na Tiganya Vincent, Dodoma
MKUU wa Mkoa wa Singida, Parseko Kone, ametoa wito kwa taasisi za elimu nchini kuandaa wataalam watakaobuni mipango ya ujenzi wa nyumba za ghorofa ili watu wengi wapate makazi.
Alisema, ujenzi huo utasaidia kupunguza tatizo la wananchi kujenga katika maeneo ambayo ni muhimu katika uzalishaji wa mazao mbalimbali.
Kone alitoa kauli hiyo jana mjini Dodoma alipotembelea Chuo cha Mipango cha Dodoma katika banda Wizara ya Fedha katika maonesho ya Nanenane.
Alisema taasisi za elimu zatakiwa kuzalisha wataalamu watakaosaidia wananchi kujenga nyumba za ghorofa ili kufanya maeneo ya kilimo yaendelee kwa shughuli ya uzalishaji wa mazao.
Alisema utaratibu wa hivi sasa wa kila mtu kuchukua eneo kubwa na kujenga nyumba inayochukua idadi ndogo ya watu unasababisha watu wajenge hata katika maeneo muhimu ya uzalishaji wa chakula ambayo ni hatari kwa maisha ya baadaye ya watu katika suala la upatikanaji wa chakula na mazao mengine.
Alisema miaka 15 ijayo kama jitihada za kuzuia ujenzi wa nyumba ndogo zisipofanywa kuna kila dalili kuwa sehemu kubwa ya maeneo ya kilimo ikajaa majengo.
“Tunaweza tukajikuta ujenzi wa nyumba ukawa mkubwa zaidi na ukasambaa kila sehemu na kufanya eneo la uzalishaji wa mazao kuwa dogo kuliko la makazi, tujihadhari tusifike huko,” alisema.
Kone aliongeza kuwa ni vema eneo ambalo linastahili kwa uzalishaji wa mazao mbalimbali likabaki na shughuli ya kilimo badala ya kukimbilia kulijenga na ujenzi ufanyike katika maeneo ambayo hayafai katika shughuli za kilimo.
Hivyo, ameomba watalaam kutokuwa waoga katika kuandaa mipango ambayo faida zake zinataonekana miaka 100 ijayo.
Mkuu wa mkoa huyo alisema kuwa hivi sasa ni vema watalaamu wakaangalia utaratibu mpya wa mazishi ili ikiwezekana badala ya makaburi kuwa na eneo kubwa basi kuwepo na utaratibu wa kuchoma moto.
Maonesho ya wakulima ya Nanenane yanatarajia kufikia kilele keshokutwa ambapo kitaifa yanafanyika mjini Dodoma.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment