Florence Majani, Dodoma
NAIBU Waziri wa Kazi na Ajira, Dk Makongoro Mahanga amewataka wabunge kushirikiana na Serikali na wananchi wa maeneo yao kuibua miradi mbalimbali itakayoweza kutoa fursa za ajira kwa vijana waishio vijijini.
Dk Mahanga aliyasema hayo alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema) Christowaja Mtinda ambaye aliitaka Serikali kuanzisha miradi ya maendeleo vijijini ili kupunguza tatizo la ajira linalosababisha vijana kukimbilia mjini na kuishia kufanya kazi zinazowadhalilisha, kama kuuza miili, kupiga debe na kuokota chupa tupu.
Dk Mahanga alisema Serikali inafanya jitihada kadha wa kadha ikiwamo kutenga fedha nyingi katika bajeti yake kwa ajili ya maendeleo ya vijijini.
“Tumetenga fedha kwa ajili ya miradi kilimo, uvuvi, huduma za jamii, miundombinu na utunzaji wa mazingira, hizi zitasaidia kupunguza tatizo hili la ajira kwa vijana linalowafanya kukimbilia mijini,” alisema Mahanga.
Aliongeza kuwa Serikali imekuwa ikishirikiana na wadau katika kutekeleza miradi mbalimbali vijijini ikiwamo inayofadhiliwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii(TASAF) na Miradi ya Kilimo ngazi za Wilaya (DADPs,) miradi ambayo ina fursa kubwa kutoa ajira kwa vijana.
“Wizara ya Kazi na Ajira imeanzisha utaratibu wa kuziwezesha wizara na taasisi za umma kutambua fursa za ajira katika mipango na programu za maendeleo. Hatua hii itawezesha Serikali kutambua idadi na fursa za ajira zinazotokana na utekelezaji wa mipango yake katika maendeleo kila mwaka,” alisema Waziri huyo.
Kuhusu vijana kufanya kazi ya kuokota chupa tupu za maji, Mahanga alisema ujasiriamali una mambo mengi urejelezi likiwa ni moja wapo, hivyo basi hakuna tatizo kwa vijana kujiajiri katika kitengo hiki iwapo chupa hizo hutumika kutengeneza chupa nyingine.
Chanzo: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment