesse
Mlaki(Babati),Eustach Temu(Muheza),Jacob Kayange(Ngorongoro),Hamida
Kikwega. (Chato),Majuto Mbuguyu(Tanga) na Raphael Mbunda halmashauri
ya Manispaa ya Arusha.
Waziri Ghasia aliwataja wakurugenzi ambao wamepewa onyo kali kuwa ni
Judetatheus Mboya(Newala),Lameck Masembejo(Masasi),Abdallah
Njovu(Tandahimba),Jane Mutagurwa(Shinyanga),Silvia
Siriwa(Sumbawanga),Kelvin Makonda(Bukombe),Alfred
Luanda(Ulanga),Fanuel Senge(Tabora),Maurice Sapanjo(Chunya),na
Beatrice Msomisi halmashauri ya Wilaya ya Bahi.
Pia waziri huyo alibainisha kuwa katika mabadiliko hayo wakurugenzi
watatu ambao ni Xavier Tiweselekwa wa halmashauri ya Wilaya ya
Misungwi,Erica Mussica kutoka halmashauri ya Sengerema na Theonas
Nyamhanga wamepumzishwa kufanya kazi katika halmashauri hizo.
“Maamuzi haya yalifanyika katika kipindi cha mwaka 2011/12 na hawa
waliopewa onyo walitendeka makosa yao katika halmashauri zao hivyo
pia wakurugenzi 22 wamehamishwa katika vituo vyao vya kazi na
kupangiwa sehemu nyingine ili waweze kuimarisha utendaji kazi
wao”alisema.
Alisema tayari wakurugenzi wanne waliotuhumiwa katika ubadhilifu
mbalimbali katika halmashauri zao wameshafikishwa mahakamani huku
wengine wakiendelea kufanyiwa uchunguzi ambapo amesema wakibainika
watapelekwa mahakamani pia.
Alisema wale ambao walionekana hawakuhusika katika ubadhilifu katika
vituo vyao vya kazi walipangiwa kazi nyingine huku wale walionekana
utendaji wao sio mzuri walipumzishwa kabisa.
Waziri huyo pia aliwataka wakurugenzi wapya walioteuliwa na wale wa
zamani kuhakikisha wanafanya kazi kwa uhadilifu ili kuweza kuendelea
kuboresha utendaji wa kazi katika mamlaka za serikali za mitaa nchini.
Hata hivyo alisema hataweza kumchukulia hatua yoyote mkurugenzi kwa
kusikia taarifa za mitaani na kuwataka wale wenye malalamiko kupeleka
ushahidi kwake ambapo atafanya uchunguzi kabla ya mhusika kuchukuliwa
hatua za kisheria.
‘’Tukisema tuanze kuchukuwa hatua kwa kusikia taarifa za mitaani basi
tutajikuta tukifukuza wakurugenzi wote kinachotakiwa ni kuwa na
ushahidi uletwe na utafanyiwa kazi na hatua zitachukuliwa kwa Yule
atakayebainika”alisema waziri Ghasia.
0 comments:
Post a Comment